Monday, April 3, 2017

WATUHUMIWA UHALIFU WALIOVALIA HIJABU WAUWAWA NA POLISI

Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki moja wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu wakiwa wamevalia hijabu wameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kukaidi amri ya kutakiwa kusimama.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga alisema kuwa pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa kukimbia.
Lyanga akielezea juu ya tukio hilo alisema kuwa lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya saa 12:00 mchana eneo la kizuizi cha Mwembe Muhoro wilaya ya Rufiji mkoani Pwani barabara kuu ya Dar es Salaam Lindi.
“Siku ya tukio askari walipata taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini zikiwa zimebeba watu watatu kila moja huku miongoni mwa pikipiki hizo kati yake mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.
Alisema kuwa askari wa barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na kuwasimamisha ili wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi cha Ikwiriri lakini walikaidi kusimama.
“Baada ya hapo walifika kizuizi cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo walipofika kituo cha Muhoro hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria wakiwa kwenye gari waliwafuatilia wakijaribu kuwafuatilia na wakavuka daraja la Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga risasi hewani,” alisema Lyanga.
Aidha alisema kuwa baada ya hapo watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza kukimbilia msituni na ndipo askari walipowapiga risasi za miguu na kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.
“Majeruhi hao walijulikana ni wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi ambapo watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha Hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.
Lyanga alisema kuwa walipofikishwa hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia ambapo hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili zilitoroka na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili wawakamate.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa jeshi hilo limeimarisha doria katika kukabiliana na uhalifu.
Mwisho.

Tuesday, March 28, 2017

MBUNGE AZINDUA UJENZI WA UZIO WA KITUO CHA AFYA



 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akionyesha shehena na saruji mifuko 500 kwa ajili ya uzio wa Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akiwa amebeba saruji ambayo itatumika kwenye ujenzi wa uzio wa kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani 







 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akizindua ujenzi wa uzio wa Kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani


Na John Gagarini, Kibaha

KITUO cha Afya cha Mlandizi kimeanza mchakato wa kuelekea kuwa Hospitali ya wilaya kwa kuanza ujenzi wa uzio ambapo Mbunge wa Jimbo la Kibaha 
Vijijini wilayani Kibaha mkoani Pwani Hamoud Jumaa amewataka wafadhili mbalimbali kujitokeza kusaidia ujenzi wa uzio huo ambao utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 200.

Akizungumza na waandishi wa habari Mlandizi wakati akizindua ujenzi huo mbunge huyo alisema kuwa wameanza kuboresha huduma zinazotolewa kituoni hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uzio huo ikiwa ni moja ya vigezo vinavyotakiwa kufikia hadhi hiyo.

Jumaa alisema kuwa Kituo hicho cha afya ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa Jimbo hilo ambalo kwa sasa lina wakazi 70,000 na wilaya jirani za Bagamoyo na miji ya Chalinze na Kibaha wanapata huduma hapo.

“Mpango huu nimeuanzisha kwa jitihada zangu binafsi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo hadi sasa nimepata mifuko 500 ya saruji, kokoto lori saba mchanga, mchanga na tani moja ya nondo ambavyo vitasaidia katika ujenzi wa uzio huu tunaomba wadau wengine waendelee kutusaidia,” alisema Jumaa.

Alisema kuwa kutokana na kituo hicho cha afya kuwa tegemeo kubwa kwa wameona kuna haja ya kuwa Hospitali ya Wilaya ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi watakaokuwa wanapata huduma hapo.

“Tumekubaliana vitongoji 26 na madiwani sita watoe 240,000 huku mfuko wa jimbo ukitoa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa ajili ya tofali za uzio ambao utasaidia kuondoa uingiaji holela wa watu bila ya sababu za msingi ndani ya eneo la Kituo cha afya,” alisema Jumaa.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mlandizi Eufrasia Kadala alisema kuwa wataungana na Mbunge huyo kuhakikisha wanafanikisha ujenzi huo ili kuboresha kituo hicho cha afya.

Kadala alisema kuwa kutokana na kutokuwa na uzio kumekuwa na mwingiliano wa watu kuingia kiholela hasa kutokana na kituo hicho kuwa jirani na makazi ya watu. 

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Mlandizi Tatu Jalala alisema kuwa waliupokea mkono mpango huo na kuupeleka kwa jamii kwa lengo la kumuunga mkono mbunge wao.

