Sunday, April 14, 2024

KIMITI AIPONGEZA SERIKALI YA AWAMU YA SITA YA MH DKT SAMIA SULUHU HASSAN RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA






MWENYEKITI wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Taifa Mh Paul Kimiti ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassani namna anavyoenzi fikra na falsa za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kuweza kutenga eneo la kujenga Makumbusho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Dodoma.

Kimiti ameyasema hayo katika Maadhimisho ya kitaifa ya kumbukumbu ya miaka 102 ya kuzaliwa kwa Mwl Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Ukumbi wa Mtumba tarehe 13.4.2024 mkoani Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Dkt Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wengi waliojitokeza kushuhudia Maadhimisho ya kumbukumbu hiyo.

Kimiti amesema kuwa jambo hilo litasaidia kutunza Kumbukumbu za Mwasisi huyo wa Taifa kwa kufanya vijana na makundi mengine kwenda kujifunza pia itaongeza pato la Taifa akiamini watu wa mataifa mengi watakuja kujifunza mambo mbalimbali yaliyofanywa na Nyerere.


Saturday, April 13, 2024

JAMII YAASWA ISILE MALI ZA YATIMA


SHEIKH Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamis Mtupa amewataka watu wanaodhulumu mali za yatima waache kwani ni sawa na kula moto ambao utawachoma matumbo yao.

Mtupa aliyasema hayo Wilayani Bagamoyo wakati wa dhifa kwa ajili ya watoto yatima, wajane na wazee iliyoandaliwa na Taasisi ya (SHAKIBA) Islamic Foundation ya Bagamoyo.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwadhulumu mali za wazazi wao na kuzitumia huku watoto hao wakiwa hawaruhusiwi kuzitumia.

"Watu wanaokula au kujinufaisha na za yatima ni sawa na kula moto sawa na kaa la moto kulitia tumboni hivyo moto huo utawachoma na kila watakalolifanya halitafanikiwa,"alisema Mtupa.

Aidha alisema kuwa mtu anayekula mali ya yatima anamkanusha Mungu siku ya malipo atalipia dhuluma aliyoifanya kwa yatima hao ambao wanahitaji kusaidiwa.

"Tunapaswa kuwafadhi watoto yatima badala ya kuwatesa ili tupate thawabu wawekeni kwenye sehemu yao kwani ukimtunza kumpa faraja na kumlea utajiwekea mahala pema peponi,"alisema Mtupa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa SHAKIBA Alhaj Abdul Sharifu alisema kuwa taasisi hiyo ina lengo la kusaidia watu mbalimbali wenye mahitaji wakiwemo wajane, yatima na wazee.

Sharifu alisema kuwa tayari wameanzisha kituo cha kulea yatima ambapo 124 anawalea huku 24 akiwa anawsomesha wakiwa madarasa mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Firdaus Centre Kituo cha Kulea Yatima cha Kongowe Kipala Mpakani Dk Sheikh Sharifu Firdaus alisema kuwa hakuna jambo baya kama kufiwa na wazazi.

Dk Sheikh Firdaus alisema kuwa watoto yatima wanapata tabu sana na wanachangamoto nyingi sana wanazokutana nazo hivyo wanahitaji misaada mbalimbali.

Kwa upande wake mwenyekiti idara ya wanawake Jamila Suleiman alisema kuwa wanawake wanahitaji kusaidiwa na waume zao na siyo kuwapa mizigo wanawake.

Suleiman alisema kuwa wao wanapigania haki za wanawake ambapo dini haitaki wanawake wanyimwe haki zao ambapo vipigo huondoa upendo na kusababisha visasi na majadiliano ni suluhu ya ugomvi.

Mratibu wa SHAKIBA Taifa Dk Fakhad Mtonga alisema kuwa lengo la kuanzishwa ni kusaidia jamii kwenye masuala mbalimbali yakiwemo ya afya, elimu, kilimo, uvuvi na elimu ya dini.

Dk Mtonga alisema kuwa pia wamekuwa wakitoa elimu ya kukabili vitendo vya ukatili na ukatili wa jinsia, kujitambua na kukabili vitendo viovu na wanatarajia kuanzisha kituo cha afya ambapo wasiojiweza waratibiwa bure na watu wengine watalipia gharama za matibabu kwa bei nafuu kilianzishwa 2020.

