Tuesday, February 16, 2016

KATA KUKUTANA NA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Na John Gagarini, Pwani
KATA ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani imeweka mpango wa kukutana na wakulima na wafugaji ili kukabiliana na changamoto za jamii hizo ambazo zimekuwa zikigombana kutokana na wafugaji kudaiwa kulisha mazao mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu diwani wa kata hiyo Hussein Malota alisema kuwa lengo la kukutana na pande hizo ni kujadili jinsi gani ya kukabili changamoto hizo ambazo zimekuwa zikisababisha mapigano.
Malota alisema kuwa wiki tatu zilizopita kulitokea ugomvi baina ya pande hizo mbali baada ya wafugaji kudaiwa kuachia ngombe na kula mazao ya wakulima hali ambayo ili sababisha vurugu za hapa na pale.
“Tayari tumeunda kamati za maridhiano za wakulima watano na wafugaji watano ili kutunga sheria ndogondogo ambazo endapo mmoja atakiuka ataadhibiwa kulingana na makubaliano ya kamati hiyo ili kudhibiti wale watakaokiuka makubaliano hayo,” alisema Malota.
Alisema kuwa tatizo kubwa ni baadhi ya wafugaji wapya wanaoingia kwenye vijiji mbalimbali kwani hawajui taratibu mara waingiapo kwenye maeneo ya wenyeji hali ambayo inasababisha migogoro baina ya pande hizo.
“Tumeunda kamati hizi ili zitunge sheria ambazo zitawaabana wale watakaokiuka kwani wajumbe wa hizo kamati watawajulisha wenzao makubaliano yaliyoafikiwa lengo likiwa ni kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji waishi kwa amani kama jamii moja,” alisema Malota.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine walioiona ni baadhi ya wafugaji kuwaachia watoto wachunge mifugo hiyo ambayo ni makundi makubwa na kushindwa kuyamudu wakati wakichunga na kusababisha matatizo.
Mwisho.

          

MADEREVA BODABODA KUWA NA UTAMBULISHO

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki wilayani Kibaha mkoani Pwani (CHAWAMAPIKI) kimeandaa utaratibu wa kuwa na makoti maalumu ambayo yanayongaa ambayo yatakuwa na namba mgongoni ili kukabiliana na madereva wanaokiuka taratibu za uendeshaji pikipiki.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa chama hicho Hussein Kijazi alisema kuwa kumekuwa na lawama nyingi kwa madereva wa Bodaboda kukiuka taratibu za uendeshaji hali ambayo inaweza kuchangia kuongezeka kwa ajali.
Kijazi alisema kuwa ili kuwadhibiti madereva wanaokiuka taratibu wameona bora waanzishe utaratibu huo ili iwe rahisi kuwabaini wale wanokwenda kinyume cha sheria na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Utaratibu huu tunatarajia utaanza wakati wowote kuanzia sasa kwani kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa watu mbalimbali wakilalamika kuwa madereva hao wanavunja sheria na kuwa moja ya chanzo cha ajali,” alisema Kijazi.
Alisema kuwa mtu akiona kuna tataizo kwa dereva fulani anataja tu namba na wao watafuatilia ni dereva gani mwenye hiyo namba kisha chama kitamwita na kumpa adhabu inayostahili kutokana na kosa lake.
“Makoti hayo yanayongaa hata nyakati za usiku yatatusaidia kuwabaini madereva wanaokiuka utartibu wetu ambao tumejiwekea kwani baadhi ya watu wanalalamika kuwa madereva wengine wanajihusisha na vitendo vya uhalifu lakini wakiwa na makoti hayo itakuwa ni vigumu kuvunja taratibu kwani lazima watajulikana na wataadhibiwa,” alisema Kijazi.
Aidha wameipongeza serikali kwa kufuta baadhi ya kodi zikiwemo zile za TRA 90,000, Motor Vehicle 50,000 na kodi ambazo zilikuwa ni kero kwao. Chama hicho kinawanachama 400 na wamiliki zaidi ya 100 na wana vituo 13 na kina lengo la kusaidia wakati wa matatizo ikiwa ni pamoja na kufiwa.
Mwisho.

WAUZA MAJI WANAWAKE KWENYE MAGARI WAILILIA HALMASHAURI KUVUNJA VIBANDA VYAO

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wanawake  wanaouza Maji ya kunywa kwenye magari  ilipokuwa mizani ya zamani ya Maili Moja wilayani Kibaha wameilalamikia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa kuwavunjia vibanda vyao kwa madai kuwa ni uchafu licha ya kuwa wanakusanya ushuru kwao.
Moja ya wafanyabiashara hao ambao ni Veronica Damiani akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa wanashangaa Halmashauri hiyo kuwavunjia vibanda vyao bila ya kuwaandikia barua ya kuwataka wasifanye biashara zao.
Damiani alisema kuwa wao wanajua serikali kabla ya kufanya kitu lazima itoe taarifa ya maandishi kabla ya kufanya jambo lolote lakini wao wanashangaa kuondolewa bila ya kupewa barua ya kuwahamisha katika eneo hilo.
“Sisi hatukatai kuondoka ila wangetupa taarifa juu ya kututaka tuondoke katika eneo hili na siku chache zilizopita walikuja wakatuambia kuwa tuendelee na biashara wakati majadiliano yanaendelea lakini tunashangaa jana wamekuja na migambo na kutubomolea vibanda vyetu huku wakitupa masaa matatu kwa ajili ya kuhama,” alisema Damiani.
Alisema kuwa sasa wao watenda wapi kufanya biashara kwani maji wanayouza wengine wamekopa mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa lengo la kujipatia kipato chao na familia zao ambapo wengine ni wajane.
“Tunakopa fedha kwa ajili ya kufanyabiashara hizi sasa tutarejeshaje fedha tulizokopa tunaomba viongozi wa ngazi za juu watuangalie kwa jicho la huruma hatuna kipato kingine zaidi ya biashara hizi ambazo zinatusaidia kuwasomesha watoto wetu kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo,” alisema Damiani.
Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dismas Marango akijibu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Gladys Dyamvunye alisema kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakifanyabiashara zao kimakosa kwani hawakuwa na kibali chakufanyia biashara kwenye eneo hilo.
Marango alisema kuwa hawakuwapa barua kwani sehemu hiyo si kwa ajili ya kufanyabiashara na kwamba mabanda hayo yanaonekana kama uchafu na waliwapa taarifa kwa maneno wiki tatu zilizopita za kuwataka waondoke kwenye eneo hilo.
Mwisho.

NGO ZATAKIWA ZISIJIINGIZE KWENYE SIASA

Na John Gagarini, Kibaha
MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali wilayani Kibaha mkoani Pwani yametakiwa kutojiingiza kwenye masuala ya kisiasa badala yake wajikite katika kuwaletea wananchi maendeleo kama yalivyoandikishwa kwenye maeneo yao husika.
Akizungumza mjini Kiabaha kwwenye Jukwaa la Uwajibikaji kwa asasi isiyo ya kiserikali ya kitaifa ya ushirikiano wa Maendeleo kwa Vijana (YPC) mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa mashirika kama hayo endapo yatajihusisha na siasa yatafutwa.
Kihemba alisema kuwa mashirika hayo yalianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi katika masuala ya kimaendeleo na si kujihusisha na siasa kama baadhi yanavyofanya kwa kujiingiza kwenye siasa.
“Msijiingize kwenye siasa bali mnapaswa mshirikiane na serikali katika kukabiliana na changamoto lakini endapo mtaingia kwenye siasa mnaweza kuathiri utendaji kazi wenu na tutayafuta yale ambayo yanajiingiza kwenye siasa kwani vyama vya siasa ndiyo vinapaswa kushiriki siyo nyie kwani kazi yenu ni maendeleo,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa shirika hilo limefanya kazi kubwa kuwahamasisha vijana kushiriki kwenye kuwania nafasi za uongozi pamoja na kuwajengea uwezo wa uwajibikaji ni vema wakaendelea na shughuli za kimaendeleo kwa kuwaonyesha wananchi fursa za maendeleo kwani wao ni wabia.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mwenyekiti wa bodi ya YPC Mkuku Mlongecha alisema kuwa asasi yao haijihusishi na masuala ya kisiasa bali ni kuwajengea uwezo vijana kushiriki kwenye shughuli za maendeleo pamoja na uongozi.
Mlongecha alisema kuwa malengo mengine ni kuwajengea uwezo wa kisiasa, kijamii, uchumi, kujitolea pamoja na mafunzo kwa vijana ambapo asilimia zaidi ya 70 ya madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji ni vijana.
Mwisho.

MASHAMBAPORI YARUDI SERIKALINI


Na John Gagarini, Kibaha
KATIKA kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kuwanyanganya watu wasioendeleza mashamba kwenye wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imerudisha mashamba 17 serikalini ambayo yatatumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba wakati wa kuzindua Jukwaa la Uwajibikaji kwa Asasi ya Kitaifa ya Ushirikiano wa Maendeleo  ya Vijana (YPC) ya mkoa wa Pwani na kusema kuwa mashamba hayo pia yatatumika kwa ajili ya makazi.
Kihemba alisema kuwa mashamba hayo yalikuwa kero kwa wananchi kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu na wamiliki licha ya kutakiwa kuyaendeleza kisheria lakini wameshindwa na kuyafanya mapori makubwa.
“Baadhi ya mashamba yamerudishwa serikalini kama tulivyoagizwa na tutahakikisha tunayapima kwa ajili ya viwanda ili kuweza kuimarisha uchumi wa wakazi wa wilaya ya Kibaha pia sehemu yatapimwa kwa ajili ya makazi,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa maeneo hayo yaliyorejeshwa hayapaswi kuvamiwa kwani kuna taarifa baadhi ya watu wameanza kuyavamia mashamba hayo jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwani yatatumiwa kwa mipango itakayokuwa imepangwa na si kwa watu kuyavamia.
“Ni marufuku watu kuyavamia maeneo hayo ambayo yalirejeshwa serikalini na kwa wale watakaojenga nyumba zao zitabomolewa wanachotakiwa ni kusubiri utaratibu utakaowekwa na serikali na si kujichukulia kinyume cha sheria,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imepania kuinua uchumi wa Watanzania kupitia viwanda ili wawe na uchumi wa kati ni vema na wao wakaunga mkono mpango huo kwa kuanzisha viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwisho.

MADIWANI KUHAKIKI MAPATO YA STENDI

Na John Gagarini, Kibaha
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha wanatarajiwa kusimamia utaratibu wa mapato kwenye stendi kuu ya mabasi ya Maili Moja ili kuhakiki ni magari mangapi ya abiria yanayolipa ushuru kwenye stendi hiyo.
Utaratibu huo ulipitishwa kwenye baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo ukiwa na lengo la kuhakikisha kuwa fedha zinazopatikana kwenye chanzo hicho kikubwa cha mapato cha Halmashauri hiyo.
Akizungumza kwenye kikao hicho mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Leonard Mloe alisema kuwa madiwani hao watakaa kituoni hapo ili kupata ukweli wa magari mangapi yanayolipa ushuru yanapopita hapo stendi.
“Tumeamua kufanya hivyo kwani mapato yanayopatikana kwa sasa hayana usahihi kwani idadi ya magari yanayolipa ushuru ni machache huku magari yanayopita hapo ni kubwa hivyo kukaa hapo kutatusaidia kujua ukweli wa mapato halisi ya stendi,” alisema Mlowe.
Mlowe alisema kuwa wanataka wakadirie mapto kwa uhakika na si kubahatisha kwani kwa sasa hawaridhiki na mapato yanayopatikana kwa sasa hivyo wameamua madiwani wake hapo ili kupata majibu sahihi.
“Hichi ni moja ya chanzo chetu cha mapato cha uhakika hivyo lazima tujue tunapata nini na kujua ni magari ya abiria ni mangapi yanayolipa ushuru wa stendi kwani iatatusadia kuwa na uhakika wa mapato ya chanzo hicho,” alisema Mloe.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Tumbi Hemed Chanyika alisema kuwa mapato ya stendi hayafahamiki undani wake kwani inaonekana baadhi ya watu wanatumia risiti feki za ushuru wa stendi kujinufaisha.
Chanyika alisema kuwa kwa madiwani hao kukaa hapo itasaidia sana kwani idadi ya magari ya abiria yanayoingia na kutoka kwenye stendi hiyo ambapo mabasi madogo yanalipia kiasi cha shilingi 500 na makubwa 1,000 kila yanapoingia na kutoka.
Mwisho.

Sunday, February 14, 2016

MAMA AMFANYIA UKATILI MWANAE WA KAMBO AMVUTA SEHEMU ZA SIRI


Na John Gagarini, Kibaha
SHEILA Husein mkazi wa Janga Kata ya Janga Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani amejikuta matatani baada ya kumpiga mtoto wake wa kambo wa kiume mwenye umri wa miaka (2) na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili ikiwa ni pamoja na kumvuta sehemu zake za siri.
Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa Mtaa wa Janga na Diwani wa kata hiyo Chande Mwalika alisema kuwa mtoto huyo amekuwa akipigwa kila siku kwa fimbo hali ambayo imemfanya awe na makovu mengi mwilini.
Mwalika alisema kuwa moja ya majirani ambaye alishindwa kuvumilia vitendo hivyo Adinani Mkupa nakutoa taarifa hiyo alisema kuwa vitendo vilivyokuwa vikifanywa na mtuhumiwa huyo ni vya kikatili na haviwezi kuvumilika.
“Amekuwa akimchapa mwanae kwa fimbo bila ya kumuonea huruma hali ambayo imemfanya mtoto huyo aharibike mwili mzima kutokana na vipigo hivyo na kibaya zaidi ni pale alipofikia hatua ya kumvuta sehemu zake za siri na hakuna sababu maalumu inayomfanya amwazibu mtoto huyo kwani bado ni mdogo sana na hana uwezo wa kuongea,” alisema Mwalika.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo ilibidi watoe ripoti kwa kwenye uongozi wa kata kwa ajili ya hatua zaidi kwa mtuhumiwa ambaye ni mama wa nyumbani huku mumewe aliyetajwa kwa jina moja la Abdul akiwa ni mfanyabiashara kwenye magulio.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kata ya Janga Michael Mwakamo alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo ilibidi mgambo wapelekwe nyumbani kwa mtuhumiwa kwa ajili ya kumchukua kwa ajili ya kutoa maelezo ni kwanini anamtesa mtoto huyo.
Mwakamo alisema kuwa mtuhumiwa huyo alichukuliwa na kwenda ofisini hapo na baada ya mahojiano ilibidi apelekwe polisi kwa hatua zaidi na baada ya mahojiano kukamilika alipelekwa Mahakama ya Mwanzo ya Mlandizi.
“Tulimuuliza ni kwani ni anamfanyia vitendo vya ukatili mtoto wake huyo wa kambo alijibu kuwa hata mumewe humpiga mtoto huyo hivyo nay eye akaona afanye hivyo lakini hakuna sababu nyingine ya yeye kumchapa kupita kiwango mtoto huyo;” alisema Mwakamo.
Hakimu wa mahakama ya Mwanzo ya Mlandizi Sharifa Mtumuya alimsomea mashitaka ya shambulio ambapo mtuhumiwa alikana shitaka hilo na kupelekwa mahabusu baada ya taratibu za dhamana kushindikana na kesi hiyo itasikilizwa tena Februari 16 mwaka huu.
Mahakama iliamuru mtoto huyo akae kwa ofisa kilimo wa kata ya Janga Neema Sonje hadi itakapoamuliwa vingine wakati kesi hiyo ikiwa inaendelea kwani haitawezekana kuendelea kukaa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
Mwisho.      
Na Mwandishi Wetu, Kibaha

MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewaonya baadhi ya  madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuacha mara moja tabia ya kumtishia kumfukuza kazi  Mkurugenzi  Mtendaji wa Mji huo pamoja na Mweka Hazina wake kwa madai kwamba amekataa kulipa deni la shilingi milioni 231 la mkandarasi mmoja  anayayetoa huduma mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa mji huo mkuu huyo wa mkoa aalisema kuwa anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya madiwani hao wa kusimamia halmashauri ili iweze kufanya kazi kwa makini na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi na  badala  yake wanafanya kazi ya kuihujumu halmashauri kwa maslahi yao binafsi.

Ndikilo alisema kuwa madiwani hao badala ya kushinikiza Halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo lakini wamekuwa wakiwapigia debe watoa huduma na kuwatisha watendaji.

“Shutuma ya baadhi ya madiwani kuhujumu halmashauri hiyo kwa kuwatishia kuwaazimia watendahi  wakuu wa mji huo kuwafukuza kazi kwa madai kwamba wamekataa  kulipa deni la shilingi milioni 231 ambazo halmashauri hiyo inadaiwa na mkandarasi mmoja anayetoa huduma ndani ya mji wa Kibaha haipendezi na wanapaswa kuangalia wajibu wao wa kuwatumikia wananchi;” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa si vema kuegemea kwa mtoa huduma wanapaswa kuacha mara moja tabia ya kuwatishia watendaji ambao wamekataa kulipa deni la mzabuni huyo
na kuacha kuingiza maslahi binafisi katika utendeji wa kazi na badala yake watimize wajibu wao wa kuisimamia halmashauri.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo Leonard Mloe alikiri kuwepo kwa taarifa za baadhi ya madiwani kutaka waungwe mkono kuweka maazimio ya kumfukuza kazi mweka hazina wa mji wa kibaha kwa kukataa kuizinisha malipo hayo.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM mkoa wa Pwani kimempongeza Rais wa awamu ya Tano Dk John Pombe Magufuli kwa kuweza kuzuia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuwabana wakwepa kodi na kuliingizia Taifa mapato yanayozidi kiasi cha trilioni tatu kwa kipindi chake cha siku 100 madarakani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu cha mkoa huo katibu mwenezi wa CCM mkoa Dk Zainab Gama akisoma tamko la mkoa kuhusu utendaji kazi wa Rais Magufuli alisema kuwa ni wa kutukuka.

Dk Gama alisema kuwa Rais ameweza kubana matumizi ya serikali na kufanikisha nchi kupata fedha nyingi ikiwa ni pamoja na kupunguza safari za nje kwa viongozi hivyo kuiwezesha serikali kubana matumizi yasiyo ya lazima ya shilingi bilioni 7 ambazo zitatumika kwenye miradi ya maendeleo.

“Jambo linguine ni kubadilisha mfumo wa sherehe za Kitaifa uliyokuwa unatumia gharama kubwa na badala yake siku za sherehe hizo ni kufanya usafi wa mazingira kote nchini;” alisema Dk Gama.

Alisema kuwa katika kuonyesha dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi aliteua baraza dogo la mawaziri ambao ni makini na hata baada ya kuteuliwa tayari wameanza kazi kwa kasi kubwa inayoendana na kauli Mbiu yake ya Hapa Kazi Tu.

“Tunaunga mkono dhamira yake ya dhati ya kuinua uchumi kuwa wa kati kwa kusisitiza kujenga viwanda na pia kuboresha mtandao wa barabara za juu katika Jiji la Dar es Salaam Fly Overs pamoja na barabara za njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze,” alisema Dk Gama.

Aidha alisema kuwa katika kipindi hicho aliweza kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji wabovu katika taasisi mbalimbali za serikali ambazo walisababisha wananchi kuichukia serikali yao/
Awali akifungua kikao hicho mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao alisema kuwa katika uchaguzi ujao wa Chama utakaofanyika mwakani viongozi wanaoteua wagombea wanapaaswa kuwa makini ili kupata viongozi bora.

Mlao alisema kuwa viongozi wanaoteuliwa kukisimamia chama wanapaswa kuwa na uwezo na si mradi tu ambao baadaye wanakuja kufanya chama kinapata wakati mgumu wakati wa uchaguzi mkuu.

Mwisho.