Jalala alisema kuwa wanaendelea kuihamasisha jamii ili iweze kuchangia ujenzi huo wa uzio ukamilike kwa wakati lengo likiwa ni kufanikisha harakati za kuwa Hosptali ya wilaya.

Mwisho. 

Thursday, March 23, 2017

MWENYEKITI ANUSURIKA KIFO RISASI ZAMJERUHI

Na John Gagarini, Rufiji

MWENYEKITI wa Kitongoji cha Mpalange Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini wilayani Rufiji mkoani Pwani Bakari Mpawane amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika.

Mpawane alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 19 mwaka huu majira ya saa 2 usiku akiwa dukani kwake ambapo alipigwa risasi mkononi na tumboni.

Alisema kuwa mtu aliyempiga alikuwa amepakizwa kwenye pikpiki akampiga kisha wakatokomea kusikujulikana kwa kutumia pikpiki hiyo ambayo namba zake hazikuweza kutambulika mara moja.

“Watu hao ambao walikuwa wamepakizana kwenye pikipiki walifika hapo na mmoja wao kumwita jina lake mara nikashtukia napigwa risasi ambazo hata hivyo namshukuru Mungu ziliniparaza tu na hazikuweza kuniletea madhara makubwa ambayo yangehatarisha uhai wangu,” alisema Mpawane.

Aidha alisema kuwa anamshukuru Mungu na sasa anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri hata hivyo ana hofu na anafikiria atakaporudi kwake baada ya matibabu ataishije baada ya kunusurika kwenye tukio kubwa na la uuaji kama hilo.

“Naomba serikali na jeshi la polisi liweke mikakati kabambe ili kuvunja ngome za kiuhalifu na mtandao unaomaliza hasa viongozi bila kujua chanzo ni masuala ya kisiasa ama nini,”alisema Mpawane.

Akizungumza mara baada ya kwenda kumtembelea mwenyekiti huyo katika kituo cha afya cha Mchukwi anapopatiwa matibabu Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi  Evarist Ndikilo alisema kuwa hilo ni tukio la tatu kwa mwezi mmoja likiwemo lililotokea machi 13 mwaka huu kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo wilayani hapa, Hemed Njiwa (45) kuuwawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani na tukio lililohusisha kifo cha OCCID.

Ndikilo alisema kuwa wanaendelea kuwasaka watu hao usiku na mchana hadi kuhakikisha wanawakamata ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kuhusiana na tukio hilo.

“Tutawasaka na hatafanikiwa  kwa mipango yao waliojiwekea tumejidhatiti na tutahakikisha tunategua mipango yao na kurejesha amani kwa wananchi,”alisema Ndikilo.

Aidha aliwashukuru wahudumu wa afya katika kituo cha afya cha Mchukwi kwa kuokoa maisha ya mwenyekiti huyo pamoja na kutoa huduma nzuri kwa majeruhi na wagonjwa wengine wanaofikishwa hapo kupata matibabu.

Naye Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga,aliomba ushirikiano wa wananchi kutoa taarifa polisi mara wanapopata wasiwasi wa watu wanaoingia kwenye maeneo yao.

Kamanda Lyanga alisema ameletwa mkoa wa Pwani kutoka Simiyu kwa ajili ya kufanya kazi na jambo kubwa analohitaji ni ushirikiano na jamii ili waweze kupunguza matukio yanayotikisa ikiwemo la kuuwa wa wenyeviti wa vitongoji,watendaji na wenyeviti wa vijiji.


Mwisho 

MADEREVA SABA WAPORA FEDHA NA SIMU WAJERUHIWA

Na John Gagarini, Kibaha

MADEREVA saba wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kisha kuwapora fedha kiasi cha shilingi 920,000 baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kufunga barabara ya Kilwa kwa kutumia magogo.

Aidha watu hao licha ya kuwajeruhi na kuwapora fedha pia waliwaibia madereva hao simu saba na kutoweka kusikojulikana.

Kwa Mujibu wa taarifa zilizotolewa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 majira ya saa saba usiku katika kijiji cha Kitembo kata ya Mchukwi wilaya ya Kibiti.

Kamanda Lyanga amesema kuwa watu hao sita wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi walikuwa na silaha za jadi ikiwa ni pamoja na mapanga na marungu na walizitumia kuwajeruhi madereva hao.

Amesema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusina na tukio hilo na wanaendelea na msako kuhakikisha watu hao wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria waweze kujibu tuhuma hizo.

