Tuesday, January 5, 2016

WALIOTELEKEZA VIWANJA VYA KITOVU CHA MJI WAPEWA MIEZI SITA KUVIENDELEZA

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha imetoa muda wa miezi sita kwa watu walionunua viwanja kwenye kitovu cha mji kujenga kama sheria za ujenzi vinavyoonyesha na kwa sasa hawatakuwa tena na majadiliano kwa watakaoshindwa kujenga watanyanganywa viuwanja hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua ambazo watachukua kwa watu walioshndwa kuendeleza viwanja hivyo tangu walipovinunua mwaka 2010 ofisa ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Edward Mbala alisema kuwa watu hao walipew ahadi mwaka 2015 wawe wamejenga.
Mbala alisema kuwa licha ya kupewa muda wote huo lakini watu hao wameshindwa kujenga hadi sasa licha ya kuwa na maongezi ya mara kwa mara kati ya Halmashauri na wawekezaji hao mara kwa mara lakini hadi sasa wameshindwa kuyaendeleza maeneo hayo.
“Mara ya mwisho tuliwaita Aprili mwaka jana lakini walisema kuwa tatizo kubwa lililowafanya washindwe kuanza ujenzi kwenye viwanja hivyo ni hadi pale Halmashauri itakapokuwa imefanya ujenzi wa Stendi na Soko jambao ambalo tuliwaambia kuwa wao waendelee na ujenzi huku sisi tukitafuta wabia kwa ajili ya ujenzi wa vitu hivyo,” alisema Mbala.
Alisema tayari wameshapata benki ambayo itawakopesha kwa ajili ya ujenzi wa soko pamoja na stendi ambapo zaidi ya bilioni 20 zinatarajiwa kutumika kujenga miuondombinu hiyo hivyo wale walionunua viwanja waanze ujenzi.
“Tumesha waambia wayaendeleze maeneo hayo na tayari tumewapa miezi  sita kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo na endapo watashindwa kujenga sheria itachukua mkondo wake kwa kuwanyanganya na kuwapa wengine,” alisema Mbala.
Aidha alisema kuwa tayari wameshatoa matangazo sehemu mbalimbali na kwa wamiliki hao ili waendeleze maeneo yao ambayo ndiyo yanaonyesha sura ya mji  wa Kibaha lakini kwa sasa maeneo hayo bado ni vichaka.
Mwisho.

Sunday, January 3, 2016

KIBAHA KUJENGA STENDI NA SOKO

Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unatarajia kujenga Kituo Kikubwa cha Mabasi pamoja na Soko baada ya kupata mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 20 toka Benki ya Uwekezaji ya (TIB) na kuufanya mji wa Kibaha kuwa wakisasa.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Pwani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo na kusema kuwa kwa sasa taratibu zinaendelea baina ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha na benki hiyo.

Ndikilo alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa mara taratibu za kitaalamu zitakapokamilika ambapo kwa sasa bado zinaendelea ikiwa ni pamoja na kupata kibali .

“Tunatarajia kuwa na stendi ya kisasa ambayo thamani yake itakuwa ni shilingi bilioni 20 pamoja na soko litakalokuwa na thamani ya shilingi bilioni 9 hasa ikizingatiwa mkoa ulikuwa hauna soko kubwa bali lililopo ni dogo na halina uwezo wa kuchukua bidhaa nyingi,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa wafanyabiashara wa mkoa wa Pwani hususani wale wa makao makuu ya mkoa Maili Moja na vitongoji vyake huwalazimu kwenda kununua bidhaa Kariakoo au kwenye masoko mengine Jijini Dar es Salaam jambo ambalo linafanya bei za bidhaa kuwa juu.

“Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa ni kama malango wa Jiji la Dar es Salaam lakini bidhaa zimekuwa zikipita hapa na kwenda huko kisha wafanyabiashara kwenda kununua na kuzirudisha hapa hivyo kupandisha bei kutokana na gharama kuwa kubwa,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa soko hilo ambalo litajengwa sambamba na stendi litakuwa la kisasa ambapo magari yatakuwa na uwezo wa kuingia na kushusha bidhaa na si kama ilivyo sasa ambapo kutokana na udogo wa soko lililopo hubidi magari ya bidhaa yashindwe kuingia.

