Thursday, August 11, 2016

MAJAMBAZI YAMUUA KWA KUMPIGA RISASI MWANAMKE ALIKWENDA DUKANI KUWEKA MUDA WA HEWANII

Na John Gagarini, Kibaha

MKAZI wa Mtaa wa Karabaka-Misugusugu kata ya Misugusugu wilayani Kibaha mkoani Pwani Zawadi Halfan (25) ameuwawa kwa kupigwa risasi na majambazi wakati akisubiri kuunganishiwa kifurushi cha muda wa maongezi kwenye simu yake.

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa marehemu alikuwa amekaa kwenye benchi kwenye kibanda cha huduma za fedha kwa mtandao mali ya Gaitano Joseph (30).

Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 9 majira ya saa 2:30 usiku kwenye mtaa huo ambapo marehemu alikuwa akisubiri huduma hiyo kabla ya mauti kumkuta.

“Marehemu hakuwa mlengwa bali walikuwa wamemlenga Yohana Koseja (24) ambaye ni mfanyakazi wa Mchungaji Raphael John ambaye ni mmiliki wa duka la M-Pesa ambapo majambazi hao baada ya kufika walimwamuru Yohana asimame baada ya kufunga duka hilo lakini alikimbia na kukaidi agizo la majambazi hayo ambayo yalikuwa matatu,” alisema Mushongi.

“Kutokana na Yohana kukimbia majambazi hayo yalianza kufyatua risasi ndipo moja ilimpata marehemu sehemu ya mgongoni upande wa mgongoni na kufariki papo hapo ambapo  walikuwa wakifyatua risasi hizo kwa Yohana wakimhisi kuwa alikimbia na fedha bada ya kufunga duka,” alisema Mushongi.

Alisema baada ya majambazi hao kutoka kwenye tukio la kwanza walivamia duka lingine la M-Pesa lililopo pamoja na duka la madawa ya binadamu linalomilikiwa na Renovatus Katabalo (29) mfanyabiashara na mkazi wa Kongowe ambapo duka lake lipo eneo hilohilo la Karabaka na kupora kiasi cha shilingi 300,000.

“Chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali na msako unaendelea mkoa mzima ili kuwakamata watuhumiwa ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili za mauaji ambapo eneo la tukio maganda ya risasi aina ya SMG/SAR,” alisema Mushongi.  

Mwisho.


Monday, August 8, 2016

MWILI WAKUTWA VICHAKANI UKIWA UMEPIGWA RISASI KIDEVUNI


Na John Gagarini, Kibaha

MWILI wa mtu mmoja ambaye jina lake ambalo halikuweza kufahamika mara moja mwenye umri kati ya miaka (33) na (38) umeokotwa huku ukiwa umepigwa risasi chini ya kidevu na kutokea utosini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa mtaa wa Lulanzi kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani Thobias Shilole alisema kuwa marehemu aliuwawa na watu wasiofahamika.

Shilole alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 7 majira ya saa 3 asubuhi kwenye korongo lililopo kwenye shamba linalomilikiwa na Saeed Yeslam Saeed ambapo watoto waliokuwa wakichunga mbuzi ndiyo waliogundua mwili huo na kutoa taarifa kwa wazazi wao ambao walitoa taarifa kwa balozi wao na ndiye aliyemjulisha juu ya tukio hilo.

“Mwili huo ulikuwa na jeraha la risasi chini ya kidevu na kufumua kichwa na mtu huyo anahusishwa na tukio lililofanyika siku kama tatu zilizopita kwa kumpiga risasi kwenye makalio na kumpora fedha mtu aliyetambulika kwa jina la Beno Nyoni (36) mkazi wa Picha ya Ndege ambaye alikuwa akijenga nyumba yake eneo la mtaa wa Lulanzi,” alisema Shilole.

Shilole alisema kuwa watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi baada ya kumshambulia walikimbia na kusababisha majeruhi huyo kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi lakini ilishindikana na kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi ambako hadi sasa anatibiwa baada ya kutolewa risasi iliyokuwa mwilini.

“Tunaiomba serikali kumlazimisha mmiliki kulifanyia usafi kwani pori kubwa ambalo limekuwa likitumiwa na wahalifu kwa ajili ya kujificha na kufanya wizi kisha kujificha huko kwani hata mwaka jana tulikuta mtu akiwa amejinyonga hivyo sehemu hiyo usalama wake ni mdogo hasa ikizingatiwa eneo hilo liko umbali wa kilometa 2 toka barabara kuu ya Morogoro,” alisema Shilole.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa baada ya kuangaliwa marehemu alikutwa na jeraha kidevuni na kichwani huku mwili wake ukianza kuharibika.

