Saturday, February 4, 2023

RAIS DK SAMIA APONGEZWA MIRADI YA MAENDELEO



RAIS APONGEZWA KUHAMASISHA MAENDELEO KUINUA UCHUMI.                

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM NEC) Taifa Hamoud Jumaa amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuhamasisha maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.

Jumaa aliaysema hayo alipowaongoza wana CCM na wananchi kuadhimisha miaka 46 ya CCM Kibaha Vijijini na kuwa Tanzania ilipofikia kwa kipindi hicho kuna mengi ya kujivunia.

Alisema kuwa wumuunge mkono Rais na kuacha maneno kwani sekta zote zikiwemo afya, elimu kujengwa, vikundi vya ujasiliamali na machinga wanawezeshwa mikopo na miradi mikubwa ya kimkakati haijasimama ikiwa ni pamoja na reli ya mwendo Kasi SGR, Bandari kavu ya Kwala, Daraja la kisasa la Wami.

Jumaa aliwataka wana CCM kuwa wamoja kuimarisha ushirikiano ili kuiletea ushindi CCM uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 pia aliweka jiwe la msingi ujenzi wa ofisi ya kata Mtongani ambao ulianza tangu mwaka 2017 kwa njia ya kujitolea ambapo amechangia 500,000 na rafiki yake 500,000 kwa ajili ya ujenzi huo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini Mkali Kanusu alieleza kuwa Rais Samia apewe ushirikiano na kuyaeleza yale aliyoyatekeleza nchini na alisisitiza kwa wana CCM kuwa na umoja na mshikamano na pasipo kutengana ili chama kiweze kusonga mbele.

Katibu wa CCM Kibaha Vijijini Safina Nchimbi alieleza kuwa maadhimisho hayo yameambatana na tukio la kuchangia damu kupanda miti kufanya usafi kituo cha afya Mlandizi na zahanati

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mtongani Gloria Kirei alisema ujenzi huo mbali ya wanaCCM kujitolea pia wabunge viti maalum Hawa Mchafu ,Subira Mgalu, wilaya na Mwenyekiti wa UWT mkoa Zainabu Vullu nao walichangia vifaa mbalimbali.


Friday, February 3, 2023

MIAKA 46 CCM JUMUIYA YA WAZAZI BAGAMOYO YAPANDA MITI SHULENI

WAKAZI wa Chalinze wilayani Bagamoyo wametakiwa kupanda miti ili kutunza mazingira kuzuia upepo wa mara kwa mara unaoezua mapaa katika majengo yao.

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji wa miti katika shule ya msingi Bwilingu Kata ya Bwilingu Chalinze Mwenyekiti wa Wazazi wilaya ya Bagamoyo Aboubakary Mlawa alisema kuwa wananchi wanapaswa kuwa na utamaduni wa kupanda miti mara kwa mara na si kusubiri wakati wa sherehe ama ugeni.

Mlawa alisema kuwa kwa eneo la chalinze eneo kubwa lipo wazi kwa kutokuwa na miti kutoka na ujenzi hivyo ni muhimu sasa kila mkazi awe na utamaduni wa kupanda miti.

"Kumekuwa na matukio mengi ya upepo kuezua mapaa katika majengo ya watu binafsi sambamba na majengo ya taasisi zikiwemo shule dawa pekee kuzuia hali hii ni kupanda miti kwa wingi,"alisema Mlawa.

Alisema kuwa kama kila mtu akipanda mti mmoja katika maeneo yanayomzunguka ana hakika mazingira ya majengo yao yatakuwa na usalama.

"Wao kama Jumuiya ya Wazazi jukumu mojawapo walilopewa na Chma cha Mapinduzi ambalo pia katika dhumuni la kuwepo kwa jumuiya hiyo ni utunzaji wa nazingira hivyo ni muhimu kusimamia na kuhakikisha upandaji wa miti unakuwa endelevu,"alisema Mlawa.

Aidha alisema anaomba upandaji wa miti usiwe wakati wa ujio wa wageni ama wakati wa sherehe,zoezi la upandaji miti liwe la kila siku.

Awali Diwani wa kata ya Bwilingu Nasser Karama alisema kama Diwani alihakikisha kuwa maeneo mbalimbali ya Taasisi yanapata huduma ya maji kwa kuchimba visima vya kisasa. 

Karama alisema kuwepo kwa visima hivyo kutachochea utunzaji wa miti hiyo na uboreshaji wa mazingira.

Jumuiya wa Wazazi wilaya ya Bagamoyo katika kusherekea miaka 46 ya kuzaliwa kwake ilifanya shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji misaada mbalimbali, upandaji miti na uchangiaji wa damu. 


MTAA WA BAMBA KUJENGA SEKONDARI

MTAA wa Bamba Kata ya Kongowe Wilayani Kibaha imesafisha eneo kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari kwa wanafunzi wanaotoka Mtaa huo ambapo hutembea umbali wa kilometa 16 kwenda Shule ya Sekondari Mwambisi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi huo Mwenyekiti wa Mtaa huo Majid Kavuta amesema kuwa tayari wana vifaa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo kwa awali madarasa manne.

