Tuesday, July 26, 2016

WADAU WACHANGIA BWENI LA SEKONDARI YA CHALINZE ILIYOUNGUA

Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA kuungua bweni la shule ya sekondari ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kuungua kwa moto baadhi ya wadau wameanza kuichangia shule hiyo ili kusaidia wanafunzi ambao vifaa vyao vyote viliungua.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi diwani wa kata ya Bwiringu Lucas Lufunga alisema kuwa kutokana na tukio hilo waliitisha kikao cha kata kwa ajili ya kuangalia namna ya kuisaidia shule hiyo.
Lufunga alisema kuwa katika kikao hicho walifanikiwa kupata kiasi cha shilingi 449,000 na kunua vyakula kwa ajili ya kusaidia kwani vyakula viliungua na moto huo ambao ulitokea usiku wakati wanafunzi wakiwa wanjisomea masomo ya usiku.
“Tunaomba watu mbalimbali wajitokeze kuwasaidia wanafunzi walikuwa wakiishi kwenye bweni hilo kwani kufuatia moto huo hakuna kilichotoka kwani vyote viliteketea kabisa hivyo kuna haja ya kulichukulia kwa uzito wake tatizo hilo,” alisema Lufunga.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwalimu mkuu wa Shule hiyo Emanuel Kahabi alisema kuwa moto huo ulitokea wakati wanafunzi hao wakiwa wanajisomea madarasani usiku.
Kahabi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 12 majira ya saa 2:50 usiku ambapo moto huo haukuweza kufahamika ulitokea wapi na kusababisha hasara kubwa ya bweni hilo na vifaa mbalimbali vikiwemo vya wanafunzi.
“Bweni hilo ambalo lilikuwa bwalo la chakula baada ya wanafunzi hao zaidi ya 100 kuhamishiwa humo kutokana na bweni lao kuungua kwa moto miezi michache iliyopita,” alisema Kahabi.
Alisema kuwa anawashukuru wadau ambao wameanza kuisaidi shule yake kutokana na moto huo ambao hadi sasa haijafahamika chanzo chake ni nini na kuwataka watu wakiwemo wakazi wa Chalinze, wilaya na mkoa amzima kuwasaidia wanafunzi hao.
Mwisho. 

