Friday, February 23, 2024

KIJANA WA KITANZANIA AGUNDUA MFUMO WA KITAALUMA KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA MSINGI HADI CHUO KIKUU

NA WELLU MTAKI Dodoma.

KIJANA wa Kitanzania Alpha Mbennah mwenye taaluma ya Uhandisi amegundua Mfumo wa Uchakataji,Uhifadhi na Uandaaji wa Taarifa za Kitaaluma za wanafunzi kuanzia ngazi ya Elimu msingi mpaka Vyuo Vikuu uitwao "SPIN-ED Academic Performance Management System utakaowezesha kuleta ufanisi katika kazi.

Akizindua mfumo huo  Jijini Dodoma katika Mkutano wake na Wanahabari Mhandisi Mbennah amesema kuwa mfumo huo unamruhusu mwalimu katika ngazi tajwa kuweza kukusanya na kuingiza alama za mwanafunzi aliyesajiliwa katika mfumo kisha huchukua alama hizo na kuzichakata kwa kutengeneza wastani uliopimwa au usiopimwa kubaini gredi ya alama hizo, yaani A, B, C, n.k.

“Pia huu mfumo unaweza kubaini wastani wa darasa husika, nafasi aliyoshika kila mwanafunzi katika somo husika na katika darasa kwa ujumla pamoja na kutengenza ripoti ya maendeleo ya kitaalamu kwa kila mwanafunzi aliyesajiliwa kwenye mfumo, katika darasa husika, kutoa maoni ama comments zinazohusiana na ufaulu wa mwanafunzi na kuchora grafu ya maendeleo ya kitaaluma kwa kila mwanafunzi".

Mbenah amesema kuwa vyote hivyo hufanywa moja kwa moja huku akisema kuwa hivo ni baadhi ya vipengele vilivyopo katika mfumo wa SPIN-ED.

“Niseme tu kwamba vina umuhimu mkubwa sana katika uchakataji wa taarifa za kitaaluma za wanafunzi kwani huwasaidia walimu na wadau mbalimbali wa elimu kufanya maamuzi mbalimbali na hatimae kuongeza ufanisi katika mbinu za ufundishaji na ujifunzaji".

Aidha amesema sababu kubwa ya yeye kufanya ugunduzi wa mfumo huu wa SPIN-ED ni kutokana na changamoto alizoziona wakati akiwa mwalimu wa kujitolea katika moja ya shule hapa nchini, hususan katika uandaaji wa ripoti za maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi.

wakati mwingine huchukua muda mrefu kwa Walimu kuandaa na hata wakati mwingine Walimu kukosa hamasa ya kutoa majaribio ya mitihani ya Mara kwa Mara ya kuwapima wanafunzi wakihofia kuchukua muda kwa uandaaji wa ripoti na Maendeleo yao.

Mfumo huu wa SPIN-ED ameugundua mwaka 2021 na kuanza kufanya kazi mwaka huohuo ambapo mpaka kufika sasa zipo shule 3 zinazotumia mfumo huu.

SERIKALI KUENDELEA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA NA RUSHWA



NA WELLU MTAKI , DODOMA.

SERIKALI inaendelea kukabiliana na masuala ya  biashara ya dawa za kulevya na rushwa nchini  ili kuhakikisha wanajenga taifa lililo imara kwa kutoa Elimu kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya  Aretas Lyimo Jijini Dodoma   wakati  akifunga mafunzo kuhusu mkakati  wa habari , Elimu , mawasiliano  na programu ya TAKUKURU rafiki pamoja na  tatizo za dawa za kulevya , mapambano dhidi ya rushwa kwa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano.    

Lyimo amesema kupitia mafunzo waliopewa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano yatasaidia kuleta matokeo chanya ya  kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na Rushwa kwani ni vitu vinavyofanana.

