Saturday, March 19, 2016

RAS PWANI KUFUNGUA MAFUNZO YA MPIRA WA WAVU

Na John Gagarini, Kibaha
KATIBU Tawala (RAS) Mkoa wa Pwani Mgeni Baruani anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya walimu wa mchezo wa wavu Volleyball yatakayoanza Machi 24 hadi Aprili Mosi mwaka huu kwenye viwanja vya shule ya Msingi Kibaha.
Akizungumza na waandishi wa habari katibu wa chama cha mchezo huo mkoani Pwani (COREVA) Lonjin Mzava alisema kuwa wanatarajia mafunzo hayo yatawahusisha walimu wa mchezo huo kwa shule za msingi walimu wanne , sekondari walimu wanne , vyuo pamoja na wadau wengine wanaopenda kujifunza mchezo huo.  
Mzava alisema kuwa washiriki watatoka wilaya zote za mkoa wa Pwani ambapo kwa walimu tayari barua za kuomba ushiriki wao zimepelekwa kwa wakurugenzi wa Halmashauri ili kuwpaatia ruhusa ya kushiriki mafunzo hayo.
“Wanafunzi wa mchezo huo watajifunza masomo ya darasani pamoja nay a vitendo ili kuwajengea uwezo wa kuujua mchezo huo hata watakapokwenda kuwafundisha wengine wawe na maarifa ya kutosha na mafunzo haya yameandaliwa kwa pamoja na chama cha mchezo huo nchini (TAVA) alisema Mzava.
Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa ujuzi wa kutosha walimu wa mchezo huo ili waweze kujua sheria na namna mchezo unavyochezwa na kuusimamia kama sheria za mchezo huo zinavyoonyesha na kupitishwa na chama cha mchezo huo cha kimataifa FIVB.
“Hadi sasa walimu kutoka Hlamashauri za Bagamoyo, Mkuranga, Rufiji na Kibaha Mji tayari wamethibitisha kushiriki mafunzo hayo na waliobaki wanapaswa kuthibitisha kabla ya tarehe 22 Machi ili waweze kuwekewa utaratibu wa kushiriki mafunzo hayo,” alisema Mzava.
Aidha alisema kuwa walimu watakaofanya vizuri kwenye mafunzo hayo watapata nafasi ya kushiriki mafunzo ya Kimataifa ya Beach yatakayofanyika Aprili mwaka huu Jijini Dar es Salaam hivyo itasaidia kuutangaza mkoa kupitia mchezo huo.
“Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kudhamini mafunzo haya kwani hata wakitoa maji au kitu chochote itasaidia kupunguza gharama za kuendesha mafunzo hayo kwani hadi sasa hakuna wadhamini waliojitokeza kuzamini mafunzo hayo,” alisema Mzava.
Alibainisha kuwa matarajio ni kuzalisha walimu wengi wa mchezo huo hasa mashuleni na itasaidia kupunguza gharama za kuwalipa walimu toka nje hawa wakati wa mashindano ya Umoja wa Shule za Msingi na Utamaduni Tanzania( UMITASHUMTA) na Umoja wa Shule za Sekondari na Sanaa Tanzania (UMISSETA).

Mwisho. 