ZOEZI LA UBOMOAJI LAZUA TAFRANI

     
Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la ubomoaji kwa amri ya Mahakama vibanda vya biashara vilivyopo eneo la mtaa wa Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani umeingia kwenye mgogoro baada ya familia ya iliyodaiwa kujenga kwenye eneo ambalo si lao wamedai vimebomolewa kimakosa.
Ubomoaji huoa ambao ulifanywa Julai 15 na kampuni ya udalali ya Coast Auction Mart baada ya kesi hiyo ambayo imedumu kwa kipindi cha miaka 35 familia hiyo ya iliyoongozwa na Eva Pwele ambaye alikuwa mlalamikaji bada ya baba yake mzazi Pwele Showe ailiyefungua kesi hiyo kufariki dunia kumlalamikia Tonga Fueta kudai eneo hilo ni mali yake ambapo mahakama ilimpa ushindi.
Akizungumza na mwandishi wa habari mdai Eva Pwele alisema kuwa maamuzi ya mahakama yalikuwa ni  mlalamikiwa kupewa eneo lenye ukubwa wa mita 3 na nchi 7 kwa mita 3 na nchi 5 na si mita 352.92 ikiwa ni maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya Mwanzo Kibaha mwaka 1980.
Pwele alisema kuwa baada ya maamuzi ya mahakama hayo miezi mitatu iliyopita alifuatwa na dalali na kutakiwa avunje mwenyewe lakini yeye hakufanya hivyo na kusema kuwa yeye anachojua ni kumkabidhi eneo lenye ukubwa wa mita 3 na nchi 7 tu na si hadi kwenye eneo walilojenga mabanda hayo ya biashara.
“Cha kushangaza siku ya tukio nililiona watu wakija wakiwa Dalali na kuanza kubomoa mabanda yetu ambayo yalijengwa hivi karibuni baada ya kutokuwa na wasiwasi juu ya eneo hilo kwani mapitio ya hukumu yalisema kuwa katika maamuzi ya mwanzo hayakuonyesha ukubwa wa eneo lakini mapitio hayo ya mwaka 2005 ndiyo yaliyosema kuwa mlalamikiwa alipaswa kurudishiwa sehemu iliyotajwa hapo juu,” alisema Pwele.
Alisema kuwa mbali ya maamuzi kukiukwa pia alishangaa wahusika wa bomoa hiyo kutokuwa na barua yoyote ambayo inawaruhusu kufanya ubomoaji huo ambao umewatia hasara kubwa kutokana na mabanda hayo kuvunjwa kwa madai ya kujengwa kwenye eneo la mlalamikiwa.
Kwa upande wake Tonga Fueta alisema kuwa kwanza anamshukuru Mungu kwani baada ya kuhangaika kwa miaka 35 hatimaye haki yake imepatikana kwani tangu mwanzo wa kesi hiyo ilipofunguliwa na mlalamikaji alikuwa akishinda kuanzia mahakama ya mwanzo hadi mahakama kuu kabla ya kukatiwa rufaa na mlalamikaji baada ya hukumu ya kwanza iliyotolewa na hakimu Chungulu mwaka 1981.
Fueta alisema kuwa alinunua eneo hilo mwaka 1969 kwa kiasi cha shilingi 400 toka kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Ramadhan na mwaka huo huo alimpa sehemu ya eneo hilo Pwele Showe ambaye kwa sasa ni marehemu lakini aliongeza na eneo lake.
“Mwaka 1971 nyumba zetu na mdai wangu zilivunjwa kupisha ujenzi wa barabara ya Morogoro ndipo naye akamfuata Ramadhan ili amuuzie eneo na kumuuzia kwa shilingi 500 na ndipo aliponimbia nivunje banda langu kwakuwa yeye ameshanunua ndipo tatizo hilo lilipoanzia,” alisema Fueta.
Kufuatia bomoabomoa hiyo familia ya Pwele imesema kuwa itatafuta haki yao kwenye vyombo vya kisheria kwani ubomoaji huo umekiuka amri ya mahakama kwa kuvunja sehemu ambayo haihusiki kwani wao walikuwa wakijiandaa kumkabidhi eneo kama ilivyoagizwa na mahakama.

Mwisho.

MAKUSANYO YA STENDI YAMSIKITISHA MKUU WA WILAYA


Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Asumter Mshama amesikitishwa na mapato yanayokusanywa kama ushuru ya shilingi milioni 1.5 kwa mwezi kwenye soko kuu la Maili Moja kuwa ni madogo sana ikilinganishwa na idadi ya wafanyabiashara sokoni hapo.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Kibaha wakati alipofanya mkutano na wafanyabiashara wa soko hilo kujua changamoto zinazowakabili na kusema kuwa mapato hayo ni madogo sana na Halmashauri hiyo inapaswa kuangalia namna ya ukusanyaji mapato hayo ili yaendanena na hali halisi.
Mshama alisema kuwa soko hilo ni chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri lakini ukusanyaji huo unakatisha tamaa kwani inaonekana kuna fedha hazifiki hivyo kuna haja ya suala hilo kufanyiwa kazi ili mapato halali yaweze kuonekana.
“Kiasi kilichotajwa cha shilingi milioni 1.5 kwa mwezi hakikubaliki vinginevyo tutafanya uhakiki wa wafanyabiashara wote kwa kupitia kibanda kwa kibanda ili tuweze kujiridhisha juu ya usahihi wa mapato sokoni hapo ambapo ushuru ni shilingi 300 kwa siku kwa kila mfanyabiashara ambapo kuna wafanyabiashara zaidi ya 500,” alisema Mshama.
Alisema kuwa kama ni mgodi soko hilo ndiyo mgodi wa kuchimbwa hivyo lazima makusanyo yake yafanywe kwa usahihi ili kutopoteza fedha kwenda kwenye mifuko ya watu binafsi.
“Makusanyo kama haya haiwezekani kwa soko hili hapa kuna tatizo lazima tupate ukweli kwani hili halikubaliki au mmeshindwa kukusanya kama tunakuja hapa kudaili milioni moja nadhani hata hichi kikao hakina maana ni bora tuondoke tukaendelee na shughuli nyingine,” alisema Mshama.
Akizungumzia juu ya Halmashauri kujitoa kuweka ulinzi alisema kuwa hilo ni kosa lazima ulinzi uwe chini ya Halmashauri na si kuwatwika mzigo wafanyabiashara mzigo huo kwani huduma hiyo ni faida kwa Halamshauri hivyo hakuna sababu ya wao kulinda wenyewe.
“Inashangaza kuona kuwa eti sehemu inayotuingizia mapato hatuiwekei ulinzi mbona pale ofisini mmeweka walinzi tena wa kampuni na hapa lazima mlinde hamna hoja katika hili ninachotaka jukumu hili mlichukue kama mlivyokuwa mkifanya zamani kama hamna fedha chukueni hizo mnazokusanya hapo za ushuru mlipe walinzi hili halina mjadala,” alisema Mshama.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi Lucy Kimoi alisema kuwa juu ya ulinzi ni utaratibu uliowekwa na Halmashauri kuwaondoa vibarua wote hali iliyosababisha na walinzi ambao walikuwa vibarua kuondolewa hivyo kukodisha kampuni ya ulinzi kulinda ofisi ya Halmashauri na sokoni jukumu hilo likaudi kwa wafanyabiashara.
Kimoi alisema kuwa hiyo ni sheria ya kuwaondoa vibarua ikiwa ni utaratibu wa serikali ndiyo sababu ya kulirudisha suala hilo kwa wafanyabiashara wa soko hilo ambao walikuwa wakichanga fedha kwa ajili ya ulinzi.

