Saturday, April 9, 2016

HOSPITALI YA BAGAMOYO YADAIWA M 220 NA MSD

Na John Gagarini, Kibaha
HOSPITALI ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa dawa baada ya kukosa dawa kuanzia Januari mwaka huu kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kutokana na kudaiwa deni la shilingi milioni 220.
Hayo yamesemwa na mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali hiyo Tumaini Byron wakati Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo kutembelea wagonjwa na kuwapa misaada mablimbali katiaka kusherehekea miaka 61 ya kuanzishwa Jumuiya hiyo.
Dk Byron amesema kuwa kutokana na deni hilo Hospitali hiyo kwa sasa imeonekana haikopesheki kutokana na deni hilo hivyo kunywimwa dawa hadi pale watakapolipa deni hilo la madawa.
Amesema wanakosa dawa kutokana na deni hilo kwani hata wakiomba hawapati hivyo kuwapa wakati mgumu wao pamoja na wagonjwa ambao hutakiwa kwenda kununua kwenye maduka ya madawa.
Aidha amesema kuwa wanashindwa kupewa au kukopeshwa vifaa tiba pamoja na vipimo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipimo vya wingi wa damu mkojo na malaria.
Amebainisha kuwa changamoto nyingine ni upungufu wa watumishi kwani kwa sasa wana watumishi 147 huku mahitaji yakiwa ni watumishi 250, vitanda vilivyopo ni 24 tu ambapo walau vingepatika japo 100 pamoja na uchakavu wa miundombinu ya umeme..
Kwa upande wake Mfamasia wa wilaya ya Bagamoyo Mohamed Makarai amesema kuwa mbali ya deni hilo la dawa pia MSD kutokuwa na dawa hivyo kuwa ni tatizo la nchi nzima kuanzia Oktoba na Novemba mwaka jana.
Makarai amesema kuwa serikali ilibadilisha mfumo wa kutoa tenda kwa wazabuni kwa ajili ya kuwapelekea dawa ambapo kwa sasa utaratibu umebadilika kwani hakutakuwa na kutoa tenda tena.
Amesema kuwa walikuwa wakichukua dawa kwa mali kauli na kutoa fedha baadaye hata hivyo walitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 100 ambapo moja ya changamoto ya kukosa fedha ni pamoja na kuwa na misamaa ikiwemo ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wazee, wajawazito na wale wenye magonjwa sugu hivyo serikali inapaswa kufidia pengo la makundi hayo ambayo yanapewa dawa bure.
Mwisho.

Monday, April 4, 2016

UVCCM WATAKIWA KUTUMIA KILIMO KAMA FURSA NA SIO KAMA ADHABU

Na John  Gagarini, Kibaha
VIJANA wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  CCM (UVCCM) wilayani Kibaha wametakiwa kukitumia kilimo kama moja ya chanzo cha kujikomboa kiuchumi kwani hiyo ni fursa na si adhabu.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa CCM (MNEC) Rugemalila Rutatina wakati akifungua mkutano wa Baraza la (UVCCM) Kibaha Mjini na kusema kuwa kilimo endapo kitatumia vizuri kinaweza kuboresha uchumi wao badala ya kumtegemea mtu kuwasaidia.
Rutatina alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwafanya vijana kama ngazi ya kupandia kwa kuwafanikishia mambo yao kisha kuwaacha bila ya kuwajengea mazingira endelevu.
“Uzuri ni kwamba Chama pamoja na umoja wenu una mashamba ambayo ni kama mtaji wa kuanzia kwa ajili ya kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija kwa kutumia mipango mbalimbaili ya kuendeleza kilimo ikiwa ni pamoja na Kilimo Kwanza,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa ili vijana wajikomboe wanapaswa kuanzisha miradi ya kudumu kupitia rasilimali za chama ambazo endapo zingetumika ipasavyo zingewaondoa vijana ndani ya chama na nje kuwa tegemezi katika kuendesha umoja wao.
“Kilimo ni moja ya njia za kuwakomboa na kuacha kumtegemea mtu lakini endapo mtaanzisha miradi ya kilimo itawaondoa huko mliko na kuwafanya mjitegemee na kuendesha mambo yenu bila kuwa tegemezi,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kuwa kwa sasa fursa ni nyingi kwa vijana ikiwa ni pamoja na mikopo kwa ajili kujikwamua kiuchumi na zana za kilimo kama matrekta wanaweza kuazima kwenye chama.
Kwa upande wake katibu wa (UVCCM) Kibaha Mjini David Malecela alisema kuwa wana maeneo mengi ambayo hata hivyo hayajaendelezwa hali ambayo imesababisha watu kuyavamia.
Malecela alisema kuwa kwa sasa wako kwenye mipango ya kuhakikisha wanayamiliki kisheria ili kukabiliana na watu wanaoyavamia maeneo yao ambayo yakiendelezwa yatakuwa ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato ya umoja.
Mwisho.

