Tuesday, August 29, 2023

PWANI YASHEREHEKEA USHINDI WA KWANZA NCHINI MKATABA WA LISHE

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mh. Angela Kairuki, akikabidhi Ngao ya Ushindi wa Kwanza kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mh. Abubakar Kunenge (katikati pichani) leo Agosti 29, 2023 kwa Mkoa wa Pwani kuibuka mshindi katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2022/23. Mwingine ni Katibu Tawala Mkoa huo na Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchata.

*Mkoa wa Pwani waongoza utekelezaji Mkataba wa Lishe kitaifa*

Mkoa wa Pwani umeongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kwa tathmini ya Saba (7) ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa Mwaka 2022/2023.

Taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa - (OR - TAMISEMI) zimeeleza kuwa Mkoa huo umefuatiwa na Lindi katika nafasi ya pili huku nafasi ya tatu ikienda kwa mkoa wa Iringa.

Kwa upande wa nafasi za Halmashauri, Mkoa wa Pwani umefanikiwa kuingiza halmashauri za Kibaha TC na Kibaha DC katika nafasi kumi za mwanzo.

Kibaha TC imekuwa ya na Kibaha DC ikiwa ni ya 10 huku hamashauri zingine za mkoa huo zikiwa zimeshika nafasi juu ya 100 za mwanzo.

Halamshauri hizo na nafasi zao kitaifa kwenye mabano ni Kisarawe (17), Rufiji (25), Bagamoyo (26) na Kibiti (54).

Zingine ni Chalinze (59), Mafia (91) na Mkuranga (93).

HIFADHI YA TAIFA KITULO KUTANGAZWA KITAIFA NA KIMATAIFA ILI KUVUTIA WATALII NA WAWEKEZAJI

 

Serikali imeendelea kujizatiti kwa  kuitangaza  Hifadhi ya Taifa ya Kitulo  ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kuwavutia watalii na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali Duniani kupitia maonesho, matamasha na kwa  njia ya kidijitali.

Kauli hiyo imesemwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.

Amefafanua kuwa hifadhi hiyo imekuwa ikitangazwa katika matamasha mbalimbali ya Karibu Kusini, Kilifair na Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba na Nanenane na kwa njia ya kidigitali, mitandao ya kijamii, majarida na Safari Channel.

Kufuatia hatua hiyo Serikali imeanza kuboresha  miundombinu ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo kufanya ujenzi wa nyumba tatu za malazi ya watalii na pia inatarajia  na kujenga nyumba mbili  na kambi moja  ya kuweka hema katika mwaka huu wa fedha 2023/2024, pamoja na  kukarabati miundombinu ya barabara.

Kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka kati ya hifadhi hiyo na wananchi, Mhe. Masanja amesema tathmini ilishafanyika na kulielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuweka vigingi katika maeneo ambayo yameshaainishwa.

Saturday, August 26, 2023

WANANCHI TUMIENI VITUO VYA MSAADA WA SHERIA KUSULUHISHA KESI ZA MADAI KUPITIA VITUO VYA MSAADA WA SHERIA-KPC

WANANCHI Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wametakiwa kutumia vituo vya msaada wa sheria kusuluhisha kesi za madai nje ya mahakama ili kuokoa muda na kuipunguzia mahakama mzigo wa mashauri.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Mlenga alisema kuwa baada ya bunge kufanya marekebisho sheria inaruhusu wadai kukubaliana nje ya mahakama kwa maridhiano ya pande mbili na kumaliza shauri kisha kufutwa na mahakama.

"Tunawashauri wananchi watumie vituo hivi ili kutatua mashauri ya madai nje ya mahakama endapo watakubaliana na makubaliano hayo yatasajiliwa na mahakama na kuimaliza kesi hiyo,"alisema Mlenga.

Alisema kuwa faida ya kumaliza mashauri ya madai nje ya mahakama ni kuokoa muda na hakutakuwa na uadui baina ya pande hizo mbili tofauti na kuendesha kesi mahakamani.

"Njia hii ya usuluhishi na upatanishi ni nzuri kwani ni rafiki na haina uhasama ambapo kesi inapofanywa mahakamani kunakuwa na uhasama sana hivyo wananchi watumie fursa hii,"alisema Mlenga.

Aidha aliwataka wananchi kutumia zaidi maridhiano katika changamoto za mashauri ya madai ambapo itaipunguzia mahakama mlundikano wa kesi hivyo kutotumia muda mrefu.

Kwa upande wake meneja wa KPC Dismas Chihwalo alisema kuwa kituo chao kinatoa huduma bure kwa watu wenye mashauri mbalimbali ya kisheria.