Monday, March 14, 2016

CHUO CHA KILIMO NA MIFUGO CHAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA ZANA ZA KILIMO

Na John Gagarini, Bagamoyo
CHUO cha Kilimo na Mifugo Kaole wilayani Bagamoyo kinachomilikiwa na Jumuiya ya wazazi Tanzania kinakabiliwa na upungufu wa madawa ya kujifunzia kwenye maabara pamoja na zana za kujifunzia hali ambayo inasababisha wanachuo kushindwa kujifunza kikamilifu.
Hayo yalisemwa Bagamoyo na Rais wa Chuo hicho Abas Kasusumo wakati wa ziara iliyofanywa na Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo ambao walitembelewa na Jumuiya hiyo wilaya ya Temeke kuangalia shughuli zinazofanywa na Jumuiya hiyo.
Kasusumo alisema kuwa changamoto hizo zinawasababisha washindwe kujifunza ipasavyo hali ambayo inawafanya wawe katika wakati mgumu kuelewa masomo yao.
“Tunaomba tusaidiwe vifaa vya kujifunzia kama vile matrekta ambayo hapa yapo lakini hayafanyi kazi hivyo tunaiomba serikali na Jumuiya ambayo ndiyo wamiliki wa chuo chetu ili tupate vifaa vya kujifunzia,” alisema Kasusumo.
Alisema kuwa kutokana na chuo hichi kuwa cha mifugo pia kuna changamoto ya ukosefu wa madawa mbalimbali kwa ajili ya kujifunzia masomo yetu kwani wakitoka hapo watategemewa kufanya kazi kutokana na walivyojifunza.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa chuo hicho Carthert Liwa alisema kuwa changamoto nyingine ni umeme ambapo wanatumia mita ya Luku ambayo haiwezi kumudu matumizi makubwa.
Liwa alisema kuwa changamoto zimekuwa nyingi kwani chuo hicho kimeanza upya baada ya kutokea matatizo hivyo wadau wanaombwa kujitokeza kukisaidia ili kiweze kutoa mafunzo kwa viwango vinavyotakiwa.
Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo ambao ndiyo wamiliki wa chuo hicho Abdul Sharif alisema kuwa watahakikisha wanshirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha kinatoa mafunzo kwa ubora.
Sharif alisema kuwa changamoto zilizotajwa ni za kweli na Jumuiya kwa kushirikiana na makao makuu watazifanyia kazi changamoto hizo ili elimu bora iweze kupatikana chuoni hapo. Chuo hicho kina wanafunzi 36 lakini uwezo wake ni wanachuo 600 ambapo hali hiyo ilitokana na kuchelewa kuandikisha wanachuo.
Mwisho.    
    
  
  

    

Thursday, March 10, 2016

DIWANI AKUMBWA NA BOMOBOMOA KIBAHA


Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la bomoa bomoa kwa watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara ya Morogoro lililoanza Machi 8 mwaka huu wilayani Kibaha mkoani Pwani limemkumba diwani wa kata ya Sofu Yusuph Mbonde ambaye alijenga chumba cha biashara kwenye  eneo la Picha ya Ndege naye amekumbwa na kadhia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo hilo diwani huyo alisema kuwa yeye naye alikuwa akifanya biashara ya kujipatia riziki yake hapo na alijua bomoa bomoa hiyo ilikuwa ni kwenye barabara mpya lakini akashangaa zoezi hilo kupita hadi barabara ya zamani.