Kavuta ametaja vifaa hivyo kuwa ni tofali 3,600, saruji mifuko 50, mchanga lori tatu, kokoto lori mbili na wanatafuta mdau ili awapatie nondo ambapo kila kaya inatakiwa kutoa tofali 10.

"Kutokana na wanafunzi hao kusoma mbali kunasababisha utoro na wanafunzi wa kike kurubuniwa na kujiingiza kwenye mapenzi na wale wa kiume kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na uvutaji wa bhangi,"amesema Kavuta.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kongowe Simon Mbelea amesema ujenzi huo ni kutekeleza ilani ya chama kuhakikisha watoto wanapata elimu kwenye mazingira rafiki.

Mbelwa amesema pia ni kuunga mkono jitihada za Rais DK Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta ya elimu ambapo ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu nchini.

RC ATAKA WANAOSUBIRIA MABADILIKO KUCHAPA KAZI



MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewataka Wakurugenzi na viongozi ambao nafasi zao zinatokana na uteuzi wa Rais kutofanya kazi zao kwa hofu ya kutochaguliwa kwani hiyo ni mipango ya Mungu.

Kunenge aliyasema hayo Mjini Kibaha alipokuwa akiwaapisha wakuu wapya wa Wilaya na kuwakaribisha waleo waliohamishiwa vituo vyao vya kazi na kuja kwenye mkoa huo.

Alisema kuwa hakuna sababu kwa viongozi hao kutofanya kazi kwa ufanisi kuhofia uteuzi kwani hiyo itasababisha shughuli za maendeleo kutofanyika kikamilifu.

"Wakurugenzi na wale ambao nafasi zao bado hazijafanyiwa mabadiliko na Rais fanyeni kazi mambo mengine mwachieni Mungu mbona mimi nafanya kazi zangu kama taratibu zilivyo mengine tumuachie Mungu yeye ndiye anayejua,"alisema Kunenge.

Aidha alisema kuwa kuchaguliwa hiyo ni mipango ya Mungu hivyo kila mtu afanye kazi kwa mujibu wa sheria msihofie uteuzi kwani kazi za mtu ndiye zitakazomfanya achaguliwe tena.

"Yawezekana unaangaliwa hivyo ukifanya kazi chini ya kiwango unaweza ukajiharibia ni vema ukaendekea kuwajibika bila kujali mbele kutakuwa na nini kwani hayo ni majaaliwa,"alisema Kunenge.

Aliwataka viongozi hao ambao nafasi zao zinatokana na uteuzi wa Rais kutatua changamoto za wananchi kwani ndiyo wajibu wao na wamewekwa hapo kutokana na uwezo wao.

"NIKI WA PILI" AKABIDHIWA KIJITI NA SARA MSAFIRI KUONGOZA WILAYA YA KIBAHA BAADA YA MABADILIKO YA WAKUU WA WILAYA.

MKUU mpya wa Wilaya ya Kibaha Nickson John ambaye amehamishiwa hapa kutoka Wilaya ya Kisarawe amesema kuwa ili kufikia ndoto za Rais DK Samia Suluhu Hassan na matarajio ya wananchi ni kujenga timu ya pamoja.

John aliyasema hayo alipokuwa akikaribishwa Wilayani hapo na viongozi na watendaji wa taasisi na wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Mji Kibaha na kumuaga aliyekuwa mkuu wa Wilaya hiyo Sara Msafiri.

Alisema kuwa wananchi wana matarajio makubwa ya kupata maendeleo kutoka kwa viongozi hivyo anachohitaji ni ushirikiano ili kuwa na timu itakayofanya kazi kwa pamoja.

"Ndoto yangu ni kuhakikisha tunashirikiana na Rais ili ndoto za kuleta maendeleo zitimie kwa ushirikiano wetu sisi tukiwa ni viongozi,"alisema John.

Aidha alisema kuwa wananchi wanamatumaini makubwa makubwa na viongozi hivyo watazingatia vipaumbele vya Rais na vya wananchi ili kuleta maendeleo.

"Ili tufanye kazi vizuri napenda uwazi na utu ambacho ni kitu kikubwa pamoja na nidhamu na uwajibikaji haya yatatusaidia katika kufikia malengo tuliyojiwekea,"alisema John.

Kwa upande wake mkuu wa zamani wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri aliwashukuru viongozi na watendaji wa Wilaya hiyo kwa ushirikiano waliompa alipokuwa hapo na kuwatakia heri wanaoendelea na utumishi kushirikiana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala alisema kuwa watahakikisha wanashirikiana na Mkuu wa Wilaya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Makala alisema kuwa kwa kushirikiana na Mkuu huyo wa Wilaya wanaamini watakuwa na ushirikiano kufikia ndoto za wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba alisema kuwa watamapa ushirikiano mkuu mpya wa Wilaya ili kuwatumikia wananchi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alisema kuwa watashirikiana naye ili kufikia pale wanapopataka.