Aidha amewataja madereva waliojeruhiwa kwa mapanga kuwa ni Issa Juma (26) mkazi wa Jijini Dar es Salaam aliyejeruhiwa shavu la kulia, Badru Uwesu (31) mkazi wa Kisemvule Mkuranga aliyejeruhiwa shavu la kulia na mgongoni, Edward Safari (37) mkazi wa Morogoro.

Amewataja wengine kuwa ni Ramadhan Ally (34), Nasoro Mohamed (26), Kassimu Omary (36), Khalifa Mohamed wote wakazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambapo majeruhi wote walitibiwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Mchukwi na kuruhusiwa kuondoka.

Katika tukio lingine ngombe 102 wamekufa baada ya kunywa maji ambayo yanasadikiwa kuwa hayafai kutumika kwa matumizi yoyote kwenye machimbo ya kokoto.

Kamanda Lyanga amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 mwaka huu majira ya saa 9 alasiri kwenye Kijiji cha Pongwe Msungura Chalinze wilayani Bagamoyo.

Mwisho.  

  

Monday, March 20, 2017

MLANDIZI QUEENS YAPONGEZWA KWA KUWA MABINGWA NCHINI

Na John Gagarini, Kibaha

SHIRIKISHO la Soka Nchini (TFF) limeombwa kuhamasisha uanzishwaji wa mashindano ya soka kwa wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki ili kuendeleza vipaji vya wanawake kimataifa.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mratibu wa timu ya Mlandizi Queens Florence Ambonisye wakati wa sherehe za kuipongeza timu hiyo kwa kutwaa ubingwa huo na kuwa mabingwa wa kihistoria wa kwanza kwa soka la Wanawake Tanzania.

Ambonisye alisema kuwa kwa kuwa kuna mashindano ya soka la wanawake ngazi ya nchi na nchi kuna haja ya kuwa na mashindano ya vilabu kama ilivyo kwa wanaume.

“Imefika wakati TFF kuhamasisha kuanzishwa mashindano ya vilabu vya soka la wanawake ili kuinua soka la wanawake hapa nchini kwani itasaidia kuwa na timu bora kutokana na kushindana na wenzao wa nchi zingine,” alisema Ambonisye.

Ambonisye ambaye pia ni katibu wa chama cha soka la wanawake mkoa wa Pwani alisema kuwa mashindano hayo pia yatasaidia kuimarisha timu ya soka ya Taifa ya wanawake Twiga Stars.

“Tukianzisha mashindano ya nchi za Afrika Mashariki tutakuwa na timu ya Taifa ya wanawake imara kwani watapata uzoefu mkubwa hivyo nchi itaweza kufika mbali kwenye mashindano ya Kimataifa,” alisema Ambonisye.

Aidha alisema kuwa washindi wa mashindano hayo watakuwa hawana mashindano yoyote hadi mwakani lakini wangekuwa na mashindano ya vilabu vya nchi nyingine ingewasaidia sana kuendeleza vipaji vyao ambapo kwa sasa watakaa muda mrefu bila ya kucheza.

Naye mgeni rasmi kwenye sherehe hizo Ivan Chenga ambaye ni katibu msaidizi wa chama cha soka wilayani Kibaha Ivan Chenga alisema kuwa timu hiyo haitakiwi kubweteka kwa kutwaa ubingwa huo.

Chenga alisema kuwa katika kipindi hichi wanapaswa kuendelea na mazoezi na kuachana na vitendo ambavyo vitasababisha kushusha viwango vyao.

Kwa upande wake mwakilishi wa chama cha soka mkoa wa Pwani COREFA Simon Mbelwa alisema kuwa timu hiyo imeleta mafanikio makubwa kwa kuweka historia kwa kuitoa Pwani kimasomaso kwa kutwaa ubingwa huo.

Mbelwa alisema kuwa timu za soka za wanaume za mkoa wa Pwani zimekuwa zikifanya vizuri kwenye ligi Kuu lakini hazijawahi kutwaa ubingwa lakini hii ya wanawake imeweza kuleta kombe na kuonyesha mfano mzuri.

Mwisho.

 Diwani wa Kata ya Mlandizi Ephrasia Kadala akibusu kombe la soka la Wanawake lililotwaliwa na timu ya soka ya wanawake ya Mlandizi Queens wakati wa sherehe za kuipongeza timu hiyo zilizofanyika Mlandizi hivi karibuni.

