Wednesday, September 2, 2015

CCM MUFINDI WATAMBA KUSHINDA UCHAGUZI MKUU

Na John Gagarini, Mafinga
KUTOKANA na Utekelezaji wa Ilani kikamilifu chama cha mapinduzi kinatarajia kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao kwenye nafasi zote za Urais Ubunge na Udiwani
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kimeweka mikakati ya kupata ushindi wa kishindo kwa wagombea wake kwenye nafasi tatu za Urais Wabunge na Madiwani kutokana na utekelezaji wa ilani ya chama.
Hayo yalisemwa na mjini Mafinga na katibu wa CCM wilaya ya Mfundi Jimson Mhagama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa ushindi wa chama unatokana na ilani kutekelezwa kwa asilimia 95.
Mhagama alisema kuwa wilaya hiyo ina majimbo matatu ya Mufindi Kaskazini ambalo linaongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmoud Mgimwa, Mufindi Kusini linaongozwa na Menrad Kigora na Mafinga Mjini litakalowaniwa na Cosatu Chumi pamoja na kata 36 vyote vikiwa chini ya CCM  hivyo wana uhakika wa kuendelea kuyaongoza maeneo hayo.
“Sisi hatuna wasiwasi tunaendelea kuweka mikakati ya suhindi lakini ushindi wetu utatokana na utekelezaji wa ilani ya chama juu ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali za huduma za jamii ambazo zimeboreka kutokana na uongozi mzuri wa viongozi wa chama,” alisema Mhagama.
Alisema kuwa mfano kwenye huduma za jamii ujenzi wa baadhi ya barabara kwa kiwango cha lami na changarawe zinazofanya kupitika kwa kipindi chote cha mwaka, uboreshaji wa huduma za afya kwenye Hospitali ya Mafinga na ujenzi wa zahanati kwenye vijiji, uanzishwaji wa vikundi vya ujasiriamali, huduma za taasisi za fedha na ujenzi wa shule za sekondari, uanzishwaji wa vyuo mbalimbali.
Aidha alisema kuwa CCM itaendelea kusimamia ilani yake kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanapatikana ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ambao wamekiamini chama kutokana na kuongoza kwa manufaa ya jamii.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa amemwagia sifa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmoud Mgimwa kutokana na uchapakazi wake kwenye wizara pamoja na kuhamasisha maendeleo kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini analoliongoza.
Akihutubia wakazi wa mji wa Mafinga wakati wa mkutano wake wa kampeni Lowassa alisema kuwa mbunge huyo ni mchapakazi na amefanya mabadiliko makubwa kwenye Jimbo hilo na kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii.
Lowassa alisema kuwa Mgimwa ni moja ya viongozi wazuri ambao wanawajibika vizuri katika maeneo ambayo wamepewa kuwajibika lakini angekuwa kwenye chama kama CHADEMA angefanya vizuri zaidi.
“Mgimwa namfahamu ni muwajibikaji mzuri katika maeneo ambayo anayaongoza lakini angekuwa upinzani angefanya vizuri zaidi kwani wapinzani wanafanya kazi sana na wana uwezo wa kuleta maendeleo,” alisema Lowassa.
Kwa upande wake katibu wa CCM wilaya ya Mufindi Jimson Mhagama akizungumzia juu ya kauli ya Lowassa alisema kuwa Mgimwa ni zao la CCM ambalo limeandaliwa kwani ndiyo kazi yao kutengeneza viongozi bora.
Mhagama alisema kuwa kiongozi bora anatoka CCM na kazi ya wapinzani ni kuchukua watu ambao uwezo wao umeshakuwa mdogo hivyo kushindwa kuwajibika hali ambayo haitawaletea maendeleo wananchi.
Aliwataka wananchi kuiunga mkono CCM na kuachana na vyama vya upinzani ambavyo havina sera za kuwaletea maendeleo wananchi badala yake ni kuwagawa na kuendeleza malumbano ambayo hayana faida kwa wananchi.
Naye mkazi wa Mafinga Edina Peter alisema kuwa wao wanataka kiongozi ambaye atawasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi na Mgimwa ni moja ya viongozi bora ambao wanajali maslahi ya wananchi.
Mwisho.
    