Msuhongi alisema kuwa pembeni yake kulikutwa kofia ya kuficha sura ganda la risasi aina ya SMG/SAR na nyaraka mbalimbali ambazo ni ramani za nyumba mbili, stakabadhi za kibali cha ujenzi, hati ya hukumu ya shauri la mgogoro wa ardhi.

Alisema vitu vingine vilivyokutwa ni kadi za biashara, kadi za benki za posta, NBC, Posta na CRDB, kadi ya kupigia kura na leseni ya udereva vyote vikiwa na majina ya Nyoni ambaye ni mfanyabiashara wa Picha ya Ndege.

“Vitu hivyo ni vya Majeruhi huyo aliyofanyiwa tukio hilo la unyanganyi wa kutumia silaha na kupora mali na walifika kwenye kwenye hilo kwa lengo la kugawana mali hizo lakini inaonyesha walihitilafiana ndipo walipompiga marehemu risasi na kumuua kisha walimpekekua kwani mifuko ya suruale yake ilkuwa iko nje na hakukutwa na kitambulisho chochote na mwili umehifadhiwa hospitali ya Tumbi,” alisema Mushongi.

Naye diwani wa kata hiyo Robert Machumbe alisema kuwa shamba hilo lilikofanyika tukio hilo lina pori kubwa sana hivyo ni vema Halmashauri likafanya utaratibu kama mmiliki kashindwa litolewe kwa mtaa ili kuweza kujengwa huduma za jamii kama shule, zahanati na huduma nyingine kwani kwa sasa limekuwa hatari kwa wananchi.

Mwisho.       


  



  




WATU ZAIDI 20 WANUSURIKA KUUNGUA MOTO

Na John Gagarini, Kibaha

FAMILIA nane zenye watu zaidi ya 20 kwenye mtaa wa Mharakani kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani zimenusurika kufa baada ya moto kutokea wakati wamelala.

Wakizungumza na mwandishi habari hizi wahanga wa tukio hilo la moto huo ambao ulitokea Agosti 7 usiku kuamkia Agosti 8 majira ya saa 6;30 usiku walisema kuwa watu waliokuwa jirani na nyumba yao ndiyo waliowafahamisha juu ya moto huo ambao unasadikiwa ulianzia kwenye moja ya maduka yaliyo kwenye nyumba hiyo.

Emanuel Mhina alisema kuwa wao walikuwa wamelala na ilipofika majira ya saa saba kasoro waliamshwa na watu na walipoamka walikutana na moto mkubwa ambao hawakujua ulianza saa ngapi ndipo walipoanza kujiokoa.

“Tunamshukuru mungu tumenusurika licha ya mali zetu zote kuteketea kwa moto ambao ulianzia kwenye moja ya maduka ambayo yameungana na nyumba hii ambayo tulikuwa tunaishi,” alisema Mhina.

Naye Said Juma alisema kuwa moto huo umewapa hasara kubwa kwani amepoteza vitu karibu vyote na kufanikiwa kuokoa vichache hali ambayo inamfanya aanze upya maisha.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Yahaya Abdala alisema kuwa wananchi, Zimamoto pamoja Jeshi la polisi walifanikisha kuzimwa moto huo ambao ulisababisha vitu vote kuteketea lakini hakuna mtu aliyedhuriwa na moto huo zaidi.

Naye diwani wa kata ya Picha ya Ndege Robert Machumbe alisema kuwa wahanga hao hawakuweza kuokoa kitu kwani vitu vyote viliteketea kwa moto huo uliokuwa mkali.

Machumbe alisema kuwa baada ya tukio hilo walichangisha kwa majirani na kupata kiasi cha shilingi 80,000 ambazo ziligawanywa kwa wahanaga hao angalau wapate fedha kwa ajili ya chakula na wahanga hao wamehamia kwa ndugu jamaa na marafiki zao wakiangalia namna ya kutafuta nyumba nyingine.

Katika hatua nyingine mtoto mwenye umri kati ya miaka minne na nusu amenusurika kufa baada ya mama yake kumwacha kwenye nyumba huku akiwa amemfungia ndani na yeye kwenda kusikojulikana ambapo kati ya majirani waliounguliwa nyumba ambaye ni mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alijitosa na kumwokoa mtoto huyo.

Mwisho.   

DC ASHANGAA WATU KUFANYA NGONO KWENYE MAKABURI

Na John Gagarini, Kibaha

MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Asumter Mshama amesikitrishwa na baadhi ya wakazi wa mtaa wa Mwanalugali kata ya Tumbi wanaoshiriki kwenye vitendo vya kishirikina kwa kufanya ngono kwenye makaburi ya Air Msae yaliyopo katika mtaa huo na kusema kuwa serikali haitatoa fedha kwa ajili ya kuweka uzio kwenye makaburi hayo ili kuzuia vitendo hivyo.

Makaburi hayo ambayo yalianzishwa na halmashauri ya Mji wa Kibaha baada ya basi la Air Msae kupata ajali kwenye barabara kuu ya Morogoro ambapo ili ua watu wengi na maiti nyingi zilizikwa hapo baada ya kukosa ndugu.

Akizungumza na wakazi wa mtaa huo alisema kuwa inasikitisha kuona watu wanafanya vitendo hivyo juu ya makaburi kwani hiyo ni laana kwa watu wanaojihusisha na vietendo hivyo na serikali haitapeleka fedha kwa ajili ya kuweka uzio badala yake fedha hizo ni afadhali zipelekwe kwenye shughuli za maendeleo.

Mshama alitoa kauli hiyo kufuatia uongozi wa kata hiyo ambapo mtendaji wa kata hiyo Msemakweli Karia akisoma risala alisema kuwa moja ya changamoto zilizopo kwenye kata ni baadhi ya watu kujihuisha na uovu huo nyakati za usiku juu ya makaburi hayo pamoja na vitendo vingine viouvu ikiwa ni pamoja na uvuitaji wa bangi hivyo kuomba kupewa fedha kwa ajili ya kuweka uzio kuzuia watu hao.

“Haiwezekani kuweka uzio kwani watu wanaofanya vitendo hivyo wanajitafutia laana kwani hawawezi kupata utajiri kwa kufanya vitendo hivyo kwenye makaburi hayo ya umma ambayo yanatumika kuzika watu kwenye mji wa Kibaha na hiyo ni laana kwani wanaofanya hivyo wanasema kuwa kwa kuwa ajali hiyo iliua watu wengi hivyo na wao watapata utajiri mkubwa jambo ambalo ni dhana ambayo haipaswi kupewa nafasi kwani uchawi unarudisha nyuma maendeleo na mji unaoendekeza imani hizo hauwezi kupiga hatua,” alisema Mshama.

Aidha alisema ili wananachi wa weze kujiletea maendeleo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na si kuwa na imani za kishirikina ili kupata maendeleo suala hilo halipaswi kupewa kipaumbele bali jitihada za kufanya kazi kwa bidii ndizo zitakazowafanya wawe na maisha mazuri.

Awali akisoma risala ya Kata ya Tumbi mtendaji wa kata hiyo Msemakweli Karia amesema kuwa changamoto nyingine zilizopo katika eneo hilo ni ubovu wa barabara.

Mwisho. 
 




  




Tuesday, July 26, 2016

WADAU WACHANGIA BWENI LA SEKONDARI YA CHALINZE ILIYOUNGUA

Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA kuungua bweni la shule ya sekondari ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kuungua kwa moto baadhi ya wadau wameanza kuichangia shule hiyo ili kusaidia wanafunzi ambao vifaa vyao vyote viliungua.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi diwani wa kata ya Bwiringu Lucas Lufunga alisema kuwa kutokana na tukio hilo waliitisha kikao cha kata kwa ajili ya kuangalia namna ya kuisaidia shule hiyo.
Lufunga alisema kuwa katika kikao hicho walifanikiwa kupata kiasi cha shilingi 449,000 na kunua vyakula kwa ajili ya kusaidia kwani vyakula viliungua na moto huo ambao ulitokea usiku wakati wanafunzi wakiwa wanjisomea masomo ya usiku.
“Tunaomba watu mbalimbali wajitokeze kuwasaidia wanafunzi walikuwa wakiishi kwenye bweni hilo kwani kufuatia moto huo hakuna kilichotoka kwani vyote viliteketea kabisa hivyo kuna haja ya kulichukulia kwa uzito wake tatizo hilo,” alisema Lufunga.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwalimu mkuu wa Shule hiyo Emanuel Kahabi alisema kuwa moto huo ulitokea wakati wanafunzi hao wakiwa wanajisomea madarasani usiku.
Kahabi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 12 majira ya saa 2:50 usiku ambapo moto huo haukuweza kufahamika ulitokea wapi na kusababisha hasara kubwa ya bweni hilo na vifaa mbalimbali vikiwemo vya wanafunzi.
“Bweni hilo ambalo lilikuwa bwalo la chakula baada ya wanafunzi hao zaidi ya 100 kuhamishiwa humo kutokana na bweni lao kuungua kwa moto miezi michache iliyopita,” alisema Kahabi.
Alisema kuwa anawashukuru wadau ambao wameanza kuisaidi shule yake kutokana na moto huo ambao hadi sasa haijafahamika chanzo chake ni nini na kuwataka watu wakiwemo wakazi wa Chalinze, wilaya na mkoa amzima kuwasaidia wanafunzi hao.
Mwisho. 

