Sunday, December 7, 2014

OUT KUTUMIA MAMILIONI KUFUNDISHA WALIMU WA MASOMO YA SAYANSI



Na John Gagarini, Kibaha
CHUO Kikuu Huria Tanzania (OUT) kimepata fedha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 50 kutoka benki ya dunia kwa ajili ya kuwajengea uwezo walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati hapa nchini.
Aidha fedha hizo pia zitatumika kwa ajili ya kujenga maabara mchanganyiko, mabweni na ofisi za walimu kwa lengo la kuboresha ufundishaji wa masomo chuoni hapo.
Hayo yalibainishwa na mgeni rasmi kwenye mahafali ya kwanza ya OUT kituo cha mkoa wa Pwani, Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho kitengo cha Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa Profesa Modest Varisanga.
Prof. Varisanga alisema kuwa kuna uhaba mkubwa wa walimu wa masomo hayo hivyo wameamua kuwekeza kwenye masomo hayo kwani ndiyo msingi wa kupata wataalamu mbalimbali.
“Chuo kinaendelea kujiimarisha kwenye maeneo mbalimbali pamoja na kuhakikisha tunazalisha wataalamu na msingi ni masomo ya Sayansi ndiyo sababu ya kuweka mkakati wa makusudi wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo walimu hao wanaosoma kwenye chuo chetu,” alisema Prof Varisanga.
Alisema kuwa fedha hizo pia zitatumika kujenga maabara mabweni na ofisi za walimu ili kuboresha utoaji elimu kwa wanachuo ambao hupata masomo yao kwa elimu ya masafa.
Katika hatua nyingine alisema kuwa wameiomba serikali kuvibadili vyuo hivyo kutoka vituo hadi kuwa vyuo vya mikoa ambapo maombi hayo yamefikishwa kwenye baraza la Mawaziri na yamekubaliwa huku kwa sasa mchakato ukiwa unaendelea.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kituo cha mkoa wa Pwani Abdala Alli alisema kuwa elimu ya masafa ambayo inatolewa na chuo hicho imekuwa suluhisho la elimu hapa nchini wakiwemo wanawake.
Alli alisema kuwa elimu ya masafa ndiyo elimu bora kwa sasa kwani inatolewa huku kwa wale watumishi wakiendelea kufanyakazi bila ya kuathiri utendaji kazi tofauti na elimu ya moja kwa moja ambayo humtaka mwanachuo kukaa darasani pamoja na kuwa kwenye bweni ambapo gharama zake ni kubwa.
Akisoma risala ya wahitimu Stella Mapunda alisema kuwa kituo chao kinakabiliwa na uhaba wa walimu pamoja na kumbi za mikutano na mihadhara kwa ajili ywa wanachuo kujadiliana na kujifunzia.
Mapunda alisema kwa sasa wanatumia majengo ya Shirika la Elimu Kibaha ambayo hayatoshelezi mahitaji ya wanachuo ambapo kumekuwa na ongezeko la udahili wa wanachuo wapya kila mwaka.
Jumla ya wahitimu 98 toka kituo cha mkoa wa Pwani walihitimu na kutunukiwa vyeti ngazi mbalimbali kwenye mahafali ya Kitaifa yaliyofanyika kwenye makao makuu ya chuo hicho yaliyopo Bungo wilayani Kibaha wiki iliyopita.
Mwisho.       