  

   

WODI YA WAZAZI MAFINGA YAHITAJI MAMILIONI YA FEDHA KWA AJILI YA VIFAA VYA UPASUAJI

Na John Gagarini, Mafinga
HOSPITALI ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa inahitaji kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa vya upasuaji kwenye wodi ya wazazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Mafinga Dk Innocent Mhagama alisema kuwa fedha hizo ni pamoja na ukarabati wa chumba cha upasuaji kwenye wodi hiyo.
Dk Mhagama alisema kuwa jengo hilo la wodi ya wazazi limekamilika na linatumika lakini halina huduma ya upasuaji kwa wanawake wajawazito.
Alisema kuwa wanafanya mipango mbalimbali kwa ajili ya kupata fedha hizo ili kutoa huduma bora za idi ya hapo kwani matatizo yote yatakuwa yakitatuliwa ndani ya jengo hilo pasipo kumhamisha mgonjwa.
“Wodi hii iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 320 imekamilika tangu mwaka jana na inatoa huduma zote isipokuwa upasuaji ambapo kwa sasa tunatafuta fedha hizo ili kuwe na huduma hiyo,” alisema Dk Mhagama.   
 Alisema kuwa kukamilika kwa wodi hiyo kumepunguza tatizo la akinamama kutopata huduma bora lakini sasa huduma zimeboreka.
“Wodi ya awali ilikuwa na uwezo wa kuzalisha akinamama wawili au watatu lakini kwa sasa wanazalisha akinamama nane kwa wakati mmoja ambapo inauwezo wa kulaza akinamama 60 toka 20 kwa  wakati mmoja ambapo wanaojifungua kwa siku ni kati ya 18 na 20 na wanaofanyiwa operesheni kwa siku ni kati ya wanne hadi sita,” alisema Dk Mhagama.
Moja akinamama wanaotumia wodi hiyo Blandina Mpyanga alisem akuwa wanaishukuru serikali na wadau mbalimbali waliofanikisha ujenzi huo.
Mpyanga alisema kuwa kwa kipindi cha nyuma wakinamama wajawazito walikuwa wakilala wanne kwenye kitanda kimoja lakini kwa sasa kila mgonjwa na kitanda chake.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
KATIKA kukabiliana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi wa kike kupata ujauzito pamoja na kuozwa katika umri mdogo Jimbo la Mufindi Kaskazini wilayani Mufindi mkoani Iringa imewekwa mikakati ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi kwa shule za sekondari.
Akizungumza na waandishi wa habari mbunge wa Jimbo hilo ambaye anatetea kiti hicho Mahmoud Mgimwa alisema kuwa ujenzi huo ni kwa ajili ya shule zote za kata na zingine ili kukabiliana na changamoto hizo.
Mgimwa ambaye ni Naibu waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa hadi sasa shule ya sekondari ya Isalavanu tayari imekamilika huku ile ya Kibengu ikiwa ujenzi unaendelea.
“Hii ni moja ya mikakati ambayo nimeiweka kama kipaumbele cha utekelezaji wa ilani ya chama ambapo nimechangia hosteli hizo bati 170 na vifaa mbalimbali katika kukamilisha ujenzi huo,” alisema Mgimwa.
Alisema kuwa endapo kila kata itakuwa na hosteli ni dhahiri tatizo la mimba na wanafunzi kuozwa wakiwa bado wanafunzi litapungua au kwisha kabisa.
“Unajua wanafunzi wa kike wanachangamoto kubwa kwani baadhi ya watu wamekuwa wakiwarubuni kutokana na mazingira wanayoishi hasa kutokana na umbali wa shule wanazosoma lakini wakijengewa mabweni itawasaidia,” alisema Mgimwa.
Mmoja ya wakazi wa Mji wa Mfainga Anna Karoli alisema kuwa mpango huo ni mzuri na utasaidia kuwanusuru wanafunzi wanaopewa mimba na kuozwa.
Karoli alisema wanafunzi wa kike wakikaa shule itawasaidia kujiepusha na vishawishi mbalimbali mara watokapo au kwenda shule.
Moja ya wanafunzi wa kike Anita Michael ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya JJ Mungai alisema kuwa mpango huo ni mzuri na utawasadia wanafunzi wa kike kukabiliana na changamoto hizo.
Anita alisema kuwa baadhi ya changamoto wanazozipata ni kurubuniwa na baadhi ya watu wakiwemo madereva wa bodaboda ambao wamekuwa wakiwadanganya kwa kuwapa lifti wakati wakwenda shule.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
WATUMISHI wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kuacha kujihusisha na mambo ya siasa ili kutozorotesha utoaji huduma kwenye sehemu zao za kazi.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shaib Nnunduma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Mafinga na kusema kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Nnunduma alisema kuwa kama mtumishi anataka kujihusisha na sisa kuna taratibu ambazo anatakiwa afuate lakini si kufanya siasa akiwa kazini.
“Kufanya siasa ofisini ni kosa kisheria na mtumishi ambaye anafanya hivyo ni kinyume cha sheria za kazi hivyo hawapaswi kufanya hivyo kwani ni kukwamisha utendaji kazi,” alisema Nnunduma.
Alisema kuwa endapo mtumishi anabainika kujihusisha na siasa kazini sheria inambana na anaweza kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
“Kila mtu kuna chama anachokipenda lakini huwezi kuonyesha itikadi zako za chama ofisini kwani kuna baadhi ya watu utawabagua kutokana na vyama vyao hivyo hilo ni kosa kisheria,” alisema Nnunduma.
Aidha alisema kuwa ataandaa mkutano na watumishi wote wa Halmashauri ili kuwajulisha kujiepusha na siasa kazini ambapo wakuu wa shule za sekondari alishaongea nao juu ya kujiepusha na siasa shuleni.
Mwisho.


