Monday, July 22, 2024

KAMPENI KUPINGA UKATILI DHIDI YA WATOTO NA WATU WENYE UALBINO




(ATFT) KWA KUSHIRIKIANA NA  HALMASHAURI YA KIBAHA MJI Yaendeleza kampeni yake ya  kupinga ukatili dhidi ya watoto na watu wenye mahitaji maalum, kwakutumia michezo na sanaa, kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka (18) na kuendelea, kama njia moja wapo ya kutoa elimu kwa jamii mbalimbali, ATIFITI CUP) Itakayo zinduliwa trh 23/08/2024 ikidhaminiwa vinywaji na kampuni U-FRESH, tarehe 20/07/2024, USHIRIKI WAKO NI MUHIMU  KUENEZA ELIMU TAJWA HAPO JUU.

AWESO AAHIDI KUONDOA CHANGAMOTO UKOSEFU MAJI KILUVYA




WAZIRI wa Maji Juma Aweso ameahidi kupeleka wataalamu Kata ya Kiluvya Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani ili kufanya tathmini ya maeneo yenye changamoto ya maji.

Aweso alitoa ahadi hiyo kwa njia ya simu kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti uliofanyika eneo la Kiluvya Madukani kutatua changamoto za wananchi.

Alisema atatuma timu yake leo Jumatatu ili wafanye kazi hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi hao wanapata maji na kuondokana na changamoto za ukosefu wa maji.

"Ombi lenu nimelisikia Jumatatu natuma timu itakuja kufanya tathmini kwa yale maeneo ambayo yana changamoto hivyo msiwe na wasiwasi tutatatua shida hiyo,"alisema Aweso.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti alipiga simu ili kuwapatia majibu wananchi waliokuwa wakilalamika kukosa maji kwenye baadhi ya maeneo.

Magoti alisema kuwa wananchi wawe na uvumilivu kidogo kwani serikali inawasikiza na wanafanya kazi kwa kushirikiana na ndiyo sababu amempigia Waziri wa Maji.

Alisema kuwa suala la maji ni jambo muhimu sana hivyo lazima lishughulikiwe kwa uharaka ili kuondoa changamoto ambapo Rais Dk Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua mama ndoo kichwani.

Kwa upande wake meneja wa DAWASA Emanuel Mbwambo alisema kuwa mpango uliokuwa ni mwezi wa Agosti kuhakikisha baadhi ya maeneo yenye changamoto yanafikiwa na huduma hiyo.

Mbwambo alisema kuwa baadhi ya maeneo ambayo yana changamoto ya ukosefu wa maji kwenye Kata hiyo.

Moja ya wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Meri Charles mkazi wa eneo la Makurunge Majumba 6 alisema kuwa maji kwao hawana maji kabisa.

Charles alisema kuwa wao wanakunywa maji ya bwawani huku wanafunzi wakitakiwa kubeba maji lita tano kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya shuleni.


Sunday, July 21, 2024

JISAJILI KWENYE KANZI DATA KWA USALAMA WAKO.





Jeshi la Polisi Mkoani Pwani kwa kushirikiana  na Maafisa usafirishaji Wilaya ya Kibaha (bodaboda) limezindua zoezi la uvaaji viakisi mwanga katika Wilaya hiyo ili kuwezesha  kuwa rasmi na kuepuka kukumbwa na majanga mbalimbali ikiwemo kuporwa vyombo vyao vya moto.

Akizungumza katika uzinduzi huo,  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Pius Lutumo amewataka maafisa hao kuhakikisha wanajisajili katika kanzi data ili kutambulika wao na vijiwe wanavyofanyia kazi.

Amesema endapo wadau hao watajisajili kati kanzi data na kutii sheria za usalama barabarani ajali zitapungua kwa kiasi kikubwa, matukio ya wizi kwa kutumia Bodaboda yatakwisha na wahalifu wanaojificha kwa mgongo wa  bodaboda watadhibitiwa.

