Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam
(DAWASCO) wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imetakiwa kuwaunganishia maji wananchi
wa Mlandizi bila ya kujali uwezo wa mtu ili kila mtu aweze kunufaika na mradi
wa maji kwenye Kitongoji cha Janga.
Hayo yalisemwa na mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijni
Hamoud Jumaa wakati alipofanya ziara kutembelea mradi wa maji wa ya mkopo
kwenye kitongoji cha Janga kata ya Janga wilayanai Kibaha.
Mbunge huyo alitoa wito huo kufuatia mwenyekiti wa
kitongoji hicho Josephine Maendaenda kudai kuwa baadhi ya wananchi wanalalamika
kuwa watu wanaotoa fedha taslimu ndiyo wanaounganishiwa maji huku wale
wanaokopa kutakiwa kusubiri.
“Kwanza nawapongeza wananchi kwa kuchimba mitaro ya
kulaza mabomba hivyo thamani ya nguvu zao lazima zithaminiwe sawa na wale
wanaotoa fedha taslimu kwani mitaro hiyo isingechimbwa na wananchi hao maji
yasingeweza kufika kwenye maeneo ya watu,” alisema Jumaa.
Alisema kuwa thamani ya watu iko palepale lakini
haiwezi kwani wanaotoa fedha na wale waliotumia nguvu zao kuchimba mitaro wamefanya
kazi kubwa ambayo inapaswa kuungwa mkono na siyo ya kubezwa.
“Wananchi hawa wameonyesha uzalendo wa hali ya juu
kwa kufanyakazi ya kujitolea na ndiyo tunataka utamaduni huu ufanyike kwenye
kila jambo na si kusubiri serikali iwafanyie wananchi kila kitu kwani hata
kwenye mikoa iliyoendelea kama Moshi na Arusha imefanikiwa kwa wananchi
kujitolea kama huku,” alisema Jumaa.
Kwa upande wake meneja wa Dawasco wilaya ya Kibaha
Erasto Emanuel alisema kuwa suala hilo watalifanyia kazi kwa kuwaunganishia
wananchi bila ya kujali kama ni malipo ya moja kwa moja au mkopo.
Emanuel alisema kuwa hadi sasa wameweza
kuwaunganishaia maji wananchi 40 huku wakitarajia kuwafikia wateja 300 katika
hatua ya pili huku wakitarajia maji kuanza kutoka mwezi Oktoba na kuwafikia wateja
600.
Alisema kuwa mradi huo ulikumbwa na changamoto
mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa jambo ambalo lililalamikiwa na
wananchi lakini yote hiyo ilitokana na kila mwaka kuwa na zoezi la kufunga
mwaka ambalo huambatana na uhakiki wa vifaa.
Naye mwenyekiti wa Kitongoji cha Janga Josephine
Maendaenda alisema kuwa changamoto ya maji ni kubwa kwenye kitongoji hicho na
wananchi wamekuwa wakilalamika kiu yao kubwa ikiwa ni kupata maji ambapo
wamekuwa wakienda mwendo mrefu kufuata maji ambapo huuziwa dumu la lita 20 kwa
shilingi 500.