Na John Gagarini,
Kibaha
KONSTEBO wa Polisi
aliyeuwawa na majambazi waliovamia kituo cha Polisi cha Ikwiriri wilayani
Rufiji mkoani Pwani Judith Timoth (32) juzi aliagwa mjini Kibaha na mamia ya
watu wakiwemo askari wenzake aliowahi kufanya nao kazi kabla ya kuhamia Rufiji.
Mwili huo uliagwa
kwenye hospitali ya Polisi mkoa na kuongozwa na ofisa wa jeshi hilo Thabita
Makaranga, kwa safari ya kuelekea mkoani Mbeya kwa ajili ya mazishi na kuliibua simanzi kubwa kwa watu
waliohudhuria tukio hilo na kuvuta hisia na vilio kutoka kwa waombolezaji.
Akiongoza kwenye ibaada
ya kumwaga marehemu mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Usharika wa Maili Moja alikokuwa akisali kabla ya kuhamia wilayani Rufiji,
Josephine Urio alisema kuwa watu wanapaswa kujiandaa kwa kusali muda wote kwani
hawajui siku wala wakati watatwaliwa.
“Wanadamu wanapaswa kuacha
roho za mauaji kama hao waliofanya mauaji hayo kwani hawako salama kama
wanavofikiri Mungu atawapa pigo kama walivyotoa roho za watu wasiokuwa na hatia
na watu wenye uovu waache njia hizo,” alisema Urio.
Akisoma wasifu wa
marehemu moja ya wafanyakazi wenzake Robert Munisi alisema kuwa jeshi hilo
litapambana na watu wote waliohusika na tukio hilo na kuliomba kanisa
lilisaidie polisi kukabiliana na wahalifu hao na watasimamia amri kumi za
Mungu.
Munisi alisema marehemu
alizaliwa mkoani Mbeya na kupata elimu ya Msingi na Sekondari na kupata mafunzo
ya sheria mkoani Mbeya kisha kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Polisi huko Moshi
kuanzia Oktoba 30 mwaka 2004 na kuhitimu Fabruari 25 mwaka 2005 pia alipata
mafunzo mbalimbali yakiwemo ya Upelelezi.
Aidha amesema marehemu
kabla ya umauti alikuwa akisoma masomo ya Sociology mwaka wa pili Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT) ameacha mtoto mmoja wa kiume aitwaye Bryan.Marehemu
alivamiwa juzi akiwa kazini na mwenzake majira ya saa 8 usiku na kushambuliwa
na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi waliokuwa na silaha na kufariki dunia
yeye na mwenzake Koplo Edger Milinga.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
WAZAZI wa shule ya
Msingi Juhudi kata ya Visiga wilayani Kibaha wameulalamikia uongozi wa shule
hiyo kwa kuwarudisha watoto wao wanaojiunga darasa la kwanza kwa kushindwa
kulipa kiasi cha shilingi 15,000 kwa ajili ya kuwaandikisha.
Moja ya wazazi hao
Mabeka Mabeka akizungumza kwenye kikao cha wazazi alisema kuwa wanashangazwa na
taratibu za kuwatoza kiasi hicho licha ya kuwa serikali imekataza michango hiyo
na kusababisha wazazi kuwa kwenye wakati mgumu kupata fedha hizo.
Mabeka alisema kuwa
wanaushangaa uongozi wa shule hiyo kwa kuwaandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza kwa
kututoza fedha hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwani serikali ilitamka
kuondoa michango kwa wanafunzi wanaoanza ili kuondoa kero kwa wazazi.
“Michango hii ni
kikwazo kwa wazazi kuwapeleka watoto shule huku serikali ikitaka watoto wote
waliofikia umri wa kwenda shule waandikishwe ili waweze kupata elimu ya msingi,”
alisema Mabeka.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Theobad Rwegalulila alikiri kuwepo kwa jambo
hilo na kusema kuwa limekuwa changamoto kubwa kwa wazazi ambao wamekuwa
wakilalamika kupinga malipo hayo ili watoto waweze kupata fursa ya kujiunga na
darasa la kwanza.
Naye mwalimu mkuu wa
shule hiyo Hawa Mgogolo alikiri kuwepo kwa michango hiyo na kusema kuwa
walikubaliana na wazazi kwenye kikao cha wazazi mwaka 2012 lakini anashangaa
wazazi hao kuanza kulalamika wakati wao wenyewe walikubali mchango huo.
Mgololo alisema kuwa ni
kweli walikuwa wakiwatoza fedha hizo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na fedha
hizo zinatumika kununulia vitu mbalimbali kama vile chaki, madaftari ya
maendeleo na vifaa mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi hao.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
SHULE ya Msingi ya
Maili Moja iliyopo wilayani Kibaha inakabiliwa na ubovu wa madarasa ambayo
yanaweza kuanguka wakati wowote hali ambayo inahatarisha usalama wa wanafunzi
na walimu kwenye shule hiyo.
Kutokana na ubovu huo
madarasa matano kati ya 11 ndiyo yanayotumika ambapo wanafunzi wanasoma zaidi
ya wanafunzi 150 hadi 200 kwenye darasa moja.
Akizungumza na
waandishi wa habari wakati wa kikoa cha dharura cha wazazi kuzungumzia ubovu wa
madarasa hayo, mwalimu mkuu wa shule hiyo Reginald Fanuel alisema kuwa madarasa
hayo yamebomoka vibaya.
“Madarasa hayo yako
kwenye hali mbaya na wakati wowote yanaweza kuanguka na kusababisha maafa kwa
wanafunzi na walimu endapo hazitachukuliwa hatua za haraka za kunusuru hali
hiyo ambayo sasa imefikia hatu mbaya,” alisema Fanuel.
Fanuel alisema kuwa kutokana
na hali hiyo wanaomba msaada wa kusaidiwa ujenzi ili kunusuru hali hiyo ambayo
ni hatari kwa wanafunzi na walimu wanaotumia madarasa hayo pia mlundikano
kwenye madarasa mazima ni mkubwa sana.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa kamati ya shule Said Chitenje alisema kuwa tatizo hilo lilianza
muda mrefu ambapo wamekuwa wakiakabiliana na hali hiyo kwa kuchangisha michango
wazazi lakini michango imekuwa ikisusua.
“Kweli hali ni mbaya
na kutokanana hali kuzidi kuwa mbaya tumekubaliana na wazazi kuwa kila mzazi
ambaye ana mwanafunzi shuleni hapa atoe kiasi cha shilingi 5,000 kwa ajili ya
kufanya ujenzi wa madarasa hayo,” alisema Chitenje.
Naye diwani wa kata ya
Maili Moja Andrew Lugano alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na mchakato wa
kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya ujenzi wa madarasa hayo yaliyoharibika ili
kuwanusuru wanafunzi hao.
Lugano alisema kuwa
wazazi hao waliomba wakutane na mkurugenzi wa halmashauri ya Mji ili
wazungumzie suala hilo na namna ya kuwez akukabiliana na tatizo hilo na
kuwaomba watu na wafadhilimbalimbali kujitokeza kusaidia ujenzi wa majengo
hayo.
Mwisho.