FAMILIA ya Watu saba wasioona |
Na John
Gagarini, Kibaha
JUMUIYA ya
Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa
Maili Moja imetoa misaada ya nguo na vyakula kwa familia yenye wasioona saba
inayoishi kwenye Mtaa wa Simbani wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza
na gazeti hili mara baada ya kukabidhi misaada hiyo ambayo ilipelekwa na
Jumuiya hiyo mwenyekiti Jacob Samson alisema kuwa waliamua kupeleka misaada
hiyo baada ya kupata taarifa za familia hiyo.
Samson
alisema kuwa wametoa misaada hiyo pia ni katika kuwafanya nao waweze
kusherehekea siku kuu ya X- Mass na wenzao wakiwa na furaha hasa ikizingatiwa
wao ni wahitaji na wanahitaji misaada mbalimbali.
“Tunaamini kusaidia
jamii zenye mahitaji ni ibaada kamili na inawatia moyo na kujiona kuwa hawako
peke yao kwani kuna watu wanawaunga mkono na kushiriki nao kwa pamoja,” alisema
Samson.
Alisema kuwa
Jumiya yao hufanya ibaada za nyumba kwa nyumba ambapo hutembeleana na
kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na ya kiimani.
“Jumuiya yetu
iko kwa ajili ya kusaidiana kwenya matatizo na furaha hivyo wanajumuiya
walisema kuwa twende kwenye hiyo familia iwe sehemu ya ibaada ya yetu ya kila
Jumamosi ili kuwafariji na wamejitolea sana ili kuhakikisha familia ile nayo
inafurahia kipindi hichi cha mwisho wa mwaka,” alisema Samson.
Aidha alisema
kuwa wanaomba watu wengine nao wajitokeze kuisaidia familia hiyo ambayo ina
hitaji misaada mbalimbali kutokana na kuwa kwenye mazingira magumu.
“Kutoa ni
moyo na si utajiri kwani watu wenye moyo wanapaswa kwenda kuwasaidia kwa jambo
lolote la kijamii hasa ikizingatiwa familia hiyo inasimamiwa na mwanamke ambaye
alitengana na mumewe,” alisema Samson.
Kwa upande
wake mama wa familia hiyo Mwajuma Maulid alisema kuwa anaishukuru Jumuiya ya
maili Moja kwa kuwapatia misaada hiyo ambayo wameitoa kwani wameonyesha moyo wa
kipekee.
Maulid
alisema kuwa vyakula vilivyotolewa vitawasaidia katika kusherehekea sikukuu ya
X-Mass kwa furaha kama wanavyofurahia watu wengine na kuwataka watu wengine
waendelee kuwasaidia.
“Tuko kwenye
mazingira magumu sana kwani hali yetu si nzuri ambapo tunaishi maisha ya
kubahatisha kwa hiyo wanapokuja watu kama hawa na kutupa misaada tunashukuru
sana,” alisema Maulid.
Familia hiyo
inaishi mtaa wa Simbani kata ya Kibaha ina watu saba ambao hawaoni ambapo wasioona
ni mume wake ambaye walitengana,watoto wanne wasioona na wajukuu wawili wote hawaoni na inaishi kwa
kutegemea kuchoma mkaa na kusuka mikeka.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja Jacob Samson kushoto akimkabidhi moja ya
msaada uliotolewa na Jumuiya hiyo kwa familia ya watu saba wasioona anayepokea
ni Mwajuma Maulid ambaye ndiye mama anayeihudumia familia hiyo