Thursday, August 3, 2017

KIJANA AIGIZA SAUTI YA KIKE AVAA DERA NA HIJABU BODABODA AINGIA MKENGE


Na John Gagarini, Kibaha

KIJANA mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka (19) mkazi wa Mbagala Maji Matitu amejikuta yuko kwenye wakati mgumu baada ya kukutwa akiwa amevaa nguo za kike aina ya dera na kusababisha taharuki kwa wakazi wa Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa wa Picha ya Ndege Joseph Zambo alisema kuwa kijana huyo alikuwa akiwasiliana na mtu akijifanya kuwa yeye ni mwanamke.

Zambo alisema kuwa kijana huyo alifika kwenye mtaa wake Agosti 2 majira ya sa 4:30 asubuhi akimfuata mtu waliokuwa wakiwasiliana naye kwa njia ya simu ambaye inadaiwa kuwa ni dereva bodaboda.

“Watu hawa walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na kijana huyo alikuwa akiigiza sauti ya kike na dereva bodaboda alijua fika kuwa aliyekuwa anawasiliana naye ni mwanamke,” alisema Zambo.

Alisema kuwa dereva bodaboda huyo alimwona kijana huyo kupitia ukurasa wake wa facebook ambapo ulipambwa na picha za msichana hali ambayo ilimfanya avutiwe naye.

“Mawasiliano yalianza kama siku tatu zilizopita na walikubaliana na ndipo bodaboda huyo alimwambia njoo Picha ya Ndege Kibaha lakini kijana huyo alipitiliza hadi Kongowe na ilibidi arudi ashukie Picha ya Ndege na alimwelekeza akishuka apande bodaboda ili aende kwake eneo la Sofu,” alisema Zambo.

Aidha alisema kuwa aliposhuka waendesha pikipiki walikuwa wakimfuatilia na wlimwona amevaa dira na usoni kajifunga kitambaa ambacho kiliacha wazi macho tu kama vile ninja akapandishwa kwenye pikipiki na kuanza safari ya kwenda kwa mtu wake.

“Wakiwa njiani upepo ulipuliza na dereva wa bodaboda akashangaa kuona miguu ya kiume lakini amevaa viatu vya kike akashtuka na kugeuza pikipiki kule alikotoka na ndipo madereva bodaboda walipojaa na kuanza kumzonga hali iliyowabidi wamlete ofisini kwangu na ilikuwa tafrani kubwa huku wengine wakitaka kumpiga wakidai ni mwizi wa pikipiki,” alisema Zambo.

Alibainisha kuwa baada ya kumfikisha walimfunua na kukuta kuwa ni mwanaume na kuanza kumhoji ndipo aliposema kuwa alikuja Kibaha kuja kuchukua hela na haikujulikana alikuja kuzichukua hizo fedha kwa njia gani.

“Zogo lilizidi pale huku bodaboda wakitaka kumpiga ndipo ikabidi tuchukue gari na kumpeleka polisi kwa ajili ya usalama wake na kueleza ni kwa sababu gani alijifanya mwanamke na fedha hizo anazichukua kwa njia gani,” alisema Zambo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa atalitolea taarifa tukio hilo baada ya kutoka kwenye msafara wa kiongozi.


Mwisho.   

Thursday, July 27, 2017

AKIMAMA WAFANYABIASHARA WALALAMIKA KUNYANYASWA


                                    Na John Gagarini, Kibaha

MTAA wa Maili Moja umesema utawafuatialia na kuwachukulia hatua mgambo ambao waliwadhalilisha akina mama wafanyabiashara ndogo ndogo kwa kuwadai rushwa ya ngono kwa madai kufanyabiashara kwenye eneo ambalo haliruhusiwi.