“Zoezi hili limeathiri watu wengi na wote tuliojenga hapa na kufanyabiashara hapa tulipewa taarifa ya kubomoa lakini nilijaribu kumwomba meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutuongezea muda lakini alisema watu wabomoe ambapo walitoa muda wa kubomoa na watu wengi hawakuamini kama watabomolewa kwani taarifa zilikuwa zikitolewa bila utekelezaji,” alisema Mbonde.
Alisema eneo ambalo limebomolewa ni zaidi ya wafanyabiashara 200 ambako ni pamoja na eneo la soko na maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali pamoja na nyumba za makazi ya watu wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 1,000 kwa mitaa miwili ya Picha ya Ndege na Msufini ambayo ina wakazi 13,000.
“TANROADS iliwataka watu wanaotumia eneo la hifadhi ya barabara kutojenga vibanda vya kudumu lakini watu walijenga vibanda vya kudumu pamoja na nyumba kama siyo sehemu ya muda tunakubaliana na serikali hatuna jinsi tutatafuta eneo mbadala kwa ajili ya kufanya biashara,” alisema Mbonde.
 Naye Zakia Yusuph alisema kuwa zoezi hilo limewaathiri sana hasa akinamama ambao walikuwa wakiendesha biashara zao za kujipatia kipato ambapo wengine ni wajane na wana watoto ambao wanasoma.
Yusph alisema kuwa yeye yeye alikopa mkopo benki wa shilingi milioni tano na hajui atazirudisha vipi na kuiomba serikali kuwapatia eneo lingine kwa ajili ya kufanyia biashara zao za kuwapatia kipato cha kuendeshea familia zao.
Kwa upande wake meneja wa TANROADS Tumaini Sarakikya alisema kuwa zoezi hilo la bomoabomoa litadumu kwa kipindi cha siku 15 ambapo wataondoa nyumba zote zilizojengwa kwenye hifadhi ya barabara zilizo ndani ya mita 22.5 kila upande wa barabara kwa sheria ya barabara ya mwaka 1930 baada ya kutoa notisi za mara kwa mara.
Sarakikya alisema kuwa zoezi hilo ni la kudumu na litafanyika kwenye barabara zote zilizochini ya wakala kwenye wilaya za mkoa huo ambapo kwa njia ya Morogoro zoezi hilo litaenda hadi Bwawani mpakani mwa mikoa ya Pwani na Morogoro.
“Barabara ya Tanga watatekeleza zoezi hilo hadi eneo la Manga mpakani mwa mikoa hiyo huku kwa upande wa Bagamoyo litafanyika hadi Bunju mpakani mwa Pwani na Dar es Salaam na Kongowe hadi Marendego kwa barabara iendayo mikoa ya Kusini,” alisema Sarakikya.
Akizungumzia kuhusu eneo la Maili Moja ambako ndiyo makao makuu ya mkoa wa Pwani amesema kuwa eneo hilo litakuwa la mwisho kutokana na halmashauri kuomba hadi pale watakapojenga Stendi na soko ambavyo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri hiyo lakini mara ujenzi huo utakapokamilika watabomoa ndani ya mita 100 kila upande.

