Wednesday, November 22, 2023

PWANI YAMSHUKURU RAIS KWA KUIPATIA FEDHA ZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO.

SERIKALI Kuu imeupatia Mkoa wa Pwani kiasi cha shilingi  trilioni 1.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imeainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hayo yamesemwa na Kamisaa ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge  wakati akiwasilisha taarifa ya miradi iliyotekelezwa mkoani humo katika kipindi cha Machi 2021 hadi Juni 2023 kwenye kikao cha Kamati kuu ya Chama hicho mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kwa Mfipa wilayani Kibaha.

Kunenge amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni mafanikio makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya utawala wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, nishati, maji na miundombinu ya barabara.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao amesema chama kimeridhika na miradi  iliyotekelezwa na serikali imetimiza  matakwa yaliyopo kwenye Ilani ya CCM  katika kuwaletea  maendeleo wananchi wake.

Kwa upande wake Katibu  wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani  Benard Ghatty amesema hadi sasa serikali imefikisha asilimia 98 ya  utekelezaji wa miradi na kwamba sehemu iliyosalia ni ndogo ambapo wanaamini ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu miradi yote itakamilika.

Monday, November 20, 2023

MAOFISA TARAFA NA WATENDAJI KATA PWANI WATAKIWA KUWA WABUNIFU KULETA MAENDELEO KWA WANANCHI

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka Maofisa Tarafa na Watendaji Kata kuwa wabunifu kwa kutafuta suluhisho la kutatua changamoto za wananchi.

Ameyasema hayo Mjini Kibaha wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ili kuboresha utendaji kwa maofisa hao kutoka Halmashauri tisa za mkoa huo.

Kunenge amesema kuwa kazi kubwa ya kiongozi ni kutatua changamoto ili kuwaletea wananchi maendeleo kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo pia kujua jamii inataka nini.

"Inashangaza kuona Rais anapelekewa malalamiko kutoka kwa wananchi na sisi tupo ambapo tungeweza kutatua changamoto husika lazima tuwe na ubunifu na kufanya kazi kwa weledi,"amesema Kunenge.

Naye Mkurugenzi msaidizi idara ya serikali za mitaa Ibrahim Minja amesema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuwaendeleza kiuwezo katika utekelezaji wa majukumu yao, kuwajengea uwezo na ufanisi na kujua na kuzifuata taratibu  kanuni, sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Minja amesema kuwa yanawahusisha maofisa hao 160 ambapo waliofika ni 152 ambapo ni ya awamu ya pili kwa Kanda ya Mashariki Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara awamu ya kwanza yalifanyika kwenye mikoa ya Songwe, Njombe, Rukwa na Katavi na timu nyingine ikifanya kwenye mikoa ya Singida, Tabora na Shinyanga.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo Jane Mwanamtwa ofisa Mtendaji kata ya Kawawa wilaya ya Kibaha amesema yana umuhimu kwa sababu wanakumbushwa wajibu wao pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo kukamilika kwa wakati pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wananchi wanaowahudumia.



Friday, November 17, 2023

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA NYERERE YAADHIMISHA SIKU YA WATOTO NJITI DUNIANI YATOA MISAADA





KATIKA kuadhimisha siku ya watoto waliozaliwa kabla ya muda (Watoto Njiti) Duniani Tasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na baadhi ya wadau imetoa misaada kwa watoto njiti kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzila.

Aidha imetoa misaada kwenye sekta ya elimu ili kuboresha mazingira ya usomaji na vifaa kwa wanafunzi wa baadhi ya shule Wilayani Kibaha.

Misaada hiyo ambayo ni saruji, sabuni, mafuta ya watoto na mavazi ya michezo vimetolewa leo  mbali ya Hospitali ya Mloganzila ni pamoja na Shule ya Msingi Kambarage na Mlandizi.

Katibu wa Taasisi hiyo ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani Omary Punzi amesema kuwa wamefikia hatua hiyo ili kuendelea kutimiza malengo ya Taasisi hiyo ambayo ni mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na uamsikini.