Chihwalo alisema kuwa wameweza kutatua changamoto nyingi za kisheria na kufanikisha wananchi kupata haki zao kwa njia usuluhishi kwenye mashauri mbalimbali.


TUME YA TAIFA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA YAFADHILI MRADI UTAFITI CHANGAMOTO YA SOMO LA HISABATI

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imesema kuonekana na kuwepo kwa changamoto ya matokeo mabaya ya somo la hisabati katika matokeo ya Darasa la saba na kidato cha nne tume hiyo imefadhili mradi wa utafiti ili kugundua sababu ya tatizo hilo.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo ,Agosti 25,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Dkt.Amos Nungu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli na mafanikio ya tume hiyo.

Vilevile Dkt.Nungu ametaja baadhi ya shughuli zilizotekelezwa na Tume hiyo kuwa ni pamoja na kuibua na kufadhili miradi ya kimkakati ambayo tayari michakato yake imefanyika na sasa ipo katika hatua ya mikataba ambapo Serikali kupitia COSTECH imeidhinisha jumla ya miradi saba kwa thamani ya shilingi milioni 150 kila mradi.

Amesema Miradi hiyo itafanyika ndani ya miaka miwili na inahusisha watafiti na wabunifu kutoka sekta zote za umma na binafsi.

Aidha amesema kuwa Serikali kupitia COSTECH, imeidhinisha miradi miwili kwa thamani ya shilingi milioni 120 kila mradi ambapo utekelezaji wake pia unahusisha watafiti kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini na itafanyika ndani ya miaka miwili, sasa ipo hatua ya kusaini mikataba.

Akizungumzia majukumu na vipaumbele vya tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, Dkt.Nungu amesema kuwa Tume hiyo imeendelea kusimamia miradi inayoendelea ukiwemo wa Kigoda cha Utafiti katika SUA na NM-AIST ambao ni mradi wa miaka mitano, wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 5 pamoja na kushirikiana na Mabaraza ya Kikanda na Kimataifa kuhakikisha tunashiriki kutafuta fursa ambazo zitaendelea kuleta fedha za utafiti kupitia COSTECH au kuhamasisha Taasisi za ndani kuomba hizo fursa.

Kukamilisha zoezi la ufadhili wa pamoja miradi ya utafiti wa Mabaraza ya Utafiti duniani ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza kuonekana kwa watafiti wetu na kuitangaza nchi yetu katika nyanja hii ya utafiti pamoja na kukamilisha mchakato na kutoa fedha kwa maandiko mawili kwa kutoa mrejesho kwa walioshiriki lakini wakakosa, na kuwatembelea walioshinda.

Vilevile, kupitia mradi wa HEET, tunaboresha mifumo mbalimbali ili kuongeza ufanisi zaidi katika suala la uratibu wa ume. Ikumbukwe kuwa mradi huu ni mahususi kwa Taasisi za Elimu ya Juu hivyo, inabidi tuwe tayari kuwahudumia baada ya kukamilisha mabadiliko wanayofanya kupitia mradi huo.

MAOFISA MANUNUZI WATAKIWA KUZINGATIA UKOMO MATUMIZI YA KEMIKALI

Serikali imewataka maafisa ununuzi na ugavi kuzingatia ukomo wa matumizi ya kemikali na vifaa vyenye kemikali ambazo zinamong’onyoa tabaka la ozoni au kuwa na athari kwa afya ya binadamu na mazingira.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Agosti 25, 2023 Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa Maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Dkt. Mkama amesema mwanzoni mwa miaka ya 1970, wanasayansi walibaini baadhi ya kemikali zinazotengenezwa na binadamu ikiwemo majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto na utengenezaji wa magodoro vimejipenyeza angani na kumong'onyoa tabaka la hewa ya Ozoni na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Matokeo ya kumong’onyoka kwa Tabaka la Ozoni ni kuruhusu mionzi zaidi ya urujuani kufikia uso wa dunia ambayo husababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu na mazingira. Madhara hayo ni kama vile saratani ya ngozi, uharibifu wa macho unaosababisha upofu na athari kwa kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine” amesema Dkt. Mkama

Aidha Dkt. Mkama amesema matokeo ya uvumbuzi huo yalisababisha Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Mazingira (UN Environment) kufanya tathmini ya kisayansi na kuamua kuchukua hatua madhubuti kulinda tabaka la Ozoni kwa kuanzisha Itifaki ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni iliyopitishwa mwaka 1987.