Saturday, December 6, 2014

WANAFUNZI WALIOPATA UJAUZITO WANENA

Na John Gagarini, Rufiji
BAADHI ya wanafunzi walioacha masomo baada ya kupata ujauzito  Wilayani Rufiji mkoani Pwani wameonyesha kujutia makosa hayo na kumuomba mkuu wa wilaya kuwasaidia warudi shuleni.
Wanafunzi hao ambao walifika kituo cha polisi cha wilaya ya Rufiji kufuatia agizo la mkuu wa Nurdin Babu kuwataka wafike kwenye kituo hapo na kutakiwa  kuwataja wale waliowapa mimba ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Hata hivyo zoezi la kuwataja wahusika wa mimba hizo lilikuwa gumu kutokana na kubainika kuwa wenye watoto hao baadhi yao walikuwa ni wajenzi wa barabara ya kuelekea mikoa ya Kusini.
Wakizungumza na waandishi wa habari wanafunzi hao ambao walikuwa wakisoma kidato cha pili shule ya sekondari ya Kazamoyo walifika kituoni hapo wakiwa na wazazi na walezi wao huku wakiwa na watoto wao mgongoni wamesema wako tayari kurudi shuleni na kuendelea na masomo.
Semeni Ismail aliyekuwa akisoma kidato cha pili mwaka huu alikuwa akisoma shule ya sekondari Kazamoyo alisema kuwa yeye alipata ujauzito baada ya kukosa huduma muhimu ya shuleni hali ambayo ilimfanya aache shule na kuwa mitaani kwani alikuwa akiishi na mama yake ambaye wakati huo hakuwepo nyumbani kwani alikuwa akiumwa.
“Maisha yalikuwa magumu chakula cha shida ada na mahitaji mengine nilikuwa nikiyapata kwa shida sana kwani baba aliashafariki na mama alikuwa mgonjwa sana, ndipo nilipokutana na huyo mwanaume ambaye alikuwa fundi wa ujenzi kwenye barabara ya Kusini na baada ya ujauzito alinikataa hadi sasa hakuna mawasiliano yoyote,” alisema Semeni.
Kwa upande wake Hafsa Twalibu alisema kuwa yeye alifukuzwa shule baada ya kufanya makosa ikiwa ni pamoja na kuchana barua ya kumsimamisha masomo kwa makosa mbalimbali.
“Nilifanya makosa na mlezi wangu alipokwenda shule kuusihi uongozi wa shule unisamehe ikiwa ni pamoja na kufanya adhabu ambazo nilikataa kuzifanya walikataa na kusema labda nihamishiwe shule nyingine lakini siyo pale tena na waligoma kabisa mimi kuendelea kusoma pale ndipo alipoacha shule na kujihusisha na masuala ya kimapenzi na kupata ujauzito huo,”  alisema Hafsa.
Wanafunzi hao walisema kuwa wanaomba msamaha kwa makosa waliyo yafanya na kusema kuwa wako tayari kuendelea na masomo kama walivyo wenzao na kusema hawatarudia tena.
Naye moja ya wazazi Sauda Said alisema kuwa walikuwa wakijitahidi kuwapatia mahitaji muhimu watoto wao ili wasome lakini kumbe walikuwa wakijihusisha na masuala ya kimapenzi hata hivyo wanapoulizwa waliowapa mimba hawataki kuwataja.
Mkuu wa wilaya ya Rufiji Babu alisema kuwa kwa kuwa wanafunzi hao wameomba msamaha na kusema kuwa wataendelea na masomo atawaombea wanafunzi hao ili ikiwezekana Januari mwaka 2015 waendelee na masomo yao.
Jumla ya wanafunzi 26 wa shule za sekondari kwenye wilaya ya Rufiji walipata mimba wakiwa vidato mbalimbali hali iliyosababisha washindwe kuendelea na masomo yao ambapo wawili kati yao walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
Mwisho.



Wednesday, December 3, 2014

WAWILI WAKUTWA NA MAGUNIA 12 YA BANGI


Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wawili wakazi wa mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kupatikana na magunia 12 ya Bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na askari waliokuwa doria.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea huko Desemba 2 mwaka huu majira ya 4.40 usiku kwenye pori la Vikawe kata Pangani wilaya ya Kibaha.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Sabas Petro (25) na Emily Magomba (21) ambao walikamatwa na askari waliokuwa doria.
“Watuhumiwa walikutwa wakishusha magunia hayo kwenye pori hilo kwa lengo la kuyaficha kutoka kwenye gari namba T 773 ELB,” alisema Kamanda Matei.
Mwisho.