Punzi amesema kuwa mbali na hilo pia hatua hiyo inalenga kuikumbusha jamii ili kutambua kuwa bado tatizo la watoto njiti lipo na linaendelea kuwaandama wajawazito wengi hivyo ni vema likapewa kipaumbele na kuongeza nguvu katika kukabiliana nalo.

Amesema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza malengo yake kwa kujiweka karibu na jamii ambapo katika msaada huo imeshirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki wanathamini wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi huduma za tiba wa Hospital ya Mloganzila Dk Faraja Chiwanga amesema kuwa sababu mbalimbali zinatajwa kuchangia hali hiyo ni pamoja na magonjwa yasiyoambukiza na ukosefu wa lishe bora.

Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Kambarage Happynes Tesha amesema kuwa msaaada wa mifuko 50 ya saruji iliyotolewa na taasisi hiyo itaongeza nguvu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea shuleni hapo.

Monday, November 13, 2023

KAMATI YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA YARIDHISHWA MRADI WA MAJI WAMI AWAMU YA TATU.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imetembelea mradi wa Maji wa Wami awamu ya tatu kwenye chanzo Mto Wami na kufurahishwa na jitihada za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha huduma ya upatikanaji maji inakuwa ya uhakika.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Deus Sangu wakati wa ziara iliyofanywa kutembelea mradi huo kuangalia maendeleo ya mradi huo ambao kwa awamu zote umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 160.

Sangu amesema kuwa wameridhishwa na jitihada za Dawasa na kuahidi kuendelea kuipambania ili iweze kukabili changamoto za upungufu wa maji na kupitia Bunge kati ya maazimio 14 mawili ni ya kuisaidia mamlaka hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa upatikanaji wa maji kwa mkoa huo ni asilimia 86 ambapo aliomba miradi itekelezwe vizuri ikizingatiwa ni mkoa wa uwekezaji wa viwanda na mahitaji ya maji kwa sasa ni makubwa kwani kuna ongezeko la watu na uwekezaji mkubwa ambapo bila ya maji hakuna uwekezaji.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ameishukuru kamati hiyo kwa kupambani Chalinze kupata maji kwani kwenye mikutano yake hakuna jambo ambalo lilikuwa kero kwa wananchi kuhitaji maji ambapo kwa sasa changamoto ya maji imepungua kwa kiasi kikubwa.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo wa awamu ya tatu Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Kiula Kingu amesema kuwa maji yatazalishwa kutoka lita milioni saba hadi lita milioni 21 ambapo mabomba yatatandazwa kwa kilometa 124 na matenki 18 na kutakuwa na vituo vikubwa vya maji Miono, Msoga na Mboga.


Mwisho.

Monday, November 6, 2023

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KULIPA KODI KWA HIYARI

WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kulipa kodi kwa hiyari ili wawe huru kufanyabiashara na kuchangia mapato ya serikali ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Taifa Hamis Livembe alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Wilaya ya Kibaha wakati wa ziara yake kutembelea Mkoa wa Pwani.

Livembe alisema kuwa kila upande una wajibu kwa mwenzake ambapo serikali inaweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na kwa wafanyabiashara kazi yao ni kulipa kodi.

"Naombeni wafanyabiashara mlipe kodi kwa hiyari kwani serikali imeweka mazingira mazuri ya sisi kufanya biashara na hata kama kuna changamoto imeacha milango wazi kwa ajili ya majadiliano kama kuna kero kuhusiana na kodi,"alisema Livembe.

Alisema kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameamua kufungua milango ya biashara ili wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa uhuru na hataki kuona wanabughudhiwa.

"Tumuunge mkono jitihada za Rais anazo zifanya kwa wafanyabiashara kwa kutatua kero zetu hivyo tukilipa kodi vizuri nchi itasonga mbele kwenye suala la maendeleo na nchi itafunguka,"alisema Livembe.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta alisema kuwa Jumuiya hiyo inafanya kazi kubwa ya kizalendo kwani nchi inapokusanya vizuri mapato yanarudi kwa wananchi kwa kutoa huduma kwa ufanisi.

Mchatta alisema kuwa wajibu wa kulipa kodi ni muhimu na kama kuna changamoto watashirikiana na wafanyabiashara kuzitatua kwa pamoja ili mazingira ya biashara yawe rafiki.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka alisema kuwa wanaishukuru serikali kwa kutatua baadhi ya changamoto za wafanyabiashara.