Mwisho.

WATAKA SOKO LIJENGWE JIRANI NA STENDI

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABISHARA wa soko la Maili Moja wilayani Kibaha wamesema kuwa endapo soko lao litahamishwa kutokana na kuwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara na kuhamishiwa eneo la Kitovu cha Mji endapo halitajengwa jirani na stendi hawatakuwa tayari kwenda huko.
Waliyasema hayo wakati wa mkutano wao na mkuu wa Wilaya ya Kibaha Asumter Mshama ambaye alikwenda sokoni hapo kusikiliza changamoto zinazowakabiliwa wafanyabiashara hao ambao wanatakiwa kuondoka kwenye eneo hilo ifikapo Septemba mwaka huu.
Aliyekuwa mwenyekiti wa soko hilo Ally Gonzi alisema kuwa tayari wameshaambiwa waondoke hapo lakini wanashindwa kuhama kutokana na Halmashauri kushindwa kujenga soko tangu mwaka 2013 ambapo walidai kuonyeshwa hadi michoro.
“Sisi hatutakuwa tayari kuhamia huko wanakotaka endapo hatawajenga soko letu jirani na stendi kwani vitu hivi vinakwenda kwa pamoja awali ramani ilionyesha kuwa tungekuwa jirani na stendi lakini baadaye tukasikia wanataka kutupeleka eneo la Mnarani maarufu kama Loliondo au Sagulasagula huko stendi ikiwa kitovu cha Mji,” alisema Gonzi.
Alisema kuwa kuwatenganisha kutawafanya wasipate wateja kwani wanunuzi wengi ni wale ambao wanasafiri pamoja na wateja kupata urahisi wa usafiri mara wanaponunua bidhaa ambapo kwa sasa soko lilipo ni jirani na stendi hivyo wanataka viende kwa pamoja.
“Awali Halmashauri walitushirikisha vizuri lakini walipobadili jinsi tutakavyokaa huko hawakutushirikisha lakini sisi tunasema tukitenganishwa hatutakuwa tayari kuhamia huko hivyo katika mipango yao wahakikishe wanatuweka pamoja na stendi ili huduma ziwe bora na sisi tupate wateja,” alisema Gonzi.
Akijibu suala hilo kaimu mkurugenzi Lucy Kimoi alisema kuwa ujenzi wa soko la kisasa unatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka huu ya 2016-2017 na taratibu za ujenzi zitafuatwa ili wafanyabiashara wawe kwenye mpangilio mzuri na wasiwe na wasiwasi.
Kimoi alisema kuwa waliomba mkopo kutoka benki ya uwezeshaji ya TIB kwa ajili ujenzi wa soko na stendi ambapo kwa sasa wanakamilisha kupata vibali toka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kupata fedha za kuanza ujenzi huo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Asumter Mshama aliitaka Halmashauri kuhakikisha inafanya ujenzi huo kwa muda uliopangwa na haitawahamisha wafanyabiashara hao hadi pale soko hilo litakapokuwa limejengwa ili kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara hao mara zoezi la bomobomoa litakapofanyika.
Mshama alisema kuwa stendi na soko vitakuwa pamoja hivyo wasiwe na wasiwasi kwani taratibu zote zitawekwa vizuri ili waweze kufanya biashara vizuri na kwa utaratibu na wafanyabiashara wote watapata nafasi kwenye soko jipya kwa kuzingatia aina ya biashara.