MWANAFUNZI AJERUHIWA KWA KIPIGO CHA MWALIMU

Na John Gagarini, Mafinga
MWANAFUNZI wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya JJ Mungai Octavian Luoga (20) amejeruhiwa kichwani kwa kupigwa fimbo na mwalimu wake kwa tuhuma za kushindwa kuingia darasani.
Akizungumza jana mjini Mafinga na waandishi wa habari mara baada ya kutoka kwenye Hospitali ya Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa alipotoka kupatiwa matibabu mwanafunzi huyo alisema kuwa mbali ya kupigwa na fimbo kichwani pia alipigwa makofi na mateke.
Luoga alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya asubuhi Septemba  Mosi akiwa bwenini amepumzika kutokana na kuumwa na mishipa ya kichwa huku akiwa na wenzake wawili Wilson Due na Nsajigwa Moses ambao wote walikuwa wakiumwa jambo lililomfanya ashindwe kuingia darasani.
“Walimu wawili walikuja na kunitaka niende ofisini kwa ajili ya kupewa adhabu nikawaambia mimi naumwa ndiyo sababu ya kushindwa kuingia darasani mara wakaanza kunipiga nikawaambia nuamwa naomba mnisikilize wakakataa wakasema nimewajibu vibaya,” alisema Luoga.
Alisema kuwa kutokana na kipigo hicho ikabidi aende ofisini na kufika kule akaanza kupigwa makofi,mateke na fimbo maeneo mbalimbali ya mwili na mwalimu mkuu msaidizi Huruma Nyalusi akidai kuwa nawadharau walimu.
“Mwalimu alinipiga fimbo kichwani na damu zikaanza kunitoka hata hivyo hawakutaka kunipeleka hospitali ndipo wanafunzi wengine wakalazimisha nipelekwe ambapo tulienda polisi na baadaye hospitali kwa ajili ya matibabu nikashonwa nyuzi kadhaa,” alisema Luoga.
Aidha alisema kuwa walimu na wanafunzi wanafahamu matatizo yake na wiki moja iliyopita alilazwa kutokana na tatizo lake hilo hilo hali ambayo ilimfanya ashindwe kuingia darasani ambapo hata mahudhuria yake darasani ni mazuri lakini huwa anashindwa kuingia darasani kutokana na kuumwa kwake.
Baadhi ya wanafunzi walisema kuwa baadhi ya walimu wa shule hiyo wamekuwa na tabia ya kupiga wanafunzi kupita kiasi huku wakati mwingine wakiwapiga ngumi, makofi, vichwa mateke na kuwachapa fimbo zisizo na idadi.
Jitihahada za kumpata mwalimu Nyalusi aliyehusika na tukio hilo hazikuweza kufanikiwa kwani alikuwa akihojiwa kwenye kituo cha polisi cha Mafinga kuhusiana na tukio hilo baada ya wanafunzi wa kidato cha sita kuandamana kwenda polisi kulalamika.
Hata hivyo  jitihada za kumpata mwalimu mkuu wa shule hiyo Mariano Mwanyingu hazikuweza kufanikiwa kwani hakuwepo shuleni hapo kwani aliondoka kabla ya tukio hilo kutokea na haifahamiki atarudi baada ya muda gani.
Kwa upande wake mkuu wa polisi wilaya ya Mufindi Ambwene Mwanyasi alikiri kupokelewa kwa mwalimu huyo ambaye alihusika na tukio hilo kwa ajili ya kuhojiwa.
Mwisho.
