Friday, March 1, 2013

MTOTO AUNGUZWA NA MAJI YA MOTO




Na John Gagarini, Kibaha
MKAZI wa Mtaa wa Kwa Mfipa wilayani Kibaha Nuru Rashid amewashangaza wakazi wa mtaa huo kwa kushindwa kumpeleka hospitali mwanae mwenye umri wa miaka miwili na nusu baada ya kuungua na maji ya moto.
Akizungumza na baba mzazi Ally Said alisema mwanae ambaye ni wa jinsi ya kiume ameungua kifuani na kusababisha kidonda kikubwa hadi kwenye mkono wake wa kushoto hakumpatia matibabu yoyote hadi siku iliyofuata.
Said alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 27 mtaani hapo nyumbani kwa mama yake mazazi ambaye walitengana naye zaidi ya mwaka mmoja uliopita ambapo aliolewa na mume mwingine.
“Mimi baada ya kupata habari juu ya mwanangu kuunguzwa na maji siku iliyofuata nilikwenda nyumbani kwake kutaka kumchukua mwanangu ili nimpeleke hospitali lakini alikataa na kusema hadi baba yake wa kambo aje jambo ambalo alilikataa na kumchukua kwa nguvu,” alisema Said.
Alisema kuwa mkewe amekuwa akimficha juu ya matatizo hasa pale anapoumwa na mbaya ni pale alipomficha mwanae baada ya kuungua na kushangaa ni kwanini hataki kumpeleka hospitalini.
Jitihada za kumpata mama huyo yazikuweza kuzaa matunda licha ya mwandishi kufika nyumbani kwake na kuambiwa kaenda dukani na hata aliposubiriwa hakuweza kutokea.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Hai Hai alikiri kupata tukio hilo na kusema kuwa ukweli halisi alikuwa nao mama huyo ambaye ndiye aliyekuwa akiishi na mtoto huyo ambaye alikuwa akilia kutokana na maumivu makali aliyoyapata.
Hai alisema kuwa hatua aliyoichukua ni kuandika barua ambayo ilibidi ipelekwe polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria na kupatiwa matibabu kwa mtoto huyo na kusema hicho ni kitendo cha unyanyasaji na kuwanyima haki watoto wadogo.
Mwisho.     
 Mtoto aliyeunguzwa na maji ya moto akiwa amepumzika huku nyumbani kwao huko Kwa Mfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani (Picha na John Gagarini)






MBUNGE ALIPA HASARA ILIYOSABABISHWA NA MGAMBO


Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Silvestry Koka amelazimika kuwalipa fedha kiasi cha shilingi 275,000 wanawake watatu wanaouza samaki baada ya mgambo wa kata ya Maili Moja kumwaga samaki wao kwa madai ya kukiuka kanuni za afya.
Koka ilibidi alipe fedha hizo kwa wafanyabiashara hao baada ya kuangua kilio mbele ya mbunge huyo wakati wa mkutano na wananchi wa Kibaha.
Alisema hayo yalikuwa makosa ya kibinaadamu yaliyofanywa na mgambo hao wakati wakitekeleza zoezi la usafi kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Kibaha.
“Suala la afya ni muhimu na mgambo hawa waliteleza na kujikuta wakiharibu mali za wafanyabiashara ambao wanajitafutia riziki zao huku wengine wakiwa wamekopa fedha kwa ajili ya kufanyia biashara hiyo,” alisema Koka.
Mbunge huyo alisema kuwa kuanzia sasa wafanyabiashara na mgambo hao kwa kushirikiana na ofisi ya afya ya kata kila upande kufuata kanuni na sheria ili kufanikisha suala la afya.
Kwa upande wao wakinamama hao mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Riziki Said alisema kuwa mgambo hao walifika kwenye biashara yake na kusema kuwa kwakuwa hakupima afya yake na kuwamwaga samaki wake wenye thamani ya shilingi 65,000.
Naye mfanyabiashara mwingine Nuru Msangi alisema kuwa mgambo hao walichukua samaki wake wenye thamani ya shilingi 75,000 na kuzimwaga kwa madai kuwa naye hakupima afya yake.
Alisema kuwa wafanyabiashara wengi wanashindwa kupima afya zao kutokana na gharama kubwa ya kupima ya shilingi 5,000 na pia walisema wao kama wanshinikizwa kupima je kwa wateja wanaokwenda kununua mbona hawabanwi.
Mbunge huyo alizitaka pande mbili hizo kati ya idara ya afya ya kata hiyo na wafanyabiashara kuanza mahusiano mazuri upya ili kuondoa ugomvi unaojitokeza mara kwa mara pia halmashauri itoe elimu juu malipo hayo ya kupima afya ya shilingi 5,000.
Mwisho.    

Thursday, February 28, 2013

FRIENDS OF SIMBA WATAKIWA KUJITOKEZA KUTATUA MGOGORO



Na John Gagarini, Kibaha
MARAFIKI wa Simba (Friends of Simba) wametakiwa kuingilia kati tatizo lililopo kwenye klabu yao ili iweze kuwa na mwenendo mzuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki timu yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi msemaji wa tawi la Simba wilayani Kibaha “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa hadi sasa timu hiyo bado haijapata tiba ya tatizo lililopo ndani ya klabu hiyo.
Lardhi alisema kuwa wakati huu wa matatizo wanachama na wadau wa Simba lazima wajitokeze kusaidia timu ili iweze kufanya vema kwani kwa sasa mwenendo wake ni mbaya.
“Marafiki wazuri huonekana wakati wa shida hivyo tunataka marafiki wetu wajitokeze kuinusuru timu kwani kwa sasa timu inaonekana kufanya vibaya kwenye michezo yake tofauti na matarajio ya wengi,” alisema Lardhi.
Alisema kuwa marafiki wa Simba mbali ya kusaidia fedha pia wanatakiwa kuisaidia timu hiyo kwa mchango wa mawazo ili kujua tatizo lililopo hadi timu kufanya vibaya kwenye michezo yake.
“Wanapaswa kuonyesha upendo wao kwa klabu kwani hadi sasa hatujaona jitihada zozote walizofanya kuinusuru timu na matokeo mabaya, tunawpongeza wanaposaidia timu katika mazingira yote pia waonyeshe upendo hata kama timu inafanya vibaya ili kuinusuru timu yetu ambayo inatetea ubingwa wake wa ligi kuu ya Tanzania Bara,” alisema Lardhi.
Msemaji huyo wa tawi la Simba wilayani Kibaha alisema kuwa Wanasimba wanatakiwa kuungana katika kipindi hichi kigumu kinachoikabili timu yao kwa kuwa na matokeo mabaya inayoyapata ili kujinusuru na kupata matokeo mazuri.
“Tunapaswa kuungana na kuonyesha mshikamano ili kuisaidia timu yetu kwani timu inapofanya vibaya tunaumia sana hivyo tuungane ili kuiletea maendeleo mazuri,” alisema Lardhi.
Ameipongeza kamati ya utendaji kwa kuandaa mkutano wa kujadili kiini cha timu kufanya vibaya katika michezo yake hali ambayo inaifanya timu hiyo kuwa kwenye mashaka ya kutetea ubingwa wake.
Mwisho.    

KAYA ZAIDI YA 1000 ZAKUMWA NA NJAA



Na John Gagarini, Bagamoyo
KAYA 1,138 katika vijiji vitano kwenye kata ya Miono wilayani Bagamoyo mkoani Pwani vinakabiliwa na baa la njaa na kuhitaji msaada wa chakula.
 Kwa mujibu wa Diwani wa kata hiyo Sangali Kiselu alisema kuwa kaya hizo zinahitaji msaada ili kukabiliana na njaa hiyo.
Kiselu alisema kuwa kutokana na tatizo hilo uongozi wa kata ya Miono umeiomba serikali Mkoani Pwani  kuharakisha kuwapatia msaada wa chakula kaya hizo ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Hali kwa sasa inazidi kuwa mbaya katika kaya hizo ikiwa ni kati ya kaya 4,271 zenye watu zaidi ya 20,000 ambazo zimekumbwa na baa hilo la njaa,” alisema Kiselu.

Alivitaja vijiji ambavyo vimepata athari hiyo kuwa ni
Kweikonje, Masimbani, Mihuga, Kikalo na Miono kwenye kata hiyo.

Kwa upande wake mtendaji wa kata hiyo Ramadhani Nguya alisema kwa sasa wanahofia kutokana na hali kufikia pabaya hivyo haina budi kutoa kilio hicho kwa niaba ya wananchi ili kunusuru maisha yao.

Naye Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi amekiri kuwepo kwa hali hiyo nakusema si kweli kuwa serikali inachelewesha kupeleka msaada wa chakula katika maeneo hayo.

“Serikali imeshaidhinisha tani 400 ambazo zitasambazwa katika maeneo mbalimbali yaliokumbwa na baa hilo wilayani humo, ikiwa ni pamoja na kata ya Kibindu, Mbwewe, Kimange, Miono na Kiwangwa ambayo haijapata athari sana.

Kipozi alisema kuwa janga la njaa limezikumba kata hizo kutokana na mavuno hafifu kwa mwaka jana yaliyosababishwa na mvua iliyokuwa hairidhishi hivyo kwa sasa amehimiza kilimo cha mhogo na mtama ambayo yanahimili ukame.

Mwisho

Tuesday, February 26, 2013

WALIOMTEKA MWANAFUNZI WASHIKILIWA NA POLISI


Mwandishi Wetu, Kibaha
JESHI la polisi mkoani Pwani linawashikilia vijana watatu kwa tuhuma za kumteka mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Pangani Kata ya Pangani wilayani Kibaha mkoani Pwani ambaye alikuwaaingie kidato cha pili mwaka huu mwenye umri wa miaka (16) na kushindwa kwenda shule baada ya kutekwa na vijana watatu kwa kipindi cha miezi mitatuambapo alipata mimba na vijana hao waliitoa.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwao Kidimu wilayani Kibaha huku akibubujikwa na machozi alisema kuwa vijana hao ambao ni wakulima kati yao wawili ni ndugu walimteka kwa kutumia visu vitatu walivyokuwanavyo.

Aliwataja vijana hao ambao anawatuhumu kumfanyia kitendo hicho kuwa ni
Jovinas Oswald , Isaka Joseph na Faida Joseph (22) ambao ni ndugu walimteka Novemba 3 mwaka jana baada ya kumdanganya kuwa anatakiwa kwenda kuchukua mzigo wa ndugu yake.

“Baada ya kwenda kufuata mzigo huo niliwakuta wakiwa na visu vitatu ambapo
kila mmoja alikuwa na kisu na kunipeleka kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi
kusema kuwa hapo ndipo nitakapokuwa naishi na endapo nitajaribu kutoka basi
wataniua,” alisema.

Alisema kuwa kwa kipindi chote hicho walikuwa wakifunga mlango kwa nje kwa
kutumia kufuli kwa nje huku wakiwa wamemhifadhi kwenye kisehemu mithili ya kajeneza kwani juu waliweka miti na pembeni waliweka matofali na juu waliweka godoro huku yeye akiwa chini hali ambayo ilimfanya ashindwe kutoka pia
ikizingatiwa kuwa nyumba hiyo iko mbali na nyumba zingine na kuwa katika
kichaka.

“Faida ambaye ndiye aliyenifanya kama mke wake alinipa mimba lakini baada
ya kuona hivyo walinilazimisha kuitoa kwa kutumia majani ya chai ambayo
yalichemshwa na maji na kuniamuru ninywe na kusababisha mimba kutoka ambapo nilitokwa na damu nyingi na kupata maumivu makali,” alisema mwanafunzi huyo.

Aidha alisema kuwa walimtengenezea kajumba kadogo kwa kupanga matofali na
miti kisha yeye kuingia humo mfano wa kaburi ambapo alikuwa akijisaidia
kwenye mifuko ya plastiki na chupa kwa ajili ya haja ndogo na kuoga ni humo
ndani.

“Kwa upande wa chakula walikuwa wakipika usiku tu kwani walikuwa wakifika
majira ya saa sita au saba usiku wanapika tunakula ila asubuhi na mchana
nilikuwa sili chakula hata mavazi yangu waliyachoama moto nikawa navaa nguo
ya moja ya vijana hao,” aliongeza.

Aliongeza kuwa siku moja vijana hao walisahau kufunga mlango na ndipo
alipotoka na kuomba msaada kwa mtu ambaye alimpeleka hadi nyumbani kwa
walezi wake ambao ni babu na bibi yake ambao ndiyo waliokuwa wakiishi naye
kwa muda wote.