Akifafanua zaidi Dkt. Mkama amesema katika kutekeleza Itifaki hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kuondosha Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni Jamii ya Hydrochlorofluorocarbons (HCFCs) ifikapo mwaka 2030 pamoja na Mpango wa utekelezaji wa Marekebisho ya Kigali ya kupunguza matumizi ya kemikali jamii ya hidrofluorokaboni.

“Chini ya Mipango hii mojawapo ya shughuli zinazotelekezwa na zinazopaswa kutekelezwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kutoka katika Taasisi mbalimbali kukusu utekelezaji wa Itifaki husika ikiwemo utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni) za mwaka 2022” amesema Dkt. Mkama.

Dkt. Mkama amesema maafisa ununuzi na ugavi ni wahusika wakuu katika mchakato wa wa kushugulikia manunuzi ya vifaa mbalimbali katika ofisi za umma, hivyo wana wajibu mkubwa wa kutoa elimu ya Ozoni kwa wengine ili kuongeza juhudi za kuhifadhi Tabaka la Ozoni na kuokoa Maisha ya binadamu na viumbe hai.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa amesema katika kutekeleza Itifaki hiyo, Ofisi hiyo imeendelea kutoa mafunzo wa wadau mbalimbali wakiwemo maafisa ununuzi na ugavi kutoka katika Wizara mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu matakwa ya Itifaki ya Montreal.

“Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango Tanzania na Vyuo mbalimbali vya Mafunzo ya Ufundi tumeendelea kutoa mafunzo kwa maafisa mbalimbali kuhusu usimamizi na udhibiti wa kemikali na vifaa vyenye kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki hii” amesema Kemilembe.

Friday, August 25, 2023

𝗖𝗕𝗪𝗦𝗢𝘀 𝗦𝗔𝗦𝗔 𝗞𝗨𝗧𝗨𝗠𝗜𝗔 𝗠𝗙𝗨𝗠𝗢 𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗝𝗜𝗜𝗦

Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) vinavyosimamiwa na Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), vimetakiwa kutumia Mfumo wa pamoja wa Ankara za Maji (MAJIIS), ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kisare Makori, wakati akifunga mafunzo ya siku saba kwa Maafisa wa CBWSOs wa mkoa wa Kilimanjaro yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha USHIRIKA mjini Moshi .

Alisema, Serikali imedhamiria kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma ili  kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu mahali walipo.

“Serikali ya awamu ya sita inachukua jitihada mbalimbali katika kuhakikisha TEHAMA inarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, ambapo kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, imetengeneza mfumo wa MAJIIS ili kutatua changamoto mbalimbali zilizokua zinaikabili Sekta ya Maji”, alisema.

Alifafanua kuwa, Serikali imewekeza katika mfumo huo hivyo ni jukumu la watumishi wa sekta ya Maji kufanya kazi ili kuhakikisha mfumo huo unakua mkombozi kwa wananchi.

Kwa upande wake mtaalamu wa TEHAMA kutoka Wizara ya Maji Mha. Masoud Almas alisema, mfumo wa MAJIIS umeboreshwa ili uweze kutumiwa na Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) vinavyotoa huduma vijijini ili kuhakikisha TEHAMA inarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi mahali walipo.

“Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ni mkoa wa kwanza kuanza kutumia mfumo huu wa MAJIIS kwa CBSWOs na Wizara itaendelea kuhakikisha CBSWOs zote katika mikoa mingine zinatumia mfumo huu ili kurahisisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi waishio vijijini” alisema.

Aliongeza kuwa, hadi sasa mfumo huo umeleta mafanikio makubwa kwa Wizara ya Maji ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato na kurahisiha upatikanaji wa taarifa za Mamlaka zote za Maji nchini.

“Hadi sasa, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingiara za miji mikuu ya mikoa, miradi ya kitaifa, miji ya Wilaya na miji Midogo 87 Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Bodi za Maji za Mabonde 9 zinatumia Mfumo huu wa Pamoja”, alifafanua Almas.

Aidha, alibainisha kuwa ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, mfumo wa MAJIIS umeunganishwa na mifumo mingine ya Serikali ikiwa ni pamoja na mfumo wa GePG, Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS), Mfumo wa Ujumbe Mfupi wa Simu za mkononi ambao hutumika kutoa taarifa za huduma kwa Wateja ikiwemo kutuma bili, mfumo wa NIDA na mfumo wa BRELA.

Jumla ya washiriki 72 kutoka Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) 39 vya mkoa wa Kilimanjaro walihudhuria mafunzo hayo.