Mwisho.
  

   


Saturday, January 2, 2016

MKULIMA AOKOTA BOMU LA KUTUPWA KWA MKONO

Na John Gagarini, Kibaha
MKULIMA wa Mtaa wa Sagare wilayani Kibaha mkoani Pwani Hassan Omary ameokota bomu la kutupwa kwa mkono  ambalo lilisahaulika wakati wa Operesheni Tokomeza iliyofanyika nchini Julai mwaka 2015.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonventura Mushongi alisema bomu hilo lilisahaulika wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo la kukamata wahalifu mbalimbali waliokuwa wakiiba Maliasili za nchi.
Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 31 mwaka 2015 majira ya saa 5 asubuhi wakati mke wa Omary alipokuwa akilima aligonga kitu kigumu cha chuma na alipokitoa aliona kitu kama bomu na kumwita mumewe aliye waita watu wakiwemo viongozi wa mtaa huo.
“Baada ya kuona hivyo Omary alitoa taarifa polisi na kusema kuwa wameona bomu ndipo polisi walipofika na kubaini kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono ambalo fuse yake ili haribika,” alisema Mushongi.
“Halikuweza kulipuka lakini endapo lingepata joto kali mfano joto la moto lingeweza kulipuka lakini hata hivyo tumeshukuru Mungu kuwa halikuweza kulipuka kwa muda wote huo kwnai endapo lingelipuka lingeweza kuleta madhara,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa baadaye ilibainika kuwa inawezekana bomu hilo la kutupwa kwa mkono liliachwa kwa bahati mbaya  wakati wa Operesheni Tokomeza iliyofanyika Julai mwaka jana.
“Kwa kushirikiana na jeshi letu tutalipelekwa kwa wataalamu wa mabomu ambao ni Jeshi la wananchi (JWTZ) kwa ajili ya kujua zaidi kuhusiana na bomu hilo ikiwa ni pamoja na kuliharibu ili lisiweze kuleta madhara,” alisema Mushongi.
Awali mwenyekiti wa mtaa wa Sagale Bernego alisema kuwa mama huyo alikuwa akisafisha shamba kwenye eneo la Omary ambalo limekuwa likichimbwa vitu vilivyoachwa zamani na watawala wa Kijerumani na Kiarabu maarufu kama Tunu.
Bernego alisema kuwa machimbo hayo ya Tunu yalikuwa yakifanywa na mmiliki huyo ambapo eneo hilo lilizua utata miaka michache iliyopita kwani kumekuwa na mambo ya miujiza yamekuwa yakitokea kwenye machimbo hayo.
Mwisho.        


DEREVA BODABODA ACHOMWA KISU AFA WALIKUWA WAKIGOMBEA MWANAMKE

Na John Gagarini, Kibaha
DEREVA Bodaboda Ally Kasimu (23) mkazi wa Kilimahewa wilayani Kibaha mkoani Pwani amefariki dunia kwa kuchomwa kisu na waendesha pikipiki wenzake wakati wakigombea mwakanamke.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa wa Mtakuja kata ya Pangani, Ramadhan Mwaya alisema kuwa marehemu alikufa wakati wa mkesha wa kukaribisha mwaka mpaya wa 2016 na kuaga mwaka 2015.
Mwaya alisema kuwa marehemu alikutwa na umauti huo akiwa amekaa pembeni na pikipiki yake huku wenzake wakimgombea mwanamke kisha kumchoma yeye kutokana na ugomvi wa wenzake waliokuwa wakigombana.
“Madereva hao pamoja na watu wengine walikuwa kwenye sherehe hizo ambazo ziliandaliwa na Halima Kitwana ambazo ziliambatana na muziki maarufu Kigodoro ulianza majira ya saa 2 usiku na baada ya muziki kwisha baada ya saa sita kamili waliondoka lakini baadaye walionekana kumgombea mwanamke ndipo walipomchoma mwenzao,” alisema Mwaya.
Alisema kuwa marehemu alichomwa kisu sehemu ya tumboni na kujeruhiwa vibaya ambapo walijaribu kumkimbiza hospitali ya Rufaa ya Mkoa  ya Tumbi kwa ajili ya matibabu lakini alifariki wakiwa njiani.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonventura Mushongi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa watu waliohusika na tukio hilo walikimbia na wanaendelea kutafutwa kujibu tuhuma za mauaji.
Mushongi aliwataka wananchi wa mkoa huo kuwa makini katika kipindi hichi cha sherehe za kusherehekea kuukaribisha mwaka mpya kwa kutotumia vilevi kupita kiasi ili kuepukana na matukio ya uvunjifu wa amani.

