Thursday, September 12, 2019

CCM YACHANGIA MABATI 500 ELIMISHA KIBAHA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)Taifa kimekabidhi mabati 500 kwa ajili ya kuunga mkono kampeni ya wilaya ya Kibaha ya Elimisha Kibaha yenye lengo la kujenga madarasa ili kukabiliana na changamoto upungufu wa madarasa 65 unayoikabili wilaya hiyo.

Akikamkabidhi mabati hayo mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama ambaye ndiyo muasisi wa kampeni hiyo katibu Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole alisema kuwa wameamua kuunga mkono kampeni hiyo ambayo inaisaidia serikali na inatekeleza ilani ya chama ambayo inatekelezwa na Rais ya kutoa elimu bila ya malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Polepole alisema kuwa  tangu Rais Dk John Magufuli alivyotangaza elimu bure kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi zaidi ya mara tatu na hivyo kuongeza mahitaji ya uhaba wa madarasa, madawati na walimu ambalo serikali inalifanyia kazi na wamesha ongea na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) ili Kibaha ipewe kipaumbele kwenye mgawanyo wa walimu.

“Wakuu wa chama wamefurahi sana kwa hili lililofanywa na waliridhia mimi kuja kushiriki nanyi na tunapopata watendaji na viongozi wa serikali wanaojituma wanapaswa kuungwa mkono na kusimama nao na ndiyo tuliweka ahadi ya chama ya kuchangia mabati 600 na tumeanza na mabati 500 kwa awamu hii ya kwanza na awamu ya pili tutatoa mabati 100 na mifuko ya saruji 100,” alisema Polepole.

Alisema kuwa wanafurahishwa na kazi inayofanyika kwani inatekeleza ilani ya chama na uongozi wa wilaya umepanda mbegu bora kwani kwani mkuu wa wilaya ya Kibaha amepanda kitu kizuri na viongozi wengine wamepata hamasa kwani wameanza kufanya kama yeye hiyo ni hamasa si lazima kusubiri fedha ya serikali kwani wananchi wako tayari kuchangia maendeleo yao wenyewe.

“Tunataka viongozi wahamasishe umma kama ulivyofanya wewe angalia tumeokoa shilingi ngapi kwa jitihada mlizozifanya kwa madarasa 26 ya mwanzo kati ya 65 yanayotarajiwa kujengwa kupitia kampeni hiyo ambapo fedha zilizookolewa zitakwenda kusaidia wale ambao hawajaweza kufanya kama mlivyofanya nyie Kibaha huu ndiyo uongozi unaotakiwa,” alisema Polepole.

Alisema viongozi wanapaswa kufanya mambo mema ya maendeleo kama hakuna watu wanaowaona hiyo ndiyo tafsiri ya uongozi au mtumishi mwadilifu usifanye ili watu waone kwani watakuwa si waadilifu bali wafanye kama jambo binafsi fanya kama lako mwenyewe na wakipatikana viongozi kama hao ambapo wapo tayari watamsaidia Rais kwa ndoto za kuibadilisha nchi zitatimia mapema kabla ya muda.

Awali mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema kuwa baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika hivi karibuni walipata vifaa na fedha zilizokusanywa vitatosha ujenzi wa madarasa 26 kwa Halmashauri mbili za Kibaha Mjini na Wilaya ya Kibaha ambapo kila moja imeanza ujenzi wa madarasa 13.

Mshama alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo umeanza baada ya wakurugenzi wa Halmashauri hizo kupatiwa vifaa vya ujenzi ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa 65 ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 1.3 na hii imetokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu darasa la saba.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaofaulu darasa la saba ambapo kwa mwaka 2017 jumla ya wanafunzi walifaulu 3,560, mwaka 2018 wanafunzi 3,938 walifaulu na mwaka 2019 wanafunzi waliongezeka na kufika 4,930 hali ambayo imesababisha kuwa na upungufu mkubwa wa madarasa hayo yanayohitajika.

Mwisho.

