Sunday, April 21, 2013

RIZIWANI KUKABIDHI KOMBE


Na John Gagarini, Kibaha
RIZIWANI Kikwete kesho anatarajiwa kuwakabidhi kombe la ubingwa mabingwa wa mkoa wa Pwani wa daraja la tatu timu ya Kiluvya United.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa chama cha soka mkaoni Pwani (COREFA) Victor Masangu alisema kuwa Riziwani ndiye atakayekuwa  mgeni rasmi kwenye sherehe za kuikabidhi kombe timu hiyo kwenye uwanja wa Ruvu Jkt Mlandizi wilayani Kibaha.
Alisema kuwa maandalizi ya sherehe hizo za kuwakabidhi ubingwa United zimekamilika na kinachosubiriwa ni muda ili kuikabidhi ubingwa timu hiyo.
“Ili kunogesha sherehe hizo mabingwa hao wa mkoa wanatarajiwa kucheza siku hiyo na timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Ruvu Shooting kwa lengo la kusindikiza sherehe hizo,” alisema Masangu.
Aidha alisema kuwa timu hiyo iliweza kunyakua ubingwa wa mkoa kwa kuifunga timu ya Baga Friends magoli 3-0 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.
“Tunawapongeza viongozi, wachezaji, wanachama na wadau wa timu hiyo ya Kiluvya United kwa ushindi walioupata na tunawataka wajipange vizuri kwa ajili ya kuwakilisha mkoa kwenye ligi ya Kanda ambako watakutana na mabingwa wa mikoa mingine,” alisema Masangu.
Aliwataka wadau na mashabiki wa soka mkoa Pwani kujitokeza kuipongeza timu yao kwa kufanikiwa kuwa mabingwa ili kuwapa hamasa ya kujiandaa vema na mashindano ngazi ya Taifa.
Mwisho.

WATOTO WACHANAGA KUPATIWA CHANJO

Na John Gagarini, Kibaha

JUMLA ya watoto 2,628 kati ya watoto 38,356 wenye umri chini ya mwaka mmoja wanatarajiwa kupatiwa chanjo mbalimbali mkoani Pwani.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Simon Malulu mratibu wa maandalizi ya uzinduzi wa chanjo kitaifa yatakayofanyika Aprili 22 hadi 28 shule ya Msingi Mlandizi wilayani Kibaha ambapo mgeni rasmi atakuwa mke wa Raisi Mama Salama Kikwete.

Malulu alisema kuwa hiyo ni awamu ya tatu ya chanjo ambapo watoto hao hawakuipata ilipoanza Januarimwakahuu    

“Jumla ya vituo kimkoa ni 258 na vinavyotoa chanjo ni 206 ambayo ni sawa na asilimia 80," alisema Malulu.

Alitaja chanzo zitakazotolewa kuwa ni homa ya matumbo, homa ya uwati wa mgongo na magonjwa mengine.

“Mkoa umeweza kupiga hatua katika kiwango cha utoaji chanjo zote na kuwa juu ya lengo la taifa la asilimia 90,” alisema Malulu.

Malulu ambaye pia ni ofisa afya wa mkoa alisema kuwa uzinduzi wa Chanjo hiyo inalenga watoto ambao hawakukamilisha ama hawajawahi kupatiwa chanjo mbalimbali.

Akizungumzia kukamilika kwa maandalizi ya shughuli hiyo mkuu wa wilaya
ya Kibaha  Halima Kihemba alisema anategemea wananchi kukusanyika
kwa wingi ili kupata uelewa wa chanjo mbalimbali zinazoweza kukinga
magonjwa kwa watoto.

mwisho.