Tuesday, December 2, 2014

JENGENI BARABARA ZA LAMI

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI za wilaya mkoani Pwani zimetakiwa kuwa na ubunifu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kujenga barabara badala ya kuisubiri Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Kutokana na kutokuwa na ubunifu baadhi ya wilaya hazina hata kilomita moja ya barabara ya iliyojengwa kwa kiwango cha lami.
Ushauri huo ulitolewa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza, wakati wa kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo.
Mahiza alisema kuwa inashangaza kuona kuwa hakuna jitihada zozote zikifanyika za kuhakikisha kunakuwa na ujenzi wa barabara za lami.
“Kaeni na wadau wenu jengeni barabara za lami hata kilomita moja moja mfano mzuri ni Halmashauri ya Mji wa Kibaha imejenga lami kidogo kidogo kwenye baadhi ya maeno lakini zingine hazifanyi jitihada kama hizo,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kama halamashauri hazina uwezo zinaweza kuingia mikataba na wajenzi wa barabara ili baadaye wawalipe.
“Mji wa Kibaha ulikopa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zake kwa kiwango cha lami kwa hiyo na Halmashauri nyingine ziige mfano huu kwani kikubwa ni ubunifu msikubali kukaa tu,” alisema Mahiza.
Alibainisha kuwa kuna Halmashauri zina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza kuwasaidia katika kufanikisha ujenzi huo kwani haipendezi kutokuwa na lami ambayo inapendeza na inapunguza ukarabati wa mara kwa mara unaotumia fedha nyingi.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Injinia Tumaini Sarakikya alisema uwezo wao siyo mkubwa kutokana na kutokuwa na fedha nyingi kwani wanategemea kutoka serikalini.
Injinia Sarakikya alisema kuwa wao wataendelea kuboresha barabara pamoja na miundombinu yake ikiwemo madaraja, makalavati na shughuli nyingine zinazohusiana na masuala mazima ya barabara.

Mwisho.

Wednesday, November 26, 2014

BONDIA KIBAHA ATAKA KUZICHAPA NA MACHALI NA NYILAWILA

Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA Zumba Kukwe wa Maili Moja wilayani Kibaha Mkoani Pwani ambaye leo anapambana na bondia Sweet Kalulu amesema kuwa lengo lake kubwa ni kupambana na Thomas Mashali au Kalama Nyilawila.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha wakati wakipima uzito na kupima afya kwenye ukumbi wa Container Bar alisema kuwa leo atamshinda mpinzani wake raundi ya tatu.
Kukwe alisema kuwa kwenye pambano lake la leo anatarajia kufanya vizuri kwa kumpiga mpinzani wake na kuwapa raha wapenzi wa ngumi wa mkoa wa Pwani.
“Nimejipanga vizuri kwenye pambano langu na sitawaangusha wapenzi wangu kwani niko kwenye uwanja wa nyumbani, naangalia mbele zaidi ninaowataka ni Mashali au Nyilawila,” alisema Kukwe.
Aidha alisema kuwa anatarajia kuiweka Pwani kwenye ramani ya mchezo huo wa ngumi hivyo malengo yake ni kupambana na mabingwa wa Tanzania.
“Najiamini kuwa nina uwezo na baada ya pambano la leo safari yangu ya kuanza kutamba kwenye ulimwengu wa ngumi itaanza na nitahakikisha ngumi inakuwa juu mkoani Pwani,” alisema Kukwe.
Kwa upande wake Kalulu alisema kuwa yeye hana maneno mengi anachosubiri ni muda tu ufike na kila mtu atajua  nini kilichomleta Kibaha kwnai anauwezo.
Naye muandaaji wa pambano hilo George Nyasulu alisema kuwa lengo la kuandaa pambano hilo ni kuwahamasisha vijana wanaopenda mchezo huo kujitokeza ili kucheza mchezo huo.
Nyasulu alisema kuwa huo ni mwanzo kwani baadaye ataandaa mapambano mengi zaidi na nia ni kutoa bingwa wa ngumi Taifa kwani vijana wana uwezo.Jumla ya mapambano saba ya utangulizi yatachezwa.

Mwisho.
Mabondia Sweet Kalulu kushoto na Zumba Kukwe kulia katikati mwandaaji wa pambano hilo George Nyasalu akishuhudia mara baada ya kupima uzito na afya kabla ya pambano lao 
 