Friday, December 29, 2017

RC NDIKILO AIPIGA TAFU KILUVYA UNITED MILIONI MBILI

 Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo

 Baadhi ya wachezaji wa Kiluvya United inayoshiriki ligi daraja la kwanza wakimskiliza mkuu wa mkoa wa Pwani hayupo pichani walipomtembelea ofisini kwake mjini Kibaha

 Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimkabidhi kiongozi wa timu ya Kiluvya United kiasi cha shilingi milioni 2 kwa ajili ya kuihamaisha iweze kushinda michezo yake na kuingia Ligi Kuu ya Voda Com

 Nahodha wa Timu ya Kiluvya United ya mkoani Pwani Ramadhan akishukuru baada ya kukabidhiwa fedha kwa ajili ya hamasa na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.






Na John Gagarini, Kibaha
KUELEKEA mchezo wake wa ligi daraja la Kwanza leo dhidi ya Ruvu kuwania kupanda Ligi Kuu unaotarajiwa kuchezwa  kwenye uwanja wa Filbert Bayi wilayani Kibaha mkoa wa Pwani umeipatia timu ya Kiluvya United kiasi cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya hamasa ili waweze kushinda mchezo huo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo kwa viongozi wa timu hiyo walioambatana na wachezaji ofisini kwake mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa lengo ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo. 
Ndikilo alisema kuwa viongozi wa timu hiyo walifika ofisini kwake na kuomba msaada wa kuisaidia timu yao ili iweze kufanya vizuri kwenye michezo yake mitano iliyosalia ya ligi hiyo na endapo watashinda watafanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Voda Com.
“Tuko pamoja na timu yetu ambayo inawakilisha mkoa na leo tunawakabidhi fedha ambazo zimetolewa na wadau wa mkoa ili kufanikisha malengo ya kupanda Ligi Kuu kwani uwezekano huo upo,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wadau wanachotaka ni timu yao kushinda kwani imeonyesha ina uwezo wa kufanya hivyo kutokana na uwezo inaounyesha wanaamini inaweza kufanya vizuri na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya harakati zake za kiutaka kupanda daraja ili kufikia Ligi Kuu ya Voda Com.
“Wadau wa soka wa mkoa wa Pwani wamejitolea fedha hizo kama hamasa ya kufanya vyema kwenye mchezo wa leo ambao utakuwa na ushindani mkubwa kwani timu hizo ziko kwenye nafasi nzuri ya kupanda Ligi Kuu ambapo Ruvu ndiyo kinara wa kundi hilo na United wakiwa kwenye nafasi ya tatu,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa mdau ambaye anataka kuipeleka timu ya Kiluvya United nchi ya Ulaya ya Finland atafurahi kuona timu hiyo inashinda mchezo huo na kutoa zawadi ya mwaka mpya kwa wadau wa mkoa wa Pwani.
Naye nahodha wa timu hiyo Ramadhan Ally alisema kuwa wao wkao tayari kwa pambano hilo na watahakikisha wanapambana kwa nguvu zote ili wapate ushindi na kujiweka vizuri kwenye harakati zao za kupanda daraja.
Ally alisema kuwa kutokana na kupewa fedha hizo zitawasaidia kama morali kwao kwa ajili ya kupata ushindi huo ambao utakuwa muhimu ili kuwapa raha watu wa mkoa wa Pwani.
Mwisho.

MWENYEKITI UVCCM AWASHUKIA WATENDAJI WA SERIKALI NA VIONGOZI WA KUCHAGULIWA

 
 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Kheri James akisalimiana na mwenyekiti wa UVCCM Kibaha Mjini Azilongwa wakati alipowasili wilayani Kibaha kwenye mkutano wa kumpongeza kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo uliofanyika kata ya Kongowe. 

 Moja ya Vijana wa UVCCM Kibaha Mjini akimvalisha skafu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Kheri James alipowasili wilayani Kibaha

 Baadhi ya Vijana wa UVCCM Mkoani Pwani wakishanglia jambo wakati wa mkutano huo

 Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo akiongea kwenye mkutano huo.
 
 
Na John Gagarini, Kibaha
 
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Kheri James amewataka viongozi wa serikali na wale wa kuchaguliwa nchini kuhakikisha wanashiriki kwenye mikutano ya viongozi wa kitaifa ili waweze kupokea maagizo mbalimbali.

Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa sherehe za kumpongeza kwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo zilizoandaliwa na Uvccm Kibaha Mjini na kusema kuwa maagizo yanayotolewa hayawezi kufanyiwa kazi kutokana na wahusika kutokuwepo.

