Wednesday, August 9, 2023

MAOFISA UGANI WATAKIWA KWENDA VIJIJINI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bahi na Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa Mhe. Donard Megitii amewataka maafisa ugani kwenda vijijini kutoa elimu juu ya ufugaji bora na wenye tija kwa ajili ya manufaa ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Megitii ametoa rai hiyo Jijini Dodoma katika ufunguzi wa kongamano la kuku Katika viwanja vya maonesho ya nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.

Amesema vijijini bado kuna shida ya wataalam na maafisa hao hawatembelei Wafugaji hivyo kama Mkoa jambo hilo walipe uzito wasiishie kwenye kongamano kwamba watu wameonesha nia njema na ndio maana wanakuja wapate elimu, ujuzi na kuwaunganisha na maafisa ugani kwa maana ya Mifugo, Kilimo kwenda vijijini kuwatembelea Wafugaji na kuwapa elimu.

“Wafugaji wa kuku wanapaswa kuongeza uzalishaji wenye tija Dodoma ili kujivunia uwepo wa makao makuu na nawaomba wataalam nendeni mkawape elimu bora ya kufuga washiriki waliofika na kwamaana wana nia njema ya kutaka kutambua mbinu za ufugaji bora ili waweze kupata tija nakuongeza mitaji pamoja na uchumi wao,”amesema.

Aidha, amewataka wafugaji kuzingatia ulishaji na utunzaji wa chakula cha mifugo pamoja na kuzingatia kanuni za magonjwa.

“Tunashindwa kufuga kwa tija kwasababu hatuzingatii kanuni za kiafya kwa maana ya ufugaji bora kwahiyo tukizingatia kuchanja kuku yaani kuwapatia kinga ili wasipate maradhi ya kuambukiza halafu ukawapa maji ya kutosha nina uhakika tutabadilisha maisha na kuuza kuku kila siku.” amesema.

Akifanya majumuisho baada ya kuzunguka katika baadhi ya mabanda amesema amefurahi kuona kikundi cha vijana wanufaika wa Mikoa ya vijana ya 4% ilivyoweza kubadilisha maisha ya vijana watano na kuajiri vijana wengine watano.

“Hii inaonesha kuwa mafanikio kwa vijana ni makubwa na utayari wa vijana kujifunza ni mkubwa hivyo kinachobaki kwetu Viongozi ni kuhamasisha wananchi kukubali na kuanza kutumi bidhaa zetu,”amesema.

WIZARA YATAMBUA MCHANGO WA WAFUGAJI KWENYE MAENDELEO YA TAIFA

Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema dhamira ya maonyesho ya wanyama wafugwao ni kutambua mchango na juhudi za wafugaji katika kuchangia maendeleo ya Taifa na mtu mmoja mmoja.

Silinde amesema hayo katika viwanja vya Ranchi ya Taifa vilivyopo katika maonyesho ya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi rasmi wa maonyesho ya Mifugo ambayo maonyesho hayo huambatana na mashindano ya kushindanisha na kumpata mfugaji aliyefuga kwa tija na mafanikio katika Mifugo yake.

“Mashindano haya hufanyika katika nchi mbalimbali yakiwa na lengo la kutambua mchango na juhudi za wafugaji katika kuchangia maendeleo ya Taifa na mtu binafsi na huongeza ari kwa wananchi kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia”,amesema Silinde.

Aidha Mhe. Silinde amesema kuwa kuendelea kufanyika kwa maonesho na mashindano hayo kunachangia na kuhamasisha kuendeleza ufugaji bora nchini.

“Wizara inaangalia namna ya kufanya maonesho haya kuwa na Taswira na hadhi ya Kitaifa kama ilivyokusudiwa na wafugaji wa walioshinda katika Kanda mbalimbali watakuja Dodoma kushindana hapa Kitaifa hivyo Wizara itaendelea kuboresha tuzo na zawadi kwa washindi ili kuwapa hamasa zaidi”, amedokeza Mhe. Silinde.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amesema Mkoa wake unashika nafasi ya tano Kitaifa kwa kuwa na Mifugo Mingi hivyo hawana budi kuimarisha juhudi za kukuza uchumi wa wananchi wa Mkoa huo ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoyumbisha uzalishaji wenye tija.