Lutumo amewakumbusha madereva waliosajiliwa kwenye kanzi data kutowaazima viakisi mwanga vilivyo na namba za utambulisho kwa wenzao ambao hawajajisajili kwani wanaweza kufanya matukio ya kihalifu na viakisi mwanga vikatumika kama utambulisho wa watuhumiwa hao kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake Katibu wa  Chama cha Maafisa Usafirishaji Wilaya ya Kibaha Mwinyichande Mungi amesema watatekeleza zoezi hilo kwa weledi na kuhakikisha kila anayetaka kufanya kazi hiyo anafuata taratibu ikiwa ni pamoja na kujisajili na kupata namba ya utambulisho.

Aidha mwenyekiti wa CCM Kata ya Kongowe Saimon Mbelwa amewataka madereva hao kutambua kazi yao ina mchango mkubwa kwa jamii hivyo wale wenye kuingia kwenye kazi hiyo kwa lengo la kufanya vitendo vya Uhalifu wanapaswa kupigwa vita na kufichuliwa.

MADEREVA WA SERIKALI PWANI WAKUMBUSHANA UWAJIBIKAJI




Na Mwandishi wetu, KIBAHA 

CHAMA cha Madereva wa Serikali Mkoa wa Pwani kimewakumbusha madereva kuwajibika katika majukumu yao Ili waweze kupata haki zao wanazostahili.

Mwenyekiti wa Chama hicho Michael Mbilinyi aliyasema hayo Julai 21 katika mkutano uliofanyika mjini Kibaha ambao ulihudhuriwa na viongozi wa chama hicho kutoka Halmashauri za mkoa wa Pwani .

Katika mkutano huo ambao ulilenga kujadili mambo mbalimbali ya chama uliambatana na semina elekezi ilivyokuwa ikielezea wajibu wa madereva wawapo kazini na mambo ya kufuata kabla hawajadai haki zao za msingi.

"Tutekeleze wajibu wetu halafu tutadai haki zetu za msingi, tuzingatie kufuata muda wa kazi na lugha sahihi pindi tunapokuwa na viongozi wetu utii na uwajibikaji utaondoa ukakasi wakati wa kudai haki," amesema Mbilinyi.

Mwenyekiti huyo amesema chama hicho ambacho uongozi wake ni kuanzia ngazi ya Taifa pamoja na mambo mengine kinatetea haki za madereva kwa mwajiri pindi anapoenda tofauti lakini pia dereva akienda kinyume wanamrudisha kwenye maadili.

Katibu wa chama hicho Isack Chambo aliwasisitiza wanachama kuzingatia michango waliyoiweka Ili kuendelea kuwa hai lakini pia kufanya mambo ambayo yapo ndani ya chama hicho kwa mujibu wa katiba yao.

Naye mmoja wa Wajumbe wa mkutano huo kutoka Halmashauri ya Chalinze Mkombozi Maskuzi ameomba viongozi wao kuwaandalia semina elekezi za mara kwa mara lakini pia waweatembelee kwenye maeneo yao huku wakizingatia kutoa taarifa sehemu zao za kazi Ili kuonyesha umuhimu wa nafasi zao.

Mjumbe mwingine aliyeshiriki mkutano huo Briton Kidinzi amewataka madereva kuwa mfano kwenye utendaji kazi wao mahala pa kazi kwa kufuata Sheria na maadili.


Mwisho

Wednesday, July 17, 2024

FANYENI UCHUNGUZI WA MACHO ANGALAU MARA MOJA KWA MWAKA






Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wananchi wameshauriwa kufanya uchunguzi wa macho angalau mara moja kwa mwaka ili kubaini kama kuna viashiria vya shambulizi la ugonjwa wa sukari katika jicho, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho, Dkt Joshua Mmbaga, ameshauri.

Dkt Mmbaga, ambaye anatoka Kliniki ya Macho ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ameyasema leo wakati akiwasilisha mada katika programu maulumu ya mafunzo maarufu kama Continues Medical Education (CME) inayotolewa kila Jumatano ikihusisha watumishi wote wa BMH. 

