Monday, June 20, 2016

MWENYEKITI WA MTAA AWAZAWADIA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI

Na John Gagarini, Kibaha

MTAA wa Zegereni wilayani Kibaha mkoani Pwani umewapa zawadi mbalimbali wanafunzi wa darasa la saba waliofanya vizuri kwenye mitihani yao ya katikati ya muhula.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wakati wa kukabidhi zawadi hizo kwa wanafunzi hao Rashid Likunja alisema kuwa ameweka utartibu huo kwa wanafunzi wa darasa la saba ili kuwapa hamasa ya kufanya vizuri kwenye mtihani wa kumaliza darasa la saba.

Likunja alisema kuwa zawadi anazotoa ni mfuko wake aliouanzisha kwa ajili ya kuwapa hamasa ya wanafunzi wa mtaa huo kusoma kwa bidii na kuongeza ufaulu.

“Unajua mtaa huu hakuna shule ya msingi ambapo wanafunzi huwabidi kwenda kusoma mtaa jirani wa Visiga ambapo wengine wanatembea kilometa nane kila siku hivyo kuwakatisha tamaa watoto hivyo kutotilia makazo elimu,” alisema Likunja.
Aidha alisema kuwa kabla ya kuanza utaratibu huo wanafunzi wa mtaa huo walikuwa wakishika nafasi za nyuma kuanzia 35 na kushuka chini lakini a kwa sasa wameanza kuhamasika na wameweza kuingia kwenye 10 zaidi ya wanafunzi watano.

“Nimeanzisha mfuko wa kuwasaidia wanafunzi wa mtaa wetu naomba na wadau wengine wajitokeze kusaidia ili zawadi ziwe kubwa kwani nianazotoa ni ndogo lakini naamini wadau zaidi watajitokeza kuniunga mkono juu ya suala la elimu ambalo nimelipa kipaumbele cha kwanza,” alisema Likunja.

Moja ya wazazi ambao mwanae kapewa zawadi baada ya kuwa moja ya wanafunzi walioingia kwenye 10 bora Mwajabu Suleiman alisema kuwa mwenyekiti wao amewapa changamoto kubwa ya kuwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii.

Suleiman alisema kuwa watamuunga mkono mwenyekiti wao kwa kuwahamasisha watoto wao kusoma kwa bidii ili wawe chachu ya wanafunzi wenzao wanaoanza madarasa ya awali.


Mwisho.    

SIDO YATUMIA DOLA MILIONI 2

Na John Gagarini, Kibaha

SHIRIKA la Kuendeleza  Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) kwa kushirikiana na wafadhili wake limetumia kiasi cha dola milioni mbili za Kimarekani kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uzalishaji bidha za vyakula zisizo na madhara kwa wajasiriamali zaidi ya 700.

Mratibu wa mafunzo hayo Happines Mchomvu alisema kuwa mafunzo hayo ambayo yametolewa kwa kipindi cha miaka miwili kwa lengo la kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa hazina madhara kwa watumiaji zinakuwa na usalama.

Mchomvu alisema kuwa mbali ya kuwa na usalama pia zinakuwa na viwango vya wa ubora wa kimataifa ili viweze kuuzwa sehemu yoyote ile duniani.

“Mafunzo hayo yalikuwa na malengo ya kuboresha bidhaa za maembe, viungo na asali ambapo wameweza kuwajengea uwezo wajasiriamali hao kutoka mikoa ya Tabora, Singida, Shinyanga, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,” alisema Mchomvu.

Aidha alisema lengo ni kuhakikisha wajasiriamali kote nchini kuanzia ngazi ya mikoa hadi kwenye mitaa wanazalisha bidhaa zenye ubora na viwango kwa lengo la kuwa na soko la uhakikka la ndani na nje ya nchi ambapo bidhaa za Tanzania zinapendwa kutokana na uhalisia wake.

