Sunday, February 21, 2016

WAZIRI SIMBACHAWENE ALIPA NENO SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imesema kuwa itaangalia upaya uendeshaji wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ili lizalishe liweze kujiendesha kwa ufanisi badala ya kuitegemea serikali ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene alipotembelea Shirika hilo kujionea utendaji kazi wake na na kuongea na wafanyakazi kujua changamoto zinazowakabili na kusema kuwa linapaswa kujiendesha kwa faida na si kuwa tegemezi.
Simbachawene alisema kuwa Shirika hilo la Umma lilianzishwa kwa lengo la kusaidia wananchi hasa wale wa vijijini kwa wakati ule lakini linapasw akubadilika kutokana na wakati na kuacha mifumo ya uendeshaji wa kizamani ambayo haiendani na hali halisi ya wakati uliopo hivyo kushindwa kunufaisha watumishi na wananchi.
“Haiwezekani Shirika kama hili lenye rasilimali na vyanzo vingi vya mapato ikiwa ni pamoja na ardhi kubwa linakuwa na watumishi ambao ni maskini huku wakikosa stahiki zao za kimsingi na kufanya liyumbe ni jambo la kusikitisha sana hivyo serikali itakaa na kuangalia njia za kuweza klirudisha kwenye uhalisia wake,” alisema Simbachawene.
Alisema kuwa Shirika linayumba kw asababu hakuna mipango mikakati ya kujiendesha kisasa kwani maono yake yanaonekana bado ni ya kizamani kwa kuendelea kudeka kwa serikali licha ya kuwa na fursa nyingi zianazolizunguka.
“Mbali ya mfumo wa uendeshaji kuwa na matataizo mengi pia wafanyakazi wamelalamika sana juu ya maslahi yao ikiwa ni pamoja na malipo ya kazi z aziada, kupandishwa madaraja na maslahi mengine nitakuja na majibu ya maswali yenu pia tume itaundwa kila sekta ili kubaini matatizo yaliyopo na kuyafanyia kazi,” alisema Simbachawene.
Kwa upanade wake mwenyekiti wa bodi ya Shirika Patrick Makungu alisema kuwa watazifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wafanyakazi ambazo zinawafanya watumishi washindwe kutoa huduma bora.
Naye mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Dk Cyprian Mpemba alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawafanya washindwe kutoa huduma bora ikiwa ni pamoja na kuwa na mahitaji ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya uendesheaji.
Dk Mpemba alisema kuwa mbali ya changamoto hizo wamepata mafaniko kupitia mfumo wa kieletroniki wa ukusanyaji wa mapato ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi ambayo iko chini ya Shirika hilo kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 3,000,000 toka 300,000 kwa siku.
Waziri alitembelea Hospitali hiyo, aliangalia mfumo wa ukusanyaji mapato wa kieletroniki uliobuniwa na shirika hilo, kampuni ya ufugaji kuku ya Organia, Shirika hilo lilianzishwa miaka zaidi ya 40 iliyopita na nchi za NORDIC likiwa na lengo la kupambana na adui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi na lina wafanyakazi zaidi ya 900 na lina miliki Hospitali ya Tumbi, Chuo cha Waganga wasaidizi, Chuo cha Ufundi Stadi VETA, Shule z a sekondari Kibaha wavulana na Wasichana, Tumbi, shule ya msingi Tumbi na awali     

 MWISHO

MBUNGE AKABIDHI VITABU VYA SAYANSI

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kushoto akimkabidhi kitabu ofisa elimu wa mji wa Halmashauri ya Chalinze Zainab Makwinya kulia na katikati ni mwanfunzi wa shule ya sekondari ya Mdaula Budi Tanganyika  