ZOEZI LA UBOMOAJI LAZUA TAFRANI

     
Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la ubomoaji kwa amri ya Mahakama vibanda vya biashara vilivyopo eneo la mtaa wa Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani umeingia kwenye mgogoro baada ya familia ya iliyodaiwa kujenga kwenye eneo ambalo si lao wamedai vimebomolewa kimakosa.
Ubomoaji huoa ambao ulifanywa Julai 15 na kampuni ya udalali ya Coast Auction Mart baada ya kesi hiyo ambayo imedumu kwa kipindi cha miaka 35 familia hiyo ya iliyoongozwa na Eva Pwele ambaye alikuwa mlalamikaji bada ya baba yake mzazi Pwele Showe ailiyefungua kesi hiyo kufariki dunia kumlalamikia Tonga Fueta kudai eneo hilo ni mali yake ambapo mahakama ilimpa ushindi.
Akizungumza na mwandishi wa habari mdai Eva Pwele alisema kuwa maamuzi ya mahakama yalikuwa ni  mlalamikiwa kupewa eneo lenye ukubwa wa mita 3 na nchi 7 kwa mita 3 na nchi 5 na si mita 352.92 ikiwa ni maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya Mwanzo Kibaha mwaka 1980.
Pwele alisema kuwa baada ya maamuzi ya mahakama hayo miezi mitatu iliyopita alifuatwa na dalali na kutakiwa avunje mwenyewe lakini yeye hakufanya hivyo na kusema kuwa yeye anachojua ni kumkabidhi eneo lenye ukubwa wa mita 3 na nchi 7 tu na si hadi kwenye eneo walilojenga mabanda hayo ya biashara.
“Cha kushangaza siku ya tukio nililiona watu wakija wakiwa Dalali na kuanza kubomoa mabanda yetu ambayo yalijengwa hivi karibuni baada ya kutokuwa na wasiwasi juu ya eneo hilo kwani mapitio ya hukumu yalisema kuwa katika maamuzi ya mwanzo hayakuonyesha ukubwa wa eneo lakini mapitio hayo ya mwaka 2005 ndiyo yaliyosema kuwa mlalamikiwa alipaswa kurudishiwa sehemu iliyotajwa hapo juu,” alisema Pwele.
Alisema kuwa mbali ya maamuzi kukiukwa pia alishangaa wahusika wa bomoa hiyo kutokuwa na barua yoyote ambayo inawaruhusu kufanya ubomoaji huo ambao umewatia hasara kubwa kutokana na mabanda hayo kuvunjwa kwa madai ya kujengwa kwenye eneo la mlalamikiwa.
Kwa upande wake Tonga Fueta alisema kuwa kwanza anamshukuru Mungu kwani baada ya kuhangaika kwa miaka 35 hatimaye haki yake imepatikana kwani tangu mwanzo wa kesi hiyo ilipofunguliwa na mlalamikaji alikuwa akishinda kuanzia mahakama ya mwanzo hadi mahakama kuu kabla ya kukatiwa rufaa na mlalamikaji baada ya hukumu ya kwanza iliyotolewa na hakimu Chungulu mwaka 1981.
Fueta alisema kuwa alinunua eneo hilo mwaka 1969 kwa kiasi cha shilingi 400 toka kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Ramadhan na mwaka huo huo alimpa sehemu ya eneo hilo Pwele Showe ambaye kwa sasa ni marehemu lakini aliongeza na eneo lake.
“Mwaka 1971 nyumba zetu na mdai wangu zilivunjwa kupisha ujenzi wa barabara ya Morogoro ndipo naye akamfuata Ramadhan ili amuuzie eneo na kumuuzia kwa shilingi 500 na ndipo aliponimbia nivunje banda langu kwakuwa yeye ameshanunua ndipo tatizo hilo lilipoanzia,” alisema Fueta.
Kufuatia bomoabomoa hiyo familia ya Pwele imesema kuwa itatafuta haki yao kwenye vyombo vya kisheria kwani ubomoaji huo umekiuka amri ya mahakama kwa kuvunja sehemu ambayo haihusiki kwani wao walikuwa wakijiandaa kumkabidhi eneo kama ilivyoagizwa na mahakama.