Mwisho.

DK KIGANGWALA AMPA SAA 24 MKURUGENZI KUANDIKA BARUA YA KUJIELEZA KWANINI ASIONDOLEWE KWENYE NAFASI HIYO, AFUNGA CHUMBA CHA MAITI ATAKA WAFANYE MAREKEBISHO NDANI YA SIKU TATU

Na John Gagarini, Kibaha
NAIBU Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dk Hamis Kigangwala ametoa saa 24 kwa Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Dk Cyprian Mpemba kuandika barua ya kwa nini asiondolewe kwenye nafasi hiyo kwa kushindwa kuendesha Hospitali Teule ya Rufaa ya Tumbi iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Waziri Dk Simbachawene alitoa agizo hilo huku mkurugenzi huyo akiwa hayupo na kumwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo Anase Nko kumfikishia ujumbe huo Dk Mpemba kwa ajili ya kutoa maelezo hayo.
Dk Kigangwala aliyasema hayo jana mara baada ya kutembelea hospitali hiyo kutokana na kuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kushindwa kusimamia maslahi ya watumishi ambao wamekosa morali ya kufanya kazi.
Alisema kuwa hali iliyopo kwenye hospitali hiyo ni mbaya sana na inasikitisha sana huku ofisi ya mkurugenzi ikiwa inatumia fedha ambazo zingesaidia kuboresha huduma kwenye hospitali hiyo.
“Shirika limeshindwa kuendesha natoa saa 24 hadi leo saa nane mchana awe ameandika barua ya kujieleza kwanini asiondolewe kwenye nafasi hiyo kwani ameshindwa kusimamia hospitali hiyo kwani vitu vingi haviko sawa kuanzia mochwari ambapo imekuwa ikitoa harufu mbaya kutokana na baadhi ya vifaa vya majokofu kuharibika,” alisema Dk Kigwangala.
“Nataka atoe maelezo yanayojitosheleza kwani inaonekana hakuna jambo ambalo linaweza kufanyika kwenye hospitali bila ya mkurugenzi ambapo fedha za hospitali zimekuwa zikitumika kwenye matumizi mengine,” alisema Dk Kigangwala.
Aidha alisema kuwa mbali ya hivyo pia kuanzia sasa shirika hilo lisisimamie masuala ya fedha za Hospitali hiyo bali ijisimamie yenyewe ili kuangalia vipaumbele vinavyohusu hospitali kwani huduma hazisubiri utaratibu.
“Tumeona kuwa tatizo ni utawala ambao unaonekana umeshindwa kusimamia hospitali nilipokuja nilifikiri tatizo ni meneja wa Huduma za afya Dk Peter Datani lakini una bahati nilikuja kwa ajili ya kukutimua wewe kumbe wewe huusiki,” alisema Dk Kigwangwala.
Alibainisha kuwa kuna changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na chumba cha upasuaji kutokuwa na hadhi kwani ni sawa na stoo, viyoyozi havifanyi kazi, chumba cha wagonjwa mahututi nacho hakiko sawa na vifaa vinaharibika hakuna matengenezo hivyo huduma kuwa mbaya.
“Inashangaza kuona kuwa hospitali inakosa vifaa tiba pamoja na madawa licha ya kuwa inaingiza fedha nyingi kati ya shilingi milioni 120 hadi 150 kwa mwezi lakini inashindwa kujiendesha inashindwa hata kutoa milioni sita kwa ajili ya kununulia mifuko ya kuhifadhia damu inasikitisha sana hospitali hii inaendeshwa kiujanja ujanja tu lazima mjiendeshe kwa mikakati siyo kwenda tu,” alisema Kigwangwala.
Kutokana na hali hiyo ameagiza chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ifungwe na iwe imefanyiwa matengenezo ndani ya siku tatu na watajua maiti watazipeleka wapi kwani haiwezekani chumba hicho kuwa kwenye hali hiyo pia miezi mitatu wanatakiwa wawe wamehakikisha maji yanapatikana kwa kujenga matenki ya kuhifadhia maji.
Alimtaka mkuu wa mkoa kupata ushauri kwa  wataalamu ili kuangalia mahusiano baina ya hospitali hiyo na sekretarieti ya mkoa pia inaonekana ni vema hospitali hiyo ikasimamiwa na mkoa badala ya shirika.
Alisisitiza kuwa endapo watashindwa kukarabati chumba hicho cha maiti ndani ya siku tatu atawaondoa kwenye nafasi zao kwani watakuwa wameshindwa kutekeleza agizo la serikali kwani haiwezekani huduma kutolewa kwenye mazingira magumu wakati fedha zinapatikana.
Kwa upande wake msajili wa hospitali nchini Dk Pamela Sawa alisema kuwa walifanya ukaguzi kwenye hospitali mwaka 2010 hadi 2011 ambapo walikuta hospitali nyingi zina mapungufu mengi mafano hospitali ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro ilikuwa ikitumia chumba cha upasuaji kilichokuwa kikitumika enzi za mkoloni lakini walibadilisha baada ya kuifunga pia hospitali ya Mbeya nayo ilikuwa na matatizo ya maji.
Naye Dk Datani alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo hospitalini hapo ni ukosefu wa fedha kwani waliomba kiasi cha shilingi milioni 600 lakini walipewa kiasi cha milioni sita tu hivyo kujikuta wakiwa kwenye wakati mgumu wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi pamoja na kununua vifaa tiba pamoja na madawa.
Mwisho.

   