Thursday, April 11, 2024

SERIKALI YAFANYA UWEKEZAJI MFUMO MPYA WA KIELETRONIKI WA UNUNUZI WA UMMA NeST

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma unaojulikana kama National e-Procurement System of Tanzania (NeST) kabla ya uwekezaji huu.

Ununuzi wa umma ulikuwa ukifanyika kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma uliojulikana kama Tanzania National e-Procurement System (TANePS) ambao ulijengwa na kampuni ya kigeni kutoka Ugiriki lakini Serikali ilibaini changamoto nyingi  kwenye ununuzi uliokuwa ukifanyika kupitia mfumo wa TANePS ikiwemo taarifa zote za Ununuzi wa umma kuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya kigeni nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa kujenga uwezo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Amin Mcharo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dodoma, kuhusu mafanikio makubwa waliyopata katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa changamoto hii na nyinginezo zilipelekea uamuzi wa kuanzisha mfumo mbadala ambao utakuwa bora zaidi, wenye kuleta tija, unaojengwa na wataalam wa ndani na kusimamiwa na Serikali. 

Aidha  amewaasa wananchi kujisajili katika mfumoNeST na kuomba zabuni mbalimbali zinazotangazwa na Serikali ili kuweza kujipatia kazi na kuhakikisha anayeomba amekidhi vigezo vinavyotakiwa katika kuomba zabuni husika na pindi wanapopata zabuni wazifanye kwa uadilifu na ufanisi ili waendelee kuaminiwa katika miradi mingine kutokana zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inatumika kwenye ununuzi wa umma.



Ikumbukwe kuwa PPRA imekuwa ikitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwahudumia wananchi ili kutimiza lengo la Serikali iliyopo madarakani  ya kupeleka huduma kwa wananchi na kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo, kama inavyoonyesha katika Sura ya kwanza,Kipengele cha 8(e) ya Ilani hiyo wakati sura hiyohiyo kipengele cha 8 (f) ikielezea kujikita katika  kutengeneza ajira zisizopungua milioni 8 katika sekta rasmi na zisizo rasmi kwa ajili ya vijana.

Tuesday, April 9, 2024

*WMAs ZATAKIWA KUWA NA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA*

 

Serikali imewataka viongozi wa Jumuiya za Hifadhi Wanyamapori (WMAs) kuzingatia matumizi sahihi ya fedha  ili kuwanufaisha wananchi wa vijiji wanachama   pia kuzingatia mikataba inayoingiwa na WMAs hizo  kwa maslahi ya Taifa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ametoa kauli hiyo  leo Aprili 8,2024 Jijini Dodoma wakati wakati wa kikao cha viongozi wa Jumuiya hizo pamoja  na baadhi ya maofisa wanyamapori wa wilaya kuhusu changamoto za usimamizi wa maeneo ya WMAs nchini.

Amesema rasilimali fedha ni lazima  zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo ya vijiji kwa kuwashirikisha wananchi wa vijiji hivyo. 

 “Ni lazima muweke mkazo katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwazi na matumizi sahihi ya fedha pamoja na  utoaji wa taarifa kwa wanufaika kwenye vijiji husika, msipofanya hivyo uongozi utageuka shubiri mtakapofanyiwa ukaguzi” Mhe. Kairuki alisisitiza.

Amesema kuwa katika kipindi cha Mwaka wa fedha  2022/2023 Serikali imetoa mgao wa takribani bilioni 9.6 ambazo Serikali  inaamini zimetumika kwa mujibu wa Kanuni za WMAs ambazo zinaelekeza kuwa sehemu ya fedha hizo zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo ya vijiji. 

Amesema kupitia kanuni hizo za uanzishaji na uendelezaji wa maeneo ya hifadhi kwa sasa kuna jumla ya WMAs 22 zilizodhinishwa na kupata haki ya matumizi ya rasilimali za wanyamapori lakini kuna nyingine 16 ambazo ziko kwenye mchakato wa kuanzishwa.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuzishukuru WMAs kwa mchango wao katika kusaidia  kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na katika jamii  pamoja na kusaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jamii na vijiji wanachama.