MWANAFUNZI wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya JJ Mungai iliyopo kwenye Halmashauri ya Mji wa Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa  Octavian Luoga (20) amejeruhiwa kichwani kwa kupigwa fimbo na mwalimu wake kwa tuhuma za kushindwa kuingia darasani.
Akizungumza jana mjini Mafinga na waandishi wa habari mara baada ya kutoka kwenye Hospitali ya Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa alipotoka kupatiwa matibabu mwanafunzi huyo amesema kuwa mbali ya kupigwa na fimbo kichwani pia alipigwa makofi na mateke.
Luoga amesema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya asubuhi Septemba  Mosi akiwa bwenini amepumzika kutokana na kuumwa na mishipa ya kichwa huku akiwa na wenzake wawili Wilson Due na Nsajigwa Moses ambao wote walikuwa wakiumwa jambo lililomfanya ashindwe kuingia darasani.
Amesema kuwa walimu wawili walikwenda na kumtaka aende ofisini kwa ajili ya kupewa adhabu kwani hakwenda darasani akawaambia anaumwa ndiyo sababu ya kushindwa kuingia darasani mara wakaanza kumpiga licha ya kuwaomba wamsikilize wakakataa wakasema amewajibu vibaya.
Amesema kuwa kutokana na kipigo hicho ikabidi aende ofisini na kufika kule akaanza kupigwa makofi,mateke na fimbo maeneo mbalimbali ya mwili na mwalimu mkuu msaidizi Huruma Nyalusi akidai kuwa nawadharau walimu.
Aidha amesema kuwa mwalimu alimpiga fimbo kichwani na damu zikaanza kumtoka hata hivyo hawakutaka kumpeleka hospitali ndipo wanafunzi wengine wakalazimisha apelekwe ambapo walienda polisi na baadaye hospitali kwa ajili ya matibabu nikashonwa nyuzi kadhaa.
Amesema kuwa walimu na wanafunzi wanafahamu matatizo yake na wiki moja iliyopita alilazwa kutokana na tatizo lake hilo hilo hali ambayo ilimfanya ashindwe kuingia darasani ambapo hata mahudhuria yake darasani ni mazuri lakini huwa anashindwa kuingia darasani kutokana na kuumwa kwake.
Baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa baadhi ya walimu wa shule hiyo wamekuwa na tabia ya kupiga wanafunzi kupita kiasi huku wakati mwingine wakiwapiga ngumi, makofi, vichwa mateke na kuwachapa fimbo zisizo na idadi.
Jitihahada za kumpata mwalimu Nyalusi aliyehusika na tukio hilo hazikuweza kufanikiwa kwani alikuwa akihojiwa kwenye kituo cha polisi cha Mafinga kuhusiana na tukio hilo baada ya wanafunzi wa kidato cha sita kuandamana kwenda polisi kulalamika.
Hata hivyo  jitihada za kumpata mwalimu mkuu wa shule hiyo Mariano Mwanyingu hazikuweza kufanikiwa kwani hakuwepo shuleni hapo kwani aliondoka kabla ya tukio hilo kutokea na haifahamiki atarudi baada ya muda gani.
Kwa upande wake mkuu wa polisi wilaya ya Mufindi Ambwene Mwanyasi alikiri kupokelewa kwa mwalimu huyo ambaye alihusika na tukio hilo kwa ajili ya kuhojiwa.

