Thursday, February 25, 2016

ZIMAMOTO PWANI WAZUIA UUZAJI PETROLI MAJUMBANI

Na John Gagarini, Kibaha
KIKOSI cha zimamoto na uokoaji mkoni pwani kimewata wananchikuacha kuuza mafuta aina ya Petroli majumbani mwao ili kuepukana na milipuko ya moto inayotokana na mafuta hayo ambayo ni hatari.
Hayo yalisema mjini Kibaha na kamanda wa kikosi hicho Goodluck Zelote alipoongea na mwandishi wa habari hizi na kusema kuwa uuzaji huo wa kiholela ni hatari kwani umesababisha madhara makubwa ya uharibifu wa mali na watu kupoteza maisha.
Zelote alisema kuwa uuzaji huu si salama kwani kuhifadhi mafuta ya petrol ndani ni hatari kutokana na mafuta hayo kuwa ni rahisi kuwaka hivyo kuyauza kwenye nyumba za kuishi ni hatari sana kwa maisha ya watu.
“Utaratibu wa kuuza mafuta unafahamika lakini kwa sasa kumeibuka watu kuweka mafuta kwenye madumu pamoja na kwenye chupa za maji kisha kuyauza kwa madereva pikipiki na mafuta haya huhifadhiwa ndani jambo ambalo ni la hatari sana kwani watu wamepoteza maisha,” alisema Zelote.
Alisema kuwa mafuta hayo yanatakiwa yawekwe kwenye matenki na kuchimbiwa chini ndiyo utaratibu unaotakiwa lakini baadhi wanakiuka taratibu hizo kwa kuyahifadhi kwenye madumu ya maji.
“Tayari tumeshatoa elimu kuhusiana na kuepuka vitu ambavyo vinachangia moto kuwa majumbani ikiwa ni pamoja na kuepukana na utaratibu huo pamoja na kutohifhadhi pikipiki ndani ya nyumba kwani ni hatari bali wamiliki wangeangalia namna ya kuzihifadhi pikipiki zao,” alisema Zelote.
Aidha alisema kuwa bado wanendelea na utaratibu wa kutoa elimu kwenye maeneo mbalimbali ambayo yana mikusanyiko ya watu kama vile mashuleni, vituo vya mabasi, mikutano na kwenye masoko kwa lengo la kuwapatia elimu juu ya kujikinga na majanga.
“Vifaa vya kuzimia moto vinapaswa kuwa kwenye sehemu mbalimbali za huduma pamoja na majumbani ambapo sheria iko wazi na kuna adhabu kutegemeana na kosa na ukubwa wa huduma na kuna faini ambayo inaanzia 100,000 au kifungo cha miezi sita,” alisema Zelote.
Mwisho.

WAJERUMANI WAFAGILIA ELIMU BURE TANZANIA

Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya Raia wa nchi ya Ujerumani waliokuja nchini kwa ajili ya kufanya shughuli za kujitolea kwa jamii wilayani Kibaha mkoani Pwani wameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuanzisha utaratibu wa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha wakati wa zoezi la kusafisha eneo la kujenga shule ya sekondari ya mtaa wa Mbwate raia hao walisema kuwa utaratibu huo unatoa fursa kwa watoto wengi waliofikia umri wa kwenda shule kupata nafasi hiyo.
Laura Pommerenke alisema kuwa utoaji wa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari utalifanya Taifa la Tanzania kuwa na watoto wengi watakaokuwa wemekwenda shule tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Utaratibu wa elimu bure ni mzuri kwani hata kule kwetu ambako watu wanauwezo wanafunzi wanapata elimu bure hali ambayo inawafanya watoto kupata elimu inayostahili kwa wakati na kuondokana na watu kutokuwa na elimu,” alisema Pommerenke.
Alisema kuwa msingi wa elimu ya awali ukiwekwa utasaidia nchi kukabiliana na tatizo la watoto wa Tanzania kukosa elimu hali ambayo itazidi kuongeza umaskini lakini wakipata elimu watakuwa na uwezo wa kujitegemea.
Naye Marie Vogel alisema kuwa alisikia kuwa elimu ya Msingi na Sekondari ili kuwa na gharama jambo ambalo liliwafanya watoto wengi washindwe kwenda shule hivyo kuwafanya watoto wengi kuwa mitaani au kuanza maisha kabla ya wakati wao.
Vogel alisema kuwa serikali ya Tanzania inapongezwa kutokana na kuchukua maamuzi hayo ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari kwani mpango huo utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Abdala Mtandio alisema kuwa mpango wao wa kujenga shule ya sekondari kwenye mtaa wao umezingatia tatizo la watoto wengi kusoma mbali na kujikuta wakitumia mwingi njiani.
Mtandio alisema kuwa malengo yao ni kujenga madarasa manne ya kuanzia ili wanafunzi waanze kusoma hapo na wanahitaji kiasi cha shilingi milioni 50 za kuanzia pia wamewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia.
Mwisho.