KIAMA KWA MADEREVA WANYWA VIROBA KIMEFIKA


 Na John Gagarini, Kibaha
HATIMAYE baada ya kilio cha muda mrefu cha abiria juu ya madereva ambao wamekuwa wakiweka pombe za viroba kwenye chupa za maji na kujifanya wanakunywa maji, kimesikika baada ya jeshi la polisi mkoani Pwani kupata vipima ulevi 100.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Nasoro Sisiwaya alisema kuwa vifaa hivyo vitasaidia kukabiliana na madereva walevi ambao wamekuwa wakisababisha ajali kutokana na ulevi.
Sisiwaya alisema kuwa kutokana na kero ya ulevi kuwa kubwa kwa baadhi ya madereva wamekuja na njia hiyo ili kuwadhibiti madereva hao ambao wamekuwa wakinywa pombe huku safari ikiendelea.
“Vifaa hivi vitatusaidia katika kukabiliana na madereva hao ambao ni chanzo kikubwa cha ajali kwani hupoteza umakini wakati wa kuendesha na kusababisha ajali ambazo zingeweza kuepukika,” alisema Sisiwaya.
Aidha alisema kuwa kitengo cha usalama barabarani kinaendelea kukabiliana na changamoto za ajali kwa kuweka askari mbalimbali wakiwemo ambao wanakuwa wamevaa kiraia ili kudhibiti madereva ambao wanakiuka sheria za usalama barabarani.
“Tunamshukuru Mungu kuwa ajali zinaendelea kupungua kutokana na udhibiti kuwa mkubwa ambapo kwa sasa makosa madogo yameongezeka ambayo yanaashiria kupungua kwa ajali katika mkoa,” alisema Sisiwaya.
Aliongeza kuwa kwa sasa wanashirikiana na mamlaka ya kudhibiti usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) katika kuwakamata madereva wanaovunja sheria ambapo mafanikio yameanza kuonekana kwani makosa makubwa ya barabarani yamepungua kwa asilimia 26.
Aliwataka wananchi na abiria kutoa taarifa mbalimbali kuhusiana na madereva ambao hawazingatii taratibu za uendeshaji wawapo barabarani na wataendelea kufanya operesheni za mara kwa mara ili kuwabaini madereva wazembe.
Mwisho.
  

Friday, April 19, 2013

MICHEZO PWANI


Na  John Gagarini, Kibaha
BONDIA wa Maili Moja Kibaha mkoani Pwani Nzumba Nkukwe leo Jumamosi anatarajia kupanda ulingoni kupambana na bondia Yusuph Yusuph wa Chalinze wilayani Bagamoyo.
Kwa mujibu wa katibu wa katibu wa chama cha ngumi mkoa wa Pwani Halfan Mrisho “Swagala” alisema kuwa pambano hilo litachezwa kwenye ukumbi wa Ndelema uliopo Chalinze.
Swagala alisema kuwa pambano hilo litakuwa ni la kirafiki kwa kuwapima uwezo wao mabondia hao pamoja na kuhamasisha watu kucheza mchezo huo mkoa Pwani.
“Lengo kuu ni kumwandaa Nkukwe ambaye anatakiwa kucheza mapambano 12 ili aweze kushiriki kwenye mashindano ya ubingwa hapa nchini,” alisema Swagala.
Aidha alisema kuwa pambano hilo lililodhaminiwa na Big Right litakuwa la raundi 12 na linatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa mabondia hao wa mkoa huu.
“Nawaomba mashabiki waje kwa wingi ili kuwahamasisha mabondia wa nyumbani na kutakuw ana usafiri kutokea Maili Moja hadi Chalinze hivyo itakuwa ni nafasi kwa wadau wa ngumi kujionea vipaji vya vijana wao,” alisema Swagala.
Alitoa shukrani kwa mdhamini wa mapambano Omary Kimbau kwa jitihada zake za kuhamasisha mchezo huo kwa vijana wa mkoa wa Pwani kwani amekuwa akiwaandalia mapambano mbalimbali mabondia.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MCHEZO wa nusu fainali kati ya Fire na Lisborn ulishindwa kutoa mshindi baada ya mwamuzi wa pambano hilo Hamad Mbegu kutimua mbio kuhofia usalama wake baada ya kumaliza mpira zikiwa zimesalia dakika chache zikiwa hazijatiamia dakika 90 na kuamuru yapigwe matuta timu hizo zikiwa sare ya 1-1.
Mchezo huo wa nusu fainali ya pili kuwania kombe la Kibaha Super Cup ulipigwa kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani Kibaha ulizikutanisha timu hizo ili kupata mshindi ambaye angeungana na Mwanalugali kucheza hatua ya fainali.
Chanzo cha mwamuzi huyo kukimbia ni pale alipoashiria mpira kwisha huku zikiwa bado dakika 5 kutimia dakikia 90 alimaliza pambano na kuashiria matuta lakini washabaiki wa timu ya Lisborn walimfuata na kumzonga huku wakimtishia kumpiga.
Kutokana na mzozo huo mwamuzi aliwaita wachezaji wa Lsborn kwa ajili ya kupiga matuta lakini walionekana kusuasua hali iliyofanya muda mwingi upotee karibu dakika 10 hivi huku washabiki wakiwa wamezingira eneo la goli zilipotakiwa kupigwa penati hali iliyomtia hufo mwamuzi huyo na kukimbia.
Mbali ya hali hiyo pambano hilo lilikuwa na mvutano mkubwa huku timu hizo zikionyesha kandanda safi na walikuwa Lisborn walioandaika bao la kuongoza kupitia kwa Kulwa Mwanda dakika ya 72 na Fundikira Fundikira wa Fire alisawazisha kwenye dakika ya 80 ya mchezo, mchezo huu utarudiwa leo Jumamosi kwenye uwanja huo huo.
Mwisho.