“Naamini kupitia muunganiko wetu na klabu ambazo tayari tumeshanzianzisha huko mashuleni itasaidia kuwafikia kwa uharaka zaidi watu katika ngazi za mitaa hadi huko kwenye Halmashauri  wanafunzi wengi wanatokea kwani huko,”amesema. Lyimo

Amesema matunda ya ushirikiano kati ya TAKUKURU na taasisi ya kupambana dawa za kulevya tayari yameanza kuonekana kwani vitu hivyo vimekuwa vikiisumbua serikali katika kuhakikisha wote wanao husika wanatiwa mbaroni na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Nitoe wito kwa wadau kuwa nyenzo pekee ya kuepusha watu kujiingiza kwenye Rushwa na dawa za kulevya ni kutoa elimu hata tukiendelea kukamata kwa namna gani lazima tuhakikishe tunatoa elimu pamoja na kushirikiana na vyombo vya habari ili watusaidie kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja,”amesema.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU Bi. Neema Mwakalile amesema kilichotokea kwenye mafunzo hayo kinadhihirisha ushirikiano  uliopo kati ya TAKUKURU na Mamlaka ya Kupambana na dawa za Kulevya ni mkubwa kwani vitu hivyo vinafanana na mapambano yanapaswa kuimarishwa zaidi.

Mwakalile amesema kuwa washiriki wamejifunza juu ya tatizo la dawa za kulevya, sababu za matumizi ya dawa hizo pamoja na kutambua dawa tiba ambapo vijana wengi wameonekana kujiingizia kwa kiasi kikubwa katika janga hilo huku akiongeza kuwa elimu waliyo wapatia washiriki katika mkutano huo itaenda kuumarisha zaidi mapambano na hatimaye kufikia hazma ya Serikali.

“Washiriki walipitishwa kwenye mkakati wa kupambana na Rushwa ili kuelewa zaidi na namna ya kwenda kuelimisha wanafunzi pia mafunzo haya yatasaidia jamii kuichukia Rushwa na kuepukana na Dawa za kulevya,”amesema.Mwakalile

Pia ameongeza kuwa katika mambo mengi waliyowafundisha wataenda kutoa elimu hasa kwa wanafunzi kwani swala hilo limekuwa mtambuka. 

 “Ni lazima kuanza kuwajenga wanafunzi wa shule msingi na sekondari kwani wao ndio watakuwa msingi mzuri kwenda kupinga na kukataa dawa za kulevya pia  Rushwa na dawa za kulevya vina madhara makubwa kwenye nyanja zote elimu na uchumi,”ameongeza.

Taasisi ya kupambana na Rushwa na TAKUKURU waliingia makubaliano 20/5 2023 kwaajili ya kutoa elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya.

Thursday, February 22, 2024

CHESTMOKA MABINGWA KIBAHA VIJANA CUP

TIMU ya soka ya Chestmoka imetwaa ubingwa wa Kibaha Vijana Cup kwa kuifunga Muharakani kwa penati 6-5 na kujinyakulia kiasi cha shilingi milioni 1.

Mchezo huo wa fainali ulichezwa kwenye uwanja wa Mwendapole Wilayani Kibaha Muharakani walijinyakulia kiasi cha shilingi 500,000 na washindi watatu Tp Pwani wakijinyakulia seti ya jezi.

Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mussa Ndomba ambaye alimwakilisha mdhamini wa ligi hiyo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amesema michezo ni afya na ajira.

Ndomba amesema kuwa Halmashauri itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya michezo ili vijana waweze kucheza na kujipatia ajira.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani COREFA Mohamed Lacha amesema kuwa malengo ni kutaka soka lichezwe ndani ya mkoa huo.

Lacha amesema ili soka likue ni kuwa na michezo mingi ili kuibua vipaji vingi na kuviendeleza ili kuwa na timu nzuri.

Naye meneja wa mashindano hayo Walter Mwemezi amesema jumla ya timu 16 zilichuana kwenye mashindano hayo.

Mwemezi amesema kuwa matarajio yao kwa mwakani ni kushirikisha timu nyingi ili mashindano hayo yawe na msisimko zaidi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Koka Said Mbecha amesema kuwa Mbunge ameahidi kuendelea kusaidia michezo ili vijana wengi wapate fursa mbalimbali zilizopo kwenye michezo.