Mwisho.

Sunday, December 27, 2015

HABARI MBALIMBALI ZA MKOA WA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unatarajiwa kuwa moja ya mikoa ambayo itakuwa kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa shughuli nyingi za uwekezaji za kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari wilayani Bagamoyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa mkoa una fursa nyingi za uwekezaji na watu binafsi pamoja na makampuni yameonyesha nia ya kuwekeza.

Ndikilo alisema kuwa uwekezaji umeanza kuchukua nafasi yake baada ya Jiji la Dar es Salaam kuonekana kuwa limejaa hivyo fursa iliyopo ni mkoa huo ambao uko jirani na Dar es Salaam.

“Kwa sasa tunajivunia na mojawapo ya uwekezaji mkubwa ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo itaongeza pato la mkoa huo kwani utazalisha ajira nyingi na wageni wengi wataingia kwa ajili ya shughuli nyingi za kibiashara,” alisema Ndikilo.

Alisema uwekezaji mwingine ni pale Kisarawe ambapo kimejengwa kiwanda cha saruji, Kibaha kuna viwanda vya Jipsam, Nondo na uwekezaji sehemu nyingine mbalimbali za wilaya zinazounda mkoa huo.

“Tukija kwenye zao kuu la biashara la Korosho nalo limezidi kunufaisha wakulima ambapo kwa sasa kilo ya korosho imepanda na kwa mnada sasa inauzwa kati ya 2,600 na 2,700 kutoka chini ya shilingi 1,000 na hii ni kutokana na mfumo wa stakabadhi ghalani,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa kwa kipindi kirefu mkoa huo haukuwa na fursa nyingi hali ambayo ilisababisha uonekane kama uko nyuma kiuchumi tofauti na ilivyo sasa fursa zimekuwa nyingi sana hivyo mafanikio ya kiuchumi yatakuwa makubwa.

Aliwataka watu wa mkoa huo hususani vijana kutumia fursa hizo zilizopo ambazo zimejitokeza kwa sasa ili kujikwamua na hali ngumu ya kimaisha pia watumie fursa za kilimo ambazo ni nyingi.

Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unaendelea na uhakiki wa watu walioweka mashamba pori ili taarifa zipelekwe kwa Waziri husika na baadaye kwa Rais ili kutengua umiliki wao endapo watashindwa kuyaendeleza hususani wale walionunua kwenye kitovu cha Mji wa Kibaha.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kuna mashamba pori mengi makubwa ambayo hayajaendelezwa kwenye wilaya zote za mkoa huo ikiwa ni pamoja na Kibaha, Kisarawe, Rufiji, Bagamoyo na Mkuranga.

Ndikilo alisema kuwa tayari wameshaanza kuyafanyia kazi mashambapori hayo kwa kushirikiana na wakurugenzi wa Halmashauri kwa mashamba yasiyoendelezwa.

“Tayari tumeshawapelekea notisi baadhi yao ili wajieleze ni kwanini wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo na kwanini wasinyanganywe kutokana na kushindwa kuyaendeleza,” alisema Ndikilo.

Kwa upande wa kitovu cha Mji wa Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa huo alisema kuwa wamiliki binafsi pamoja na taasisi ambazo ni nyingi wameshapewa barua kujieleza kwanini hawakuviendeleza viwanja hivyo.

“Tunawashangaa ni kwa nini wameshindwa kuendeleza viwanja hivyo ambavyo endapo vingejengwa vingeweka suraa nzuri ya mji kwani hapo ndiyo kwenye mandari ya uso wa mji,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa licha ya kutakiwa kujieleza kwa nini hawakuviendeleza viwanja hivyo pia waeleze kuwa watavijenga lini na muda watakaokubaliana hawapaswi kuupitisha tena.