“Hii imejidhirishisha katika Sekta ya uwindaji wa Kitalii na utalii wa picha ambapo tumeshuhudia umekuwa chachu ya uchumi  kwa vijiji wanachama ambao wanaunda jumuiya zetu” Mhe. Kairuki amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wadau wa uhifadhi imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha Jumuiya zinaendelea kuimarika ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo viongozi wa WMAs kwa lengo la kuimarisha utawala na usimamizi wa maeneo hayo na kuwezesha mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS) ambapo takribani VGS 540 wamepata mafunzo katika Chuo cha Wanyamapori Likuyuseka – Maganga.

Pia amesema Serikali imewezesha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo magari ya doria kwa baadhi ya Jumuiya kama Mbarangandu na Nalika, Vilevile, Jumuiya zimewezeshwa vifaa vya uwandani kama vile mahema, GPS, kamera, sare za Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) na vifaa vya ofisini kama kompyuta katika Jumuiya za MBOMIPA, WAGA na UMEMARUWA.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna CP Benedict Wakulyamba, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe ,Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA,wawakilishi wa Makamishna Uhifadhi wa TANAPA, NCAA na TFS, Wakuu wa Idara na Taasisi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Maafisa Wanyamapori wa Wilaya, Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii na  Viongozi wa Jumuiya za Wanyamapori.

Sunday, April 7, 2024

WASICHANA WATAKIWA KUWA MABALOZI KUPINGA VITENDO VYA UKATILI


Kamati ya Kupinga Ukatili wa kijinsia iliyo chini ya Wanawake na Samia imewataka wasichana ( Mabinti ) kuhakikisha wanakuwa viongozi wa kujiongoza wenyewe ili kuhakikisha wanapingana na suala zima la ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri Ili kukomboa jamii inayokumbana na suala la unyanyasaji wa Mabinti na wanawake.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati ya ukatili wa kijinsia mkoa wa Dodoma  Grace Ringo wakati wa mafunzo ya utoaji  wa elimu katika chuo Mipango  chini ya uongozi wa Binti Makini kuhusu kupinga unyanyasaji kwa wanawake.

Amesema yapo mambo ambayo mwanamke wanakutana nayo kama Ulawiti, kupigwa , pamoja na kukosa haki ambazo zinamfanya mwanamke akashidwa kujiamini katika nafasi yake na kupelekea anguko  la uchumi katika jamii hata familia hivyo niwaombe Mabinti ambao mmepata elimu leo muhakikishe mnasaidia jamii

Kwa upande wake Mjumbe wa kamati ya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Dodoma Irene Sanga amewasihi Mabinti kutumia mitandao kwa ajiri ya kuwaingizia kipato na sio kutumia mitandao kwa kufanya mambo maovu huku akiwasisitiza wawe na nidhamu Katika jamii ya leo

"Wapo Mabinti ambao wanatumia mitandao kwa kuangalia vitu visivyofaha na kupelekea Vijana kualibika kwa kuiga mambo ambayo kwa nafasi na umri bado na kulazimisha kufanya vitu kama rushwa za ngono," amesema Sanga.

Naye Mjumbe wa kamati ya kupinga ukatili chini ya ofisi ya Mkoa wa Dodoma  Rhoda Denis amewataka wasichana kuzingatia kujithamini na kujitambua  Ili kujikomboa katika maisha ya jamii ya leo.

"Wapo wanawake wanapigwa na waume zao sababu kukosa kujitambua ila kama utajua thamani yako utaweza kufika sehem ambayo utaweza kupata msaada," amesema Rhoda

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Binti Makini Chuo Cha Mipango Dodoma Swaumu Rajabu amewahimiza wanawake kujitokeza kugombania nafasi mbalimbali za uongozi kwani wanawake tunanafasi kubwa sana katika jamii leo hivyo tuwe mstari wa mbele kuwasihi na wengine unaowaona wanaweza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika nchi yetu .

