Sunday, January 4, 2015

WALILIA WODI YA WAZAZI

Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wa Kijiji cha Kwaruhombo kwenye Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametoa kilio cha kujengewa wodi ya wazazi kwenye kituo cha afya cha Kwaruhombo ili wanawake wajawazito wasijifungue kwenye wodi za kawaida.
Akizungumza kijijini hapo wakati wa ziara ya maendeleo ya mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, Hadija Stambuli alisema kuwa akinamama wamekuwa wakijifungulia kwenye wodi hivyo kutokuwa na usiri.
Stambuli alisema kuwa hiyo imekuwa changamoto kubwa kwa akinamama wanapokwenda kujifungua wamekuwa wanashindwa kusitiriwa wakati wa uzazi.
“Tunakuomba Mbunge wetu utusaidie wakinamama ili tunapokwenda kujifungua kwani hakuna usiri hivyo tungepata jengo maalumu kwa ajili ya kujifungungulia ingekuwa vizuri,” alisema Stambuli
Akijibu malalamiko hayo mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kujifungua ni jambo jema na linahitaji usiri.
Ridhiwani alisema kuwa kwa kushirikiana na halmashauri ili kuhakikisha kunakuwa na jengo kwa ajili ya kinamama kujifungulia.
“Tutakaa na uongozi wa Halmashauri ili kuhakikisha kunakuwa na jengo maalumu kwa ajili ya kujifungulia ili kuwaondolea fadhaa akinamama wakati wakijifungua,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisikitishwa na matumizi mabaya ya mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa wanaopata rufaa na kuutaka uongozi wa kituo hicho kuhakikisha kinadhibiti matumizi hayo.

Mwisho.

WANANCHI WAMLALAMIKIA MWEKEZAJI

Na John Gagarini, Chalinze
WAWEKEZAJI kwenye Kijiji cha Changarikwa wametakiwa kufuata taratibu za kisheria ili kuondoa migogoro baina yao na wananchi.
Hayo yalisemwa na mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho kwenye ziara yake ya maendeleo jimboni humo.
Ridhiwani alitoa ushauri huo kufuatia wananchi hao kulalamika dhidi ya moja ya wawekezaji kwenye kijiji hicho kuchukua eneo lenye ukubwa wa hekari 500 na kutotimiza ahadi za kuwasaidia kwenye huduma za kijamii.
Moja ya wananchi wa Kijiji hicho Bakary Hatibu alisema kuwa mwekezaji huyo wakati anaomba ardhi hiyo moja ya masharti waliyokubaliana naye ni kuwajengea shule, zahanati na trekta lakini sasa ni miaka 15 hakuna hata kimoja alichotekeleza.
“Tumekuwa tukipata tabu kwani wakati mwingine tnazuiwa kupita kwenye maeneo amabayo yanamilikiwa na mwekezaji,” alisema Hatibu.
Kwa upande wake Mbunge huyo alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi dhidi ya wawekezaji kujipatia maeneo pasipo kutimiza masharti ya maombi ya ardhi.
“Jambo la kushangaza ni mwekezaji kupewa hekari 500 na kijiji jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya ardhi namba 5 ya mwaka 1999 inayosema kuwa kijiji kinauwezo wa kumpa mwekezaji si zaidi ya hekari 50,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa kama wameona mwekezaji hafai kwani wao ndiyo waliompa ardhi wanauwezo wa kumnyanganya kwa kufuata taratibu za kisheria endapo wataona ameshindwa kutekeleza ahadi wakati anaomba ardhi.
“Mnauwezo wa kumuondolea umiliki endapo atakiuka masharti kwani huo ni mkataba na endapo atakiuka masharti unaweza kuvunjika na ardhi ikarudishwa kwa wanakijiji,” alisema Ridhiwani.
Alisema ni vema wawekezaji wakatekeleza tatatibu ili kuwa na ushirikiano na wananchi ambao wanatoa ardhi yao ili nao wanufaike nayo.
Mwisho.