WAPEWA SIKU 60 KUHAMA ENEO LILILOFUTIWA HATI YA UMILIKI

Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wakazi wa Kitongoji cha Vinziko Kijiji cha Kikongo wilayani Kibaha mkoani Pwani wameitaka Halmashauri ya wilaya kutowaondoa kwenye eneo ambalo wanaishi kwani hawana pa kwenda.
Serikali iliwapa siku 60 wawe wameondoka kwenye eneo hilo ambalo lilikuwa chini ya kampuni ya United Framing Cooperation (UFC) ambao walishindwa kuliendesha na kuwa shamba pori kabla ya serikali haijalifutia hati Mei 28 mwaka 2015.
Moja ya wakazi wa eneo hilo Athuman Fundi (90) alisema kuwa wao wako hapo muda mrefu tangu operesheni vijiji ambapo walihamishwa toka maeneo ya mbali na kupelekwa maeneo ambayo yalikuwa karibu na huduma za kijamii.
“Sisi tulifikiri ni vema wakatuacha kwenye maeneo yetu haya na si kutuondoa kwani hatuna pa kwenda na sisi hapa tumeshawekeza kwa kujenga makazi ya kudumu leo wakituambia tuondoke tutakwenda wapi vinginevyo watulipe ili tukatafute sehemu nyingine au watupatie maeneo mengine,” alisema Fundi.
Fundi alisema kuwa mbali ya kutakiwa kuondoka pia vyombo vya dola vimekuwa vikitumia nguvu kubwa kutaka wao waondoke ambapo wenzao wamekuwa wakikamatwa kutokana na mgogoro huo ambao umewanyima raha.
“Tunaomba tusaidiwe na Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi ili tupate haki yetu kwani wao kututaka tuondoke bila ya kutupa chochote au kutotupa maeneo mengine tunaona kama hatujatendewa haki kwani tuna nyumba zetu, mazao ambavyo vimo humo leo wanatuambia tuviondoe tutaishi wapi,” alisema Fundi.
Kwa upande wake Sabina Benedict alisema kuwa wamekuwa wakiteseka sana kutokana na mgogoro huo kwani wazee na vijana wamekuwa wakikamatwa na polisi na kuwekwa rumande hivyo kuishi kwa woga.
Benedict alisema kuwa tatizo kubwa linatokana na viongozi ambao wanataka kumuuzia mwekezaji ambaye anatumia kila njia kuhakikisha wao wanaondoka ili alipate eneo hilo kirahisi.
Naye mwenyekiti wa Kijiji cha Kikongo Sultan Ngandi alisema kuwa shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 3,285 lilikuwa likimilikiwa na kampuni hiyo ya UFC ambayo ilikuwa ikilima mazao mbalimbali kama vile Pamba, Mbaazi, Alizeti na mazao mengine ilishindwa kuliendeleza na kuliacha pori ambalo lilikuwa likitumiwa na wahalifu kuzuru watu.
Ngandi alisema kuwa wananchi waliomba kulima ikiwa ni pamoja na Umoja wa wakulima wa Ondoa Njaa Kikongo (ONJAKI) lakini walitakiwa wasilime mazao ya kudumu wala kujenga nyumba za kudumu badala yake walime mazao ya muda mfupi.
“Hata hivyo baadhi ya watu walikiuka makubaliano na wengine walianza kujenga nyumba za kudumu, mazao ya muda mrefu na hata wengine walifikia hatua ya kuayauza kienyeji baadhi ya maeneo nao kuondoka na kuwaacha watu ambao ndiyo wanaolalamika,” aisema Ngandi.
Akizungumzia suala hilo mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa ni kweli wametoa siku 60 kwa watu walioko kwenye eneo hilo kwani wamevamia na hawakutakiwa kuwa kwenye neo hilo kwani liko chini ya serikali.
Kihemba alisema kuwa hilo ni moja ya mashamba 16 ambayo yalifutiwa hati na kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kulitengea matumizi na waliwataka watu walioko kwenye eneo hilo wapeleke vielelezo vya kuonyesha walipataje maeneo hayo na kusema si kweli kwamba kuna mwekezaji wanataka kumpa eneo hilo.
Aidha alisema kuwa hadi sasa watu zaidi ya 100 wamepeleka vielelezo vyao nab ado wanawasubiri watu wengine ambao wako wengi ili wapeleke vielelezo vyao ili serikali iangalie namna ya kuwasaidia na kuwataka watu hao waondoke kwenye eneo hilo.
Mwisho.