WAKAMATWA NA SILAHA MMOJA ATUHUMIWA MAUAJI

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia mtu mmoja mwanaume (53) ambaye jina limehifadhiwa mkulima mkazi wa Kijiji cha Ruvu Stesheni Wilaya ya Kibaha akiwa na silaha aina ya Shortgun Greener yenye namba za usajli 729 na maganda sita ya Risasi za Shortgun na unga wa baruti.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa kukutwa na silaha hiyo.

Lutumo alisema kuwa mtuhumiwa huyo alishafanya tukio la mauaji huko Kisarawe na kutorokea katika kijiji cha Ruvu Stesheni Wilaya ya Kibaha.

"Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika na kuwataka watu waache kutumia silaha hizo kinyume cha sheria,"alisema Lutumo.

Katika tukio lingine ambalo lilitokea mnamo Januari 8 mwaka huu majira ya saa 06:45 mchana huko maeneo ya Msanga Sokoni Kata ya Msanga, Tarafa ya Maneromango Wilaya ya Kisarawe mtu mmoja mwanaume (47) ambaye jina lake limehifadhiwa mfanyabiashara mkazi wa Msanga Sokoni alikamatwa kwa kukutwa na Bunduki aina ya Riffle yenye namba za usajili zilizofutika.

Lutumo alisema kuwa mtuhumiwa huyo hakuwa na vibali vya umiliki wa silaha hiyo ambapo ilikamatwa wakati Polisi wakiwa kwenye misako ambayo imefanyika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Aidha alisema kuwa pia risasi sita zilikamatwa baada ya kufanya misako katika wilaya za mkoa huo kwa lengo la kudhibiti makosa ya uvunjaji, unyang’anyi wa kutumia nguvu, wizi, wizi wa mifugo, utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na matumizi ya pombe harammu ya moshi (gongo).

"Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani limefanya misako na operesheni mbalimbali kuanzia tarehe 1 Januari hadi tarehe  31 Januari mwaka huu ambapo Jumla ya watuhumiwa 19 wanaume wamekamatwa,"alisema Lutumo.

Aliongeza kuwa katika misako hiyo walifanikiwa kukamata pikipiki mbili za aina tofauti, Televisheni Spika, deki, feni na meza ya Tv vyote kimoja kimoja
Viti 13 waya ya Fensi rola tatu, Gongo (Pombe ya Moshi) lita 140 na Bhangi gunia 12, Puli 57 na kete 157.

"Upelelzi wa matukio haya bado unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa hawa wote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowahusu,"alisema Lutumo.

Alibainisha kuwa Jeshi la Polisi linaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zozote zinazo husiana na uhalifu na wahalifu kwa wakati kwa kuwatumia wakaguzi kata waliopo kwenye maeneo yao yote ndani ya Mkoa wa Pwani nao watazifanyia kazi kwa wakati na haraka.


Thursday, February 2, 2023

WATAKIWA KUPIMA VIWANJA VIWANJA


MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ametoa mwezi mmoja kwa wananchi wa mitaa ya Lumumba na Mkombozi Kata ya Pangani Wilayani Kibaha kupima viwanja vyao ambavyo serikali ilitoa baada ya kuvamia eneo lililokuwa la Kituo cha Mitamba Kibaha.

Aidha amewataka wananchi waliovamia sehemu ya Shamba hilo kuondoka kwani wako hapo kinyume cha sheria kwani eneo hilo lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa ajili ya kuliendeleza.

Kunenge aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa mitaa hiyo kutatua migogoro ya ardhi baada ya wananchi wa mitaa hiyo kugomea zoezi upimaji ardhi wakitaka warasimishiwe eneo ambalo walipewa baada ya kulivamia.

Alisema mtu anayerasimishiwa ni yule ambaye anamiliki ardhi kihalali lakini wao walipewa tu hivyo wanapaswa kupimiwa kwa gharama ya mita za mraba shilingi kwa shilingi 1,5000.

"Natoa mwezi mmoja kwa wananchi wote kwenye mitaa hiyo kupima ardhi yao ili wamiliki kihalali na malipo yalipunguzwa kutoka 2,500 hadi 1,500 kwa mita za mraba baada ya wengi kulalamika kuwa hawana uwezo,"alisema Kunenge.

Alibainisha kuwa eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na iliyokuwa Wizara ya Kilimo na Mifugo wakati huo ambapo watu walilivamia na Wizara ilibidi ilimege na kuwaachia wananchi sehemu mwaka 2012.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alisema kuwa walitoa matangazo ya wananchi kupima viwanja lakini mwitikio ukawa ni mdogo.

Munde alisema kuwa kutokana na hali ya ugumu wa kupima maeneo hayo wakitaka wayarasimishe hivyo kwa mwezi huo mmoja wanaamini watu watajitokeza kupima maeneo yao 

Shamba hilo la Mitamba lilianzishwa mwaka 1982 na 1983 na Wizara ya Kilimo na Mifugo wakati huo kwa lengo la kutoa mafunzo na uzalishaji wa ngombe bora Mitamba lilikuwa na ukubwa wa hekari 4,000 ambapo ilitoa fidia milioni 20 kwa wananchi waliokuwa wakikaa kwenye eneo hilo wapatao 1,557.