Na John
Gagarini, Kibaha
SERIKALI
imeombwa kuwalipa walimu wanaofundisha vituo vya shule huria ambazo ziko chini
ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ili kuwapa motisha walimu hao.
Hayo
yalisemwa na meneja wa shule ya Pangani Remedial Open School iliyopo wilayani
Kibaha Ally Mohamed na kusema kuwa kuwalipa walimu hao itakuwa moja ya motisha
kuwafanya wafundishe kwa moyo.
Mohamed
alisema kuwa shule hizo zimekuwa mkombozi kwa wanafunzi ambao wamekosa nafasi
za kwenda shule za sekondari na watu wazima waliokosa nafasi hiyo.
“Shule hizi
ambazo zamani zilikuwa ni kwa ajili ya watu wazima kwa sasa zimeboreshwa na
zinatoa elimu ya sekondari kama kawaida na wanapofaulu mitihani ya kidato cha
nne wanakwenda kidtao cha tano kama wale walio kwenye mfumo rasmi hivyo kuna
haja ya walimu wake kulipwa kama walimu wenzao wa shule za serikali,” alisema
Mohamed.
Alisema kuwa
walimu hao kwa sasa wanalipwa na shule hizo lakini kwa kiasi kikubwa wamekuwa
wakijitolea kwani uwezo wa kuwalipa mishahara hawana ambapo Taasisi hiyo
imekuwa ikisimamia mitihani ya Kujipima huku ile ya kidato cha pili na ile ya
kidato cha nne ikisimamiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE).
“Shule hizi
kwa sasa zimekuwa mkombozi kwa wanafunzi hao ambao zamani walikuwa hawana pa
kwenda hivyo tunaomba serikali kuliangalia suala la kuwalipa walimu hao ili
kuwapa hamasa ya kufundisha ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hizo,”
alisema Mohamed.
Alisema kuwa
mfumo huo uliboreshwa mwaka 2014 ambapo ulisajili vituo hivyo ambavyo
vinachukua wanafunzi ambao walishindwa kuendelea na masomo kama vile ukosefu wa
ada, mimba, mazingira magumu, yatima na watu wazima waweze kujiendeleza.
Aidha alisema
kuwa kwa sasa zinachukua wanafunzi wenye umri kati ya miaka 12 hadi 24 ambao
wanasoma kwa miaka minne huku wale wenye kuanzia miaka 25 husoma kwa miaka
miwili,shule hiyo ilianza mwaka 1997 na ina wanafunzi 100.
Mwisho.