POLISI PWANI YAKUSANYA MAMILIONI


Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limefanikiwa kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 825 kutokana na makosa madogo madogo ya barabarani kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Hayo yalisemwa jana na kamanda wa polisi mkoani humo Ulrich Matei alipoongea na waandishi wa habari mjini Kibaha kuzungumzia mafanikio na changamoto zinazolikabili jeshi hilo.
Matei alisema kuwa katika kipindi hicho jumla ya makosa yliyokamatwa katika kipindi cha Januari mwaka  2011 hadi Machi 2013 ni 31,663 ambapo yaliyolipiwa yalikuwa ni 31,235.
“Katika kipindi hicho ajali zilikuwa 942 za vifo zilikuwa 190 waliokufa walikuwa 224, ajali za majeruhi zilikuwa 510 na waliojeruhiwa walikuwa 1,109 ambapo inaonyesha kupungua kwa asilimia 25 ukilinganisha na mikoa mingine,” alisema Matei.
Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Nasoro Sisiwaya alisema kuwa wanaendelea na mikakati mbalimbali ya kuzuia ajali ikiwa ni pamoja na kukamata magari mabovu.
Sisiwaya alisema kuwa wameunda vikosi maalumu viwili kwa ajili ya kukagua magari ambapo kimoja kinafanya ukaguzi kwenye barabara iendayo mikoa ya Kusini na kingine barabara ya Morogoro.
Aidha alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa kuyaondoa magari yanayoharibika barabarani kwani hawana gari la kuyaondolea na matokeo yake hutumia magari mengine kuyaondoa kwa kutumia mnyororo mgumu.
Mwisho.     

Tuesday, April 16, 2013

12,500 KUNUFAIKA MIRADI YA MAJI KIBAHA


Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya watu 12,500 kwenye vijiji vinne kwenye Halmashauri ya wilaya ya  Kibaha mkoani Pwani watanufaika  na mradi wa kitaifa wa maji wa Wami – Chalinze awamu ya pili wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kuelezea mafanikio ya wilaya kwa kipindi cha miaka saba iliyopita mkuu wa wilaya Halima Kihemba alisema kuwa mradi huo utakamilika wakati wowote mwaka huu.
Kihemba alisema kuwa kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 35 ya utekelezaji wake na kuvitaja vijiji hivyo kuwa ni Magindu, Lukenge, Gwata na Gumba.
“Mbali ya vijiji vilivyotajwa hapo juu pia tunatarajia jumla ya vijiji 45 vitanufaika na mradi mwingine ambao utasaidia kukabiliana na changamoto ya maji ambayo ni kubwa kwenye wilaya,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa kwa upande wa miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi zaidi ya bilioni mbili itategemeana na upatikanaji wa fedha kutoka wadau mbalimbali.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa bomba Vikuruti, Boko Mnemela, Dutuni, bwawa la maji Mperamumbi uchimbaji wa kisima kirefu chenye uwezo wa kutoa lita 36,000 za maji kwa saa.
“Miradi hiyo itakuwa katika vijiji vya Lupunga, Mwabwito, Kisabi, Madimla, Disunyala na Makazi Mapya,” alisema Kihemba.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Kibaha Mjini mitaa 15 ambayo ni Sofu, Muheza, Vikawe, Bondeni, Vikawe Shuleni, Kidenge, Galagaza, Sagale, Mikongeni, Mwanalugali, Saeni, Jonugha, Zogawale na Viziwaziwa miradi hii itakuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Alibainisha kuwa changamoto kubwa ni pamoja na kutegemea vyanzo vya maji vya ya juu ya ardhi, mabwawa, mito ambayo hukauka wakati wa ukame na kusababisha shida ya maji hivyo kuweka mikakati ya kuhamasisha jamii kutunza vyanzo vya maji, kuandaa andiko la miradi ya maji ili kupata wafadhili na kutumia visima virefu kwa kuwa ni vyanzo vya uhakika zaidi kulinganisha na mabwawa.
Mwisho.