Tuesday, February 20, 2024

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA KUENDELEA KUWEZESHWA

 


NA WELLU MTAKI, DODOMA

Serikali inaendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ikiwa ni pamoja na kuboresha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza kasi ya mapambano na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la dawa za kulevya nchini. 

Hayo yamesemwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera bunge na uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali Katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa Mwaka 2023

Amesema Serikali imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 Zaidi kilogramu milioni 1 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini huku Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo.

"Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 kilogramu 1,965,340.52 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini. Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo. Aidha, jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa" amesema Mhagama.

Aidha amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa zaidi kilogramu milioni 15 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria.

"Kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11. Aidha, Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria" amesema Mhagama.

Pia ameeleza kuwa kumekuwepo na ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini ongezeko hilo ni sababu ya kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za  Kulevya imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoa elimu ya dawa za kulevya na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa nchini ambapo sasa zitaitwa  klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya. 




KOKA ATOA FEDHA NA JEZI KWA WASHINDI KIBAHA VIJANA CUP





MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametoa fedha na vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 1.7 kwa ajili ya washindi wa Kombe la Kibaha Vijana Cup.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa Chama Cha Soka Kibaha (KIBAFA) ofisini kwake kwa niaba ya Mbunge huyo Katibu wa Mbunge Method Mselewa amesema fedha hizo na vifaa hivyo vitatolewa kwenye hatua ya fainali itakayochezwa Februari 21 kwenye uwanja wa Mwendapole.

Koka akizungumza kwa njia ya simu amesema kuwa ameamua kujitolea ili kuinua vipaji vya vijana wa Kibaha kwani michezo ni ajira kubwa kwa vijana na wengi wamenufaika kupitia soka na kuwa ni sehemu ya maendeleo.

Amesema kuwa ataendelea kusaidia michezo mbalimbali ili vijana wapate fursa kwenye timu kubwa ambapo chimbuko huanzia chini ambako ndiyo kwenye msingi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa KIBAFA David Mramba amesema kuwa wanamshukuru mbunge huyo kwa kuchochea sekta ya michezo kwenye Jimbo hilo na kuwafanya vijana kushiriki michezo.

Naye Mjumbe wa soka la wanawake kupitia chama hicho Jesca Sihha amesema kutolewa zawadi hizo ni chachu kwa wanasoka na kuomba na soka la wanawake nalo lipewe kipaumbele.

Monday, February 12, 2024

UJENZI MADARASA, USHIRIKIANO WAZAZI, WALIMU NA WADAU KICHOCHEO UFAULU MZURI BUNDIKANI


MTAA wa Uyaoni Kata ya Maili Moja Wilayani Kibaha umeishukuru serikali kwa kujenga madarasa saba yenye thamani ya shilingi milioni 140 kwenye Shule ya Sekondari ya Kata ya Maili Moja Bundikani kwa kipindi cha miaka mitatu na kuifanya iwe na miundombinu mizuri na kuongeza ufaulu.

Aidha serikali ilitoa fedha ambazo zimejenga vyoo matundu 18 pamoja ujenzi wa darasa moja ambalo kwa sasa liko hatua ya umaliziaji na mwaka huu imefuta daraja sifuri kwa kidato cha nne ambapo mtaa huo ni mlezi wa shule hiyo.

Mwenyekiti wa Mtaa huo Fadhil Kindamba amesema kuwa ufaulu mwaka huu wanafunzi 22 wamefaulu daraja la kwanza, 73 daraja la pili 144 daraja la tatu na 130 daraja la nne.

Kindamba amesema ufaulu huo umetokana ushirikiano uliopo baina ya walimu, wazazi na wadau wengine wa elimu na kuboreshwa kwa miundombinu ya shule.

Katika hatua nyingine mtaa huo unatarajia kujenga vibanda viwili vya biashara kwa ajili ya kuvipangisha ili kujiongezea mapato na tayari wana matofali 500 kwa ajili ya kuanzia ujenzi utakaoanza hivi karibuni.

Amesema pia wanatarajia kuanzisha mnada ambapo tayari eneo limeshapatikana baada ya mwananchi mmoja kwenye mtaa huo kujitolea eneo kwa ajilo hiyo.