Saturday, January 3, 2015

SHULE HATARIN I KUWAANGUKIA WANAFUNZI

 Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa Kijiji cha Kibindu wilayani Bagamoyo wakimsikiliza Mbunge wao wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete alipotembelea Kijiji hicho wakati wa ziara yake ya kushukuru wananchi baada ya kumchagua kuwa mbunge miezi kadhaa iliyopita

 Akinamama wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete hayupo pichani baada ya kutembelea kijiji cha Kibindu kutoa shukrani kwa wananchi kumchagua kwenye nafasi hiyo miezi kadhaa iliyopita.

 Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kibindu wilayani Bagamoyo mkoani Pwani

 Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akizungumza na waandishi wa Habari mbele ya jengo la shule ya Msingi Kibindu ambalo lilianguka kufuatia mvua kubwa ziulizonyesha mwishoni mwa mwaka jana kushoto ni diwani wa kata ya Kibindu Mawazo Mkufya.


 Moja ya madarasa ya shule ya msingi Kibindu likiwa limebomoka kufuatia mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa mwaka jana.

 Diwani wa kata ya Kibindu Mawazo Mkufya aliyenyanyua mikono juu akitoa maelezo kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kulia aliyevaa kofia ya kijani kufuatia mvua kubwa kubomoa madarasa ya shule ya Msingi Kibindu

 Moja ya Madarasa ya shule ya Msingi Kibindu likiwa limeezuliwa paa kufuatia mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha madarasa mawili na ofisi ya mwalimu mkuu kuharibika.

 Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete akikabidhi mpira kwa baadhi ya viongozi wa timu za soka za Kijiji cha Kibindu

 Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akionge na wananchi wa Kijiji cha Kibindu alipofanya ziara ya kushukuru wananchi wa Jimbo hilo kwa kumchagua kushika nafasi hiyo miezi kadhaa iliyopita.

Wednesday, December 31, 2014

WAZEE ZAIDI YA 300 WAPATIWA MATIBABU MAALUMU

Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya Wazee zaidi ya 300 kati ya wazee 2,500 kwenye kata ya Kibaha katika halmashauri ya mji wa Kibaha mkoani Pwani wamepatiwa matibabu ya maradhi mbalimbali.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msamaria Mwema Huduma za Jamii (GSSST), Elisha Sibale alipozungumza na waandishi wa habari juu ya huduma walizotoa kwa wazee.
Sibale alisema kuwa wazee hao ambao wanahudumiwa na shirika lake ni wale wenye umri kuanzia miaka 60 walitibiwa magonjwa mbalimbali kama vile Kisukari, Macho, Wingi wa damu, Uoni hafifu na ugonjwa wa Ukimwi.
“Lengo la mradi huu ni kuwawezesha wazee kupata matibabu kwa wakati kwani wengi wao wamekuwa hawapati huduma hizo kutokana na jamii kutowathamini hivyo kujikuta wakiwa na changamoto za kuumwa maradhi mengi,” alisema Sibale.
Naye mtaalamu wa maabara kwenye zahanati ya Mwendapole Hans Amon alisema kuwa wazee hao wameanza kujiamini kwenda kupata matibabu ambapo awali walikuwa na woga kutokana na jamii kutowapeleka hospitali na kuwaacha.  
Kwa upande wake moja ya wazee walionufaika na mradi huo Hadija Mbwambo alisema kuwa wameweza kujua afya zao na kujitambua na kuona umuhimu wa kuwahi kupata matibabu.
 Mradi huo wa miaka miwili unatekelezwa kwenye mitaa ya Kwa Mfipa, Simbani, Mwendapole A na B kwa Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini Mwanabwito na Kikongo na matibabu hayo yalifadhiliwa na shirika hilo kwa kushirikiana na Help Age International na Pfizer Pharmaceuticals kuanzia Oktoba Mosi siku ya wazee duniani hadi Desemba mwaka jana na litakuwa endelevu.

Mwisho.  