Akizungumza kwenye mkutano wa mtaa mwenyekiti wa Mtaa wa maili Moja Athuma Mkongota alisema kuwa baadhi ya akinamama walilalamika ofisini kwake kuwa walitakiwa watoe penzi ili wasitozwe faini kwa kudaiwa kufanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Mkongota alisema kuwa jambo la kushangaza akinamama hao waliokuwa wakifanyabiashara nje ya eneo la Hifadhi ya Barabara ambapo waliondolewa kufuatia kubomolewa soko la zamani la Maili Moja.

“Hawa mgambo walifanya makosa kuwanyanyasa akinamama hawa hata kama walikuwa na makosa taratibu za wanaokiuka sheria sizipo kwanini wadai mapenzi pia walikuwa hawafanyibiashara kwenye eneo lililokatazwa hivyo tutawatafuta na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua,” alisema Mkongota.

Mkongota alisema kuwa baada ya wakinamama hao kuondolewa eneo lililokatazwa la hifadhi ya barabara ambalo liko jirani na stendi walienda kwenye barabara za mitaa na kuendelea kufanyabiashara lakini mgambo hao waliwafuata na kuwakamata huku wakimwaga vyakula na matunda waliyokuwa wakiyauza.

“Baadhi ya akinamama walifika ofisini na kudai kuwa baadhia ya mgambo walikuwa wakiwataka kimapenzi ili wasiwapige faini wakidai kuwa wanachafua mazingira jambo hili halikubaliki kwani tutawatafuta na wakibainika watepelekwa sehemu husika kwnai kuna baadhi wanajifanya mabwana afya,” alisema Mkongota.

Kwa upande wake Mwanahamisi Shomary ambaye ni muuzaji wa samaki alisema kuwa tangu waondolewe kwenye eneo la stendi na kuhamia kwenye barabara za mitaa wamekuwa wakisumbuliwa na mgambo hao.

Shomary alisema kuwa mgambo hao wamekuwa kero kubwa kwani wanatunyanyasa sana huku wakichukua bidhaa zetu na kuziharibu ambapo inabidi tujitafutie ili tuweze kurejesha mikopo tuliyokopa.


Mwisho.   

WAASWA KUTUMIA VITUO VYA MAFUNZO

                                      Na John Gagarini, Kibaha

WALIMU wakuu wa shule za msingi, sekondari na vyuo nchini wameshauriwa kuwapeleka wanafunzi wao kwenye vituo vya mafunzo badala ya kuwapeleka kwenye sehemu za starehe.

Ushauri huo umetolewa na makamu mwenyekiti wa wataalamu wasaidizi wa mifugo nchini Tavepa Ephrahim Masawe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Masawe ambaye pia ni mkurugenzi wa shamba darasa Kibaha akizungumzia juu ya kilimo cha kisasa alisema kuwa ziara za safari ni vema zikawa za kujifunza kuliko kujifurahisha.

“Kwenye mafunzo hujifunza mambo mengi kuliko kwenda kwenye sehemu ambazao hazina faida kwani ujuzi unaweza kumsaidia mtu kuliko kufanya vitu visivyo na faida,” alisema Masawe.

Naye moja ya wanafunzi kwenye shamba darasa mkazi wa Mbweni Jijini Dar es Salaam Hilda Ngowi akiezea kilicho msukuma kwenda hapo kujifunza ni kutaka kupata ujuzi wa ufugaji wa kuku.

Ngowi alisema ushauri juu ya shule na vyuo kuwapeleka wanafunzi kwenye sehemu za mafunzo kama hayo alisema kuwa sehemu za mafunzo ni muhimu kwa vijana.

Mwisho.

DEREVA AFA AJALINI

                                 Na John Gagarini, Kibaha

DEREVA wa gari la mizigo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja amekufa baada ya gari alilokuwa akiliendesha kugongwa na gari lingine kwenye ajali iliyosababisha magari matatu kugongana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Kibaha kwa vyombo vya habari na kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana ilisema kuwa katika tukio hilo mtu mmoja alijeruhiwa.

Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 20 majira ya saa 4:20 usiku barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro eneo la Picha ya Ndege wilayani Kibaha.

