Na
John Gagarini, Iringa
BARABARA
ya Kinyanambo C hadi Kisusa yenye urefu wa kilometa 131kwenye Jimbo la Mufindi
Kaskazini wilaya ya Mufindi mkoani Iringa imetengewa kiasi cha shilingi
billioni 1.2 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.
Hayo
yalisemwa na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa wakati
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mpanga Tazara akielezea juu ya
kukabiliana na changamoto ya barabara katika Jimbo hilo.
Mgimwa
alisema kuwa fedha hizo zimetengwa katika kipindi cha bajeti ambayo imeanza
mwezi huu na tayari ujenzi wa barabara hiyo umeshaanza kwa kuweka makalavati
ikiwa ni hatua za mwanzo za ujenzi huo.
“Barabara
hii tayari imeshakabidhiwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa kutoka
Halmashauri ya mji wa Mafinga hali ambayo sasa imeipandisha hadhi hivyo itakuwa
kwenye mikakati ya kuwekewa lami kupitia kampuni ya (MCC),” alisema Mgimwa.
Alisema
kuwa matengenezo hayo yataboresha ubora wa barabara hiyo ambayo ni tegemeo na
kuifanya kupitika wakati wote bila ya usumbufu na kurahisisha mawasiliano kwa
wananchi na kwa wakulima ili waweze kupeleka mazao yao kwenye masoko baada ya
kuvuna.
“Barabara
hii ambayo inapita kwenye maeneo ya Itimbo, Ihalimba, Usokamu, Mapanda na
Kisusa itakuwa ni moja ya barabara amabzo ziko kwenye mpango wa kuboreshwa na
baada ya kupandishwa hadhi halmashauri itapata unafuu ambapo fedha ambazo
zingetumika kuitengeneza sasa zitatumiwa kwenye shughuli nyingine za
maendeleo,” alisema Mgimwa.
Aidha
alisema kuwa barabara nyingine ni Kinyanambo A yenye urefu wa kilometa 151
ambayo inapita maeneo ya Msavanu, Mkombavanu, Sadani na Madibila nayo ujenzi
wake tayari umeanza.
Pia
alisema kuwa barabara ya Johns Corner yenye urefu wa kilometa 107 tayari
imejengwa kwa kiwango cha lami urefu wa kilometa tano nab ado ujenzi wake
unaendelea.
Alibainisha
kuwa barabara hiyo inapita kwenye maeneo ya Mtili, Ifwagi, Mdabulo, Ihanu,
Lulanga hadi Mpanga Tazara iko kwenye mpango wa kupandishwa hadhi ili
ichukuliwe na (TANROADS), na barabara ya Mpanga Tazara hadi Mlimba ambayo
imetengwa kiasi cha shilingi milioni 800.
“Barabara
ya Mpanga Tazara hadi mlimba kwani inaunganisha wilaya mbili za Mufindi na
Kilombero ni muhimu sana kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa wakulima kupeleka
mazao yao kwenye masoko ambayo yana bei nzuri kama vile Makambako, Kilombero,
Mbeya na Dar es Salaam,” alisema Mgimwa.
Mgimwa
alisema kuwa barara nyingine ziko kwenye mchakato wa kuwapata makandarasi kwa
ajili ya kuanza ujenzi katika bajeti inayoanzia mwezi huu wa Julai.
Mwisho.
Na
John Gagarini, Iringa
JIMBO
la Mufindi Kaskazini wilayani Mufindi mkoani Iringa linahitaji Transfoma 60 ili
kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa umeme kwenye kata tatu za Mpanga
Tazara, Ikwea na Ikongosi.
Changamoto
hiyo ya ukosefu wa umeme iko kwenye kata hizo kati ya kata 13 za Jimbo hilo
ambapo upatikanaji wa Transfoma hizo utasaidia kuondoa kabisa ukosefu wa
nishati hiyo kwa baadhi ya vitongoji.
Akizungumza
na waandishi wa habari juu ya changamoto kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini,
Mbunge wa Jimbo hilo Mahmoud Mgimwa alisema kuwa kwa sasa mchakato wa kutafuta
Transfoma unaendelea.
“Thamani
ya Transfoma moja ni kati ya shilingi milioni 40 na 60 na tunaendelea
kuhakikisha vinapatikana ili kuondoa kabisa tatizo la umeme ndani ya jimbo letu
lakini eneo kubwa tayari wanapata umeme,” alisema Mgimwa.
Alisema
kuwa anaamini kuwa umeme utapatikana muda si mrefu na kuwataka wananchi
kutokuwa na wasiwasi juu ya upatikanaji wa nishati hiyo muhimu ya umeme.
Aidha
alisema kuwa maeneo mengi kwa sasa yanapata umeme hadi vijijini na sehemu
chache zilizobaki tatizo hilo litakwisha na jitihada zinaendelea ili
kufanikisha suala hilo.
Mwisho.