Friday, April 1, 2016

SAKATA WAFANYAKAZI HEWA RC AWATAKA WAKURUGENZI KUBAINISHA WALIOKUWA WAKICHUKUA MISHAHARA PASIPO KUWA WAFANYAKAZI

Na John Gagarini, Kibaha
SAKATA la wafanyakazi hewa mkoani Pwani limeingia hatua mpya baada ya Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kutakiwa kutoa taarifa zaidi juu ya wafanyakazi hewa 42 ambao hawapo kabisa kazini lakini wamekuwa wakipokea mishahara kila mwezi.
Jumla ya wafanyakazi 42 kwenye mkoa huo majina yao yapo lakini wao hawapo kazini lakini walikuwa wakipokea mishahara kila mwezi hali ambayo imeisababishia hasara kubwa serikali kutokana na kulipa hewa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kiwake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa wafanyakazi hao hewa wamewekwa kwenye madaraja mbalimbali ikiwa ni pamoja na hao 42 ambao hawapo kabisa kazini lakini walikuwa wanalipwa.
“Kutokana na hali hii nimewapa wakurugenzi hadi siku ya Jumatano Aprili 6 wawe wameniletea taarifa juu ya watu waliokuwa wakipokea fedha hizo kwani haiwezekani ni nani aliyekuwa akipokea fedha hizo licha ya kutokuwepo kabisa kwa wafanyakazi hao,” alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa haiwezekani fedha zilipwe kwa wafanayakazi ambao hawapo kazini kwani ni jambo la kushangaza na lazima ajulikane ambaye alikuwa akipokea fedha hizo kwani kundi hili ni hewa kabisa.
“Kundi lingine ni la wafanyakazi 58 ambao wamesimamishwa kazi kwa tuhuma mbalimbali lakini wamekuwa wakipokea mishahara kama kawaida tunataka tujuea kwa undani ni tuhuma gani zinazowakabili na hatua zilizochukuliwa dhidi yao,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kundi lingine ni la wafanyakazi ambao wako kazini lakini ni watoro hawaendi kazini lakini mishahara wanachukua kama kawaida licha ya kwamba hawawajibiki kazini kama ilivyo taratibu za utumishi wa umma.
“Tunataka kila mkurugenzi atoe taarifa sahihi bila ya kuficha kwani endapo atabainika ameficha taarifa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake hivyo ni vema wakawea wazi taarifa za hao wafanyakazi hewa,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa juu ya hasara waliyoiingiza wafanyakazi hao hewa ambapo kwa mkoa wa Pwani ni 150 bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ni kiasi gani ambacho wameliingizia Taifa hasara na mara watakapokamilisha watatoa taarifa hizo.

Mwisho.

SELEMAN TALL ATWAA MKANDA WA TPBO

Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA Said Seleman maarufu kama Tall juzi usiku alitwaa ubingwa wa taifa wa ngumi uzito wa kati kupitia shirikisho la ngumi la TPBO baada ya kumshinda kwa pointi Ambokile Chusa.
Pambano hilo ambalo lilipigwa kwenye ukumbi wa Container wilayani Kibaha mkoani Pwani lilikuwa la vuta ni kuvute kutokana na umahiri wa mabondia hao ambao hata hivyo walikuwa wakicheza kwa kuogopana kwa hofu ya kupoteza ushindi.
Hata hivyo Tall alikuwa mjanja na kumzidi mbinu mpinzani wake ambaye muda mwingi alikuwa akijihami kwa kuficha uso ili kukwepa ngumi kali zilizokuwa zikirushwa na mpinzani wake.
Kwenye mapambano mengine Yasini Said alimpiga Julius Jackson, Emanuel Endrew alimpiga Ramadhan Keshi, Ramadhan Kamage alimtwanga Kassim Chuma, Salehe Muntari alimtwanga Aziz Pendeza, Hassan Mgosi alimtwanga Hemed Hemed, Said Chino alimtwanga Idd Mgwinyo kwa TKO, huku Alfred Masinda na Nurdin Mijibwa na Abdala Luwanje na Rajabu Mbena walitoka sare.
Akikabidhi mkanda huo kutoka TPBO mgeni rasmi katika pambano hilo Selina Wilson Diwani wa Viti Maalumu aliwapongeza waandaaji wa pambano hilo Butamanya Promotion kwa kuleta shindano hilo Kibaha.
Wilson alisema kuwa kuleta mchezo huo Kibaha ni kuibua vipaji vilivyopo mikoani na kuwapa uzoefu mabondia wa hapa kuweza kujifunza mbinu za ngumi.
“Mimi ni kijana na nimeona jinsi gani watu wanavyopenda mchezo huu hapa Kibaha na mkoa wa Pwani nitahakikisha naunga mkono mchezo huu na kupeleka halamashauri changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mchezo huu,” alisema Wilson.
Kwa upande wake bondia wa zamani Habibu Kinyogoli alisema kuwa mabondia wa mkoa wa Pwani wameonyesha uwezo lakini walichokosa ni mbinu za mapigano hivyo atajitolea kuwafundisha mabondia wa mkoa wa Pwani.