  
  


Thursday, August 20, 2015

WATUMISHI WA DINI WAASWA KUELEKEA UCHAGUZI

Na John Gagarini, Morogoro
WATUMISHI wa Dini nchini wametakiwa kumtanguliza Mungu katika utumishi wao ili kuendelea kudumisha amani ya nchi iliyopo hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Ushauri huo umetolewa huko Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na Mtawa Sista Perpetua Mlamwaza (72) wakati wa maandalizi ya Jubilei ya miaka 50 ya Utawa kwenye kanisa la Katoliki na kusem akuwa siri kubwa ya mafanikio yake ya utendaji yanatokana na kumtanguliza mbele Mungu.
Mlamwaza alisema kuwa watumishi wa Mungu wana nafasi kubwa ya kuifanya nchi iendelee kudumu ni kwa wao kumtanguliza Mungu na kuliombea Taifa letu ili liwe amani ambayo imedumu tangu nchi kupata Uhuru.
“Kipindi hichi tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu hivyo lazima tupige magoti kumwomba Mungu azidi kutudumishia amani yetu iliyopo kwani yeye ndiye mwenye uwezo wa kutunusuru na hali yoyote ambayo inaashiria uvunjifu wa amani,” alisema Mlamwaza.
Mlamwaza ambaye aliwalea kiroho hadi kufanikiwa kupata upadri Mhashamu Askofu Antony Banzi wa Jimbo la Tanga na padri Peter Kunambi alisema kuwa watumishi ni kiungo muhimu kati ya wanadamu na Mungu.
“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuweza kumtumikia Mungu kwa kipindi chote cha miaka 50 ya utumishi wangu lakini amani hii iliyopo inapaswa kulindwa na kuendelezwa ili tuendelee kupata mafanikio ya kimaendeleo,” alisema Mlamwaza.
Aidha alisema kuwa Watanzania wote wanapaswa kufanya maombi ya kila wakati ikiwa ni pamoja kufunga ili kumwomba Mungu aendelee kutudumishia amani iliyopo hasa ikizingatiwa Tanzania ni Kisiwa cha amani.
Aliwataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka shule watoto wao hususani wale wa kike ili waweze kuwarithisha elimu ambayo itakuwa ni mkombozi katika maisha yao na si mali kama baadhi ya watu wanavyofikiri.
Mwisho.
  

   

MAILI MOJA WAENDELEA NA UJENZI WA SHULE ILIYOBOMOKA

> Na John Gagarini, Kibaha
UJENZI wa madarasa manne kwenye shule ya msingi Maili Moja umeanza ambapo kwa sasa wanafunzi 200 wanasoma kwenye darasa moja kutokana na baadhi ya madarasa kushindwa kutumika kutokana na kuwa mabovu hivyo kuhatarisha usalama wa wanafunzi.
Shule hiyo ambayo ndiyo shule ya kwanza kujengwa kwenye mji wa Kibaha kwenye miaka ya 70 madarasa yake yamebomoka na baadhi yameanguka kutokana na kutumika kwa muda mrefu sasa kwani yamefikisha umri wa miaka 40 sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari shuleni hapo mwalimu mkuu wa shule hiyo Reginald Fanuel alisema kuwa ujenzi huo ambao ambao utaanza na madarasa mawili tayari ujenzi umefikia hatua ya msingi na unatarajiwa kukamilika baada ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Fanuel alisema kuwa fedha zilizotumika kujenga msingi huo wa madarasa manne ni michango ya wazazi na wadau mbalimbali huku wakisubiria kutoa fedha ambazo ziko benki kiasi cha shilingi milioni 36 zilizotolewa na Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambazo ndiyo zitakamilisha ujenzi wa madarasa hayo mawili
“Kwa kweli hali ni mbaya kwa sasa kwani darasa moja linachukua wanafunzi 200 tofauti na wastani wa wanafunzi 45 kwa darasa moja lakini kutokana na ubovu madarasa imebidi mengine yasitumike kutokana na kubomoka na yanaweza kuanguka hivyo usalama wa wanafunzi na walimu kuwa mdogo,” alisema Fanuel.
Alisema kuwa shule hiyo ina jumla ya madarasa 14 lakini mazima ni manne tu ndiyo yenye unafuu kidogo licha ya kuwa si mazima huku mawili ndiyo mazima na yako imara na yanafaa kwa matumizi ya kufundishia.
“Ujenzi ulisimama kidogo kutokana na kukosekana vitabu vya hundi kutoka benki hivyo kushindwa kuwalipa wazabuni na wakandarasi na tulitumia muda mrefu zaidi ya mwezi mmoja kupata vitabu hivyo kwani akaunti ya shule ilikufa hivyo tukaanza kuifufua upya hali iliyotumia muda mrefu kufunguliwa lakini kwa sasa zoezi hilo limekamilika na wataanza kulipwa ili ujenzi uendelee,” alisema Fanuel.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Lusanda Wiliam alisema kuwa michango iliyochangwa ni mizuri kwani walitoa mifuko 250 ya saruji ambayo iilifyatuliwa tofali zaidi ya 585 na mifuko 50 ilitumika kwa ajili ya msingi uliojengwa.
Wiliam alisema kuwa wazazi ambao watoto wao wanasoma shuleni hapo walitakiwa kulipia shilingi 5,000 kila mmoja kwa ajili ya ujenzi huo na walifanikiwa kupata kiasi cha shilingi 500,000 na kuwaomba wadau wengine wajitokeze kuchangia ujenzi huo.