Kwa upande wake ofisa udhibiti wa ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Magdalena Sademaki alisema kuwa kupitia mafunzo hayo wajasiriamali hao wameweza kutengeneza mifumo yao kimataifa kwa kupambana na vihatarishi ili visiweze kuingia kwenye vyakula.
Sademaki alisema kuwa katika kuhakikisha wajasiriamali hao wanatengeneza bidhaa zenye viwango wanashirikiana na SIDO kuwatambua ili waweze kufikia viwango vya uzalishaji wa bidhaa bora ili ziendane na viwango vya kimataifa.

Na mmoja wa wajasiriamli ambaye amehudhuria mafunzo hayo Zaloki Mohamed ameishukuru SIDO kwa kuwapatia elimu juu ya viwango vya bidhaa  wanazozalisha kwa kuzingatia  utaratibu wa viwango vya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO).

Mohamed  ameiomba serikali iwapunguzie tozo zinazotozwa kwa wajasiriamali ili wapate hati ya viwango ya bidhaa wanazozalisha na kuweza kufikia malengo  ya Tanzania ya kuwa na viwanda.

Mafunzo hayo yameendeshwa kwa ufadhili wa Shirika la Biashara la Kimataifa (ITC) kupitia mpango wa kuendesha biashara wa shirika la World Trade Organisation (WTO) kwa kushirikiana na SIDO.

Mwisho. 





 

   




Saturday, June 18, 2016

WAVUNJUA VIOO VYA MADIRISHA WAPAKA KINYESI OFISI YA KATA

BOMOABOMOA YALIZA WENGI KIBAHA

MIGOGORO YA NDOA ISIWANYIME HAKI ZA MSINGI WATOTO

Tuesday, June 14, 2016

WATATU WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA DEREVA WA NOAH

Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa gari la abiria aina ya Toyota Noah Mohamed Ramadhan (21) mkazi wa Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa watu hao walimkodisha dereva huyo.
Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 13 mwaka huu majira ya saa 19:45 usiku eneo la Vigwaza Tarafa ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo.
“Watu hao walimuua dereva huyo kwa kumkaba shingoni kisha kupora gari hilo lenye namba za usajili T 119 DDM rangi nyeupe lililokuwa likitumiwa na marehemu baada ya kumkodi wakimataka awapeleke Kanisa la Pentekoste Vigwaza,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa watu hao kabla ya kumuua marehemu walimkaba wakiwa njiani ambapo alipiga kelele kuomba msaada na madereva bodaboda walizisikia na kuamua kufuatilia gari hilo barabara ya vumbi kwenye njia kuu ya umeme wa Tanesco.
“Watu wale walipoona taa za bodaboda waliamua kusimama na kutoka ndani ya gari na kuanza kukimbia kutokomea porini lakini mmoja wao alikamatwa palepale na walipoangalia ndani walikuta mwili wa marehemu ukiwa umewekwa kiti cha nyuma kwa lengo la kwenda kuutupa mwili huo porini ili kuondoka na gari hilo,” alisema Mushongi.
Aidha alisema kuwa juhudi za wananchi, dereva bodaboda na polisi zilifanikisha kukamatwa watuhumiwa wawili ambao majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa ili kutoharibu upelelezi kwani watu hao ni mtandao wa majambazi ambao wengine wako Jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi kusubiri ndugu na uchunguzi wa daktari kwa ajili ya mazishi.
Aliwataka madereva wa vyombo vya moto hasa wale wanaofanya biashara za usafirishaji nyakati za usiku kuwa makini ili kujiepusha na matukio kama hayo ya wizi.
Mwisho.         

    