Shana alisema kuwa gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 774 BBU likiendeshwa na dereva asiyefahamika liligonga gari lililokuwa likiendeshwa na dereva asiyefahamika lenye namba za usajili T 678 BRD lenye tela namba T 293 BVA na Scania T 188 AVN likiendeshwa na Hashimu Mhina (36) wa Dar es Salaam.

“Chanzo cha ajali hii ni dereva wa gari la kwanza kuyapita magari mengine bila ya kuchukua tahadhari ambapo alikimbia mara baada ya ajali hiyo na tunamtafuta tumempa siku tatu ajitokeze na asipojitokeza tutamtafuta ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema Shana

Mwisho

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia wahamiaji 44 kutoka nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa wahamiaji hao haramu walikamatiwa wilayani Bagamoyo.

Kamanda Shana alisema kuwa wahamiaji hao haramu walikamatwa eneo la Razaba kata ya Makurunge Tarafa ya Mwambao wilayani humo wakiwa wametelekezwa kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Alisema kuwa  kufuati tukio hilo jeshi lake linaendelea na uchunguzi kujua watu waliohusika na tukio la kuwasafirisha wahamiaji hao haramu kisha kuwatelekeza.

“Tunafuatilia kujua vitu vingi ikiwa ni pamoja na wanaowafadhili wahamiaji hao haramu kwani kumekuwa na baadhi ya watu wanaowasafirisha wahamiaji hao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” alisema Shana.


Mwisho

SAMATTA ASAIDIA JEZI CHAMA CHA SOKA KIBITI


                                     Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA Cha Soka wilaya ya Kibiti (KFA) mkoa wa Pwani kimemshukuru mwanasoka anayecheza soka la kulipwa kwenye timu ya KRC Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta kwa kuwapatia jozi za jezi kwa ajili ya washindi wa ligi daraja la nne.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katibu wa chama hicho Rashid Mkinga alisema kuwa wanashukuru msaada huo utakaozisaidia timu zitakazoshinda na kuwakilisha wilaya hiyo kwenye mashindano ya mkoa.

Mkinga alisema kuwa waliandika barua kwa Samata kwa ajili ya kuomba vifaa mbalimbali vya michezo ambapo aliwajibu na kusema kuwa atawapatia.

“Samatta kwa kupitia mwakilishi wake Said Ngulupi alitupatia jozi ya seti tatu ambazo tutawakabidhi washindi watatu wa juu ambao ni wawakilishi wa wilaya yetu,” alisema Mkinga.

Alisema kuwa hawana cha kusema zaidi ya kushukuru kwa msaada huo mkubwa aliowapatia licha ya yeye kuwa mbali lakini anathamini vijana wenzake ambao wanacheza soka hapa nchini.

“Tunamshukuru Samatta kwa mchango wake kwani awali tulikuwa hatuna zawadi za kuwapa washindi zaidi ya kombe kwa ajili ya mshindi wa kwanza kwani ametukomboa kwa kutupa msaada huo,” alisema Mkinga.

Aidha alisema kuwa mpira unachezwa kama kawaida na kuna amani kubwa siyo kama watu wanavyofikiria kwani ulinzi uko wa kutosha na hadi sasa hakuna tukio lolote la kutishia lililotokea.

“Kupitia michezo amani imetawala na hakuna vurugu zozote au tishio lolote la kutishia amani hivyo watu wasiwe na wasiwasi kwenye wilaya yetu ambayo ilikumbwa na mauaji na kuwafanya watu kuwa na hofu,” alisema Mkinga.

Alibainisha kuwa ligi ya Kibiti ndiyo yenye timu nyingi ndani ya mkoa wa Pwani ambapo kwenye ligi daraja la nne jumla ya timu 19 zinachuana na timu zilizosajiliwa ni 31 na bado kuna zingine zinahitaji usajili.


Mwisho.  