Na John Gagarini, Chalinze

KATIKA kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi shirika lisilo la Kiserikali la Kulea Childcare Villages la Chalinze  kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete wamekabidhi vitabu 3,438 vyenye thamani ya shilingi milioni 70.
Vitabu hivyo vya Sayansi ni kwa ajili ya wanafunzi wote wa shule za Sekondari na vichache kwa wanafunzi wa Msingi kwa wanafunzi wa Jimbo la Chalinze ili kuwahamsisha kujifunza mambo mbali mbalimbali ya Sayansi.
Akikabidhi vitabu hivyo kwa mwalimu mkuu wa shuke ya Sekondari ya Mdaula Melkisedek Komba, Mbunge wa Jimbo hilo alisema kuwa lengo la kutolewa vitabu hivyo ni kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo hayo ili kupata wataalamu wengi wa Sayansi .
Ridhiwani alisema kuwa masomo ya Sayansi ndiyo yanaotoa wataalamu mbalimbali hivyo wadau wa elimu wanapaswa kutoa hamasa ya kwa wanafunzi kujifunza Sayansi ili waongeze idadi ya wanaosoma kwa lengo la kuwa na wanasayansi wengi.
“Sisi tukiwa ni wadau wa maendeleo tutaendelea kusaidiana na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa tunawahamsisha wanafunzi kuyapenda masomo haya ambayo baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiyaogopa kwa madai kuwa ni magumu hivyo ni vema tukawawekea mazingira ya kuona kuwa ni sawa na masomo mengine,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kama ilivyo kwa shirika la Kulea Childcare ambalo limepata vitabu hivyo toka kwa marafiki zao wa nchini Marekani kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu.
Kwa upande wake mwasisi wa shirika hilo la Kulea Romie Mtenda alisema kuwa shirika lake limekuwa likisaidia sekta ya elimu ambapo hiyo ni mara ya pili kutoa msaada wa vitabu katika Jimbo hilo pia wamekuwa wakitoa misaada ya kielimu.
Mtenda alisema kuwa shirika lao limekuwa likitoa misaada kwa watoto yatima, wajane na watu wasishio kwenye mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kuwasaidiaada, malazi, makazi na huduma nyingine za kijamii.   
Naye mwalimu mkuu wa Mdaula Komba alisema kuwa vitabu hivyo vitasaidia wanafunzi kwa ajili ya kujifunza Sayansi ambayo imekuwa ndiyo somo kuu kwa ajili ya wataalamu ambao wanabuni vitu mbalimbali ambavyo hutumiwa na watu.
Komba alisema kuwa msaada huo umekuja wakati mwafaka kwani wanafunzi wamekuwa na mahitaji ya vitabu vya Sayansi kwa ajili ya kujisomea hivyo vitawasaidia sana kupenda masomo hayo ambayo ni Bioloji, Sayansi na Hesabu. Vitabu hivyo vimetolewa kwa mgawanyo wa tarafa tano ambazo ni Chalinze vitabu 998, Msoga 910, Miono 610, mSata 610 na Kwaruhombo 610.

Mwisho.

Tuesday, February 16, 2016

KATA KUKUTANA NA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Na John Gagarini, Pwani
KATA ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani imeweka mpango wa kukutana na wakulima na wafugaji ili kukabiliana na changamoto za jamii hizo ambazo zimekuwa zikigombana kutokana na wafugaji kudaiwa kulisha mazao mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu diwani wa kata hiyo Hussein Malota alisema kuwa lengo la kukutana na pande hizo ni kujadili jinsi gani ya kukabili changamoto hizo ambazo zimekuwa zikisababisha mapigano.
Malota alisema kuwa wiki tatu zilizopita kulitokea ugomvi baina ya pande hizo mbali baada ya wafugaji kudaiwa kuachia ngombe na kula mazao ya wakulima hali ambayo ili sababisha vurugu za hapa na pale.
“Tayari tumeunda kamati za maridhiano za wakulima watano na wafugaji watano ili kutunga sheria ndogondogo ambazo endapo mmoja atakiuka ataadhibiwa kulingana na makubaliano ya kamati hiyo ili kudhibiti wale watakaokiuka makubaliano hayo,” alisema Malota.
Alisema kuwa tatizo kubwa ni baadhi ya wafugaji wapya wanaoingia kwenye vijiji mbalimbali kwani hawajui taratibu mara waingiapo kwenye maeneo ya wenyeji hali ambayo inasababisha migogoro baina ya pande hizo.
“Tumeunda kamati hizi ili zitunge sheria ambazo zitawaabana wale watakaokiuka kwani wajumbe wa hizo kamati watawajulisha wenzao makubaliano yaliyoafikiwa lengo likiwa ni kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji waishi kwa amani kama jamii moja,” alisema Malota.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine walioiona ni baadhi ya wafugaji kuwaachia watoto wachunge mifugo hiyo ambayo ni makundi makubwa na kushindwa kuyamudu wakati wakichunga na kusababisha matatizo.
Mwisho.

          

MADEREVA BODABODA KUWA NA UTAMBULISHO

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki wilayani Kibaha mkoani Pwani (CHAWAMAPIKI) kimeandaa utaratibu wa kuwa na makoti maalumu ambayo yanayongaa ambayo yatakuwa na namba mgongoni ili kukabiliana na madereva wanaokiuka taratibu za uendeshaji pikipiki.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa chama hicho Hussein Kijazi alisema kuwa kumekuwa na lawama nyingi kwa madereva wa Bodaboda kukiuka taratibu za uendeshaji hali ambayo inaweza kuchangia kuongezeka kwa ajali.
Kijazi alisema kuwa ili kuwadhibiti madereva wanaokiuka taratibu wameona bora waanzishe utaratibu huo ili iwe rahisi kuwabaini wale wanokwenda kinyume cha sheria na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Utaratibu huu tunatarajia utaanza wakati wowote kuanzia sasa kwani kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa watu mbalimbali wakilalamika kuwa madereva hao wanavunja sheria na kuwa moja ya chanzo cha ajali,” alisema Kijazi.
Alisema kuwa mtu akiona kuna tataizo kwa dereva fulani anataja tu namba na wao watafuatilia ni dereva gani mwenye hiyo namba kisha chama kitamwita na kumpa adhabu inayostahili kutokana na kosa lake.
“Makoti hayo yanayongaa hata nyakati za usiku yatatusaidia kuwabaini madereva wanaokiuka utartibu wetu ambao tumejiwekea kwani baadhi ya watu wanalalamika kuwa madereva wengine wanajihusisha na vitendo vya uhalifu lakini wakiwa na makoti hayo itakuwa ni vigumu kuvunja taratibu kwani lazima watajulikana na wataadhibiwa,” alisema Kijazi.
Aidha wameipongeza serikali kwa kufuta baadhi ya kodi zikiwemo zile za TRA 90,000, Motor Vehicle 50,000 na kodi ambazo zilikuwa ni kero kwao. Chama hicho kinawanachama 400 na wamiliki zaidi ya 100 na wana vituo 13 na kina lengo la kusaidia wakati wa matatizo ikiwa ni pamoja na kufiwa.
Mwisho.

WAUZA MAJI WANAWAKE KWENYE MAGARI WAILILIA HALMASHAURI KUVUNJA VIBANDA VYAO

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wanawake  wanaouza Maji ya kunywa kwenye magari  ilipokuwa mizani ya zamani ya Maili Moja wilayani Kibaha wameilalamikia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa kuwavunjia vibanda vyao kwa madai kuwa ni uchafu licha ya kuwa wanakusanya ushuru kwao.
Moja ya wafanyabiashara hao ambao ni Veronica Damiani akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa wanashangaa Halmashauri hiyo kuwavunjia vibanda vyao bila ya kuwaandikia barua ya kuwataka wasifanye biashara zao.
Damiani alisema kuwa wao wanajua serikali kabla ya kufanya kitu lazima itoe taarifa ya maandishi kabla ya kufanya jambo lolote lakini wao wanashangaa kuondolewa bila ya kupewa barua ya kuwahamisha katika eneo hilo.
“Sisi hatukatai kuondoka ila wangetupa taarifa juu ya kututaka tuondoke katika eneo hili na siku chache zilizopita walikuja wakatuambia kuwa tuendelee na biashara wakati majadiliano yanaendelea lakini tunashangaa jana wamekuja na migambo na kutubomolea vibanda vyetu huku wakitupa masaa matatu kwa ajili ya kuhama,” alisema Damiani.
Alisema kuwa sasa wao watenda wapi kufanya biashara kwani maji wanayouza wengine wamekopa mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa lengo la kujipatia kipato chao na familia zao ambapo wengine ni wajane.
“Tunakopa fedha kwa ajili ya kufanyabiashara hizi sasa tutarejeshaje fedha tulizokopa tunaomba viongozi wa ngazi za juu watuangalie kwa jicho la huruma hatuna kipato kingine zaidi ya biashara hizi ambazo zinatusaidia kuwasomesha watoto wetu kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo,” alisema Damiani.
Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dismas Marango akijibu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Gladys Dyamvunye alisema kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakifanyabiashara zao kimakosa kwani hawakuwa na kibali chakufanyia biashara kwenye eneo hilo.
Marango alisema kuwa hawakuwapa barua kwani sehemu hiyo si kwa ajili ya kufanyabiashara na kwamba mabanda hayo yanaonekana kama uchafu na waliwapa taarifa kwa maneno wiki tatu zilizopita za kuwataka waondoke kwenye eneo hilo.
Mwisho.

NGO ZATAKIWA ZISIJIINGIZE KWENYE SIASA

Na John Gagarini, Kibaha
MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali wilayani Kibaha mkoani Pwani yametakiwa kutojiingiza kwenye masuala ya kisiasa badala yake wajikite katika kuwaletea wananchi maendeleo kama yalivyoandikishwa kwenye maeneo yao husika.
Akizungumza mjini Kiabaha kwwenye Jukwaa la Uwajibikaji kwa asasi isiyo ya kiserikali ya kitaifa ya ushirikiano wa Maendeleo kwa Vijana (YPC) mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa mashirika kama hayo endapo yatajihusisha na siasa yatafutwa.
Kihemba alisema kuwa mashirika hayo yalianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi katika masuala ya kimaendeleo na si kujihusisha na siasa kama baadhi yanavyofanya kwa kujiingiza kwenye siasa.
“Msijiingize kwenye siasa bali mnapaswa mshirikiane na serikali katika kukabiliana na changamoto lakini endapo mtaingia kwenye siasa mnaweza kuathiri utendaji kazi wenu na tutayafuta yale ambayo yanajiingiza kwenye siasa kwani vyama vya siasa ndiyo vinapaswa kushiriki siyo nyie kwani kazi yenu ni maendeleo,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa shirika hilo limefanya kazi kubwa kuwahamasisha vijana kushiriki kwenye kuwania nafasi za uongozi pamoja na kuwajengea uwezo wa uwajibikaji ni vema wakaendelea na shughuli za kimaendeleo kwa kuwaonyesha wananchi fursa za maendeleo kwani wao ni wabia.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mwenyekiti wa bodi ya YPC Mkuku Mlongecha alisema kuwa asasi yao haijihusishi na masuala ya kisiasa bali ni kuwajengea uwezo vijana kushiriki kwenye shughuli za maendeleo pamoja na uongozi.
Mlongecha alisema kuwa malengo mengine ni kuwajengea uwezo wa kisiasa, kijamii, uchumi, kujitolea pamoja na mafunzo kwa vijana ambapo asilimia zaidi ya 70 ya madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji ni vijana.
Mwisho.

MASHAMBAPORI YARUDI SERIKALINI


Na John Gagarini, Kibaha
KATIKA kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kuwanyanganya watu wasioendeleza mashamba kwenye wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imerudisha mashamba 17 serikalini ambayo yatatumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba wakati wa kuzindua Jukwaa la Uwajibikaji kwa Asasi ya Kitaifa ya Ushirikiano wa Maendeleo  ya Vijana (YPC) ya mkoa wa Pwani na kusema kuwa mashamba hayo pia yatatumika kwa ajili ya makazi.
Kihemba alisema kuwa mashamba hayo yalikuwa kero kwa wananchi kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu na wamiliki licha ya kutakiwa kuyaendeleza kisheria lakini wameshindwa na kuyafanya mapori makubwa.
“Baadhi ya mashamba yamerudishwa serikalini kama tulivyoagizwa na tutahakikisha tunayapima kwa ajili ya viwanda ili kuweza kuimarisha uchumi wa wakazi wa wilaya ya Kibaha pia sehemu yatapimwa kwa ajili ya makazi,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa maeneo hayo yaliyorejeshwa hayapaswi kuvamiwa kwani kuna taarifa baadhi ya watu wameanza kuyavamia mashamba hayo jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwani yatatumiwa kwa mipango itakayokuwa imepangwa na si kwa watu kuyavamia.
“Ni marufuku watu kuyavamia maeneo hayo ambayo yalirejeshwa serikalini na kwa wale watakaojenga nyumba zao zitabomolewa wanachotakiwa ni kusubiri utaratibu utakaowekwa na serikali na si kujichukulia kinyume cha sheria,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imepania kuinua uchumi wa Watanzania kupitia viwanda ili wawe na uchumi wa kati ni vema na wao wakaunga mkono mpango huo kwa kuanzisha viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwisho.