Monday, December 15, 2014

ZAIDI YA 500 WASHINDWA KUPIGA KURA UCHAGUZI WAHAIRISHWA

Na John Gagarini, Bagamoyo
HUKU uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ukiwa umefanyika juzi na matokeo yakiendelea kutoka wananchi 514 wa Kijiji cha Mwetemo Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo wameshindwa kupiga kura kutokana na uhaba wa karatasi za kupigia kura.
Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika kutokana na karatasi za kupigia kura kuwa chache hivyo watu wengine kushindwa kupiga kura ambapo watafanya uchaguzi huo Desemba 19.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kitongoji hicho kuangalia zoezi hilo la upigaji kura wa kuchagua viongozi akiwemo mwenyekiti na wajumbe watano msimamizi msaidizi wa uchaguzi Thomas Madega alisema kuwa wamekubaliana uchaguzi huo kufanyika siku hiyo.
“Karatasi za kupigia kura kwanza zilichelewa kwani zilifika kituoni saa 10 kasoro jioni na pia zilikuwa chache hivyo watu wachache walipiga kura na wengine walishindwa kupiga kabisa,” alisema Madega.
Madega alisema kuwa walikaa na viongozi wa vyama vyote na kukubaliana kusogezwa mbele zoezi la upigaji kura.
“Tumekubaliana na vyama vyote kusogeza uchaguzi huo hadi Ijumaa na wamekubali tumewaambia wawatangazie wafuasi wao juu ya hili,” alisema Madega.
Juu ya kuahirisha kwa muda mrefu tofauti na maeneo mengine ambayo yalikuwa na matatizo na uchaguzi kufanyika jana alisema kuwa wametoa muda mrefu ili waandaliwe vifaa vya upigaji kura kwa uhakika.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete alisema kuwa muda huo ni mrefu sana kwani maeneo mengine yalifanya uchaguzi kesho yake.
“Nadhani suala la siku ya kupiga kura lirudishwe nyuma kwani Ijumaa ni mbali sana hivyo kuna haja ya wahusika kuliangalia hilo ili wasipishane na wengine,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alishauri zoezi la namna ya kupiga kura washirikishwe zaidi wananchi kwani wale wanaowachagua ni viongozi wao hivyo wao ndiyo wenye nafasi kubwa ya kushauri na si viongozi wa vyama vya siasa.
Baadhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vilifanya uchaguzi wao jana Jumatatu badala ya Jumapili ni Kijiji cha Changarikwa, Vitongoji vya Kwamkula, Mkambala A na B, Kwaluguru A na B, Pugwe, Migola na Kwadivumo kwenye kata ya Mbwewe.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Ibrahim Matovu alipoulizwa juu ya baadhi ya maeneo kushindwa kupiga kura alisema kuwa bado hajapata takwimu sahihi ndiyo anafuatilia kujua changamoto hizo.
Uchuguzi mdogo uliofanywa na mwandishi wa habari hizi ulibaini zoezi la upigaji kura ulikumbwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa vifaa vya upigaji kura kama vile upungufu wa karatasi, picha za wagombea kuwekwa kwenye nembo ya chama kisichohusika na kukosekana kwa  fomu za wagombea wa nafasi ya ujumbe.

Mwisho.


Picha no 3942 msimamizi msaidizi wa kituo cha kupigia kura Kitongoji cha Mkwajuni kwenye Kijiji cha Miono wilaya ya Bagamoyo Faustina Oforo  akisubiria wapiga kura wa uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. 


Picha no 3940 Msimamizi msaidizi wa uchaguzi kitongoji cha Msikitini kwenye Kijiji cha Mbwewe wilaya ya Bagamoyo Said Mlinde kulia akiongea na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kushoto alipotembela kituo hicho kushuhudia zoezi la upigaji kura.
 

Monday, December 8, 2014

CHADEMA WATISHIA KUANDAMANA

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani kimetoa siku mbili hadi Desemba 10 kwa Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) Kibaha kuwarejesha wagombea wa nafasi mbalimbali kupitia chama hicho na endapo hatawarejesha watafanya maandamano kushinikiza warudishwe kuwania nafasi hizo.
Jumla ya wagombea 16 wa chama hicho wameondolewa kwenye kinyanganyiro cha kuwania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Deemba 14 mwaka huu, wakiwemo wenyeviti na wajumbe, kutokana na sababu mbalimbali za kukiuka sheria za uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Kibaha Mjini Mohamed Mnembwe alisema kuwa wametoa siku mbili Jumatatu na Jumanne ambapo Jumatano wataandamana kama endapo DAS hatawarejesha wagombea hao kwenye kinyanganyiro hicho.
Mnembwe alisema kuwa maandamano hayo watayafanya kuanzia kwenye ofisi za chama kwenda kwa DAS kudai haki za wagombea wao.
“Kuandamana ni haki ya kikatiba na si kuvunja sheria ni kutaka wagombea wetu warejeshwe kwani wameondolewa kwa uonevu na hawakutendewa haki kwani sababu zenyewe za kuwaengua si za halali,” alisema Mnembwe.
Alisema wagombea wao hawakupewa nafasi ya kupeleka ushahidi kwani wengi walienguliwa kwa madai kuwa si wakazi wa maeneo waliyoomba uongozi na kukosea kujaza fomu ikiwa ni pamoja na mtaa na mahali wanapoishi.
“Wengi waliwekewa pingamizi kuwa si wakazi wa maeneo hayo lakini wangethibitisha kwa kuwaita wahusika wakiwemo wenye nyumba kwani kusema kuwa balozi hamtambui si sawa kwani sisi pia tuna mabalozi wetu kikubwa wangepata ushahidi kama kweli si wakazi wa maeneo hayo, kwa upande wa ujazaji wa fomu ni mahali unapoishi na mtaa ndiyo walivyokosea na majina yao kuondolewa,” alisema Mnembwe.
Aidha alisema kuwa wao wanachotaka ni wagombea wao kurejeshwa kwenye nafasi za kuwania nafasi hizo na endapo DAS atafanya hivyo hawatafanya maandamano kwani wanataka uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.
“Tunajua muda umeisha ila wakirejeshwa tunauhakika wa kushinda kwenye uchaguzi huo na tutatoa taarifa polisi ili kuomba ulinzi kwani maandamano yetu ni ya amani na hatuna nia ya kufanya vurugu kikubwa tunachotaka ni haki kutendeka,” alisema Mnembwe.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA Jimbo la Kibaha alitaja maeneo ambako wagombea wake wameondolewa kuwa ni Maili Moja 2, Kongowe 6, Visiga 3, Vikawe Shuleni 1,Miswe Chini 1 na Miwaleni 3.
Hivi karibuni DAS Sozi Ngate alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo alisema kuwa kama wanaona wameonewa waende mahakamani kudai haki yao.
Mwisho.


















AFA KWA KUCHOMWA KISU NA WATU WASIOFAHAMIKA

Na John Gagarini, Kibaha
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Juma Abdala (65) mkulima wa Kitongoji cha Kwa Mwaleni kijiji cha Mbwewe kata ya Mbwewe wilayani Bagamoyo mkoani Pwani amekufa kwa kuchomwa kwa visu na watu wasiofahamika.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa mzee huyo aliitwa na vijana wawili waliofika nyumbani kwake na kumwita pembezoni mwa nyumba yake kisha kumshambulia na kumwua.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi ofisa mtendaji wa kijiji cha Mbwewe Ramadhan Mwanaagonile alisema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 6 mwaka huu majira ya saa 1:30 usiku Kitongojini hapo.
Mwanaagonile alisema kuwa siku ya tukio vijana hao ambao hawafahamiki walifika nyumbani kwa marehemu na kumtaka waongee naye wakati huo marehemu alikwenda kwenye kibanda jirani kwa ajili ya kunywa kahawa.
“Watu hao walipomuulizia marehemu walijibiwa kuwa hayupo walitaka aitwe ili waongee naye ndipo alipoitwa na kumtaka wakazungumze pembeni na ndipo walipokwenda kwenye ua wa nyumba yake na kuanza kuongea,” alisema Mwanaagonile.
Alisema baada ya muda walisikia marehemu akipiga kelele kuomba msaada huku akisema kuwa anakufa na walipokwenda walikutwa kachomwa kisu kitovuni na kifuani na mkononi.
“Marehemu alijaribu kukimbia kwenda waliko watu lakini alishindwa na kuanguka na watu walipofika walimkuta akiwa anatokwa na damu nyingi ambazo zilisababisha kifo chake huku wale watu wakiwa hawaonekani kwani walikimbia kusikojulikana,” alisema Mwanaagonile.
Aidha alisema taarifa zilitolewa kituo cha Polisi cha Mbwewe ambao walifika na kuuchukua mwili wa marehemu na baadaye mwili ulichunguzwa na daktari kisha kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
“Tulijaribu kuwatafuta vijana hao bila ya mafanikio na hatukukuta chochote pale palikotokea tukio watu hao hawakumchukulia kitu chochote kwnai alikuwa na simu na vitu vingine lakini waliviacha,” alisema Mwanaagonile.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema bado halijafikishwa ofisini kwake na kusema kuwa atafuatilia na kulitolea taarifa.
Mwisho.



Sunday, December 7, 2014

OUT KUTUMIA MAMILIONI KUFUNDISHA WALIMU WA MASOMO YA SAYANSI



Na John Gagarini, Kibaha
CHUO Kikuu Huria Tanzania (OUT) kimepata fedha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 50 kutoka benki ya dunia kwa ajili ya kuwajengea uwezo walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati hapa nchini.
Aidha fedha hizo pia zitatumika kwa ajili ya kujenga maabara mchanganyiko, mabweni na ofisi za walimu kwa lengo la kuboresha ufundishaji wa masomo chuoni hapo.
Hayo yalibainishwa na mgeni rasmi kwenye mahafali ya kwanza ya OUT kituo cha mkoa wa Pwani, Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho kitengo cha Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa Profesa Modest Varisanga.
Prof. Varisanga alisema kuwa kuna uhaba mkubwa wa walimu wa masomo hayo hivyo wameamua kuwekeza kwenye masomo hayo kwani ndiyo msingi wa kupata wataalamu mbalimbali.
“Chuo kinaendelea kujiimarisha kwenye maeneo mbalimbali pamoja na kuhakikisha tunazalisha wataalamu na msingi ni masomo ya Sayansi ndiyo sababu ya kuweka mkakati wa makusudi wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo walimu hao wanaosoma kwenye chuo chetu,” alisema Prof Varisanga.
Alisema kuwa fedha hizo pia zitatumika kujenga maabara mabweni na ofisi za walimu ili kuboresha utoaji elimu kwa wanachuo ambao hupata masomo yao kwa elimu ya masafa.
Katika hatua nyingine alisema kuwa wameiomba serikali kuvibadili vyuo hivyo kutoka vituo hadi kuwa vyuo vya mikoa ambapo maombi hayo yamefikishwa kwenye baraza la Mawaziri na yamekubaliwa huku kwa sasa mchakato ukiwa unaendelea.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kituo cha mkoa wa Pwani Abdala Alli alisema kuwa elimu ya masafa ambayo inatolewa na chuo hicho imekuwa suluhisho la elimu hapa nchini wakiwemo wanawake.
Alli alisema kuwa elimu ya masafa ndiyo elimu bora kwa sasa kwani inatolewa huku kwa wale watumishi wakiendelea kufanyakazi bila ya kuathiri utendaji kazi tofauti na elimu ya moja kwa moja ambayo humtaka mwanachuo kukaa darasani pamoja na kuwa kwenye bweni ambapo gharama zake ni kubwa.
Akisoma risala ya wahitimu Stella Mapunda alisema kuwa kituo chao kinakabiliwa na uhaba wa walimu pamoja na kumbi za mikutano na mihadhara kwa ajili ywa wanachuo kujadiliana na kujifunzia.
Mapunda alisema kwa sasa wanatumia majengo ya Shirika la Elimu Kibaha ambayo hayatoshelezi mahitaji ya wanachuo ambapo kumekuwa na ongezeko la udahili wa wanachuo wapya kila mwaka.
Jumla ya wahitimu 98 toka kituo cha mkoa wa Pwani walihitimu na kutunukiwa vyeti ngazi mbalimbali kwenye mahafali ya Kitaifa yaliyofanyika kwenye makao makuu ya chuo hicho yaliyopo Bungo wilayani Kibaha wiki iliyopita.
Mwisho.       