Mwisho.

WAWEZESHAJI KAYA MASKINI KIBAHA WAASWA

Na John Gagarini, Kibaha
WAWEZESHAJI wa mradi wa kutoa ajira za muda kwa kaya maskini kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF) wametakiwa kutowapangia miradi kwa utashi wao bali wao wabaki kama washauri tu.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Tatu Suleiman wakati akifungua mafunzo kwa wawezeshaji wa mradi huo awamu ya tatu na kusema kuwa wananchi ndiyo wenye kufahamu wanahitaji mradi gani.
Seleman alisema kuwa waratibu hao kazi yao ni kutoa ushauri kwa wananchi wanapobainisha mradi wanaoutaka kwani wanaopata changamoto ni wao na si kuelekezwa na wawezeshaji hao ila wao wanatakiwa kushauri namna ya kutekeleza miradi hiyo.
“Nyie ni wataalamu mnapaswa kuwapa ushauri wananchi ili wafanikishe miradi hiyo lakini siyo kuwapangia kuwa wafanye mradi gani kwani wao ndiyo wanaojua mahitaji yao lengo likiwa ni wao kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema Suleiman.
Alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya kunusuru kaya maskini umefikia hatua nzuri ambapo kaya maskini za vijijini zimeweza kuongeza kipato na kuzifanya zisiwe kwenye hali ngumu wakati wa kaipindi cha Hari ambacho kinakuwa baada ya muda wa mavuno kupita.
“Tumeona akaya nyingi sasa zimeweza kupita mwaka mzima zikiwa bado na hali nzuri ya chakula kwani kwa kipindi cha nyuma zilikuwa zinaishiwa chakula kutokana na kuuza chakula ili kupata kipato cha kujikimu,” alisema Suleiman.
Awali mwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa TASAF Mercy Mandawa alisema kuwa mradi huo wa awamu ya tatu emelenga kaya maskini zenye hali duni kwa lengo la kuongeza kipato kwenye mamlaka za serikali 161 nchini.
Mandawa ambaye ni Mtaalamu wa Mafunzo na Ushirikishaji wa Jamii TASAF makao makuu alisema kuwa hadi sasa miradi hiyo imeweza kuzifikia kaya milioni moja kote nchini tangu kuanzishwa mpango wa kuzisaidia kaya maskini mwaka 2012 ambayo ilizinduliwa na Rais Dk Jakaya Kikwete.
“Lengo la mradi huu ni kuhakikisha kaya maskini zinakuwa na kipato cha kuweza kujikimu kwa kuwapa ajira za muda ambapo mafanikio yameonekana kwani zimeweza kuwa na kipato na kuondokana na umaskini,” alisema Mandawa.
Aidha alisema kuwa Halmashauri zinatakiwa kuhakikisha zinapeleka fedha kwa wakati ili kuondoa malalamiko kwa walengwa ambapo kulikuwa na tatizo la ucheleweshaji wa utoaji wa fedha za ruzuku kwa kaya maskini.
Mradi huo kwa wilaya ya Kibaha utazifikia kaya 5,690 kwenye miradi ya kuhifadhi maji ya mvua, hifadhi ya misitu, miradi midogo midogo ya umwagiliaji, kilimo misitu cha kuchanganya mazao na miti, usafi wa mazingira maeneo ya mjini  (uzoaji wa taka ngumu), mafunzo hayo yamewahusisha wawezeshaji 24.