AFA KWA KUJINYONGA KISA KUUGUA MUDA MREFU

Na John Gagarini, Kibaha
HUKU leo ikiwa ndiyo siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 2015 ikiwa imeanza fundi wa kuchomelea Michael Mpondo (36) mkazi wa Machinjioni wilayani Kibaha mkoani Pwani ameamua kukatisha uhai kwa kujinyonga.
Imeelezwa kuwa chanzo cha fundi huyo kuamua kuchukua maamuzi hayo magumu ya kuamua kujiua kunatokana na kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa wa Machinjioni Evarist Kamugisha alisema kuwa marehemu alijinyonga jirani na nyumba laiyokuwa akiishi.
Akielezea kwa kina tukio hilo Kamugisha alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 30 mwaka huu majaira ya saa 4:30 asubuhi baada ya mwili wake kukutwa ukininginia kwenye mti umbali wa mita 60 na alipokuwa akiishi.
“Marehemu usiku wa majira ya saa 2:30 kabla ya kifo chake alikula chakula na ndugu zake lakini aliondoka na jitihada za kumtafuta zilifanyika bila ya mafanikio lakini asubuhi yake ndipo watu walipouona mwili wake ukinginginia,” alisema Kamugisha.
Kamugisha alisema kuwa marahemu alikuwa akiumwa ambapo baada ya chumba chake kupelkuliwa kulikutwa dawa aina ya Panadoli pamoja na Amoxilini ambazo inasemekana alikuwa akizitumia.
“Marehemu alijinyonga kwa kutumia kamba ya nguo ya jeshi ambayo aliikata na kuwa kama kamba na kujinyonga nayo na hakuacha ujumbe wowote juu ya kifo chake,” alisema Kamugisha.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha kifo hicho ni marehemu kuugua muda mrefu na kukata tamaa ya maisha.

Mwisho.   

Sunday, December 28, 2014

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA YAWA TISHIO NA WAZEE WAFURAHIA HUDUMA ZA AFYA

Na John Gagarini, Bagamoyo
WATANZANIA wametakiwa kuzingatia ulaji wa vyakula na ufanyaji wa mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanasababisha vifo vya watu wengi hapa nchini.
Hayo yamesemwa hivi karibu kwenye Kijiji cha Msoga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na katibu mkuu wa Wizara ya Afya Dk Donan Mmbando alipotembelea kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha kisasa cha Kijiji hicho.
Dk Mmbando amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na ushindani mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza na yale yanayoambukiza katika kusababisha vifo hivyo jamii inapaswa kuangalia njia za kujikinga na magonjwa hayo.
Amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na presha na mengineyo ya namna hiyo yanasababisha vifo vingi hapa nchini kwa sasa ambapo serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuyadhibiti
Ametoa mfano wa baadhi ya nchi zilizoendelea zimekuwa zikitenga hadi kufikia asilimia 15 ya bajeti katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kupunguza vifo.
Amebainisha baadhi ya vitu vinavyochangia magonjwa hayo kuongezeka ni pamoja na uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na kutofanya mazoezi ni baadhi ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa hayo. 
Aidha amesema kuwa wao kama wizara wanasisistiza kinga zaidi ili kukabilina na magonjwa hayo na ndiyo maana wamekuwa wakitoa chanjo za kinga za magonjwa mbalimbali hasa kwa watoto ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Katibu mkkuu huyo wa wizara ya Afya amesema wamekuwa wakihamasisha ulaji wa chakula kwa mpangilio kwani chakula nacho kimekuwa ni changamoto ya ongezeko la magonjwa hayo kutokana na ulaji usiofaa, na wamekuwa wakikabili magonjwa hayo kwa kuzingatia taratibu za afya kupunguza vifo.
Amewataka wananchi kupata tiba sahihi ya magonjwa ili kupunguza madhara yatokanayo na magonjwa kuwa sugu pia wajiunge na mifuko ya afya ili kupunguza mzigo wa malipo kwa ajili ya matibabu.