Mwisho.

TFS KANDA YA MASHARIKI YAKUSANYA MABILIONI

Na John Gagarini, Kibaha
WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki imefanikiwa kukusanya mapato yenye tahamani ya shilingi bilioni 13 kwa mwaka jana kutokana na tozo mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha meneja wa TFS Kanda ya Mashariki Dk Abel Masota alisema kuwa tozo hizo ni pamoja na faini zinazotokana na ukiukwaji wa taratibu za matumizi ya rasilimali za misitu ya hifadhi.
Dk Abel alisema kuwa mapato hayo ni pamoja na ukataji wa vibali kwa ajili ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu 17 kwenye misitu iliyo chini ya wakala hiyo kwenye kanda yake.
“Mapato hayo ni kwa kipindi cha mwaka uliopita wa 2015 ambapo ni pamoja na leseni za biashara za mazao ya misitu, faini na vibali mbalimbali vya biashara hizo za misitu na tunawataka wafanyabiashara hao wafuate taratibu ili kuinusuru misitu yetu kwa kuvuna kufuatatana na taratibu zilizowekwa,” alisema Dk Abel.
Alisema kuwa katika kuhakikisha misitu inakuwa salama uvunaji wa mazao ya misitu umepangwa kwenye mashamba ya miti ambayo si misitu ya hifadhi bali ni mistu ya wazi ambapo asilimia tano ya mapato hurudi kwenye maeneo ya vijiji kwa ajili ya upandaji miti.
“Tunashirikiana na serikali za vijiji kuhakikisha tano ya mapato zirudi kwa ajili ya upandaji miti kwa lengo la kuwa na sehemu ya uvunaji wa miti kwani kama hakutakuwa na mashamba ya miti ni dhahiri watu wafanyabiashara watakuwa wakivuna kwenye misitu ya hifadhi jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” alisema Dk Abel.
Alisema kuwa changamoto zinazoikabili wakala ni pamoja na uvamizi wa watu kwenye hifadhi ya misitu, vitendea kazi, kilimo na ufugaji kwenye hifadhi, uchomaji moto na uharibifu mwingine unaofanywa na watu kwenye misitu hiyo ambayo iko kisheria na kuingia humo ni kinyume cha sheria.
Aidha alisema wamekuwa wakifanya doria alkini kutokana na misitu hiyo kuwa mikubwa ni vigumu kuweza kuwadhibiti wahalifu wa misitu ambao wamekuwa wakivizia na kuingia na kufanya uharibifu na Kanda ya Mashariki inaundwa na mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam.
Mwisho.