Friday, March 4, 2016

ALBINO APOTEA

Na John Gagarini, Mkuranga
KIJANA mwenye ulemavu wa ngozi Albino Said Abdala mkazi wa Kijiji cha Mbezi Mlungwana kata ya Pazuo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani amepotea tangu Januari 31 mwaka huu na hajulikani alipo baada ya kwenda kutembea nyakati za usiku.
Abdala ambaye alikuwa akiishi na wenzake wawili wenye ulemavu huo akitokea mkoani Morogoro huku wenzake Tabora kwa lengo la kuepuka vitendo vya kushambuliwa na watu ambao wamekuwa wakiwa kata viungo au kuwaua hali iliyowafanya wakae huko chini ya Shirika la Under The Same Sun.
Akizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo, Samwel Masaga alisema kuwa mwenzao aliondoka siku hiyo majira ya jioni kwenda kutembea lakini hakurudi tena hadi wakati anatembelea mkuu huyo.
Masaga alisema kuwa mwenzao alikuwa na tabia ya kutoka na kutembetembea lakini wanashangaa ni kwa nini hajarudi na jitihada za kumtafuta zimeshindikana licha ya kutoa taarifa sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na polisi na ofisi ya mkuu wa wilaya.
“Tunasikitika kupotea kwa mwenzetu na hatuji tutampataje tunaomba vyombo vinavyohusika vitusaidie ili mwenzetu aweze kupatikana kwani hatujui mwenzetu nini kimemsibu kwani ni muda mrefu umepita hakuna taarifa yoyote juu yake,” alisema Masaga.
Alisema kuwa mazingira wanayosihi kwa bahati mbaya hayana ulinzi wowote lakini wamekuwa wakiishi vizuri na wenyeji wao ambao waliwapokea vizuri na wamekuwa wakiishi vizuri bila ya matatizo ila hawajui mwenzao yuko wapi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Hassan Kafeni alisema kuwa walemavu hao wako hapo tangu mwaka 2014 na ni wa awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kukaa hapo kisha kuondoka ndipo walipoombewa hao wakae hapo ili nao waishi kama wanakijiji.
Kafeni alisema kuwa Abdala tangu alipopotea walifanya jitihada za kumtafuta lakini hata hivyo hawajamwona na bado wanaendelea kumtafuta hadi watakapompata na wameshangazwa na tukio la kupotea kwake.
Kutokana na hali hiyo mkuu wa mkoa wa Pwani injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa shirika hilo linapaswa kuangalia upya namna ya kuwatunza watu hao kwani mazingira waliyopo usalama wake ni mdogo.
Ndikilo alisema kuwa shirika hilo linaonyesha lina nia nzuri lakini mazingira waliyopo si salama sana kwani hakuna ulinzi wa kutosha hali ambayo imesababisha Abdala kupotea na kuwataka kuwahamishia sehemu nyingine.
“Nawashauri wawatafutie sehemu nyingine ya kuishi kwani pale walipo hakuna usalama kwani kama mtu anania mbaya ni rahisi kuwazuru kwani serikali inataka waishi kwenye mazingira yenye usalama wa maisha yao,” alisema Ndikilo.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa Jeshi hilo linaendelea na msako wa kumtafuta Abdala na watahakikisha wanamtafuta hadi wanampata ili aungane na wenzake waishi kama kawaida.
Mushongi alisema kuwa ushirikiano na wananchi utasaidia kupatikana kwake hivyo watoe ushirikiano ili kufanikisha Abdala kupatikana kwani jambo hilo si la kawaida kutokea na kuwataka wananchi kuwalinda Albino kwani nao wana haki ya kuishi.
Mwisho.           