Saturday, December 6, 2014

WANAFUNZI WALIOPATA UJAUZITO WANENA

Na John Gagarini, Rufiji
BAADHI ya wanafunzi walioacha masomo baada ya kupata ujauzito  Wilayani Rufiji mkoani Pwani wameonyesha kujutia makosa hayo na kumuomba mkuu wa wilaya kuwasaidia warudi shuleni.
Wanafunzi hao ambao walifika kituo cha polisi cha wilaya ya Rufiji kufuatia agizo la mkuu wa Nurdin Babu kuwataka wafike kwenye kituo hapo na kutakiwa  kuwataja wale waliowapa mimba ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Hata hivyo zoezi la kuwataja wahusika wa mimba hizo lilikuwa gumu kutokana na kubainika kuwa wenye watoto hao baadhi yao walikuwa ni wajenzi wa barabara ya kuelekea mikoa ya Kusini.
Wakizungumza na waandishi wa habari wanafunzi hao ambao walikuwa wakisoma kidato cha pili shule ya sekondari ya Kazamoyo walifika kituoni hapo wakiwa na wazazi na walezi wao huku wakiwa na watoto wao mgongoni wamesema wako tayari kurudi shuleni na kuendelea na masomo.
Semeni Ismail aliyekuwa akisoma kidato cha pili mwaka huu alikuwa akisoma shule ya sekondari Kazamoyo alisema kuwa yeye alipata ujauzito baada ya kukosa huduma muhimu ya shuleni hali ambayo ilimfanya aache shule na kuwa mitaani kwani alikuwa akiishi na mama yake ambaye wakati huo hakuwepo nyumbani kwani alikuwa akiumwa.
“Maisha yalikuwa magumu chakula cha shida ada na mahitaji mengine nilikuwa nikiyapata kwa shida sana kwani baba aliashafariki na mama alikuwa mgonjwa sana, ndipo nilipokutana na huyo mwanaume ambaye alikuwa fundi wa ujenzi kwenye barabara ya Kusini na baada ya ujauzito alinikataa hadi sasa hakuna mawasiliano yoyote,” alisema Semeni.
Kwa upande wake Hafsa Twalibu alisema kuwa yeye alifukuzwa shule baada ya kufanya makosa ikiwa ni pamoja na kuchana barua ya kumsimamisha masomo kwa makosa mbalimbali.
“Nilifanya makosa na mlezi wangu alipokwenda shule kuusihi uongozi wa shule unisamehe ikiwa ni pamoja na kufanya adhabu ambazo nilikataa kuzifanya walikataa na kusema labda nihamishiwe shule nyingine lakini siyo pale tena na waligoma kabisa mimi kuendelea kusoma pale ndipo alipoacha shule na kujihusisha na masuala ya kimapenzi na kupata ujauzito huo,”  alisema Hafsa.
Wanafunzi hao walisema kuwa wanaomba msamaha kwa makosa waliyo yafanya na kusema kuwa wako tayari kuendelea na masomo kama walivyo wenzao na kusema hawatarudia tena.
Naye moja ya wazazi Sauda Said alisema kuwa walikuwa wakijitahidi kuwapatia mahitaji muhimu watoto wao ili wasome lakini kumbe walikuwa wakijihusisha na masuala ya kimapenzi hata hivyo wanapoulizwa waliowapa mimba hawataki kuwataja.
Mkuu wa wilaya ya Rufiji Babu alisema kuwa kwa kuwa wanafunzi hao wameomba msamaha na kusema kuwa wataendelea na masomo atawaombea wanafunzi hao ili ikiwezekana Januari mwaka 2015 waendelee na masomo yao.
Jumla ya wanafunzi 26 wa shule za sekondari kwenye wilaya ya Rufiji walipata mimba wakiwa vidato mbalimbali hali iliyosababisha washindwe kuendelea na masomo yao ambapo wawili kati yao walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
Mwisho.



Wednesday, December 3, 2014

WAWILI WAKUTWA NA MAGUNIA 12 YA BANGI


Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wawili wakazi wa mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kupatikana na magunia 12 ya Bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na askari waliokuwa doria.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea huko Desemba 2 mwaka huu majira ya 4.40 usiku kwenye pori la Vikawe kata Pangani wilaya ya Kibaha.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Sabas Petro (25) na Emily Magomba (21) ambao walikamatwa na askari waliokuwa doria.
“Watuhumiwa walikutwa wakishusha magunia hayo kwenye pori hilo kwa lengo la kuyaficha kutoka kwenye gari namba T 773 ELB,” alisema Kamanda Matei.
Mwisho.

Tuesday, December 2, 2014

JENGENI BARABARA ZA LAMI

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI za wilaya mkoani Pwani zimetakiwa kuwa na ubunifu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kujenga barabara badala ya kuisubiri Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Kutokana na kutokuwa na ubunifu baadhi ya wilaya hazina hata kilomita moja ya barabara ya iliyojengwa kwa kiwango cha lami.
Ushauri huo ulitolewa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza, wakati wa kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo.
Mahiza alisema kuwa inashangaza kuona kuwa hakuna jitihada zozote zikifanyika za kuhakikisha kunakuwa na ujenzi wa barabara za lami.
“Kaeni na wadau wenu jengeni barabara za lami hata kilomita moja moja mfano mzuri ni Halmashauri ya Mji wa Kibaha imejenga lami kidogo kidogo kwenye baadhi ya maeno lakini zingine hazifanyi jitihada kama hizo,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kama halamashauri hazina uwezo zinaweza kuingia mikataba na wajenzi wa barabara ili baadaye wawalipe.
“Mji wa Kibaha ulikopa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zake kwa kiwango cha lami kwa hiyo na Halmashauri nyingine ziige mfano huu kwani kikubwa ni ubunifu msikubali kukaa tu,” alisema Mahiza.
Alibainisha kuwa kuna Halmashauri zina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza kuwasaidia katika kufanikisha ujenzi huo kwani haipendezi kutokuwa na lami ambayo inapendeza na inapunguza ukarabati wa mara kwa mara unaotumia fedha nyingi.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Injinia Tumaini Sarakikya alisema uwezo wao siyo mkubwa kutokana na kutokuwa na fedha nyingi kwani wanategemea kutoka serikalini.
Injinia Sarakikya alisema kuwa wao wataendelea kuboresha barabara pamoja na miundombinu yake ikiwemo madaraja, makalavati na shughuli nyingine zinazohusiana na masuala mazima ya barabara.

Mwisho.