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WATAKIWA KUANDAA DAFTARI LA CHANGAMOTO ZA WANANCHI

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuanzisha daftari maalumu la wakuu wa Idara kwenda kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi Vijijini kila mwezi.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kikao baina yake na wakurugenzi walioteuliwa hivi karibuni na Rais Dk John Magufuli juu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kikazi.
Ndikilo alisema kuwa umefika wakati sasa wa watendaji kwenda kuwatumikia wananchi na si kukaa ofisini wakati wananchi wakiwa na matatizo mengi huku wao wakiwa wamekaa ofisini tu.
“Nataka nione wakurugenzi mkiwa mmetengeneza dafatari hilo ambalo litamwonyesha mkuu wa idara kazi aliyoifanya kwa ajili ya kutatua kero na kule wanako kwenda lazima kuwe na sahihi zao kuwa walifika kwenye vijiji husika ili iwe ushahidi wa utendaji kazi wao na si kukaa tu ofisini,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa sambamba na hilo wakurugenzi lazima watenge siku maalumu ya kusikiliza kero za wananchi na mfumo wa kupata taarifa za matatizo kwa kila kata ili iwe rahisi kufuatilia ikiwa ni pamoja na kuweka sanduku la kero za wananchi ili zishughulikiwe mapema.
“Mnapaswa kushughulikia kero za wananchi kwa wakati kwani ucheleweshaji wa kutatua kero kwa muda muafaka husababisha matatizo kuongezeka na kufanya malalamiko kutoisha ambapo wananchi wamekuwa wakikimbilia kwa wakuu wa wilaya na mkoa huku kukiwa hakuna utatuzi ngazi ya Halmashauri,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa wakurugenzi wanapaswa kusimamia suala la ulinzi na usalama na wasiliache kwa serikali kuu ili wananchi waweze kufanya shughuli zao wakiwa na amani kwani kukiwa na uvunjifu wa amani itakuwa ni vigumu watu kufanya shughuli za maendeleo.
“Changamoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji, migogoro kutoshughulikiwa kwa wakati na mipaka pamoja na changamoto nyingine nyingi ambapo wajibu wa wakurugenzi ni kuwasimamia watendaji mbalimbali na hawapaswi kuwa na urafiki usiokuwa wa maendeleo kwa watendaji,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wakurugenzi hao kuwasimamia watendaji wao ili wasikae ofisini kusubiri maelekezo toka ngazi za juu bali waende kwa wananchi kwani muda huu si wa kukaa bali wanapaswa kuwa wabunifu na si kukaa tu kwani lazima wawe wawajibikaji.

Mwisho.

PWANI YATAKIWA KUMALIZA ZOEZI LA WATUMISHI HEWA


Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angella Kairuki ameutaka uongozi wa mkoa wa Pwani kuhakikisha unamaliza kushughulikia tatizo la watumishi hewa haraka.
Mkoa huo una jumla ya watumishi hewa 272 ambao wamebainika na kuitia serikali hasara ya shilingi bilioni 1.4 kufuatia zoezi la uhakiki wa watumishi hewa kufanyika kutokana na agizo la Rais Dk John Magufuli.
Kairuki aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa mkutano wake na uongozi wa mkoa huo, wakurugenzi wa Halmashauri na Miji za mkoa huo pamoja na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa ili kujua changamoto zinazowakabili watumishi wa Umma.
Alisema kuwa kwa kuwa tayari agizo la Rais lilishatoka tangu mwezi Machi mwaka huu kinachotakiwa ni kuwachukulia hatua wahusika baada ya kuwabaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili na si kuwaacha tu.
“Rais alitoa maagizo kubainisha watumishi hewa na baada ya kubainika wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwani wamefanya makosa ya kuiibia serikali hivyo hakuna sababu ya kutowachukulia hatua stahiki,” alisema Kairuki.
Aidha alisema kuwa hatua stahiki zichukuliwe mapema ikiwa ni pamoja na kurekebisha taarifa za watumishi hao ikiwa ni pamoja na kusitisha mishahara yao kabla ya malipo yamwezi Agosti ili tatizo hilo lisije likaendelelea.
“Pia nataka kusiwe na data chafu ambazo Halmashauri ziliweka kwa watumishi hao ambazo ni pamoja na kutopandishwa madaraja, malipo kwa watu ambao wana umri zaidi ya miaka 60 na watumishi kutokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi huku wakiendelea kulipwa,” alisema Kairuki.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa mkoa huo una watumishi 16,156 huku ukiwa na upungufu wa watumishi 3,306 na watumishi hewa waliobainika ni 272 kwenye Halmashauri saba za mkoa huo ambazo ni Kibaha Mjini, Kibaha, Mafia, Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na Bagamoyo.
Ndikilo alisema kuwa mkoa unalishughulikia suala la watumishi hewa ambapo wanashirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kusema kuwa zoezi hilo ni gumu hivyo inabidi walifanye kwa umakini ili lisije likaleta matatizo na watalikamilisha mapema.

Mwisho.