Tuesday, November 25, 2014

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUKATIA BIMA BIASHARA ZAO KUKABILIANA NA MAJANGA

Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA maduka kadhaa kungua moto eneo la Maili Moja wilayani Kibaha  wafanyabiashara mkoani Pwani wameshauriwa kukatia bima biashara zao ili kukabiliana na hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na majanga kama hayo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mara baada ya kuwakabidhi msaada wa fedha kiasi cha shilingi 810,000 wahanga wa moto huo mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa Pwani, Abdala Ndauka alisema kuwa moto huo umewapa hasara kubwa wafanyabiashara hao.
Ndauka alisema kuwa imefika wakati sasa kwa wafanyabiashara kukata bima za biashara zao ili mara wapatapo majanga kama ya moto au wizi bima itawafidia na wataweza kuendelea vizuri na biashara bila ya kuyumba.
“Ule moto umesababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wenzetu kwani hawakuweza kuokoa bidhaa zote ziliteketea kwa moto hivyo umuhimu wa bima umeonekana kwani wangekuwa nayo wangelipwa,” alisema Ndauka.
Akizungumzia juu ya msaada huo alisema kuwa baada ya wenzao kupata tatizo hilo walichanga fedha hizo kama pole kwa wenzao watatu ambao walipata tatizo hilo la kuunguliwa maduka yao ya biashara mbalimbali.
Aidha alisema fedha hizo zimechangwa na sehemu ya wafanyabiashara wanachama wa JWT ambao ni zaidi ya 300 kati ya 800 wanaounda umoja huo.
“Kutokana na tukio  hili tumeazimia kuanzisha mfuko wa maafa ili tuweze kusaidiana mara yanapotokea matatizo kama haya na fedha zitakazopatikana ziweze kuwasaidia waathirika,” alisema Ndauka.
Naye Ally Gonzi moja ya waathirika wa moto huo aliwashukuru wanajumuiya hiyo kwa msaada walioutoa na kusema kuwa serikali inapaswa kuhakikisha mkoa huo unakuwa na huduma ya zimamoto kwani moto ulipotokea hawakuweza kupata huduma hiyo licha ya kuwa wanalipia huduma hiyo.
Gonzi alisema kuwa endapo mkoa huo ungekuwa na gari la zimamoto basi mali zilizoteketea zingeweza kuokolewa hasa ikizingatiwa  ofisi za kikosi hicho ziko jirani kabisa na tukio lilipotokea ambapo waathirika wengine ni Urisha Mwembamba na Adam Mwasha.

Mwisho.

Wednesday, November 19, 2014

DC KUDHIBITI MADK WEZI WA DAWA

Na John Gagarini, Rufiji
MKUU wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Nurdin Babu amesema atawachukulia hatua kali baadhi ya madaktari watakaobainika kuiba dawa na kuziuza kwenye maduka ya dawa.
Aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Nyambili-Bungu wilayani humo wakati akielezea umuhimu wa wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Babu alisema kuwa baadhi ya madaktari kwenye zahanati vijijini wamekuwa wakiiba dawa muhimu kisha kuziuza kwenye maduka hayo na kuacha maboksi matupu wakidai kuwa zimetumiwa na kuisha.
“Dawa hizi si sukari kusema watu wanalamba kila wakati lakini ni baadhi ya madaktari wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakiziuza dawa hizo na kila wananchi wanapoandikiwa dawa wanaambiwa zimekwisha je zinakwishaje wakati wagonjwa hawajapewa tutawashughulikia nyie tupeni taarifa,” alisema Babu.
Alisema kutokana na hali hiyo anaacha namba yake ya simu ili apewe taarifa za madaktari wanaofanya mchezo huo ili akabiliane nao na kuwataka wananchi kutoa taarifa.
Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Rufiji Dk Michael Michael alisema njia rahisi ya kupata matibabu ni kujiunga na mfuko huo ambapo familia ya watu sita inalipa 10,000 kwa mwaka lakini kwa wasiojiunga wanalipa 3,000 kila wanapomwona daktari.
“Uzuri wa sasa ni kwamba kutakuwa na kamati ya Kijiji ya afya ambayo itakuwa na uwezo wa kununua dawa wanazoona zimekwisha au zinazohitaji kutokana na tatizo la eneo husika,” alisema Dk Molel.
Aidha alisema kuwa wataingia mikataba na wamiliki wa maduka ili dawa zinapokwisha wawe wanawapa wagonjwa ili kuondoa kero na kusema kuwa mfumo huu utaondoa changamoto ya dawa.
Naye mratibu wa CHF wilaya hiyo Rashid Mihuka alisema kuwa kutaanzishwa madirisha ya dawa kwa ajili ya wanachama wa mfuko huo ili kuboresha huduma kwa wateja wa mfuko huo.
Mwisho.