“Kwa watakaoshindwa kuviendeleza baada ya makubaliano watanyanganywa viwanja hivyo ili wapewe wengine watakaoweza kuviendeleza kwa kujenga kwa wakati ukaoakuwa umepangwa,” alisema Ndikilo.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

JUMUIYA ya Wazazi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kimezigawia Jumuiya za Kata ardhi yenye ukubwa wa hekari moja kwa lengo la kuziendeleza kiuchumi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha baada ya zoezi hilo la kuwagawia ardhi hiyo ambalo lilifanyika kwenye sherehe za siku ya Uhuru, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Kibaha Mjini Dk Athuman Mokiwa alisema kuwa eneo hilo litakuwa kitovu cha uchumi wa Jumuiya hiyo.

Mokiwa alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 15 wameligawa kwa kata 14 za kichama ambapo kila kata inapaswa kuziendeleza kwa kulima na baadaye kufanya ujenzi.

“Kipindi cha nyuma tulishindwa kuliendeleza kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya kulipima lakini baada ya kulipima sasa tumegawa kila kata wawe na eneo lao kwa ajili ya shughuli za kiuchumi,”alisema Dk Mokiwa.

Alisema kuwa shamba hilo lilikuwa likivamiwa na watu kutokana na kutokuwa na hati za umiliki lakini kwa sasa wameshalimiliki kisheria hivyo hakuna mtu atakayeweza kuvamia tena.

Naye katibu wa Wazazi kata ya Kibaha lilipo shamba hilo Rehema Ally alisema kuwa wanaushukuru uongozi kwa kuwapatia eneo ambapo wanatarajia kuliendeleza na hiyo ni rasilimali yao kiuchumi.

Ally alisema kuwa baada ya kupatikana hati watawakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga taasisi zikiwemo za shule au zaahanati na huduma nyingine za kijamii.

Viongozi wa Jumuiya hizo za kata wamekubaliana kufanya usafi kila baada ya wiki mbili ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk John Magufuli juu ya usafi kukabiliana na magonjwa ya milipuko pia kuweka maeneo mbalimbali katika hali ya usafi.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

KUFUATIA dereva wa Pikipiki wa Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani Ally Rashid (35) kuuwawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kisha kumpora pikipiki aliyokuwa akiieendesha madereva wenzake wameomba uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha katibu wa Chama Cha Madereva Pikipiki Kibaha (CHAWAMAPIKI) Shaban Kambi alisema tukio hilo ni la kushangaza kwa watu kutumia bunduki kwa ajili ya kupora pikipiki likiwa ni tukio la pili.
Kambi alisema kuwa kumekuwa na matukio ya wizi wa pikipiki lakini kwa kutumia bunduki si hali ya kawaida hivyo tunaomba polisi wafuatilie tukio hilo la kusikitisha kwa mwenzetu kuuwawa.

“Matukio ya kutumia silaha ni matatu ambapo mtu mmoja alivamiwa nyumbani kwake na kupigwa risasi na kufa la pili ni mwenzetu mwingine alipigwa risasi ya mguuni na kuporwa pikipiki lakini hakufa huku mwenzetu wa juzi naye alipigwa risasi na kufa ambapo cha kushangaza matukio yote yametokea upande mmoja,” alisema Kambi.

Alisema matukio yote hayo yametokea maeneo ya machinjioni hali ambayo inawapa hofu wakazi wa Maili Moja kwa kuona kuwa maisha yao sasa yako hatarini kwa watu hao kufanya uahalifu kwa kutumia bunduki.

“Tumesha waambia madereva pikipiki kuwa makini kwani kuna baadhi ya maeneo kwa sasa ni hatarishi pia wakiwa na wasiwasi wasiwabebe watu wasiowafahamu hasa nyakati za usiku hasa katika kipindi hichi cha mwisho wa mwaka,” alisema Kambi.