Ndauka alisema kuwa changamoto zao zikitatuliwa watafanyabiashara kwa uhuru na kuwezesha biashara kukua hivyo kulipa kodi kwa hiyari na kuleta maendeleo ya nchi.

Moja ya wafanyabiashara ambaye ni mwanachama wa Jumuiya hiyo Mkoani humo Hassan Msemo alisema kuwa moja ya changamoto wanazozipata ni baadhi ya viwanda kutokuwa na stoo za kuuzia bidhaa wanazozizalisha ambapo nyingi ziko Jijini Dar es Salaam hivyo kuwagharimu kuzifuata.

Msemo alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo husababisha kuzifuata Jijini Dar es Salaam hivyo gharama kuwa kubwa na hata bei za kuuzia nazo zinakuwa juu.

Friday, November 3, 2023

MAGONJWA YAONGEZEKA MWINGILIANO WA BINADAMU WANYAMA NA MAZINGIRA

 

DODOMA.

SHUGHULI za kijamii na kiuchumi, mwenendo na mifumo ya maisha na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayoibuka kutokana na mwingiliano uliopo baina ya binadamu, wanyama na mazingira.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Jenista Mhagama , wakati akifungua kongamano la kitaifa la Afya Moja ambapo amesema kuwa duniani kote takriban visa bilioni 1 vya ugonjwa na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Aidha amezisihi Wizara za Kisekta kuwa na mipango ya kutekeleza na kuimarisha ushirikiano wa kisekta kwa kutumia mbinu ya Afya Moja na kila sekta kushiriki kikamilifu katika tafiti kuhusu magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, utunzaji wa mazingira, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, usalama wa chakula na lishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Nao baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wamesema kuwa dhana ya Afya moja faida yake ni njia inayowaleta pamoja na sekta mbalimbali ambapo ni afya, mifugo na wanyamapori ili kukabiliana na changamoto zinazohusiana na afya.

Kila ifikapo Novemba 3 ya kila mwaka wadau mbalimbali huadhimisha siku ya Afya Moja kwa lengo la kuimarisha uratibu na utendaji uliopo baina ya sekta katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na majanga ya milipuko ya magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea ambapo kauli mbiu mwaka huu inasema “Afya Moja: Mbinu ya Pamoja kuboresha afya ya binadamu, wanyama, mimea na mfumo wa ikolojia kwa ustahimilivu wa maafa.

SHUGHULI ZA KIJAMII NA KIUCHUMI ZACHANGIA ONGEZEKO LA MAGONJWA

 

DODOMA.

IMEELEZWA kuwa shughuli za kijamii na kiuchumi, mwenendo na mifumo ya maisha na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayoibuka kutokana na mwingiliano uliopo baina ya binadamu, wanyama na mazingira.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Jenista Mhagama , wakati akifungua kongamano la kitaifa la Afya Moja ambapo amesema kuwa duniani kote takriban visa bilioni 1 vya ugonjwa na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Aidha amezisihi Wizara za Kisekta kuwa na mipango ya kutekeleza na kuimarisha ushirikiano wa kisekta kwa kutumia mbinu ya Afya Moja na kila sekta kushiriki kikamilifu katika tafiti kuhusu magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, utunzaji wa mazingira, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, usalama wa chakula na lishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Nao baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wamesema kuwa dhana ya Afya moja faida yake ni njia inayowaleta pamoja na sekta mbalimbali ambapo ni afya, mifugo na wanyamapori ili kukabiliana na changamoto zinazohusiana na afya.

Kila ifikapo Novemba 3 ya kila mwaka wadau mbalimbali huadhimisha siku ya Afya Moja kwa lengo la kuimarisha uratibu na utendaji uliopo baina ya sekta katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na majanga ya milipuko ya magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea ambapo kauli mbiu mwaka huu inasema “Afya Moja: Mbinu ya Pamoja kuboresha afya ya binadamu, wanyama, mimea na mfumo wa ikolojia kwa ustahimilivu wa maafa.