James alisema kuwa viongozi na watendaji wa serikali ambao hawashiriki vikao kama hivyo hawafai waondoke kwani wameshindwa kazi.

"Hapa tunatoa maagizo na wao hawapo kwani maelekezo hayo yanapotolewa watu wa kuyapokea hawapo kuanzia ngazi ya halmashauri za wilaya, wilaya na Mkoa wanapaswa kujirekebisha kama wanaona hawawezi kazi watupishe," alisema James.

Alisema kuwa maelekezo yanayotolewa ni kuzikabili changamoto ambapo atendaji wa serikali wanaposhindwa kutatua kero za wananchi ambazo ni ilani ya chama kuna sababisha chama kuwa na wakati mgumu nyakati za uchaguzi kwa wagombea wa ccm.

"Watendaji wanaohujumu waondoke kwani wao ndiyo watekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa ajili ya wananchi," alisema James.

"Viongozi hawapaswi kulewa madaraka ambayo ni kitu kibaya sana na ni sawa na ulevi na hutafsiriwa baada ya muda wa kuwa madarakani kwisha ambapo watu watakuhukumu kwa matendo yako na kuwa bakora ya kukuchapia," alisema James.

Alisema kuwa hataki uongozi wa mitandao wa fb,insta, WhatsApp anataka viongozi wa kufanya kazi kwani kazi ya kuongoza ni ngumu sana hasa wakati wa kuhakiki mali za jumuiya hiyo watapambana na watu wenye vyeo vikubwa na fedha nyingi hivyo ni vita kubwa.

Aidha aliwata viongozi wa chama kutowatumia tu vijana wakati wa uchaguzi wasiwafanye kama ngazi ya kupandia na kama hawatawashirikisha vijana wampe taarifa na suala la ajira liangaliwe kwani baadhi ya wafanyakazi wanaajiriwa toka nje kwa kazi zinazowezwa kufanywa na watanzania.

"Wamiliki waangalie maslahi ya wafanyakazi vitendea kazi kwani baadhi wanafanya kazi kwenye viwanda ambvyo huzalisha kwa kutumia kemikali ambazo zinaweza kuwa maafa endapo hawatapewa vifaa vya kuwakinga kwani inaweza kusababisha vifo kwani viwanda si kwa ajili ya kusababisha vifo," alisema James.

Aliwataka wabunge wasiwe wa mifukoni wakichaguliwa wanaondoka na kusubiri hadi muda wa uchaguzi kwa sasa hawana nafasi wanajitokeza muda huo na kuanza vurugu wakidai fulani anampinga kumbe hawakuwajibika na kujiweka mbali na wananchi pia viongozi wa chama pamoja madiwani kuhakikisha kuwa asilimia tano ya vijana inakuwa agenda ya kudumu kwenye vikao mbalimbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ccm Mkoa Pwani Ramadhan Maneno alisema kuwa watahikikisha wana hakiki mali za umoja huo wakiwa kama wasimamiaji wa jumuiya zote za chama.

Awali mwenyekiti wa umoja huo Chalangwa Seleman wa mkoa alitaka viongozi kufuata maelekezo ya rais ili kufanya umoja huo kuwa kimbilio na watayatrkeleza yale yote yaliyotolewa na mwenyekiti wao.

Sunday, November 26, 2017

WANAONUNUA KOROSHO KINYUME CHA UTARATIBU WAKAMATWE-RC

Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akizindua ununuzi wa zao la korosho wilayani Kibiti 

 Baadhi ya viongozi wa wilaya za mkoa wa Pwani wakati wa uzinduzi wa zao la korosho wilayani Kibiti

 Baadhi ya wanunuzi waliohudhuria mnada wa kwanza wa uuuzaji zao la korosho uliofanyika Kibiti mkoani Pwani

 Wadau wa zao la korosho wakiptia taarifa mbalimbali juu ya uuzaji wa zao la korosho mkoani Pwani

Na John Gagarini, Mkuranga

MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakuu wa Polisi wa wilaya kuwakamata wafanyabiahara ambao watanunua zao la korosho la msimu huu kinyume cha utaratibu ikiwemo wale wanaonunua kwa njia ya “Kangomba”.