Monday, April 15, 2013

AMWUA MAMA YAKE MZAZI KWA KUMPIGA NA MCHI KICHWANI


JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia aitwaye Francis Siza  miaka (26) kwa tuhuma za kumuuwa mama yake mzazi Naomi Isaka (55)  kwa kumpiga na mchi kichwani.
 Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea leo  majira ya saa 1:30 asubuhi eneo la Kiluvya A wilaya ya Kisarawe.
Kamanda Matei alisema kuwa kijana huyo alifanya tukio hilo baada ya kubaki yeye na mama yake baada ya wadogo zake wawili wa kike ambao ni wanafunzi kwenda shule.
“Alimpiga na mchi kichwani mara mbili uapande wa kushoto na kulia chanzo kikiwa ni kutaka kuuza kiwanja cha mama yake ambapo ni siku moja tangu arudi baada ya kusafiri kusikojulikana,” alisema Kamanda Matei.
Baadhi ya majirani ambao walishuhudia tukio hil Nolasko Zenobisi alisema wakati alipokuwa akiendelea na shughuli zake za kulima alisikia kelele zikipigwa ndipo alipokwenda katika nyumba hiyo na aliweza kukuta tayari mama huyo ameshafariki.
 Zenobisi alisema alipowajulisha majirani na kuanza kumtafuta mtuhumiwa na kwa bahati nzuri walimpata akiwa amijificha kichakani ndipo walipomfunga kamba na kumpeleka eneo alilofanyia tukio.
 Aidha alisema kwamba kijana huyo ambaye ndiye wa kwanza kuzaliwa katika familia yao alifanya tukio hilo la mauaji  baada ya   mdogo wake wa kike anaiyeitwa Neema Siza kuondoka nyumbani na kuelekea shule ya sekondari Makulenge ambapo ndipo anaposoma kidato cha tatu.
 Naye shuhuda mwingine ambaye akutaka jina lake litajwe gazeti alisema kwamba pia nay eye asubuhi hiyo alikuwa shambani anaalia ndipo aliposikia sauti na mtu anapika makelele na kufa na alipokwenda alimwona huyo kijana anakimbia mbio ndipo wananchi wengine walipoamua kumkimbiza na kumkamata.
 Hata hivyo baadhi ya majirani wengine walisema kwamba kijana huyo alifika mnamo April 14 majira ya saa 4:30 usiku na kumgongea mama yake mzazi na alifunguliwa na kuingia ndani kulala lakini asubuhi akaamua kufanya tukio hilo.
Naye mtoto wa Marehemu Neema Siza ambaye anasoma shule ya Makurunge alisema kwamba asubuhi aliondoka na kumwaga mama yake vizuri na  kwenda shule na kwamba nyumbani alimwacha kaka  yake huyo wa kwanza pamoja na  mama yake.
Kwa upande wake mtuhumiwa huyo alisema kuwa kwa upande wake yeye hakugombana wala hawakuwa na ugomvi wowote na mama yake mzazi isipokuwa alifanya hivyo baada ya kumwona mama yake mzazi anateseka hivyo akaona bora ampige na kumuuwa ili aweze kupumzika.
 “Lakini kutokana na kosa ambalo nimelifanya kwa sasa najuta, lakini ninafahamu kuwa sheria itachukua mkondo wake, ingawa mimi nimefanya hivyo kwa sabbau tangu siku nyingi niliona mama yangu anateseka sana, na ukizingatia baba yetu naye alishafariki dunia  kwa hiyo hali halisi ndiyo iliyofanya nifanye hivyo na hakuna kitu kingine,” alisema Siza.