Mwisho.

HABARI MBALIMBALI ZA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
UMOJA wa Wafanyakazi wa Viwanda na Biashara Tanzania (TUICO) kimewataka wanachama wake kukitumia chama chao ili kujileta maendeleo.
Hayo yalisemwa hivi karibuni mjini Kibaha na mwenyekiti wa chama hicho Betty Msimbe mara baada ya uchaguzi wa chama hicho ambapo alifanikiwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho
Msimbe alisema kuwa baada ya kupata nafasi hiyo ya kukiongoza chama hicho atahakikisha kuwa wanachama wanapata maendeleo kwa kutumia chama chao ambacho kina lengo la kuwaletea umoja na kutetea haki zao.
“Malengo yangu ni kuongeza wingi wa wanachama, kutetea haki za wafanyakazi kuhakikisha mkoa unavuka malengo yake ya kazi, haki na maslahi ya wafanyakazi sehemu za kazi,” alisema Msimbe.
Alisema kuwa atafanya mafunzo maeneo ya kazi ili wafanyakazi wapate elimu juu ya haki zao na elimu kwa viongozi wa matawi kuhusu kutetea maslahi ya wafanyakazi ili waweze kuboresha utendaji kazi wao.
“Kikubwa ninachokiomba toka kwa wanachama na viongozi wenzangu ni ushirikiano ambao utasaidia kukipeleka mbele chama na kufikia malengo ya kuhakikisha haki za wafanyakazi zinapatikana,” alisema Msimbe.
Naye Naibu Katibu Mkuu Msaidizi sekta ya biashara TUICO Taifa Peles Jonathan alisema kuwa atahakikisha anasimamia haki na maslahi ya wafanyakazi kwa nchi nzima na kufanya umoja huo kuwa na demokrasia ya uwakilishi wa kulinda na kutetea haki za wanachama.
Jonatahan alitoa wito  kwa sekretarieti kufanya kazi kwa pamoja ili chama kiweze kufikia malengo waliyojiwekea ili kuwaunganisha kwa pmoja wafanyakazi ili waweze kuwajibika vizuri.
Katika uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na katibu wa chama hicho Kassim Matewele ambaye alimtangaza Msimbe kuwa mshindi kwa kura (41) ambaye alimshinda Abimelick Magoma aliyepata kura (18).
Kwenye nafasi ya wajumbe wa kamati ya utendaji mkoa nafasi mbili nafasi ya  Viwanda ni Hasan Kindagule aliyepata kura (35) na Msaidizi wake Athuman Makonga kura (22), upande wa Biashara Shukuru Goso aliyepata kura (32) na msaidizi wake Joyce Kalumuna kura (29).
Kwa upande wa Fedha Furaha Mbwambo  alishinda kwa kupata kura (45) na msaidizi wake ni Zaituni Mtoro aliyepata kura (41), Huduma na ushauri mshindi alikuwa ni Tumaini Kivuyo na msaidizi wake Kandrid Ngowi ambaye alipata kura (35).
Waliochaguliwa Mkutano Mkuu Kanda, Viwanda ni Masiku Serungwi aliyepata kura (35), biashara ni Kamatanda Kamatanda aliyepata kura (57), Fedha Furaha Mbwambo aliyepata kura (60), kwa upande wa huduma na ushauri mshindi alikuwa ni Kandrid Ngowi aliyepata kura (40).
Wajumbe wa mkutano mkuu Taifa upande wa Viwanda  mshindi ni Athuman Makonga kura (59), Biashara ni Shukuru Ngoso kura (58), Fedha Zaituni Mtoro kura (57) na huduma na Ushauri Margareth Chaleo kura ( 45).
Mwisho.

Na John Gagarini, Mkuranga

KIJIJI cha Mwanambaya Kata Mipeko wilaya ya Mkuranga kimewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuwasaidia kupata kiasi cha  milioni 150 kwa ajili ya mradi wa kuvuta maji kutoka kijiji jirani cha Kisemvule.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa kijiji hicho Abubakar Sisaga alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya maji hivyo wameanza mchakato wa kuvuta maji kutoka kijiji cha Kisemvule.