 Baadhi ya wachezaji wa timu ya Mlandizi Queens wakiwa wamepozi wakati wa sherehe za kuwapongeza baada ya kufanikiwa kuwa mabingwa wa soka la wananwake nchini.

 Baadhi ya viongozi wa timu ya Mlandizi Queens wakiwa wametulia wakifuatilia wakati wa sherehe za kuipongeza timu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa soka la wanawake nchini hivi karibuni.

 Wachezaji wa timu ya Mlandizi Queens wakicheza wakati wa sherehe ya kuwapongeza kwa kuwa mabingwa wa soka la wanawake nchini.

 Wachezaji wa Mlandizi Queens wakicheza.

 Wachezaji wa Mlandizi Queens wakicheza pamoja na viongozi wao wakati wa sherehe ya kuwapongeza iliyofanyika Mlandizi hivi karibuni.

 Katibu Msaidizi wa Chama cha soka wilaya ya Kibaha Ivan Chenga akipokea kombe toka kwa kepteni wa Mlandizi Queens Mwanahamis Gaucho katikati ni diwani wa kata ya Mlandizi Ephrasia Kadala akishuhudia. 

 Katibu Msaidizi wa Chama cha soka wilaya ya Kibaha KIBAFA Ivan Chenga akiongea wakati wa sherehe ya kuipongeza timu ya Mlandizi Queens kwa kuwa mabingwa wa soka la wanawake nchini

 Katibu Msaidizi wa Chama cha soka wilaya ya Kibaha KIBAFA Ivan Chenga akinyanyua kombe kama ishara ya pongezi kwa timu ya soka ya wanawake ya Mlandizi Queens kulia ni mjumbe wa Chama caha Soka mkoa wa Pwani COREFA Simon Mbelwa na wakwanza kulia ni Mwanahimis Gaucho Kapteni wa timu hiyo  


Tuesday, March 14, 2017

MUHONGO AZINDUA REA AWAMU YA TATU PWANI



Kushoto katibu Tawala mkoa wa Pwani Zuberi Samataba akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kulia ni mkurugenzi wa REA Injinia Gisima Nyamo-Hanga na kushoto nyuma ni mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo  wakati wa uzinduzi wa REA awamu ya tatu mkoa wa Pwani uliofanyika kwenye Kitongoji cha Msufini wilaya ya Kibaha

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisalimiana na kiongozi wa timu ya kampuni ya Steg International Services ya Tunisia ambayo imepewa zabuni ya mradi wa Umeme Vijijini REA awamu ya tatu mkoani Pwani
Wabunge Abou Jumaa kushoto na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete wakiwa wanasikiliza jambo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini REA Mkoa wa Pwani awamu ya tatu   



Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo aliyebeba udongo kwa ajili ya kuweka kwenye nguzo ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa REA awamu ya tatu mkoa wa Pwani kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete


Mkurugenzi wa REA Injinia Gisima Nyamo-Hanga akizungumza wakati wa uzinduzi huo 

Kushoto mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo akiongea huku Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akimsikiliza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umememe Vijijini REA awamu ya tatu mkoani Pwani kwenye kitongoji cha Msufini wilayani Kibaha 


Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akisisitiza jambo mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo wa kwanza kushoto mbele ya mafundi wa kampuni ya Tunisia ya Steg International Services ambao ndiyo watakaoendesha mradi huo.

 Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akiongea mbele ya mafundi wa kampuni ya Steg International Services ya Tuniasia waliopewa kazi ya kusimamia mradi wa REA awamu ya tatu mkoani Pwani, katikati ni Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Abou Jumaa.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini  

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo aliyeshika mkasi kwa ajili ya kukata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa REA mkoa wa Pwani kushoto ni mkuu wa mkoa wa Pwani injinia Evarist Ndikilo na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini Abou Jumaa akifuatiwa na Mkurugenzi wa REA Injinia Gisima Nyamo-Hanga  

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa mradi wa Umeme Vijijini REA mkoa wa Pwani kulia ni Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete na kushoto Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Abou Jumaa 

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa mradi wa REA mkoa wa Pwani kulia ni mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kushoto mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Abou Jumaa anayefuatia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete 

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo katikati akikabidhiwa mbuzi na baaadhi ya wakazi wa mkoa wa Pwani, kulia ni mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo na kushoto ni mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Abou Jumaa 

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI WAANDISHI WACHAGIZA


 Mratibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania TAMWA akizungumza wakati wa sherehe za siku ya mwanamke duniani zilizofanyika Maili Moja Kibaha mkoani Pwani zilizoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Pwani PWMO.