Ndikilo aliyasema hayo wilayani Mkuranga wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya wakulima wa zao la Korosho mkoani humo na kusema kuwa kwa msimu huu hataki kuona walanguzi wa zao hilo kwani wanawanyonya wakulima.

Alisema kuwa ununuzi kwa njia ya Kangomba ni marufuku na atakayekamatwa ananunua kwa njia hiyo ambayo inawanyonya wakulima haitakiwi.

“Ununuzi kwa njia ya Kangomba ni marufuku mauzo yote yafanyike kwa njia yam nada kwa kutumia stakabadhi ghalani hayo ndi maelekezo ya serikali atakayenunua tofauti na utaratibu huo akamatwe wakuu wa polisi wa wilaya fanyeni kazi msiwaonee huruma walanguzi wawekeni ndani,” alisema Ndikilo.

Aliitaka bodi ya korosho kuhakikisha inakabili changamoto za upatikanaji wa magunia ili korosho zilizovunwa zisiharibike na kuuzwa kwa bei ndogo kwenye soko la korosho ambapo unuzi unaanza Novemba 8 mwaka huu.

Kwa upande wake meneja wa bodi ya Korosho tawi la Dar es Salaam Mangile Malegesi alisema kuwa msimu wa zoa hilo kwa mkoa wa Pwani utazinduliwa wiki ijayo ambapo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara msimu umeshazidnuliwa.

Malegesi alisema kuwa magunia yatapatikana kwa wakati ili wakulima waweze kuhifadhi korosho zao ambapo bei elekezi ni shilingi 1,460 kwa daraja la kwanza na 1,160 kwa daraja la pili.

Naye mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU) Rajabu Ngonema alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni magunia na wakulima kutaka kuuza korosho zao kwenye maghala ya vyama vya msingi badala ya kuuza kwenye maghala makuu yaliyopitishwa na bodi ya Korosho.

Ngonema alisema kuwa maghala ni changamoto kubwa kwani wakulima wanahofia gharama na usumbufu na kutaka wauzie kwenye maghala ya vyama vya msingi.

Mwisho.  

FUNGENI NDOA KISHERIA MPATE HAKI ZENU WANAWAKE-WAASWA

 Mwenyekiti wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga

Na John Gagarini, Kibaha

WATU walioko kwenye mahusiano ya kimapenzi wametakiwa kufunga ndoa kisheria ili waweze kutambulika badala ya kuishi kwenye dhana ya ndoa ambayo imesababisha migogoro mingi mara mahusiano yanapovunjika huku watoto ndiyo wakiwa waathirika wakuu.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mwenyekiti wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga wakati wa mafunzo ya utoaji wa elimu juu ya masuala mbalimbali ya Kisehria yaliyoandaliwa na kituo hicho kwa viongozi wa serikali za Mitaa na Kata ya Kibaha.

Mlenga alisema kuwa dhana ya ndoa imekuwa ni tatizo sana ambapo mwanamke anaishi na mwanaume bila ya kufunga ndoa kisheria na kujiita mume na mke lakini mara inapotokea watu hawa wamechoka kuishi pamoja mwanamke hukosa haki zake za msingi.

“Watu wengi wamekuwa wakiishi kwa dhana ya ndoa ambayo haiwatambui kisheria watu hao kama ni wanandoa na kusababishia mara wanapotaka kutengana mwanamke hunyimwa mali ambayo waliichuma katika kipindi walipokuwa wakiishi hivyo ni vema wakafunga ndoa kisheria ili haki ipatikane,” alisema Mlenga.

Alisema kuwa kama watu wanataka kuwa wanandoa kwanini waishi bila ya ndoa kwani hali hii husababisha migogoro mingi ya ndoa hizo ambazo haziko kisheria kwa watu kuchukuana tu na kuishi kama mke na mume.

“Endapo kutakuwa na ndoa iliyo kisheria itasaidia kupunguza migogoro kwani hata kama mahusiano ya kindoa yamekwisha kila mtu atapata haki yake kuanzia mume, mke na watoto lakini watu wakiishi kwa dhana ya ndoa kuna upande ambao hautapata haki licha ya kwamba watakuwa wamfanya maendeleo muda walioishi pamoja,” alisema Mlenga.