"Ugonjwa wa kisukari ambao unasababisha kiwango cha sukari katika damu ambacho kinaharibu seli ambazo zinaenda kuharibu mishipa ya damu na kusababisha kuwa mishipa milaini hivyo kupasuka kirahisi na kusababisha kuvuja damu na kupoteza uwezo wa kuona," amesema Dkt Mmbaga.

Dkt Mmbaga ametaja sababu za  ugonjwa wa kisukari kuwa ni ulaji wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha sukari,wanga na unywaji wa kiwango kikubwa na uliopitiliza wa pombe, akisema hii inasabisha ugonjwa wa kisukari ambao baadae unaenda kushambulia jicho.

Dkt. Mmbaga ametaja dalili za ugonjwa huu kuwa ni kutokuona vizuri, kuona mawingu mawingu, kuona kama vijidudu vinaelea angani na kuona vitu katika maumbo yamebadilika au ghafla kupoteza uwezo wa kuona . 

“Nashauri watu kufanya uchunguzi wa macho angalau mara moja kwa mwaka hata kama huna tatizo la sukari lakini pia watu wajihusishe na mazoezi ya viungo ili kujiweka katika hali nzuri ya kiafya.” amesema Dkt Mmbaga.

Dkt. Mmbaga ametoa wito kwa wenye matatizo wa kisukari wafike Hospitali Benjamin Mkapa wachunguze macho yao na kufata masharti ya madaktari wao na waliokutwa na tatizo hilo waanze matibabu mara moja ili kuepuka kupata madhara makubwa zaidi.

Tuesday, July 16, 2024

WATAKIWA KUACHA IMANI ZA KISHIRIKINA KUPATA UONGOZI











VIONGOZI wanaowania nafasi za uongozi wametakiwa kuacha kuwa na imani kuwa viungo vya watu wenye Ualbino vinasaidia kupata uongozi.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Diwani wa Viti Maalum Lyidia Mgaya wakati wa Kongamano la kupinga ukatili dhidi ya ya watoto na watu wenye Ualbino Halmashauri ya Mji Kibaha. 

Mgaya amesema kuwa kumekuwa na dhana kuwa viungo vya watu wenye ualbino vinaweza vikamfanya mtu akapata uongozi au mali hali ambayo inasababisha vitendo vya ukatili.

"Uongozi hutolewa na Mungu na siyo viungo vya binadamu na hata mali hazipatikani kwa kutumia viungo bali ni kutokana na jitihada za mtu mwenyewe kwa uongozi ni kuwajibika na mali ni kuwa na jitihada,"amesema Mgaya.

Amesema kuwa kutokana na dhana hizo potofu zimeendelea kuwafanyia ukatili watu wakiendekeza mila ambazo ni potofu na zinapaswa kupigwa vita.

"Jamii ifike wakati iachane na dhana potofu ambazo zina athari kwa watu wengine na zinasababisha jamii nyingine isiishi kwa amani tuziache na kupiga vita kwa nguvu zote,"amesema Mgaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jukwaa la Vipaji Tanzania (ATF) Maryrose Bujashy amesema kuwa wameandaa kongamano hilo ni kutambua viashiria vya ukatili wa watoto na watu wenye albino na namna ya kudhibiti.

Bujashy amesema kuwa kutokana na matukio kadha ya ukatili dhidi ya watoto na watu wenye ualbino ndiyo sababu ya kuandaa kongamano hilo ambalo wameshirikiana na asasi mbalimbali za serikali na zile zisizo za kiserikali ili kutambua uelewa wa wadau mbalimbali kuhusu swala hilo na kujua namna gani linaweza kupunguzwa au kutatuliwa.

Amesema wanatarajia kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutia elimu juu ya malezi ya watoto, watu wenye ulemavu, watu wenye ualbino, viashiria vya ukatili juu ya watoto na watu wenye ulbino na mjadala juu ya namna ya kudhibiti ukatili dhidi ya watoto na watu wenye ualbino.

Aidha amesema kuwa matarajio baada ya kongamano hilo ni watoto na watu wenye ualbino kujua namna ya kutambua viashiria vya ukatili na namna ya kupambana navyo na jamii kujua wajibu wao katika kutunza watoto na watu wenye ualbino.