 Aidha amesema kuwa chuo Cha mipango kinaenda kufanyika uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanafunzi ikiwemo nafasi mbalimbali kama Rais wa chuo Cha mipango, wabunge pamoja nafasi nyingine hivyo amewaomba Binti Makini wote wenye sifa wajitokeze wakagombee nafasi hizo.

Ikumbukwe kuwa kamati ya Kupinga Ukatili wa kijinsia iliyochini ya wanawake na Samia inaendelea kufanya mafunzo ya utoaji wa elimu kwa wanawake na wanaume ili kuhakikisha elimu hii inawafikia wengi ili kutengeneza Taifa lenye nguvu kazi na lenye Maadili ikiwa na kauli mbiu IPELEKE DODOMA DUNIANI NA DUNIA  ILETE  DODOMA

Saturday, April 6, 2024

MTAA WA KWAMFIPA WAANZA UJENZI WA SEKONDARI

MTAA wa Kwamfipa Kata ya Kibaha Mkoani Pwani umeishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ambayo utawapunguzia changamoto wanafunzi wa Mtaa huo wanaotembea umbali wa Kilometa nane kwenda Shule ya Sekondari ya Simbani.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kibaha Mohamed Muanda alipotembelea kuangalia maendeleo ya ujenzi huo kwani ni ukombozi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye Mtaa huo.

Muanda amesema kuwa hicho kilikuwa kilio cha wananchi wa Mtaa huo pamoja na Mtaa wa Mwendapole ambapo Mitaa hiyo miwili ina jumla ya shule tatu za Msingi ambapo wanafunzi wote husoma Shule hiyo ya Simbani ambayo ni ya Kata.

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo Jumanne Mwinshehe amesema kuwa wananchi walijitolea kwa kufanya usafi kabla ya ujenzi kuanza huo ukiwa ni mchango wa wananchi na wataangalia fedha za Halmashauri zitaishia wapi ili wananchi wachangie ambapo ujenzi huo uko hatua ya msingi.

Naye Christina Sabai wanafunzi wanakwenda Sekondari mbali na kwa watoto wa kike ambao hukumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kurubuniwa na waendesha pikipiki na kuhatarisha masomo yao kwa kupata ujauzito.

Aidha fundi wa ujenzi wa mradi huo wa Shule hiyo Juma Mabula amesema watatumia siku 75 kukamilisha ujenzi huo kwani vifaa vyote viko hivyo wanaamini watakamilisha kwa muda uliopangwa ili wanafunzi waanze kusoma.

Friday, April 5, 2024

TAASISI YA KUMUOMBEA RAIS NA WASAIDIZI WAKE YAFANYA MAOMBI KUIOMBEA SERIKALI

 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Taasisi ya kumuombea Rais  na wasaidizi wake imefanya maombi ya kuombea viongozi wa serikali akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Spika wa Wabunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Akson pamoja na Mawaziri na Wabunge. 

Katibu Mkuu wa taasisi hiyo Angelina Malembeka akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya maombi hayo amesema lengo ni kuwaombea ili waongoze kwa hekima.

Malembeka amesema kuwa anaamini taasisi hiyo itaweza kusaidia mambo mengi yasiyofaa yasipate nafasi na malengo ya taasisi ni kumuombea Rais  na wasaidizi wake pamoja na wataalamu mbalimbali wanaofanya shughuli za jamiii ndani ya nchi.

"Katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mambo yanaenda vinzuri ila wao wanafanya kazi ya kuombea Ili kuhakikisha utekelezaji unaenda vizuri zaidi,"amesema Malembeka.

Alisema wanaona mambo yanaenda vizuri katika miradi mbalimbali na utekelezaji wa ilani ya CCM na kazi yao ni kuombea viongozi wawe na ujasiri, nguvu na kuwapa matumaini na ikumbukwe kuwa suala hili la kuombea Rais na wasaidizi wake ni suala la muendelezo na kazi yake ni kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu.

Aidha amesema kuwa idadi ya wanachama ni zaidi ya wanachama 600 lakini walioshiriki maombi hayo walikuwa ni 208 ambapo wengine hawakuhudhuria kutokana na sababu mbalimbali.