Kwa upande wake babu wa mwanafunzi huyo Daud Zakayo alisema kuwa mwanafunzi
huyo alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na walifanya jitihada
kumtafuta ambapo walitoa taarifa polisi na kwa ndugu lakini bila ya
mafanikio.

Zakayo alisema kuwa baada ya mjukuu wao kupatikana walitoa taarifa polisi
ambapo vijana hao walikamatwa kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio
hilo.
Naye mwalimu wa shule aliyokuwa akisoma Peter Mihayo alisema kuwa mwanafunzi huyo hajafukuzwa ila atasubiri hadi suala lake litakapokamilika kwani tayari liko kwenye vyombo vya sheria.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alipoulizwa kuhusiana na
tukio hilo alisema kuwa watuhumiwa wanashikiliwa na mara upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mwisho.

AKUTWA AMEFIA GESTI

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MWILI wa mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam Ambrose Mapunda anayekadiriwa kuwa na umri kati (50) na (55) umekutwa chini ya uvungu wa nyumba ya kualala wageni huku ukiwa mtupu bila ya nguo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya kamanda wa polisi mkoa wa Pwani ofisa upelelezi wa mkoa wa Pwani wa jeshi la polisi Juma Yusuph alisema kuwa tukio hilo lilitokea kwenye nyumba ya kulala wageni kwenye nyumba ya kulala wageni ya Cham Cham iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Alisema tukio hilo lilitokea kati ya Fabruari 22 na 24 kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni huku ukiwa na jeraha kubwa kichwani huku shingo yake ikiwa imenyongwa.
“Marehemu alikutwa akiwa chini ya uvungu huku mwili wake ukiwa hauna nguo na jeraha huku ukiwa umenyongwa shingo ambapo mtu aliyehusika na tukio hilo hakuweza kufahamika mara moja,” alisema kamanda Yusuph.
Alibainisha kuwa marehemu hakukutwa na kitu chochote licha ya kuwa alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa na begi kwenye chumba namba mbili.
“Ujumbe uliokutwa kwenye chumba hicho ulisema kuwa umenidhulumu tulikubaliana unilipe kiasi cha shilingi 20,000 lakini hujanilipa, ujumbe huu umeandaikwa na mtu asiyefahamika,” alisema Kamanda Yusuph.
Aidha alisema kuwa mhuduma na mlinzi wa nyumba hiyo ya kulala wageni wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusu tukio hilo na polisi wanaendelea na uchunguzi.
Mwisho.  

AKUTWA AMEFIA GESTI

Na John Gagarini, Kibaha
MFANYABIASHARA wa Jijini Dar es Salaam Ambrose Mapunda mwenye umri kati ya 50 na 55 amekutwa amekufa na mwili wake kuwekwa chini ya uvungu wa kitanda wa nyumba ya kulala wageni ya Cham Cham Msata wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kwa niaba ya kamanda wa polisi mkoa wa Pwani ofisa upelelezi wa Jeshi la polisi Juma Yusuph alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa uchi.
Kamanda Yusuph alisema kuwa tukio hilo lilitokea kati ya Fabruari 22 na 24 mwaka huu kwenye nyumba ya kulala wageni ya Cham Cham huku ukiwa na jeraha kubwa kichwani huku shingo yake ikiwa imenyongwa.
“Marehemu alikutwa akiwa chini ya uvungu huku mwili wake ukiwa hauna nguo na jeraha huku ukiwa umenyongwa shingo ambapo mtu aliyehusika na tukio hilo hakuweza kufahamika mara moja,” alisema kamanda Yusuph.
Alisema kuwa marehemu hakukutwa na chochote licha ya kuwa alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa na begi kwenye chumba namba mbili.
“Ujumbe uliokutwa kwenye chumba hicho ulisema kuwa umenidhulumu tulikubaliana unilipe kiasi cha shilingi 20,000 lakini hujanilipa, ujumbe huu umeandaikwa na mtu asiyefahamika,” alisema Kamanda Yusuph.
Aidha alisema kuwa mhuduma na mlinzi wa nyumba hiyo ya kulala wageni wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusu tukio hilo na polisi wanaendelea na uchunguzi.
Mwisho.