Mwisho.

MAKUSANYO YA STENDI YAMSIKITISHA MKUU WA WILAYA


Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Asumter Mshama amesikitishwa na mapato yanayokusanywa kama ushuru ya shilingi milioni 1.5 kwa mwezi kwenye soko kuu la Maili Moja kuwa ni madogo sana ikilinganishwa na idadi ya wafanyabiashara sokoni hapo.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Kibaha wakati alipofanya mkutano na wafanyabiashara wa soko hilo kujua changamoto zinazowakabili na kusema kuwa mapato hayo ni madogo sana na Halmashauri hiyo inapaswa kuangalia namna ya ukusanyaji mapato hayo ili yaendanena na hali halisi.
Mshama alisema kuwa soko hilo ni chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri lakini ukusanyaji huo unakatisha tamaa kwani inaonekana kuna fedha hazifiki hivyo kuna haja ya suala hilo kufanyiwa kazi ili mapato halali yaweze kuonekana.
“Kiasi kilichotajwa cha shilingi milioni 1.5 kwa mwezi hakikubaliki vinginevyo tutafanya uhakiki wa wafanyabiashara wote kwa kupitia kibanda kwa kibanda ili tuweze kujiridhisha juu ya usahihi wa mapato sokoni hapo ambapo ushuru ni shilingi 300 kwa siku kwa kila mfanyabiashara ambapo kuna wafanyabiashara zaidi ya 500,” alisema Mshama.
Alisema kuwa kama ni mgodi soko hilo ndiyo mgodi wa kuchimbwa hivyo lazima makusanyo yake yafanywe kwa usahihi ili kutopoteza fedha kwenda kwenye mifuko ya watu binafsi.
“Makusanyo kama haya haiwezekani kwa soko hili hapa kuna tatizo lazima tupate ukweli kwani hili halikubaliki au mmeshindwa kukusanya kama tunakuja hapa kudaili milioni moja nadhani hata hichi kikao hakina maana ni bora tuondoke tukaendelee na shughuli nyingine,” alisema Mshama.
Akizungumzia juu ya Halmashauri kujitoa kuweka ulinzi alisema kuwa hilo ni kosa lazima ulinzi uwe chini ya Halmashauri na si kuwatwika mzigo wafanyabiashara mzigo huo kwani huduma hiyo ni faida kwa Halamshauri hivyo hakuna sababu ya wao kulinda wenyewe.
“Inashangaza kuona kuwa eti sehemu inayotuingizia mapato hatuiwekei ulinzi mbona pale ofisini mmeweka walinzi tena wa kampuni na hapa lazima mlinde hamna hoja katika hili ninachotaka jukumu hili mlichukue kama mlivyokuwa mkifanya zamani kama hamna fedha chukueni hizo mnazokusanya hapo za ushuru mlipe walinzi hili halina mjadala,” alisema Mshama.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi Lucy Kimoi alisema kuwa juu ya ulinzi ni utaratibu uliowekwa na Halmashauri kuwaondoa vibarua wote hali iliyosababisha na walinzi ambao walikuwa vibarua kuondolewa hivyo kukodisha kampuni ya ulinzi kulinda ofisi ya Halmashauri na sokoni jukumu hilo likaudi kwa wafanyabiashara.
Kimoi alisema kuwa hiyo ni sheria ya kuwaondoa vibarua ikiwa ni utaratibu wa serikali ndiyo sababu ya kulirudisha suala hilo kwa wafanyabiashara wa soko hilo ambao walikuwa wakichanga fedha kwa ajili ya ulinzi.

Mwisho.