Aidha alisema kuwa wao wako tayari kushirikiana na jeshi la polisi katika kufuatilia watu wanaojihusisha na matukio hayo ya uporaji wa pikipiki pamoja na mali za watu.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unatarajia kujenga Kituo Kikubwa cha Mabasi pamoja na Soko baada ya kupata mkopo toka Benki ya Uwekezaji ya (TIB) na kuufanya mji wa Kibaha kuwa wakisasa.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Pwani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo na kusema kuwa kwa sasa taratibu zinaendelea baina ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha na benki hiyo.

Ndikilo alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa mara taratibu za kitaalamu zitakapokamilika ambapo kwa sasa bado zinaendelea.

“Tunatarajia kuwa na stendi ya kisasa pamoja na soko hasa ikizingatiwa mkoa ulikuwa hauna soko kubwa bali lililopo ni dogo na halina uwezo wa kuchukua bidhaa nyingi,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wafanyabiashara wa mkoa wa Pwani hususani wale wa makao makuu ya mkoa Maili Moja na vitongoji vyake huwalazimu kwenda kununua bidhaa Kariakoo au kwenye masoko mengine Jijini Dar es Salaam jambo ambalo linafanya bei za bidhaa kuwa juu.

“Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa ni kama malango wa Jiji la Dar es Salaam lakini bidhaa zimekuwa zikipita hapa na kwenda huko kisha wafanyabiashara kwenda kununua na kuzirudisha hapa hivyo kupandisha bei kutokana na gharama kuwa kubwa,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa soko hilo ambalo litajengwa sambamba na stendi litakuwa la kisasa ambapo magari yatakuwa na uwezo wa kuingia na kushusha bidhaa na si kama ilivyo sasa ambapo kutokana na udogo wa soko lililopo hubidi magari ya bidhaa yashindwe kuingia.

Mwisho.
  

   

   

  




WATAKA TAFSIRI YA UPANUZI WA BARABARA WAPATE HAKI ZAO

Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Kijiji cha Kiluvya B wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani wameiomba Wizara ya Ujenzi na Makazi iangalie upya tafsiri ya upanuzi wa barabara kuu kwani upanuzi uliofanyika ni urefu wa mita 120 upande mmoja wakati sheria inasema kila upande wa barabara itapanuliwa kwa urefu wa mita 60 kwa 60 kutoka katikati ya barabara kuu.
Kutokana na sheria hiyo kutafsiriwa mita 120 nyumba zilizojengwa kando ya Barabara ya Morogoro baadhi zimebomolewa na nyingine zimeekewa alama ya X zikitakiwa kubomolewa baada ya muda usiozidi zaidi ya wiki moja na kupelekea kilio kikubwa kwa wakazi hao.
Wakizungumza waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho moja ya wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Abubakary Yusuph alisema kuwa athari ya kubomolewa nyumba hizo ni kubwa sana hivyo kuomba suala hilo liangaliwe upya.
Yusuph alisema kuwa wao hawana tatizo la kuondoka kwenye eneo hilo kwa ajili ya kupisha shughuli za maendeleo bali wameomba sheria ifuatwe ili wasinyimwe haki zao kwani wao wako hapo tangu vilipoanzishwa vijiji vya ujamaa miaka ya 70.
“Tunaomba wizara na serikali kuliangalia upya suala hili kwani sisi hatuna shida kwa wale waliojenga ndani ya mita 60 kwani tunajua suala hilo ni la kisheria lakini mita 120 tunaona kuwa hatujatendewa haki ni vema wanapotekeleza suala hilo wakazingatia sheria ya barabara na kama wanataka eneo zaidi ni vema wakatulipa ndipo waendelee na zoezi hilo,” alisema Yusuph.
Alisema kuwa watu wengi walijenga umbali zaidi ya mita 60 kwani walikuwa wakijua kuwa kama watakuwa ndani ya mita hizo basi bomobomoa ikija wangebomolewa nyumba zao lakini walikojenga walijua wako salama wanashangaa kuona nyumba zao zinabomolewa.
Naye Alfonce Kejo alisema kuwa baadhi yao ni wastaafu na hawana kipato chochote na waliwekeza kwenye nyumba zao kwa ajili ya makazi mara baada ya kustaafu kazi hivyo wanaomba suala lao lishughulikiwe ili wapate haki yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Julius Bukoli ambaye naye amekumbwa na bomoa bomoa hiyo alisema kuwa nyumba yake aliijenga kabla ya mwaka 2000 na iko umbali wa karibu mita 100 toka barabara kuu lakini ametakiwa kubomoa.
Bukoli alisema kuwa hata wanaohusika katika kubomoa nyumba hizo hawafuati taratibu za kutoa taarifa kwenye uongozi wa Kijiji bali wanakuja nyakati za jioni na kubomoa au kuweka alama za X kisha kuondoka.
Mwisho.  
Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Kuweka na Kukopa Cha TCCIA Saccos mkoa wa Pwani kimeweza kukopesha mikopo inayofikia zaidi ya shilingi milioni 398 kwa wanachama wake.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha, Meneja wa chama hicho Arestide Temu alisema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa  wanachama waliofuata taratibu za mikopo kwa lengo la kukuza mitaji yao ya biashara.

