Na John
Gagarini, Kibaha
KIJANA mmoja
anayekadiriwa kuwa na miaka (19) mkazi wa Mbagala Maji Matitu amejikuta yuko
kwenye wakati mgumu baada ya kukutwa akiwa amevaa nguo za kike aina ya dera na
kusababisha taharuki kwa wakazi wa Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa wa
Picha ya Ndege Joseph Zambo alisema kuwa kijana huyo alikuwa akiwasiliana na
mtu akijifanya kuwa yeye ni mwanamke.
Zambo alisema
kuwa kijana huyo alifika kwenye mtaa wake Agosti 2 majira ya sa 4:30 asubuhi
akimfuata mtu waliokuwa wakiwasiliana naye kwa njia ya simu ambaye inadaiwa
kuwa ni dereva bodaboda.
“Watu hawa
walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na kijana huyo alikuwa akiigiza sauti
ya kike na dereva bodaboda alijua fika kuwa aliyekuwa anawasiliana naye ni
mwanamke,” alisema Zambo.
Alisema kuwa
dereva bodaboda huyo alimwona kijana huyo kupitia ukurasa wake wa facebook
ambapo ulipambwa na picha za msichana hali ambayo ilimfanya avutiwe naye.
“Mawasiliano
yalianza kama siku tatu zilizopita na walikubaliana na ndipo bodaboda huyo
alimwambia njoo Picha ya Ndege Kibaha lakini kijana huyo alipitiliza hadi
Kongowe na ilibidi arudi ashukie Picha ya Ndege na alimwelekeza akishuka apande
bodaboda ili aende kwake eneo la Sofu,” alisema Zambo.
Aidha alisema
kuwa aliposhuka waendesha pikipiki walikuwa wakimfuatilia na wlimwona amevaa
dira na usoni kajifunga kitambaa ambacho kiliacha wazi macho tu kama vile ninja
akapandishwa kwenye pikipiki na kuanza safari ya kwenda kwa mtu wake.
“Wakiwa
njiani upepo ulipuliza na dereva wa bodaboda akashangaa kuona miguu ya kiume
lakini amevaa viatu vya kike akashtuka na kugeuza pikipiki kule alikotoka na
ndipo madereva bodaboda walipojaa na kuanza kumzonga hali iliyowabidi wamlete
ofisini kwangu na ilikuwa tafrani kubwa huku wengine wakitaka kumpiga wakidai
ni mwizi wa pikipiki,” alisema Zambo.
Alibainisha
kuwa baada ya kumfikisha walimfunua na kukuta kuwa ni mwanaume na kuanza
kumhoji ndipo aliposema kuwa alikuja Kibaha kuja kuchukua hela na haikujulikana
alikuja kuzichukua hizo fedha kwa njia gani.
“Zogo
lilizidi pale huku bodaboda wakitaka kumpiga ndipo ikabidi tuchukue gari na
kumpeleka polisi kwa ajili ya usalama wake na kueleza ni kwa sababu gani alijifanya
mwanamke na fedha hizo anazichukua kwa njia gani,” alisema Zambo.
Kwa upande
wake Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alikiri kutokea kwa tukio
hilo na kusema kuwa atalitolea taarifa tukio hilo baada ya kutoka kwenye msafara
wa kiongozi.
Mwisho.