Thursday, June 9, 2016

RC ATAKA MKATABA WA UWEKEZAJI KUPITIWA UPYA

Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametaka kupitiwa upya mkataba wa kuuziwa mwekezaji eneo la Magofu ya Chole wilaya ya Mafia mkoani Pwani ambapo kampuni ya Chole Mjini Conservation and Development Ltd imemilikishwa ambapo eneo hilo kuna gereza walilokuwa wanafungwa watumwa enzi za ukoloni wakati wa Utawala wa Wajerumani.
Aidha ameunda tume ya kufuatilia undani wa mkataba huo na amezuia marekebisho yaliyokuwa yanafanywa na kampuni hiyo kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi pale ufumbuzi wa kujua namna mkataba huo ulivyoingiwa baina ya Kijiji cha Chole na mwekezaji huyo kama umezingatia taratibu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chole Mjini kata ya Jibondo kwenye mkutano wa hadhara Ndikilo alisema kuwa mkoa hauna nia mbaya na mwekezaji huyo ambaye amepewa hati miliki ya eneo hilo kwa kipindi cha miaka 33.
Ndikilo alisema kuwa eneo hilo ambalo lina kumbukumbu mbalimbali ambalo liko jirani na Bahari ya Hindi lilikuwa likitumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na soko la Watumwa pamoja na gereza lina ukubwa wa hekta 3.7 ambapo eneo hilo liko chini ya Wizara ya maliasili na Utalii Idara ya Malikale.
“Mkataba huo ambao ulisainiwa mwaka 2007 shamba namba 2031 baina ya mwekezaji  Dk Jean de Villiers na Kijiji hicho ambapo mwenyekiti wa Kijiji hicho Maburuki Sadiki alisaini kwa niaba ya Kijiji na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya wakati ule Manzie Mangochi pasipo kuishirikisha Halmashauri ya wilaya ambayo haipati mapato yoyote kutokana na uwekezaji huo licha ya kutoa huduma za kijamii kwa wakazi wa Kijiji cha Chole” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo amemtaka mwekezaji huyo kusimamisha ukarabati na kuunda tume ya kufanya uchunguzi na itatoa majibu baada ya mwezi mmoja ili kujiridhisha na kumilikishwa eneo hilo mtu binafsi eneo la serikali la kihistoria na kujengwa hoteli ya kitalii kwa kukarabati jengo la zamani.
Alibainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ilituma barua ambayo iliyosainiwa na John Kimaro kwa niaba ya katibu mkuu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuhirikiana na mwekezaji na kusema kuwa sheria ya Mambo ya Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979 na sera ya Malikale ya mwaka 2008 inasema Malikale au Magofu yanaweza kumilikiwa na mtu binafs, taasisi na serikali.
Barua hiyo inaendelea kusema kuwa jukumu la serikali (Idara ya Mambo ya Kale) ni kuhakikisha kuwa mmiliki hatabomoa au kufanya chochote katika magofu hayo kinyume cha sheria.
Akitoa maelezo juu ya umiliki wake mkurugenzi wa Chole Mjini Conservation and Development Company Ltd Anne De Villiers amesema kuwa kampuni hiyo iliingia Mafia na kukuta hali ya majengo hayo ya kale yakiwa kwenye hali mbaya ndipo walianza mchakato wa kuyakarabati.
Dk Villiers alisema kuwa lengo la kuchukua eneo hilo ni kuhakikisha uasili wa mahali hapo haupotei kwa kuyafanyia ukarabati magofu hayo ambapo moja lilibaki ukuta mmoja na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati huo.
Naye mkuu wa wilaya ya Mafia Dk Nasoro Hamid alisema kuwa serikali haishirikishwi jambo lolote wala haijui ni watalii wangapi wanaoingia hapo wala mapato yanayopatikana kwenye eneo hilo.
Dk Hamid amesema kuwa Kijiji cha Chole ndicho kiliingia mkataba na mwekezaji huyo ambapo hugawana asilimia kutokana na watalii wanaoingia kwenye eneo hilo la makumbusho lakini tatizo haijulikani kinachopatikana hapo ni kiasi gani katika mgawanyo huo wa mapato.
Awali baadhi ya wanakijiji wakizungumzia suala hilo wakiongozwa na Ally Sikubali na Hemed Ally walisema kuwa moja ya changamoto iliyokuwepo ni mkataba Kiswahili unasema kuwa endapo kutakuwa na kutoeleweka mkataba wa Kiingereza ndiyo utakaotumika.
Waliomba mkataba huo uangaliwe upya na kufanya marekebisho ili kila upande unufaike kwani kwa sasa inaonekana kuwa pande nyingine hazinufaiki na mkataba huo.     
Mwisho.