MJI KIBAHA KUJENGA STENDI YA KISASA KWA MABILIONI

Na John Gagarini, Kibaha

HATIMAYE Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani imeanza mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa wenye thamani ya shilingi billion 3.4.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa habari wa Halmashauri hiyo Innocent Byarugaba amesema kuwa stendi hiyo itaondoa tatizo la mji huo kutokuwa na stendi ya uhakika kwa kipindi cha takribani miaka 40.

Byarugaba alisema kuwa stendi ambayo inatumika kwa sasa ni ndogo na imejengwa kwenye hifadhi ya barabara na ambapo iko ndani ya mita 60 ikitakiwa kuondolewa na ina hudumia mabasi ya mikoa 24.

“Stendi mpya mara itakapokamilika inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 60 kwa wakati mmoja na itajengwa kipindi cha miezi sita na kukamilika mwishoni mwa mwaka huu au Januari mwakani,” alisema Byarugaba.

Alisema kuwa fedha zinazotumika kwenye ujenzi huo ni ufadhili kutoka benki ya dunia kupitia benki kuu ya Tanzania kwenye mradi wa uendelezaji wa Miji (ULGSP) unaoendeshwa kwenye miji 18 hapa nchini.

“Stendi itakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kituo cha polisi, ofisi za mabasi, sehemu ya texi, Bajaji, pikipiki, huduma ya vyoo, vibanda vya kupumzikia abiria, Atm, kituo cha mafuta,gereji, hoteli na kizimba cha kuhifadhia takataka na huduma nyingine muhimu,” alisema Byarugaba.

Aliwataka watu wenye viwanja vinavyozunguka stendi hiyo kujenga ambapo ramani iliyopitishwa ni kuanzia ghorofa moja na kuendelea pamoja na wale walioko kwenye eneo la kitovu cha mji kufanya ujenzi kama sheria zinavyowataka.

Aidha alisema kuwa ujenzi huo unafanywa na kampuni ya Group Six International Ltd ambayo ilijenga stendi ya kisasa ya Msamvu mkoani Morogoro chini ya wataalamu washauri Ace Consult, Lupta Consult na Mhandisi.


Mwisho.

WATAKIWA KUEPUKA NYAMA ZA MITAANI

Na John Gagarini, Kibaha

WANANCHI wa kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuacha kununua nyama zinazouzwa mitaani kwa bei nafuu kwani ni hatari kwa maisha yao.

Hayo yalisemwa na diwani wa kata hiyo Robert Machumbe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kuenea kwa taarifa kuwa kuna watu wanauza nyama mitaani zikiwa zimewekwa kwenye ndoo.

Machumbe alisema kuwa watu hao wamekuwa wakichukua ngombe ambao wamekufa maeneo mbalimbali kisha kuwauzia wanachi nyama hiyo kwa baei nafuu ya shilingi 2,000.

“Wananchi nawaomba mjihadhari na nyama hizi zinazouzwa mitaani ni hatari kwa afya zenu kwani hamjui nyama hizo zinatoka wapi kwani hazijapimwa na daktari hali ambayo ni hatari,” alisema Machumbe.

Alisema kuwa wananchi wasipende kununua nyama hizo bali wanunue sehemu maalumu ambako ni kwenye mabucha ya kuuzia nyama ili wale nyama ambayo imepimwa na ni salama kwa afya zao.

Kwa upande wake ofisa mifugo wa kata ya Picha ya Ndege Mlaki alisema kuwa alipata taarifa wiki iliyopita kuwa kuna ngombe walikufa kwa moja ya wafugaji wa Lulanzi na watu hao waliichukua nyama hiyo na kuiuza mtaani.

Mlaki alisema kuwa kuna athari ningi zinazotokana na watu kula nyama ambazo hazijapimwa kwani wanaweza kuambukizwa magonjwa mbalimbali kama vile tb, tumbo, kuharisha na magonjwa mengine.   

Mwisho.