Mwisho.


VIONGOZI WA DINI WAHAMASISHA WANAWAKE KUSHIRIKI CHAGUZI NA KUJIINUA KIUCHUMI





VIONGOZI wa Dini Halmashauri ya Mji Kibaha wamekuja na mkakati wa kuhamasisha ushiriki wanawake na wasichana katika uongozi na haki za kiuchumi.  

Aidha wametakiwa kuwania nafasi za uongozi kwani nao wanauwezo wa kuwa viongozi na haki yao washiriki ili walete maendeleo ndani ya jamii na nchi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mchungaji James Machage  wa Kanisa la Sabato Visiga wakati wa mafunzo ya Ushiriki wa wanawake na Wasichana katika Uongozi na Haki za Kiuchumi kwa Viongozi wa Dini yaliyofadhiliwa na UN WOMEN.

Mchungaji Machage amesema kuwa licha ya changamoto kubwa ya mila na baadhi ya imani lakini wataendelea kutoa elimu ya ushiriki kwenye uchaguzi na fursa za kiuchumi kwani wanauwezo wa kuwa viongozi.

Amesema kuwa watahakikisha wanasaidia wanawake ili waweze kupata haki zao na kuwatia moyo ili wajue fursa zilizopo kwani uongozi wa nchi unajali wanawake kwa kuwapatia fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo kupitia vikundi.

Naye Julieth Faustine katibu wa Kanisa la Katoliki Pangani amesema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kujua masuala ya uwiano kila linalofanyika lizingatie haki kwa wote na utendaji wa kazi bila ya kubagua kuwa baadhi ya kazi ni za wanawake na wanaume.

Faustine amesema kuwa kuna baadhi ya mila zinamkandamiza mwanamke ikiwa ni pamoja na ukeketaji kwa watoto wa kike, kunyimwa elimu, kunyimwa urithi wa ardhi na kutothaminiwa jambo ambalo atalipigia kelele ili jamii iachane na mila hizo.

Kwa upande wake Abdala Ngulengule amesema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea chachu ya kwenda kuwahamasisha wanawake kushiriki kwenye fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mweishoni mwa mwaka huu.

Ngulengule amesema kuwa mfano kwenye Kata ya Pangani kuna mitaa nane lakini yote ilikuwa ikiongozwa na wanaume hivyo wanatarajia kuwa na mabadiliko makubwa kwenye uchaguzi huo kwani wanawake wengi wamehamasika kushiriki uchaguzi huo ili wapatikaneviongozi wanawake angalau wawili au watatu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Kibaha Leah Lwanji amesema kuwa  wanaendelea kuwahamasisha wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili waweze kuingia kwenye vyombo vya maamuzi na kuwa na usawa katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ili waweze kujiinua kiuchumi na kupata fursa zilizopo ndani ya jamii.

Lwanji amesema kuwa Halamshauri inachokifanya ni kuwandaa wanawake kuwa na miradi mbalimbali ya kiuchumi kwa kuanzisha vikundi na kuwaunganisha katika taasisi za kifedha ambazo hutoa fursa za mikopo, mitaji, mafunzo  na masoko.

“Wanawake wengi wanakuwa na unyonge hivyo kushindwa kujiamini hivyo kupitia mradi huu tunawajengea uwezo kwani wakiwa na uwezo wa kiuchumi watakuwa na uwezo wa kujiamini na kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwania nafasi za uongozi ndani ya jamii,”amesema Lwanji.

Naye mratibu wa mradi wa (WLER) Maria Nkangali amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uelewa viongozi hao wa dini ili wakatoe elimu juu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi kuleta maendeleo kwa wananchi.

Nkangali amesema kuwa wanatoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali ili yatambue mchango wa wanawake na wasichana kwenye suala la maendeleo bila ya kujali jinsi. 

Mafunzo hayo siku moja yamewahusisha Viongozi wa Dini kwenye Kata mbalimbali na wataalamu wa idara mbalimbali za Halmashauri hiyo.