JESHI LA POLISI LAPEWA SIKU TATU KUMALIZA UHALIFU UNAOFANYWA NA WAVAMIZI

Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametoa siku tatu kwa Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo vya kuwavamia kisha kuwapora viwanja na kufanya mauji kwa wakazi wa Kijiji cha Tambani kata ya Tambani wilaya ya Mkuranga.
Kutokana na tishio hilo limesababisha uongozi wa Kijiji hicho kushindwa kwenda baadhi ya maeneo wakihofia maisha yao kutokana na watu hao kutumia silaha mbalimbali za kijadi kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Aliyasema hayo juzi Kijijini hapo alipotembelea kusikiliza kero hiyo ambayo imewafanya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuhama na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao kutokana na hofu ya kuuwawa.   
“Natoa siku tatu kuanzia leo hakikisheni mmewakamata watu hao ambao kwa bahati majina mmnayo hakuna haja ya watu kushindwa kuishi kwa amani nchi hii haijafikia hatua ya watu kushindwa kukaa kwenye maeneo yao au viongozi kuogopa kwenda kwenye eneo lao la utawala,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wananchi wa Kijiji hicho wamekwenda ofisini kwake zaidi ya mara tano wakilalamikia kundi hilo la watu ambao wametajwa kuwa ni kikundi cha watu 15 kabila la Kikurya ambao wanadaiwa kutokea eneo la Msongola wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.
“Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa licha ya kulalamika kwa Jeshi hilo ngazi ya wilaya lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa ambapo hadi sasa watu watatu wameuwawa na kundi hilo la watu ambao ni wavamizi wa ardhi pia wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu wa kuvunja nyumba, kuiba na kufanya vitendo vya ubakaji,” alisema Ndikilo.
“Inashangaza kuona kuwa mgogoro huu wa wavamizi ulianza tangu mwaka 2014 lakini hadi sasa hakuna hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa za kudhibiti kundi hili ambalo ni hatari kwa wananchi ambao hawana hatia na kilio chao lazima kisikilizwe na si kuwaacha walalamike wakati viongozi wapo,” alisema Ndikilo.
Awali mwenyekiti wa Kijiji hicho Amir Mbamba alisema kuwa walishachukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha suala hilo linakomeshwa kwa kulipeleka kwa mkuu wa wilaya lakini kundi hilo bado limeendelea kuendesha matukio hayo bila ya woga.
Mbamba alisema kuwa wananchi wake kutokana na kuona kuwa hawasikilizwi walikwenda kwa Waziri Mkuu pamoja Tume ya Haki za Binadamu ili waweze kusaidiwa tatizo lao na baadaye kwa mkuu wa mkoa ambaye leo umefika kujua ukweli wa tukio hili.
“Wananchi wamesema kuwa wataandamana hadi Ikulu kwa Rais endapo suala lao halitashughulikiwa ipasavyo hivyo kwa kuwa mkuu umekuja mwenyewe ukweli umeupata hatua madhubuti zitasaidia kumaliza mgogoro,” alisema Mbamba.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa watahakikisha kuwa watu hao wanakamatwa na amani itarudi kama ilivyokuwa zamani kwani watajipanga ili kukomesha uhalifu huo.
Mushongi alisema kuwa kwa kuanzia katika kulikabili suala hilo watashirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya Kijiji pamoja na mgambo ili nao washiriki kikamilifu katika kulifuatilia suala hilo ili watu waishi kwa amani bila ya hofu.
Mwisho.

Tuesday, March 1, 2016

RAIA 35 WA ETHIOPIA WADAKWA WAKIISHI NCHINI BILA YA KIBALI


Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia Raia 35 wa Ethiopia baada ya kukamatwa wakituhumiwa kuishi nchini bila ya kibali huku likimsaka David Myovela mkazi wa Kilangalanga wilayani Kibaha kwa tuhuma za kuwahifadhi raia hao.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoani humo Boniventura Mushongi  alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 29 mwaka huu majira ya 5:30 usiku huko Kilangalanga tarafa ya Mlandizi wilaya ya Kibaha.
Kamanda Mushongi alisema kuwa watuhumiwa hao walikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo baada ya taarifa kutolewa na wasamaria wema juu ya kuwepo kwa wageni hao ambao walikuwa hawana kibali cha kuishi nchini.
“Wahamiaji hao haramu waliingia nchini wakitokea Mombasa nchini Kenya kupitia mkoa wa Tanga kwa njia ya barabara huku wakiwa kwenye gari la mizigo aina ya Fuso na Noah na kufikia kwenye nyumba ya mtuhumiwa huyo wakijiandaa kwa safari ya kwenda Afrika ya Kusini,” alisema Mushongi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Tatela Erdadu, Tafesa Tesfaye, Ercuias Hailu, Teseahun Abrahom, Gizochew Bergeno, Meies Kasa, Azole Chebow, Samuel Game, Abtama Falak na Barka Lambamu.
Wengine ni Gazu Abame, Tesk Wark, Gejerm Ababey, Aman Ekdapu, Gadon Hayie, Danak Danel, Tamer Yoanes, Eshey Ayaia , Tasam Ayaia, Tamasoen Dam, Yesak Danei, Gezcho Sugebo, Beramu Make na Abinet Elias.
Aidha aliwataja wengine kuwa ni Mulugeta Abayno, Mehumud Kedery, Mubary Naes, Lmebo Demise, Tamesfen Tadse, Tariku Amato, Tedsue Cueba, Akhelu Moses, Tenekuden Bekeil, Aborome Arizoto, Berhom Kedir ambapo watuhumiwa hao watakabidhiwa kwa idara ya Uhamiaji kwa ajili ya hatua za kisheria.
Mwisho.