
Aidha imetaka kufanyika sensa ya wanyama hao ili idadi yake iweze kutambulika kwa wale wanaowafuga kwa utaratibu unaotambulika rasmi na kisheria.
Akitoa azimio hilo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kwa kipindi cha robo ya Aprili hadi Juni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Erasto Makala alisema kuwa mbwa hao wamekuwa kero kwa watu.
Makala alisema kuwa mbwa hao wanaozurura hawana chanjo na wamekuwa wakingata watu hivyo kuhatarisha afya zao.
"Madhara ya mtu kungatwa na mbwa ni makubwa hivyo lazima kuwamaliza mbwa wanaozurura ambao hawana mwenyewe kwani hawana chanjo ya kuwakinga na magonjwa,"alisema Makala.
Alisema kuwa sensa ni muhimu kwa wanayama hao na Halmashauri ikiona kuna changamoto kuna haja ya kumpa mzabuni kwa ajili ya kuchanja mbwa ili kuwafikia mbwa wengi.
Akiibua hoja kuhusiana na mbwa wengi kutochanjwa Diwani wa Viti Maalum ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Halima Jongo alisema mbwa hawajachanjwa ni wengi ukilinganisha na mbwa waliopo.
Jongo alitoa mfano wa Kata ya Ruvu kuna mbwa 361 lakini waliochanjwa ni 35 na Mtambani kuna mbwa 53 lakini hawajachanjwa ambapo Kata za Kwala na Magindu hakuna taarifa ya kuchanjwa mbwa.
Naye Diwani wa Kata ya Kilangalanga Mwajuma Denge alisema kuwa mbwa wasio na wamiliki ambao huzurura ndiyo wanaoleta madhara.
Mwajuma alisema kuwa ikifanyika sensa itakuwa vizuri kwani itakuwa rahisi kujua idadi na kutoa chanjo kwa mbwa na kwa wale wanaozurura wauliwe ili kuepusha madhara kwa wananchi.