Aidha alisema dhana ya ndoa pia husababisha wanandoa kutowajibika lakini kama wamefunga ndoa sheria inawataka kuwajibika na endapo mmoja atashindwa kuwajibika mwanandoa anaweze kumshtaki na mhusika kuwajibishwa.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Kibaha Omary Bula alisema kuwa ndoa nyingi zinaingia kwenye migogoro kutokana na wanandoa hasa wanawake kutojua haki zao za msingi hivyo kujikuta wakinyanyasika.

Bula alisema kuwa ili ndoa iweze kudumu ni kila upande kuwajibika kwa mwenzake kwa kupeana haki zote ndani ya ndoa na kutawaka wadau mbalimbali waendelee kutoa elimu ya sheria mbalimbali si za ndoa tu kwa wananchi kama kilivyofanya kituo hicho.


Mwisho.

USALAMA BARABARANI WAFANYA OPERESHENI USIKU WAKAMATA MADEREVA


 Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani Tanzania (RTO) Mkoa wa Pwani Salum Morimori kulia akimhoji moja ya madereva waliokuika sheria za usalama barabarani huko Msata wilayani Bagamoyo katikati ni Edward Gontako kutoka kikosi hicho.

Na John Gagarini, Chalinze

KIKOSI cha Usalama Barabarani kimefanikiwa kuwakamata madereva saba wa mabasi kwa tuhuma za kufanya makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendesha kwa mwendo kasi na kuzidisha abiria.

Madereva hao walikamatwa baada ya kikosi hicho kwa kushirikiana na kamati ya usalama barabarani ya mkoa kufanya oparesheni ya kushtukiza usiku kwenye barabara za Morogoro na ile inayoelekea Mikoa ya Kaskazini.

Akiongoza oparesheni hiyo kaimu kamanda wa kikosi hicho RTO mkoa wa Pwani Salumu Moromori amesema kuwa wameamua kufanya oparesheni hiyo usiku ili kubaini makosa yanayofanywa usiku na hapa anaongea na madereva ambao walikamatwa wakiwemo wa kutoka nchi ya Rwanda.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati uya usalama barabarani mkoa huo Josephine Protas amesema kuwa wamefanya oparesheni hiyo usiku kufuatia malalamiko.

Naye mkaguzi wa magari wa polisi Edward Gontako amesema kuwa wamekuwa wakiwapa elimu ya kuzingatia sheria za usalama barabarani na usalama wa magari.

MWISHO

KIFO MTOTO KUUWAWA SERIKALI KUFANYA UCHUNGUZI



 Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lukenge kwenye mkutano maalumu

 Mke wa mtuhumiwa Zena Manoza

 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Lukenge waliohudhuria mkutano mkuu maalumu wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kibaha hayupo pichani

 Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama akiangalia nyumba lilipotokea tukio la mtoto kuuwawa kwa kupigwa risasi,kushoto ni matundu ya risasi

Na John Gagarini, Magindu

WAKAZI wa Kijiji cha Lukenge kata ya Magindu wilayani Kibaha wametakiwa kuendelea na shughuli zao na kuishi kwa amani huku serikali ikiendelea na uchunguzi juu ya tukio la mtoto kuuwawa kwa kupigwa na bunduki na baba yake mdogo Ally Sakalawe (43) wakati akijibizana na polisi walipokwenda kukagua silaha.

Akizungumza kwenye mkutano mkuu maalumu wa Kijiji hicho mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema kuwa serikali inaendelea na uchunguzi na itatoa taarifa ili kuondoa utata ambao umegubika tukio hilo kwa baadhi ya ndugu na wakazi wa kijiji hicho kudai kuwa polisi ndiyo walimwua mtoto huyo aitwaye Mark Joel Modest (15).

Mshama alisema kuwa anajua kuwa tukio hilo limewaumiza sana wakazi hao pamoja na familia husika lakini hawana budi kuwa na subira juu ya uchunguzi ili kubaini ukweili juu ya tukio hilo.

“Nawaomba muishi kwa amani na msiwe na wasiwasi serikali inaendelea na uchunguzi na mtapewa majibu mara uchunguzi huo utakapokamilika watu wanaosema kuwa hawaishi majumbani kuhofia kukamatwa wasiogope kama si wahalifu hawana haja ya kuogopa,” alisema Mshama.

Alisema kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake na haki itatolewa kwani jambo hili linasikitisha sana kwani mtoto kapoteza uhai na alikuwa hausiki kwa lolote.