Mwisho.

Wednesday, March 30, 2016

MABONDIA KUWANIA MKANDA TPBO KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
MABONDIA Said Seleman Ambokile Chusa wajijini Dar es Salaam leo wanatarajia kupambana kwenye pambano la ngumi la kuwania ubingwa TPBO uzito wa kati pambano litakalo pigwa kwenye ukumbi wa Container Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha moja ya wasimamizi wa pambano hilo ambaye ni mwalimu wa ngumi Gordon Tambwe maarufu kama Mawe alisema kuwa pambano hilo litakuwa kali na la kuvutia.
Mawe alisema kuwa lengo la kufanya pambano hilo Kibaha ni kuhamasisha mchezo huo mikoani pia kuinua vipaji kwa mabondia wa mikoani ili nao waweze kuonyesha uwezo wao.
“Tumeleta pambano hili Kibaha ili kuhamasisha mchezo wa ngumi sehemu mbalimbali mikoani kwani michezo ni ajira na ngumi zimewasaidia vijana wengi kujiajiri kupitia mchezo huo,” alisema Mawe.
Aidha alisema kuwa mabondia hao watapigana raundi 10 na pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambayo yatausisha mabondia kutoka mkoa wa Pwani na wageni wao kutoka Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Seleman alisema kuwa amejiandaa ipasavyo na anatarajia kummaliza mapema mpinzani wake kwa KO kwani hatakuwa na muda wa kupoteza katika kumaliza pambano hilo.
Naye Chusa alisema kuwa amekwenda Kibaha kwa ajili ya kutafuta ubingwa na si kutalii na anatarajia kumpiga mpinzani wake ili kuwapa raha wapenzi wake hivyo wasiwe na wasiwasi. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa diwani wa Viti maalumu Selina Wilson.

Mwisho.

Saturday, March 26, 2016

MABASI YA MIKOANI 48 YAKUTWA NA MAKOSA MBALIMBALI

Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya mabasi 48 ya abiria ya kwenda mikoani yamekutwa na makosa mbalimbali kufuatia zoezi la ukaguzi lillofanywa kwa ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (SUMATRA).  
Zoezi hilo lilifanywa kwenye Stendi Kuu ya Ubungo, Maili Moja na Chalinze kwa lengo la kudhibiti ajali pamoja na madereva wanaokiuka taratibu za usalama barabarani kwa mabasi hayo yaendayo mikoani .
Akizungumza na gazeti hili Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini ACP Fortunatus Musilimu alisema kuwa zoezi hilo ambalo lilikuwa la kushtukiza litakuwa endelevu ili kuhakikisha ajali zinapungua na kuwaondolea usumbufu abiria.
Musilimu alisema kuwa waliyafanyia ukaguzi mabasi 169 na kuyabaini mabasi hayo 48 kuwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwendokasi mabasi 24, kutofunga mikanda mabasi tisa, kuwazidishia nauli nane, ubovu basi moja, kukiuka ratiba basi moja na leseni basi moja.
“Pia tulimakamata dereva mmoja kwa kutumia kilevi ambapo alikuwa na kiwango cha juu cha ulevi cha 77.7 ambapo kwa kawaida kinatakiwa kuwa 00.8 kwa mujibu sheria hali iliyosababisha dereva huyo kushushwa na kupelekwa rumande,” alisema Musilimu.
Alisema kuwa ukaguzi huo unandelea kote nchi ambapo tayari makamanda wa usalama barabarani mikoani wameshapewa maagizo ya kufanya ukaguzi wa mabasi kwani ukaguzi hauwezi kuyakagua mabasi yote kutokana na eneo la ukaguzi kuwa dogo hali ambayo inawafanya wafanyie ukaguzi mabasi matano matano kwa wakati mmoja huku mengine yakiendelea na safari.
Aidha alisema kuwa mbali ya kukagua mabasi hayo pia walikagua malori ya mchanga 13 na kuyakuta na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwendo kasi magari saba, mabovu matano, kuyapita magari mengine pasipo kuzingatia sheria.
Aliwataka abiria kutoa taarifa kwenye vyombo husika kwa madereva ambao wanaoendesha magari kwa mwendo wa kasi pia wasiwashabikie kwani ni moja ya vyanzo vya ajali za barabarani ambazo zinasababisha vifo vya watu wengi.
Mwisho.