Friday, June 6, 2025

WAKALA WA VIPIMO (WMA) YATAKA VIPIMO VIHAKIKIWE KILA MWAKA






WAKALA wa Vipimo Nchini (WMA) imetaka vipimo vya ujazo urefu na uzito wakati wa kupima bidhaa au kuhudumia wananchi lazima vihakikiwe kila baada ya miezi 12.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Kituo cha (WMA) kilichopo Misugusugu Wilayani Kibaha Mkoani Pwani Charles Mavunde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Mavunde amesema kuwa uhakiki huo ni takwa la kisheria ya vipimo sura 340 namba 19 ya mwaka 2002 inataka vipimo vinavyotumika kupima katika biashara au huduma nyingine za kijamii lazima vihakikiwe ndani ya muda huo.

Amesema kuwa sheria inatoa adhabu kwa mtu ambaye hata hakiki vifaa vinavyotumika katika kubebea au kupimia ambapo faini ni kati ya shilingi 100,000 hadi milioni 20 au kifungo jela miaka miwili.

"Kipimo chochote  kinachopima kuhudumia wananchi kinatakiwa  kufanyiwa uhakiki kila baada ya miezi 12 pia tunawapongeza wananchi kwa kuwa  na mwamko   kwenye uhakiki wa dira za maji kwani ni mkubwa," amesema Mavunde.

Amesema wanatarajia kuhakiki mita za maji  zaidi ya 87,000 kufikia mwishoni wa mwezi Juni 2025 ili kutambua usahihi wake kabla ya kwenda kufungwa kwa wateja na wamefanya zoezi la  uhakiki wa mita za umeme zaidi ya 5,500 za umeme mkubwa wa viwanda vya Mkoa wa Dar  es Salaam na mikoa mingine ili kuona kama zipo sahihi kulingana na matumizi viwandani. 

"Kwa upande wa dira za maji katika kipindi cha Julai  hadi Mei mwaka huu tayari wamehakiki dira  57,997 huku wakiwa na uwezo wa kuhakiki dira 100,000 kwa mwaka

Naye Ofisa  Vipimo  Mkuu Gaudence Gaspery amesema kuwa hivi sasa wanahakiki dira za  maji kwa kutumia mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuhakiki dira 10 kwa wakati mmoja.

Gaspery amesema kuwa baada ya kuhakikiwa na kuonekana zinafaa kwa matumizi huwekewa rakili yenye rangi ya chungwa  na ambazo zitagundulika zinahitaji kufanyiwa marekebisho hurekebishwa huku zile ambazo zitagundulika kwamba hazifai huteketezwa.

 

Thursday, May 29, 2025

MWANASHERIA MATATANI AKITUHUMIWA KUGHUSHI AKAUNTI YA KIJIJI NA KUJIPATIA FEDHA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 385 fedha za mauzo ya ardhi ambazo ziliwekwa kwenye akaunti ya kughushi ya mtu binafsi badala ya akaunti ya Kijiji cha Msufini Kidete Wilaya ya Mkuranga.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Domina Mukama akitoa taarifa ya Januari hadi Machi alisema kuwa fedha hizo zilikuwa ni asilimia 10 ya malipo baada ya Kijiji kuuza ardhi.

Mukama alisema kuwa mtu anayetuhumiwa kughushi akaunti hiyo ya Kijiji na kuingia kwenye akaunti yake binafsi ni mwanasheria wa kampuni ya Briliant Sanitary Ware Company Limited ambayo ilinunua eneo hilo.

"Fedha hizo ni asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya Kijiji baada ya mauzo ambapo zilipoingia mtu huyo alizitumia kwa matumizi binafsi lakini Takukuru walifanikiwa kuzirejesha fedha hizo ambapo kwa sasa kesi yake iko hatua ya uchunguzi,"alisema Mukama.

Aidha alisema kuwa fedha hizo baada ya kuzirejesha fedha hizo kwenye akaunti ya Kijiji hicho zimepangiwa matumizi ya kujenga madarasa mawili ya Shule ya Sekondari Mbezi Gogoni na madarasa mawili Shule ya Msingi Msufini.

"Katika hatua nyingine Takukuru imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 338 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 18 na utekelezaji wake unaridhisha,"alisema Mukama.

Alibainisha kuwa wamewafikia wananchi wa makundi mbalimbali ili waweze kuiunga Serikali mkono katika kuzuia vitendo ya rushwa kwa kupitia semina 67, mikutano ya hadhara 72, vipindi vya redio 5, uimarishaji klabu za wapinga rushwa 130.

"Tumejipanga Kuzuia na Kupambana na vitendo vya Rushwa katika uchaguzi Mkuu kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi kwa kuwafikia wadau wote,"alisema Mukama.

Aliongeza kuwa wanatoa elimu kwa wadau ambao ni vyama vya siasa, wasimamizi wa uchaguzi, wanahabari, wananchi na jamii nzima kwa ujumla ambapo anawaasa wananchi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuwa salama na kuepuka migogoro yenye kuleta viashiria vyenye rushwa.

"Katika kipindi tajwa Ofisi ilifanya chambuzi za mifumo 14 ikiwa ni pamoja na eneo la makadirio ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya
Mji Kibaha, Mafia, kituo cha Utalii Kazimzumbwi katika chambuzi wa mfumo wa usambazaji maji uliofanyika kuna mapungufu yalibainika na hatua zilichukuliwa.

Saturday, May 24, 2025

DIWANI MTAMBO AWASILISHA TAARIFA UTEKELEZAJI WA ILANI YA MIAKA 5

KATA ya Picha ya Ndege Halmashauri ya Mji Kibaha umeishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye kata hiyo.

Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata hiyo Karim Mtambo alipokuwa akiwasilisha utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka mitano 2020-2025.

Mtambo amesema kuwa anaishukuru serikali kwani imegusa sekta zote za kiamendeleo hivyo kufanya kero nyingi kupungua na wananchi kupata huduma kwa urahisi.

"Mfano hospitali ya Wilaya ya Lulanzi kwa sasa haina changamoto ya maji ikilinganishwa na kipindi cha nyuma na wananchi nao wanapata huduma ya maji kwa asilimia 95, ujenzi wa ofisi ya Kata ambapo iko hatua ya ukamilishaji",amesema Mtambo.

Amesema kuwa huduma za afya nazo zimetengewa fedha nyingi, miundombinu ya barabara nayo imeboreshwa, soko bado lina changamoto na kituo cha polisi nacho bado.

"Sekta ya elimu nayo imepatiwa fedha nyingi ambapo kwenye shule zetu za msingi miundombinu imeboreshwa na ufaulu umeongezeka ikilinganishwa na zamani,"amesema Mtambo.

 

GRACE JUNGULU AONGOZA KIKAO UTEKELEZAJI ILANI KATA YA PICHA YA NDEGE

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Grace Jungulu amewataka viongozi wanaotokana na chama kutoa majibu ya changamoto za wananchi baada ya vikao vya chama na siyo kubaki nayo ndani kwani wao ndiyo wanayoisimamia serikali.

Jungulu ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha uwasilishwaji wa utekelezaji wa ilani ya CCM ya miaka mitano iliyowasilishwa na diwani wa kata hiyo Karim Mtambo.

Amesema kuwa viongozi wamekuwa wakitoa majibu juu ya changamoto mbalimbali kwenye vikao vya chama hivyo kajibu hayo wayapatie na wananchi. 

"Twendeni na kwa wananchi kupitia mikutano ya kila baada ya miezi mitatu tuwajibu wananchi maswali yao kwa kupokea kero zao na kuzitafutia ufumbuzi,"amesema Jungulu.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Picha ya Ndege Karim Mtambo amesema kuwa anaishukuru serikali kwa kutoa fedha ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mtambo amesema sekta zote zimeguswa na miradi hiyo na kufanya changamoto za wananchi kupungua huku serikali ikiendelea kutatua kero zilizopo.
 

Wednesday, May 21, 2025

ATAKA SIMBA IUNGWE MKONO KUCHUKUA KOMBE LA SHIRIKISHO DHIDI YA BERKANE

 

WACHEZAJI viongozi na benchi la ufundi la timu ya Simba wametakiwa kupambana kuhakikisha wanatwaa kombe la Shirikisho.

Aidha washabiki na wapenzi wa soka nchini wametakiwa kuwa na mshikamano na kuacha tofauti zao za ushabiki na kuungana ili kuisadia timu ya Simba kwenye mchezo wao wa fainali dhidi ya Berkane mchezo utakaochezwa uwanja wa Amani Zanzibar.

Akizungumza na Brailo Media aliyewahi kuwa mlezi wa Tawi la Simba Tishio Kibaha Fahim Lardhi amesema kuwa Watanzania wanapaswa kuungana kwenye mchezo huo kwani ni wa heshima kwa nchi.

Lardhi amesema kuwa licha ya Simba kufungwa kwenye hatua ya kwanza kwa magoli 2-0 lakini wanaimani kuwa Simba itapindua matokeo na kuwa mabingwa.

"Tuenzi maneno ya Rais Hayati Dk John Magufuli aliyoitoa kwenye uwanja wa Mkapa wa kutaka Simba au timu nyingine ya Tanzania kuleta kombe la Afrika,"amesema Lardhi.

Amesema kuwa itakuwa ni fedhaha kwa Simba kuchukua kombe hilo ambalo litakuwa kwenye ardhi ya Tanzania ambapo mwaka 1993 walifungwa kwenye fainali na Stella Abidjan ya Ivory Coast.

"Mwaka huu kwa uzalendo wetu tuhakikishe tunalipigania Taifa letu kama kila mtu atatimiza wajibu wake kuanzia wachezaji hadi kwa mashabiki,"amesema Lardhi.

Amewaomba Watanzania kuwa na mshikamano kwa wakati wa maandalizi na wakati wa mchezo kwa kuungana na kuacha tofauti kwani hiyo ni mechi ya heshima kwa nchi.


Monday, May 19, 2025

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA WARIPOTI HABARI ZA UCHAGUZI KWA UMAKINI

 VYOMBO vya Habari nchini vimetakiwa kutoa taarifa za vyama vyote vya siasa kwenye kampeni wakati wa uchaguzi wa mwaka huu ili wananchi waweze kujua sera za vyama na kuchagua viongozi bora.

Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Asasi ya Maendeleo ya Vijana (YPC) Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Ilunde alisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutoa elimu ambayo itasaidia kujua sera za vyama vyote bila ya kupendelea baadhi ya vyama.

"Vyombo vya habari vitoe taarifa za vyama vyote kwa usawa bila ya upendeleo hata kwa vyama vidogo navyo vipate nafasi ili vieleze sera zao na wananchi wachague wagombea ambao wataona wanawafaa,"alisema Ilunde.

Alisema kuwa wananchi wakisikia sera za vyama vyote watakuwa na maamuzi mazuri ya kuchagua viongozi ambao wataona wana sera nzuri na watakuwa wamechagua wakiwa na uhakika wa wanao wachagua wana sera nzuri.

"Pia vyama vya siasa nchini vinatakiwa vitoe kauli za kulinda amani iliyopo na kuachana na kauli za chuki na uchochezi ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Aidha alisema kuwa amani ni tunu ya Taifa ambayo inabidi ilindwe ambapo kauli zisizo nzuri husababisha amani kutoweka na wananchi kutoelewana.

"Nayo Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ihakikishe inakutana na wadau wa siasa mara kwa mara ili kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi ambapo itasaidia kuondoa malalamiko wakati wa uchaguzi,"alisema Ilunde.

Aliongeza kuwa wananchi kwa maeneo zoezi la uhakiki wapiga kura linafanyika wajitokeze kuangalia taarifa zao na ikifika muda wa kupiga kura wajitokeze kwa wingi kwa wale wenye sifa.

"Kwa makundi ya vijana wanawake na watu wenye ulemavu wanaotaka kuwania nafasi za uongozi wajitokeze kuwania nafasi hizo kupitia  vyama vyao na vyama vitoe nafasi,"alisema Ilunde.

SERIKALI IDHIBITI FEDHA HARAMU

SERIKALI imeshauriwa kutumia sheria zilizopo kudhibiti utoroshwaji wa fedha haramu kwenda nje ya nchi ambapo husababisha kushindwa kuanzisha miradi mipya ya maendeleo na inayoendelea kukwama.

Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Maendeleo ya Vijana (YPC) Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari hizi.

Ilunde ambaye pia ni Mwentekiti wa Policy Forum alisema kuwa mbali ya miradi kushindwa kufanyika hata ajira kwa vijana hukosekana na hali hiyo huathiri bajeti ya nchi ambapo fedha nyingi hupotea.

"Watu wanaotorosha fedha haramu au utakatishaji wa fedha hufanya udanganyifu kwenye baadhi ya maeneo kwa wafanyabiashara hutumia hati za kibiashara kuweka gharama kubwa, kusafirisha bidhaa kutoka au kwenda nje ya nchi na kudanganya gharama za uendeshaji wa kampuni,"alisema Ilunde.

Alisema kuwa endapo sheria zitawabana watu hao itasaidia kulipa kodi halali kwani kupitia udanganyifu huo hawalipi kodi stahiki hivyo kuitia nchi hasara kubwa.

"Tungeomba sheria ziboreshwe ili kudhibiti watu hao kwa kuwa na mifumo ambayo itadhibiti utoroshwaji wa fedha haramu na watachukuliwa hatua kali za kisheria,"alisema Ilunde.

Aidha aliiomba serikali kuongeza bajeti kwa Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo ili waandishi waweze kupata mafunzo yatakayoweza kuwafichua watu hao wanaotumia fedha haramu na watu kulipa kodi kwa haki na wasifanye udanganyifu.

"Serikali mashirika yasiyokuwa ya kiserikali taasisi za elimu zitenfeneze vijana kuwa wazalendo watakaochukia udanganyifu ili fedha zinazotokana na kodi zilete maendeleo na itasaidia vijana kuwa na ajira,"alisema Ilunde.

Aliongeza kuwa athari zinazotokana na fedha haramu ni kuathiri sekta muhimu za kimaendeleo kama vile elimu, afya, kilimo na miundombinu na sekta nyingine.

"Vyanzo vinavyosababisha hali hiyo ya utoroshwaji wa fedha haramu ni pamoja na rushwa, hati za kibiashara, usafirishaji wa binadamu, usafirishaji wa madini na utakatishaji wa fedha,"alisema Ilunde.