Mwakilishi wa Mahakama ya Mkoa wa Pwani Herieth Mwailolo akizungumza wakati wa sherehe za siku ya mwanamke zilizofanyika Maili Moja wilayani Kibaha.
Mwenyekiti wa Kituo cha Msaada wilaya ya Kibaha KPC Catherine Mlenga akizungumza wakati wa maadhimisho hayo



Mwanasheria wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Isihaka Ibrahimu akizungumza.
  

Gladys Munuo katikati ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo akizungumza kushoto ni mwenyekiti wa chama cha waandishi wa Habari wanawake mkoa wa Pwani PWMO Mwamvua Mwinyi


Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani PWMO Mwamvua Mwinyi akizungumza wakati wa sherehe za siku ya mwanamke duniani iliyofanyika Maili Moja wilayani Kibaha kushoto ni Herieth Mwailolo mwakilishi wa Mahakam ya mkoa wa Pwani na kulia ni Gladys Munuo mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA.


Mratibu wa Chama cha waanidhi wa habari mkoa wa Pwani PWMO Selina Wilson akisoma risala ya chama hicho wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani iliyofanyika Maili Moja wilayani Kibaha.   

Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA cha waandishi wa Habari wanawake mkoani Pwani (PWMO) kimeviomba vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na Mahakama polisi na mawakili kufanya kazi wa kuzingatia haki na kumaliza kesi zinazohusisha wabakaji na wanaofanya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Chama hicho Mwamvua Mwinyi wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na (PWMO) na kusema kuwa watoto na wanawake wengi wamekuwa wakinyimwa haki zao baada ya kufanyiwa vitendo hivyo.

Mwinyi alisema kuwa kuna haja ya vyombo vinavyohusika na utoaji haki kuwajibika bila ya upendeleo au rushwa ili kusababisha haki za wahanga kupotea kutokana na sherian kupindishwa.

“Endapo vyombo hivyo vya kutoa haki vingezingatia haki hakika walengwa wanaohusika na matukio hayo wangepewa adhabu kubwa ambazo zingewafanya wasiendeleze vitendo hivyo,” alisema Mwinyi.

Alisema kuwa haki za wahanga zinapotea kutokana na mashauri hayo kuchukua muda mrefu na hatimaye haki kupotea kabisa kwani ucheleweshaji wa makausudi mashauri hayo hupoteza haki.

“Wanaume wanaofanya unyanyasaji wa kijinsia,kubaka na kulawiti tatizo kubwa ni tamaa pamoja na kujihusisha na vitendo vya kishirikina vinavyo sababisha matukio hayo inayosababisha kukua kwa vitendo hivyo naomba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake na jamii irudishe majukumu yake kwa kulinda watoto kwenye maadili mema,” alisema Mwinyi.

Akizungumzia kauli mbiu ya siku ya wanawake mwaka huu,Tanzania ya viwanda wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi,alieleza,mkoa wa Pwani umedhamiria kuwa ukanda wa viwanda na uwekezaji.

“Kutokana na hilo utakuwa mkoa wa ajabu kuwa na ufahari wa kuwa na viwanda vingi huku ukiacha kutoa ajira kwa wazawa, akinamama ,wasichana na wengine huku vijana wetu wakiwa wanaongoza kukaa vijiweni kwa kukosa ajira,”alisisitiza Mwinyi.

Naye Mwenykiti Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Kibaha (KPC) Catherine Mlenga alisema kuwa wananchi wa Wilaya hiyo wanapaswa kutembelea kito hicho ili waweze kusaidiwa masuala mbalimbali ya kisheria kabla ya kwenda mahakamani.

Mlenga alisema kuwa wao kama watoa msaada wa kisheria wamapewa mafunzo na wanauwezo wa kutatua masuala hivyo kupunguza mzigo kwa mahakama kwa kuyamaliza mashauri kituoni kwao.  

Chama cha wanahabari wanawake Pwani kilianzishwa mwaka 2013 kikiwa na wanachama 15 huku kikikabiliwa na ubaha wa fedha kufika maeneo ya vijijini kuibua vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na changamoto nyingine za kijamii.

Mwisho.