WAZIRI SIMBACHAWENE AIKATALIA KEC COTC KUWA CHUO KIKUU

Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene amelitaka Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kutokibadili Chuo cha Waganga Wasaidizi (COTC) kuwa Chuo Kikuu ili lisiharibu malengo ya chuo kusomesha watu wenye elimu ya kawaida.
Simbachawene aliyasema hayo alipotembelea Shirika hilo hivi karibuni na kusema kuwa ndiyo sababu chuo hicho hakikuingizwa kwenye Taasisi ya elimu ya juu kwani malengo yake ni kusomesha watu ambao ni wa ngazi ya kati.
Alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na hali ya kila chuo kutaka kuwa chuo kikuu hali ambayo itasababisha kusiwe na wataalamu wa ngazi ya kati ambao wameonekana kuwa ndiyo wawajibikaji wakubwa.
“Kama kila chuo au taasisi itakuwa na malengo ya kuwa chuo kikuu kuna hatari ya kuwapoteza wasomi wa ngazi ya kati kwani endapo kila mtu atakuwa amesoma chuo kikuu hakutakuwa na watu wa kufanyakazi kwani kila mtu atatakuwa mtawala,” alisema Simbachawene.
Alisema kuwa chuo hicho kilianzishwa kwa malengo ya kuwapatia elimu watu wa vijijini lakini kikishafanywa chuo kikuu wananchi wenye elimu ya kati hawatapata nafasi ya kusoma hivyo malengo ya kuisaidia jamii hayataweza kufikiwa.
“Tunashindwa kupata wagunduzi kwani wanakuwa ni watu wenye elimu ya kawaida sana kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea hawa ni watu waliosoma elimu ya kawaida na wengine wanatoka vijijini hivyo na hapa ni sehemu ya kuanzia lakini tukikibadilisha na kuwa chuo kikuu ni sawa na kuvunja daraja ambalo watu wamekuwa wakitumia kuvukia kwenda mbele,” alisema Simbachawene.
Aidha alisema kuwa kuna tatizo la wataalamu wa kati kutokana na watu wengi kuiacha elimu ya kati na kutaka kupata elimu ya juu hivyo kumekuw ana pengo hapo katikakati pia wazingatie malengo ya kuanzishwa chuo hicho ambacho zamani kilijukana kama chuo cha maendeleo ya waganga vijijini.
Mwisho.

ACHOMWA MOTO KWA WIZI WA MCHELE DUKANI

Na John Gagarini, Kibaha
MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Ngozi mkazi wa Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani ameuwawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali kwa madai ya kuiba mchele na mafuta ya kupikia dukani.
Tukio hilo lilitokea Fabruari 25 majira ya saa 9 alfajiri katika mtaa wa Tangini baada ya marehemu akiwa na mwenzake ambaye alikimbia kuvunja na kutoa mchele huo kilogramu 100 na mafuta ya lita tatu galoni mbili.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Leons Karoli alisema kuwa watu hao waligunduliwa na baadhi ya madereva wa Bodaboda waliokuwa wakipita kwenye eneo la tukio na kuwakuta watuhumiwa hao wakiwa na vitu hivyo wakiwa wamevipakia kwenye pikipiki ya marehemu aina ya Boxer.
“Mashuhuda walisema kuwa marehemu alikuwa ndani ya hilo duka na kujifanya kama ndiye mwenye duka akijifanya ndiyo analifungua lakini watu walikuwa na wasiwasi kwani ilikuwa ni asubuhi sana jambo ambalo si la kawaida kwa mmiliki huyo kulifungua muda huo huku ambaye mmiliki wake ni Mmbando,” alisema Karoli.
Karoli alisema kuwa baada ya watu kuwa na wasiwasi waliwasiliana na watu kujaa kisha kuanza kumpiga marehemu hadi alipopoteza fahamu na mwenzake alifanikiwa kutoroka kwa kukimbia na kumwacha mwenzake ambaye alibainika kuwa ni muuza matunda pia ni dereva bodaboda.
“Tulifanya mawasiliano na polisi na kuwajulisha kuwa kuna mwizi kakamatwa lakini kabla hawajafika watu hao wenye hasira walimpiga kisha kumchoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli na kusababisha kifo chake,” alisema Karoli.
Alisema kuwa marehemu alikuwa na begi ambalo lilikuwa na vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkasi mkubwa unaotumika kukatia makufuli, nondo, vocha za simu pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi 150,000.
Jeshi la polisi mkoani Pwani lilithibitisha kutokea tukio hilo na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi kwa kutoa taarifa polisi kwa hatua zaidi za kisheria na si kuwauwa watuhumiwa wa matukio ya kihalifu.
Mwisho.
  