Temu alisema kuwa hata hivyo biashara nyingi kwenye mkoa huo zinashindwa kukua vizuri kutokana na kutokuwa na mzunguko mkubwa wa fedha kwa sababu ya kuwa na shughuli chache za kiuchumi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa viwanda.

“Sababu nyingine ya wafanyabiashara kushindwa kufikia malengo ni kutokana na kufanya biashara zinazofanana na kusababisha kushindwa kufikia malengo hata hivyo tumepata mafanikio tumeweza kupata faida ya shilingi milioni 26 tofauti na lengo la kupata faida ya shilingi milioni 20 tulizokuwa tumejipangia kwa mwaka huu ambapo faida hiyo ni hadi mwezi Novemba mwaka huu,” alisema Temu.

Alisema kuwa maendeleo ya chama yanakwenda vizuri ambapo kwa sasa wamanachama wanaweza kukopa mara tatu ya fedha walaizojiwekea kama akiba na wanaweza kukopa hadi shilingi milioni 15 kwa mara moja.

“Riba ni asilimia 15 ya mkopo wowote anaoomba mwanachama ambapo hisa moja inauzwa kiasi cha shilingi 10,000 huku mwanachama akitakiwa kununua hisa kuanzia 10 na kuendelea,” alisema Temu.
Aidha alisema kuwa chama hicho cha kuweka na kukopa kilianzishwa mwaka 2001 kikiwa na wanachama 600 ambapo kwa sasa kina wanachama 227 huku wengine wakiwa wameondolewa kwa kushindwa kufuata taratibu za chama.   

Mwisho.




Saturday, December 26, 2015

BONANZA LA KUAGA MWAKA 2015 NA KUUKARIBISHA 2016 KUFANYIKA JANUARI MOSI KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
BONANZA la kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka 2016 linatarajiwa kufanyika Januari Mosi mwakani kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Msajili Msaidizi wa Vilabu na Vyama vya Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Abdul Haufi alisema kuwa Bonanza hilo litakuwa la wazi kwa watu wote.
Haufi alisema kuwa shindano hilo litakuwa la michezo mbalimbali litashirikisha mashirika ya Umma, binafsi pamoja na watu binafsi au mtu mmoja mmoja kwenye michezo ya soka, mpira wa pete kwa wanawake, kuvuta kamba, riadha mita 100.
Alitaja michezo mingine kuwa ni kukimbia na magunia, kurusha kisahani, tufe, mpira wa wavu, kijiko na ndimu ambapo usajili unafanyika kwenye ofisi za Halmashauri hiyo.
“Tunatarajia jumla ya wanamichezo 250 kushiriki Bonanza hilo la aina yake kufanyika mjini Kibaha na vitongoji vyake ambapo lengo ni kuhamasisha watu kushiriki michezo pamoja na kudumisha urafiki baina ya mashirika bianafsi, ya umma pamoja na watu binafsi,” alisema Haufi.
Aidha alisema kuwa juu ya wadhamini tayari baadhi wameshajitokeza huku wakiwasubiri wengine wamalizia taratibu za kudhamini Bonanza hilo na matarajio ni kutolewa zawadi nono.
Bonanza hilo limeandaliwa kwa pamoja na Halmashauri ya Mji Kibaha, Majeshi ya mkoani Pwani ikiwa ni pamoja na Magereza, Polisi na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Mwisho.