Na John Gagarini, Kibaha
WAZEE wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wameipongeza serikali kwa kuwatengea kitengo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mwenyikiti wa wazee Mlandizi Mohamed Pongwe wakati wa mafunzo ya kuwahudumia wazee majumbani alisema kuwa kwa sasa huduma zao zimeboreshwa tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Pongwe alisema kuwa huduma kwa wazee kwenye kituo cha Afya cha Mlandizi na sehemu nyingine za huduma za afya zilikuwa ni mbaya kutokana na wazee kutopewa kipaumbele wakati wa kupata matibabu.
“Kwa sasa tunaishukuru serikali ya wilaya kwa kutuwekea kitengo chetu dirisha malumu kwa ajili ya kuwapatiwa huduma za matibabu kwenye kituo hicho cha afya cha Mlandizi kwani tunahudumiwa vizuri,” alisema Pongwe.
Alisema kuwa kama unavyojua wazee wana matatizo mengi hasa ya kiafya lakini walikuwa wakipuuzwa kwenye suala la afya hali iliyokuwa ikisababisha waishi katika hali mbaya za kiafya.
“Tunakwenda hospitali tukiwa hautna wasiwasi wa matibabu kwani tuna dirisha letu maaalumu tunapata huduma kwa upendo kutoka kwa wahudumu wa afya kwa kweli hata afya zetu zinaridhisha,” alisema Pongwe.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Elizabeth Sekaya ambaye ni muuguzi wagonjwa majumbani na huduma kwa wazee kutoka halmashauri ya wilaya alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wazee waweze kuwasaidia wenzao kwenye huduma za afya wakiwa majumbani.
“Tumekuwa tukiwapatia mafunzo haya mara kwa mara na tumeona mafanikio kwani sasa wameweza kuyakabili baadhi ya magonjwa wakiwa nyumbani ikiwa ni pamoja na ufanyaji wa mazoezi na lishe bora,” alisema Sekaya.
Sekaya alsiema kuwa wazee wanachangamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na maumivu ya mwili na kingine ni ususaji wa chakula endapo wanaudhiwa hivyo tunawajengea uwezo wa kujiamini na kukabilina na changamoto mbalimbali.
Mwisho.

  


Wednesday, December 24, 2014

PWANIYAONGEZA UFAULU DARASA LA SABA

Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani umeongeza ufaulu kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba ambapo jumla wanafunzi 13,242 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule mbalimbali za sekondari.
Akitangaza matokeo hayo mjini Kibaha katibu tawala wa mkoa huo Mgeni Baruani na kusema kuwa wanafunzi wote waliofaulu wamepata nafasi ya kujiunga na shule za sekondari.
Mgeni alisema kuwa Idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 23,562 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, ambapo idadi ya waliofaulu wasichana walikuwa ni 6,851 na wavulana ni 6,391 huku idadi ya wanafunzi wasichana ikionekana kuwa juu.
“Kwa mwaka huu mkoa umeweza kuongeza kiwango cha ufaulu kwa asilimia 56.2 kutoka asilimia 54 ya mwaka 2013 hivyo kushika nafasi ya 13 kitaifa na kuwa moja ya mikoa iliyofanya vizuri,” alisema Mgeni.
Aidha alisema kuwa kupatikana kwa nafasi kwa wanafunzi hao kumetokana na mpango madhubuti uliowekwa na sekretarieti ya mkoa kwa kushirikiana na halmashauri mpango wa kuongeza vyumba vya madarasa katika shule zote za sekondari.
“Shule mpya zimejengwa ambazo zilisaidia kuondoa tatizo la wanafunzi kukosa nafasi katika shule za serikali na tunawaomba wazazi na walezi ambao watoto wao wameichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wanawaandikisha watoto hao na kuhudhuria shuleni pasipo visingizio mbalimbali hali inayosababisha kuwakosesha haki yao ya msingi kielimu,” alisema Mgeni.
Kwa upande wake ofisa elimu mkoa wa Pwani Yusuph Kipengele alisema changamoto kubwa inayojitokeza kwa sasa ni baadhi ya wanafunzi wanaosoma shule za binafsi kutokwenda kuripoti katika shule wanazopangiwa.
“Wanafunzi hao wanaosoma shule za binafsi unakuta wanapata nafasi za juu lakini wanaokwenda kuripoti shule za sekondari wanzochaguliwa ni wachache labda wakipangiwa shule za sekondari za  Kibaha zinazomilikiwa na shirika la elimu Kibaha hivyo kuipa shida sana idara yetu”alisema Kipengele.
Kipengele alieleza kuwa wanafunzi hao wasioripoti katika shule za sekondari wanazopangiwa wanawanyima nafasi wanafunzi wengine ambao wangepata fursa ya kwenda kwenye shule hizo.
Mwisho