MSHINDI UVAAJI SARE ZA CCM ALONGA

Na John Gagarini, Kibaha
MSHINDI wa Uvaaji wa sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM)Kibaha Mjini mkoani Pwani Said Ngombe amempongeza mwenyekiti wa chama hicho Dk Jakaya Kikwete kwa kutaka kuenziwa watu wanaokifanya chama kishinde kwenye chaguzi mbalimbali.
Mshindi huyo akizungumza na wandishi wa habari mjini Kibaha baada ya kupewa tuzo na Dk Kikwete wakati wa sherehe za kuzindua jengo la CCM Kibaha Mjini lililojengwa na Mbunge wa Jimbo hilo Silvestry Koka  alisema kuwa kuthamini mchango wa wanachama au makada wake ni moja ya njia za kuwapa motisha ili waendelee kukitetea chama chao.
Ngombe alisema kuwa anamshukuru mwenyekiti kuliona hilo na kutaka viongozi wa maeneo mengine kuiga utaratibu huo wa kuthamini mchango wa wanaccm waliosababisha chama kushinda au kukipigania.
“Tunamshukuru mwenyekiti kwa kutupa tuzo na kuwataka viongozi wa maneo mbalimbali kuwaenzi wanaccm waliojitolea kukipigania chama bila ya kuchoka na mimi nimekuwa nikivaa sare ya chama kila siku ambapo kwa sasa nina miaka tisa mfululizo bila ya kuacha,” alisema Ngombe.
Alisema kuwa anajisikia fahari kupewa tuzo hiyo ya uvaaji wa sare kwani imempa moyo wa kuendelea kukipigania chama licha ya kukumbwa na changamoto nyingi kutoka kwa wapinzani wao vyama vingine.
“Kuvaa kwangu sare za chama kwenye eneo lango la kufanyia kazi imekuwa chachu ya chama chake kufanya vizuri kwani watu wamekuwa wakinifahamu kwa uvaaji wangu huu na nimekuwa nikiwakabili wapinzani wetu kwa hoja kwani wakishaniona wamekuwa wakinitania na mimi ndo ninapopata muda wa kuwapa sera za chama huku wengine wakijiunga na chama kupitia kwangu kwani naonyesha msimamo wangu wa chama,” alisema Ngombe.
Aidha alisema kuwa anashangazwa na baadhi ya wanaccm kuogopa kuvaa sare za chama kwani hata kwenye vikao wengine wamekuwa hawavai licha ya kutakiwa kuvaa wanapokuwa kwenye mikutano na vikao vya chama.
Alishauri tuzo hizo ziambatane na fedha kidogo kwa ajili ya kuongeza motisha kwa wanaofanya vizuri kwneye nyanja mbalimbali za kukipigania chama bila ya kuwa na woga wa aina yoyote tofauti na ilivyo wanachama au wapenzi wa chama.
Mwisho.   

BIBI AINGIA MATATANI KIFO CHA MWANAE

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
BIBI Nuru Mchenga mwenye umri wa zaidi ya miaka (80) mkazi wa Maili Moja B wilayani Kibaha mkoani Pwani amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya wananchi kumlalamikia kukaa na maiti ya mwanae kwa masaa kadhaa bila ya kuwataarifu watu.
Mbali ya kumshangaa kukaa na maiti muda mrefu pia walimshangaa bibi huyo kumsafisha mwanae kwa taratibu za dini ya Kiislamu jambo ambalo ni kinyume kwani huwa linafanywa na wanaume.
Tukio hilo lilitokea Fabruari 24 majira ya mchana ambapo Mwanae Kassimu alifariki majira ya saa nane hapo nyumbani kwake baada ya kudaiwa kuwa alikuwa anaumwa.
Wakizungumza na waandishi wa habari majirani wa Bibi huyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao magazetini walisema kuwa wameshangazwa na kitendo hicho cha kukaa na maiti kwa muda wote huo bila kuomboleza kama ilivyo kwa watu wanaofiwa ambao hulio kuashiria kuwa kuna msiba.
Walisema kuwa kilichowashangaza ni jinsi gani bibi huyo alipomfanyia usafi mwanae wa kiume jambo ambalo ni kinyume na taratibu za dini ya Kiislamu hali ambayo ndiyo imezua maswali mengi.
Alisema marehemu alipaswa kufanyiwa taratibu za kidini na mwanaume na si mwanamke kama alivyofanya bibi huyo ambaye watu wengi wamemshangaa kwa ujasiri huo.
“Inasikitisha sana kuona bibi huyu anafanya vitu kama hivyo ndiyo maana kumekuwa na maneno mengi kutokana na kifo cha mwanae kutokana na alivyofanya na pia haonyeshi kusikitika kifo cha mwanae tofauti na misiba mingine,”  walisema majirani hao.
Kwa upande wake Bibi huyo akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake alisema kuwa mwanae alilogwa kwa kutupiwa jini na watu ambao hawaipendi familia yake na kusababisha kifo hicho.
Mchenga alisema kuwa siku ya tukio hilo mwanae alikuwa tu nyumbani nay eye alikuwa akiendelea na shughuli zake na kushangaa kuona mwanae hana uchangamfu.
“Ilipofika mchana mwanangu alifariki na kabla hajafariki tulikubaliana nikifa mimi yeye ataniosha na akifa yeye mimi nitamwosha ndiyo sababu ya mimi kufanya hivyo,” alisema Mchenga.
Alisema kuwa anashangaa kuona watu wanataka kumfanyia fujo nyumbani kwake na kusema kuwa watu wanasema maneno mengi juu ya kifo cha mwanae huyo.
Kutokana na watu kujazana nyumbani kwa bibi huyo ilibidi jeshi la polisi kuuchukua mwili wa marehemu majira ya saa 3 usiku na baadaye walirudi tena majira ya saa tano kasoro na kumchukua bibi huyo kutokana na kuhofia usalama wake kwani watu walikuwa wakimzonga na kumzomea, Jeshi la polisi limethibitisha kutokea tukio hilo.
Mwisho.
  