Sisaga alisema kuwa awali walikuwana wazo la kuchimba visima lakini kutokana na uwezo kutokana na gharama za uchimbaji kisima kuwa ni kubwa.

“Tunawaomba wadau mbalimbali wa maendeleo wajitokeze kutusaidia tufanikishe zoezi hilo la uvutaji maji ili kukabiliana na changamoto hiyo ya ukosefu wa maji kwani kwa sasa wanatumia maji ya visima vifupi ambavyo kipindi cha kiangazi hukauka,” alisema Sisaga.

Alisema kuwa endapo watafanikiwa kupata maji yatawasaidia kuweza kutumia muda wao kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo tofauti na sasa wanatumia muda mwingi kuhangaika na maji jambo ambalo ni changamoto kubwa.

“Mbali ya changamoto ya maji kijiji kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni za kawaida lakini wanakijiji wanajitahidi kuzitatua kadiri ya uwezo wao hivyo tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutuunga mkono kwenye jitihada zetu za kuleta maendeleo,” alisema Sisaga.

Aidha alisema kuwa wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kwa pamoja waweze kufanikiwa na kujikwamua na hali duni na kujiletea maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho Leyla Chabruma alisema kuwa wana ushirikiano mkubwa na wadau wa maendeleo ambao wanashirikiana na wananchi kwa ujumla hali inayoleta maendeleo ndani ya kijiji hicho ambacho kinategemea mapato yake kwa mauzo ya bidhaa mbalimbali ikiwemo mashamba, viwanja na vitu mbalimbali.

MWISHO.

Na John Gagarini, Kibaha

BAADHI ya wafanyabiashara na wasafiri wanaotumia kituo cha mabasi cha Maili Moja wameiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kuhakikisha wanatatua tatizo la taa kutowaka kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na kuwasababishia usumbufu mkubwa wataumiaji wa stendi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari moja ya wafanyabiashara wanaofanya biashara kwenye stendi hiyo nyakati za usiku Said Pengo alisema kuwa wamekuwa wakifanya biashara kwenye mazingira magumu kwenye eneo hilo.

Pengo alisema kuwa ukosefu wa taa hapo stendi ni changamoto kubwa sana inayowafanya kushindwa kufanya biashara kwa vizuri kutokana na kuzingirwa na giza.

“Tunaiomba Halmashauri yetu itusaidie tuweze kupatiwa huduma ya taa kwani taizo la ukosefu wa taa linatusababishia usumbufu mkubwa na tunashindwa kufanya biashara zetu kwa uhuru kutokana na giza linalokuwa linatanda,” alisema Pengo.

Alisema kuwa ni hatari kwa hali ya usalama wao pamoja na wateja wanaotumia eneo hili la stendi ya Maili Moja ambayo inatumiwa na watu wengi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Maili Moja Chichi Mkongota alikiri juu ya ukosefu wa umeme kwa kipindi hicho na kusema tayari alishatoa taarifa kwa mamlaka husika juu ya tatizo hilo.

Mkongota alisema kuwa alipotoa taarifa Halmashauri aliambiwa kuwa wanafanya utaratibu wa kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kupata taa za muda ili kukabiliana na tatizo hilo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Jenifa Omolo alisema kuwa tatizo lililopo ni kubwa kidogo kwani taa zilizowekwa zimeharibika na wanafanya mchakato wa kupata nyingine.

Omolo alisema taa zote 16 zilizopo hapo stendi zimeharibika ambapo gharama zake pamoja na kufungwa ni kiasi cha shilingi milioni 18 ambazo wanazitafuta kwa ajili ya kuzifunga.

“Tunafikiria kwa sasa tufunge taa za kawaida kwani hizo zilizopo ziliharibika na si mara ya kwanza kuzifunga kwani kila wakati zimekuwa zikiharibika,” alisema Omolo.

Aidha alisema kuwa wanahangaika kutafuta fedha hizo ili kuondoa changamoto hiyo ambayo imekuwa kero hata kwa wakala wanaokusanya ushuru wa stendi kutokana na usalama kuwa mdogo.

Mwisho.