“Kwa mujibu wa sensa ya kilimo ya mwaka 2021 mkoa wa Dodoma unashika nafasi ya 5 kwa wingi wa ng’ombe ukikadiriwa kuwa na ng’ombe 2,195,576, mbuzi 1,663,483 na wanyama wengine wafugwao hivyo juhudi zozote za kuimarisha uchumi wa wananchi wa Mkoa huu ni kipaumbele chetu, hatuna budi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazosababisha tija ndogo katika uzalishaji wa mazao na Mifugo”,amesema Senyamule.

Maonyesho hayo ya wanyama yanafanyika kwa mara ya 12 tangu kuanzishwa kwake hufanyika katika Kanda mbalimbali na baadae hutamatishwa kwa kunganishwa Kanda zote na mshindi hupatikana akiwa ndiye mshindi wa Taifa na hupatiwa zawadi na motisha kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi.

SERIKALI KUONGEZA UZALISHAJI ZAO LA ALIZETI

Serikali inalenga kuinua uzalishaji wa zao la alizeti na kukuza kipato cha wakulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa Agosti 3, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe.Suleiman Mwenda wakati wa Kongamano na Mafunzo ya wakulima wa zao la alizeti kwenye maonyesho ya nanenane Kanda ya kati katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.

Kongamano hilo limelenga kuunga mkono na kutekeleza kwa vitendo Juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuinua na kuthamini mchango wa Kilimo katika Taifa letu. Mafunzo hayo amebebwa na kauli mbiu inayosema ”alizeti kwa afya bora na kipato.

”Tumeshuhudia Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe inayotilia mkazo wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya alizeti ili kupunguza uingizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi na hivyo kupunguza matumizi ya bidhaa za kigeni. Jitihada hizo ni pamoja na kutoa ruzuku za mbegu bora na alizeti na vitendea kazi kwa maafisa ugani “ameeleza Mwenda.

Hata hivyo, Mhe. Mwenda ametoa wito kwa wadau wa kilimo kupeana uzoefu kuhusu mafanikio, changamoto na mkakati ya kuongeza tija ya uzalishaji na masoko ya zao la alizeti kwani sekta ya kilimo na mifugo inachangia uchumi wa nchi kwa zaidi ya asilimia 75 na kwa wananchi wa Dodoma na Singida huku alizeti ikiwa ni zao kuu la biashara katika Mkoa hiyo miwili .

Mhe. Mwenda amezitaja moja ya sababu zinazokabili mnyororo mzima wa zao la alizeti na hivyo kulazimu kuendelea na uingizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kuwataka wadau kutumia Kongamano hilo kuweka mikakati ya kuzipatia ufumbuzi, ambazo ni kiwango kidogo cha uzalishaji, mabadiliko ya tabia ya nchi na masoko ya alizeti yasiyo kuwa na mfumo rasmi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema amewataka wakulima wa Mikoa ya Singida na Dodoma kutumia fursa hiyo waliyoipata kufanya kilimo cha tija na kuacha kilimo cha mazoea kutokana na mafunzo waliyo yapata kuhakikisha wanafanya kwa vitendo kama ilivyo dhamira ya Serikali.

DC ATAKA MADIWANI WATUNGE SHERIA RAFIKI KWA WAWEKEZAJI

MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amewataka madiwani kutunga sheria ndogo ambazo zitaboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na wawekezaji badala ya kuweka mazingira ambayo yatakuwa kikwazo katika ukusanyaji wa mapato.

John aliyasema hayo mjini Kibaha kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Hmashauri ya Mji Kibaha na kuwa wanapaswa kuweka mazingira rafiki badala ya kuwa kero.

Alisema kuwa sheria ndogo ndogo wanazotunga ziwavutie wafanyabiashara na wawekezaji siyo ziwe kero na kusababisha kuwakatisha tamaa badala yake ziwe vichocheo vya watu kufanya uwekezaji.

"Zisiwe kikwazo kuwakwamisha wafanyabiashara na wawekezaji na zisiwaongezee gharama bali ziwe zinzoendana na mpango wa taifa wa wa uboreshaji biashara,"alisema John.

Aidha alisema kuwa gharama za tozo mbalimbali za Halmashauri ziendane na mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha mapato yanapatikana. 

