Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limefanikiwa kukusanya kiasi cha
zaidi ya shilingi milioni 825 kutokana na makosa madogo madogo ya barabarani
kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Hayo yalisemwa jana na kamanda wa polisi mkoani humo Ulrich
Matei alipoongea na waandishi wa habari mjini Kibaha kuzungumzia mafanikio na
changamoto zinazolikabili jeshi hilo.
Matei alisema kuwa katika kipindi hicho jumla ya makosa
yliyokamatwa katika kipindi cha Januari mwaka 2011 hadi Machi 2013 ni 31,663 ambapo
yaliyolipiwa yalikuwa ni 31,235.
“Katika kipindi hicho ajali zilikuwa 942 za vifo zilikuwa 190
waliokufa walikuwa 224, ajali za majeruhi zilikuwa 510 na waliojeruhiwa
walikuwa 1,109 ambapo inaonyesha kupungua kwa asilimia 25 ukilinganisha na
mikoa mingine,” alisema Matei.
Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha usalama barabarani
Nasoro Sisiwaya alisema kuwa wanaendelea na mikakati mbalimbali ya kuzuia ajali
ikiwa ni pamoja na kukamata magari mabovu.
Sisiwaya alisema kuwa wameunda vikosi maalumu viwili kwa
ajili ya kukagua magari ambapo kimoja kinafanya ukaguzi kwenye barabara iendayo
mikoa ya Kusini na kingine barabara ya Morogoro.
Aidha alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa kuyaondoa
magari yanayoharibika barabarani kwani hawana gari la kuyaondolea na matokeo
yake hutumia magari mengine kuyaondoa kwa kutumia mnyororo mgumu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment