Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani umepokea kiasi cha shilingi milioni 579.5 kwa
ajili ya utekelezaji wa dhana ya elimu bure kwa wanafunzi wa shule za Msingi na
Sekondari.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini
Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa fedha hizo
zimetolewa na Serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Ndikilo alisema kuwa fedha hizo tayari zimetumwa kwenye
akaunti za shule hizo ambapo kwa shule za Msingi zimepokea kiasi cha shilingi
milioni 167,297,00 na sekondari wamepewa kiasi cha shilingi milioni
412,249,000.
“Fedha hizo ni kwa ajili ya maendeleo ya shule ikiwa ni
pamoja na ada, chakula ,gharama za mitihani na gharama nyingine ambazo
zimetolewa maelekezo kwa walimu wakuu,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa fedha hizo zitasimamiwa na mkoa ambapo mwalimu
mkuu yoyote atakayetumia kinyume cha utaratibu kwa ubadhirifu atachukuliwa
hatua kali za kisheria.
“Walimu wakuu, Wakurugenzi wa Halmashauri na wakuu wa Wilaya
wanatakiwa kukiri kwa maandishi mara watakapoziona fedha hizo kwenye akaunti
zao,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa kutokana na kutolewa fedha hizo walimu
wakuu hawatakiwi kutoza mchango wa aina yoyotea kama vile ulinzi, maji, umeme
na michango mingine kwani fedha hizo zitatumika kwenye masuala yote.
“Michango yoyote kwa wadau kama watakuwa wamekubaliana lazima
wapate kibali cha Waziri wa TAMISEMI kupitia mkuu wa mkoa ili kuchangisha
michango kwa wananchi ambapo mkoa wetu una jumla ya shule za msingi 553 na
sekondari 108,” alisema Ndikilo.
Mwisho.