"Mmapaswa kuwa wabunifu katika utendaji kwa kubuni mambo mbalimbali ambayo yataweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwani mazingira yakiwa mazuri yatawavutia na watashiriki katika kukuza uchumi wa nchi,"alisema John.

Aliongeza kuwa wanapaswa kuhasaisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili itoe matokeo kwani ucheleweshaji hauwezi kuonyesha matokeo ya haraka kwa walengwa.

Tuesday, August 8, 2023

KATIBU WA TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYAERERE MKOA WA PWANI ATEMBELEA BANDA LA HIFADHI ZA TAIFA

 



 KATIBU wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa Pwani Ndugu Omary Punzi ametembelea Banda la Hifadhi za Taifa katika Maonyesho ya sikukuu ya wakulima nane nane 8.Agosti 2023 yaliyofanyika mkoani Morogoro Kanda ya Mashariki yakijumuisha mikoa mitatu Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Punzi amesema kitu cha Kujivunia ni kuonana kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mwasisi wa Taifa letu la Tanzania Kutolewa katika idara ya Makumbusho na Kuwekwa katika idara ya Maliasili ya Hifadhi na hii Ndiyo heshima kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chiini ya Uongozi wa Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Kilio hiki Hakika kimesikika Tangu Tarehe 14.5.2022 katika kongamano la Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere Katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete DODOMA Mgeni Rasmi alikuwa Mheshimiwa Kasimu Majaliwa Waziri Mkuu wa Tanzania akiwakilishwa na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda Waziri Mkuu Mstaafu.

Monday, August 7, 2023

BILIONI 157.5 ZATUMIKA UNUNUZI BIDHAA ZA AFYA

 

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa fedha kwa Bohari ya Dawa Tanzania ambapo kiasi cha shilingi bilioni 157.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya ikijumuisha Dawa,  Vifaa Tiba na vitendanishi vya Maabara.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania Hassan Ibrahim ambaye ni Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini amesema hayo leo Agost, 7, 2023 Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari alielezea utekelezaji wa majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD) na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/24.

Ibrahim amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 Bohari imeanza kusambaza Dawa kwa mizunguko mara sita kwa mwaka kutoka Mara nne kwa mwaka huku Akisema serikali imetoa ahadi ya kuipatia MSD mtaji ili kumaliza changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo.

Katika kufanikisha ongezeko la uzalishaji wa bidhaa za afya nchini na kuendana na azma ya Serikali ya uanzishaji wa viwanda, MSD ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miundombinu ya kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi mkoani Njombe na kuanza uzalishaji ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/24. 

Amesema katika mwaka huu wa fedha wa 2023/24, MSD inatarajia Kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuboresho matumizi ya takwimu za maoteo, kuhakikisha bidhaa zote za afya zinakuwa na mikataba ya muda mrefu na kuimarisha ushirikiano na wazalishaji wa ndani kwa kutoa fursa kwa wazalishaji wa ndani na kununua kutoka kwa wazalishaji wa nje pale inapobidi.

Kwa upande wake Michael Bajile Meneja Maoteo Ametoa wito kwa watoa huduma za Afya kuwa makini katika takwimu wanazozikusanya kwani Bohari ya Dawa huzalisha kufuata takwimu hizo.

CWT KIBAHA WATAKA MABORESHO KIKOKOTOO

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani kimeomba kanuni ya kikokotoo kuangaliwa upya au kirudishwe cha zamani ambacho kilikuwa ni asilimia 50 badala ya cha sasa ambacho ni asilimia 33.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa chama hicho Mwita Magige alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Magige amesema kuwa kanuni ya kugawa kikokotoo cha sasa iangaliwe upya ambapo mafao wanayoyapata baada ya kustaafu ni madogo tofauti na yale ya awali.

Amesema kuwa kanuni hiyo iangaliwe upya kwa kuboreshwa na ikiwezekana kirudishwe kikokotoo cha zamani ambacho ni kizuri kuliko cha sasa.

Aidha amesema kuwa kuboreshwa kikokotoo kutawafanya walimu wawe na morali ya kazi kwani watakuwa wanafuraha na malipo hayo mara baada ya kustaafu.