“Tunamasikitiko makubwa ya kumpotez amtoto huyu ambaye hakuwa na hatia lakini ninachowaomba muwe na imani na serikali kwani inalifanyia kazi suala hili ili kuweza kujua ukweli hivyo nanyi mnapaswa kuwa na imani na endeleeni na shughuli zenu za uzalishaji mali msiishi kwa hofu,” alisema Mshama.

Aidha alisema kuwa wananchi hao pia wawe makini katika kumiliki silaha ambapo mtuhumiwa licha ya kutokea kwa tukio hilo la mauaji pia alibainika kuwa alikuwa akimiliki gobore bila ya kibali pia alikutwa na vitu mbalimbali ambavyo vinaleta maswali mengi juu ya matumizi ya silaha hiyo.

“Lazima tujiulize licha ya kifo cha mtoto huyo lakini mtuhumiwa ambaye anashikiliwa na polisi alikutwa na bunduki mbili aina ya gobore, risasi ya mark 4, vipande vya nondo na gololi vyote vikitumika kama risasi hivyo lazima tujiulize matumizi ya silaha hizi,” alisema Mshama.

Awali akielezea juu ya tukio hilo mke wa mtuhumiwa Zaina Manoza alisema kuwa siku ya tukio hilo walikuwa wamelala ndani majira ya saa 8 kwenda saa 9 usiku askari walifika na kuanza kupiga bunduki na wao kuanza kupiga kelele wakiomba msaada kwa majirani.

Manoza alisema kuwa walitakiwa kutoka nje na kuambiwa watoke nje na kujitambulisha kwa majina lakini yeye akawaambia katika hao mtoto mmoja hayupo wakamwambia akamwangalie chumba kingine ambapo alipokwenda alimkuta mtoto huyo akiwa anavuja damu ubavuni.

“Baada ya hapo walinitaka nikamwite mwenyekiti wa kitongoji na alipofika wakawaambia wampeleke mtoto akapate tiba na kunitaka niongozane na huyo mtoto na mwanangu mwingine tukiwa tumembeba nikaona kama hali ni mbaya nikajua tayari kafa,” alisema Manoza.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi wa wilaya Caster Ngonyani alisema kuwa wananchi wanapaswa kuishi kwa amani na hawatakiwi kuwa na woga na hawakwenda kwa ajili ya kuwatisha wananchi na wanafanya kazi kwa kufuata sheria.

Ngonyani alisema kuwa ripoti aliyopewa juu ya tukio hilo ilisema kuwa polisi walikwenda kwenye nyumba hiyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna silaha aina ya gobore bila ya kibali ambapo taarifa hizo walizipata kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho ndipo walipokwenda kwa ajili ya kuzikamata.

“Kulikuwa na wamiliki wawili wa hizo silaha ambao ni Ally Sakalawe na Robinus Almas na hawakutoa taarifa kwa uongozi kwa hofu taarifa kuvuja na walipofika waligonga na kushindwa kuingia ndani baada ya mtuhumiwa kukataa kufungua mlango na kuanza kurusha hewani,” alisema Ngonyani.

Alisema kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi mbele ya baba Mzazi Modest na Anna Raphael mama mzazi

“Ndani ya tumbo walikuta kipande cha chuma ambacho ni kipande cha nondo kwenye tumbo la marehemu hali ambayo inaonyesh silaha iliyotumika ni gobore na silaha ya polisi haitumii chuma inatumia risasi na zingekutwa tungejua kuwa polisi walihusika,” alisema Ngonyani.

Aidha alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo ni dhahiri kuwa mtoto huyo alipigwa na mtuhumiwa kwani tumboni kilikutwa kipande cha nondo ambazo zimekatwa na hutumika kama risasi kwenye magobore hayo ambapo vipande vingine 10 vilikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 28 mwaka huu wakati polisi walipokwenda kufanya upekuzi juu ya uwepo wa silaha hizo aina ya magobore ambaye yalikuwa yakitumika kwa uhalifu na uwindaji haramu ambapo licha ya mtuhumiwa wa kwanza kukutwa na silaha hizo pia walimkamata Robson Almas naye akiwa na magobore mawili yakiwa hayana vibali vya umiliki.


Mwisho.