Sunday, February 21, 2016

WAZIRI SIMBACHAWENE ALIPA NENO SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imesema kuwa itaangalia upaya uendeshaji wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ili lizalishe liweze kujiendesha kwa ufanisi badala ya kuitegemea serikali ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene alipotembelea Shirika hilo kujionea utendaji kazi wake na na kuongea na wafanyakazi kujua changamoto zinazowakabili na kusema kuwa linapaswa kujiendesha kwa faida na si kuwa tegemezi.
Simbachawene alisema kuwa Shirika hilo la Umma lilianzishwa kwa lengo la kusaidia wananchi hasa wale wa vijijini kwa wakati ule lakini linapasw akubadilika kutokana na wakati na kuacha mifumo ya uendeshaji wa kizamani ambayo haiendani na hali halisi ya wakati uliopo hivyo kushindwa kunufaisha watumishi na wananchi.
“Haiwezekani Shirika kama hili lenye rasilimali na vyanzo vingi vya mapato ikiwa ni pamoja na ardhi kubwa linakuwa na watumishi ambao ni maskini huku wakikosa stahiki zao za kimsingi na kufanya liyumbe ni jambo la kusikitisha sana hivyo serikali itakaa na kuangalia njia za kuweza klirudisha kwenye uhalisia wake,” alisema Simbachawene.
Alisema kuwa Shirika linayumba kw asababu hakuna mipango mikakati ya kujiendesha kisasa kwani maono yake yanaonekana bado ni ya kizamani kwa kuendelea kudeka kwa serikali licha ya kuwa na fursa nyingi zianazolizunguka.
“Mbali ya mfumo wa uendeshaji kuwa na matataizo mengi pia wafanyakazi wamelalamika sana juu ya maslahi yao ikiwa ni pamoja na malipo ya kazi z aziada, kupandishwa madaraja na maslahi mengine nitakuja na majibu ya maswali yenu pia tume itaundwa kila sekta ili kubaini matatizo yaliyopo na kuyafanyia kazi,” alisema Simbachawene.
Kwa upanade wake mwenyekiti wa bodi ya Shirika Patrick Makungu alisema kuwa watazifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wafanyakazi ambazo zinawafanya watumishi washindwe kutoa huduma bora.
Naye mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Dk Cyprian Mpemba alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawafanya washindwe kutoa huduma bora ikiwa ni pamoja na kuwa na mahitaji ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya uendesheaji.
Dk Mpemba alisema kuwa mbali ya changamoto hizo wamepata mafaniko kupitia mfumo wa kieletroniki wa ukusanyaji wa mapato ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi ambayo iko chini ya Shirika hilo kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 3,000,000 toka 300,000 kwa siku.
Waziri alitembelea Hospitali hiyo, aliangalia mfumo wa ukusanyaji mapato wa kieletroniki uliobuniwa na shirika hilo, kampuni ya ufugaji kuku ya Organia, Shirika hilo lilianzishwa miaka zaidi ya 40 iliyopita na nchi za NORDIC likiwa na lengo la kupambana na adui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi na lina wafanyakazi zaidi ya 900 na lina miliki Hospitali ya Tumbi, Chuo cha Waganga wasaidizi, Chuo cha Ufundi Stadi VETA, Shule z a sekondari Kibaha wavulana na Wasichana, Tumbi, shule ya msingi Tumbi na awali     

 MWISHO