Tuesday, July 26, 2016

JAKAYA AKARIBISHWA KISHUJAA BAGAMOYO

Na John Gagarini, Bagamoyo

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne Dk Jakaya Kikwete amesema kuwa hakuna kitu kilichokuwa kikimpa wakati mgumu kama kushindwa katika uongozi wake wa miaka 10 iliyopita.

Aliyasema hayo juzi mjini Bagamoyo wakati wa sherehe iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA) ya kumkaribisha nyumbani baada ya kukabidhi uongozi kwa mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli mjini Dodoma hivi karibuni.

Dk Kikwete alisema kuwa hali ya kushindwa ilikuwa ikimpa wakati mgumu na kujiona kuwa kama endapo angeshindwa basi ange waangusha Wanabagamoyo na Pwani nzima.

“Kila nilipokuwa nikifikiria kushindwa kwenye jambo lolote la uongozi wangu kwa nchi au kwenye Chama lakini namshukuru Mungu kwani tulifanikiwa sana katika suala la maendeleo kwa nchi nzima kwani huwezi ukapendelea sehemu uliyotoka au ukawanyima maendeleo ni kitu ambacho hakiwezekani,” alisema Dk Kikwete.

Alisema kuwa wakati fulani alikuwa akilalamikiwa na baadhi ya wabunge kuwa anapendelea Bagamoyo jambo ambalo si la kweli ambapo walidai kuwa amehamisha fedha za ujenzi wa barabara na kuzihamishia kwenye ujenzi wa barabara ya Msata Bagamoyo.

“Hali kama hiyo Ilikuwa inanipa wakati mgumu kwnai kila sehemu inataka maendeleo na nisingeweza kutofanya maendeleo kwa watu wa Bagamoyo kwani hata wao wanahitaji maendeleo kama sehemu nyingine,” alisema Dk Kikwete.

Aidha alisema kuna wakati ilibidi ahamishe fedha kutoka Bagamoyo na kufanya ujenzi kwenye maeneo ya Geita-Sengerema hadi Usagara wakati huo waziri wa Ujenzi alikuwa Basil Mramba lakini hawakuliona lakini anasema alishukuru Mungu kwani ujenzi kwenye barabara hizo ulifanyika vizuri.

“Namshukuru Mungu katika uongozi wangu tulifanya kazi na kuleta maendeleo makubwa na tumeiacha nchi mahali pazuri na salama kwnai imetulia licha ya mwaka 2015 wakati wa uchaguzi ambapo baadhi ya watu walisema kuwa Rais gani hata hafanyi mpango wa kubadilisha katiba ili aendelee kukaa madarakani kwani watu walishindana lakini hawakupigana wala kumwaga damu na uchaguzi ulipokwisha maisha yaliendelea salama kabisa,” alisema Dk Kikwete.

Alibainisha kuwa Watanzania wanapaswa kumuombea Rais Dk John Magufuli ili aweze kuleta maendeleo kwani ni mpenda maendeleo hivyo lazima asaidiwe aweze kuleta maendeleo ya watu.

Akizungumzia kuhusu Chama alisema kuwa kiko vizuri na hakuna kinachoiweza CCM kwani anajua hakuna chama cha kuweza kukishinda kwani havina uwezo ikizingatiwa ni chama kikubwa na viongozi wake ni imara.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Maskuzi alisema kuwa katika uongozi wake alifanikiwa kuleta maendeleo makubwa kuanzia kwenye elimu na mpango wa shule za kata sasa umeonyesha mafanikio ambapo shule hizo kwa mwaka huu zimeongoza kwenye matokeo.

Maskuzi alisema kuwa umeme ni moja ya mafanikio ambapo kwa sasa umefika hadi vijijini kupitia mpango wa Umeme Vijijini REA, ujenzi wa barabara na masuala mengine ya kimaendeleo kwenye nchi ambayo ni ya kujivunia.

Katika sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na familia ya Dk Kikwete alipewa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mifugo kama vile ngombe, mbuzi, kuku, bata, mavazi ya jadi na vitu mbalimbali ambavyo vilitolewa na wananchi wa mkoa wa Pwani.


Mwisho.

BAGAMOYO YAGUNDUA WTUMISHI HEWA ZAIDI 83 WAGUNDULIKA

 Na John Gagarini, Bagamoyo

WILAYA ya Bagamoyo mkoani Pwani imebaini uwepo wa watumishi hewa 83 na kuifanya wilaya hiyo kwa sasa kuwa na watumishi hewa 91 ambapo wakati zoezi hilo linaanza lilibaini watumishi hewa nane tu.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuzindua madawati 300 yaliyotengenezwa na wadau mbalimbali na kuzinduliwa na mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema kuwa watumishi hao wamebainika baada ya kuundwa kikosi kazi kuchunguza watumishi hao.

Mwanga alisema kuwa awali baada ya agizo lililotolewa na Rais Dk John Magufuli kulibainika watumishi hewa nane lakini sasa idadi hiyo imeongezeka baada ya kufanywa kwa kina.

Alisema kuwa kikosi kazi kilichoundwa na watu sita wanaoundwa na kamati ya ulinzi na usalama na kugundua watumishi hewa wengi ni kutoka idara ya elimu hasa kwenye shule za msingi na sekondari.

“Watumishi wengi ni walimu ambao wengi wamekwenda masomoni bila ya kuaga na hawana ruhusa na baadhi walishaacha kazi lakini cha kushingaza mishahara yao ilikuwa inaingizwa kama kawaida jambo ambalo ni kinyume cha taratibu,” alisema Mwanga.

Aidha alisema kuwa tatizo kubwa linaonyesha ni idara ya elimu kushindwa kutoa maamuzi ya haraka mara walimu wanapoomba kwenda masomoni hivyo huamua kuondoka kienyeji.

“Watumishi wengine walibainika kuwa hawana vielelezo vyo vyote vya vya juu ya ajira zao na tunaomba hatua kali zichukuliwe kwa watumishi hao ambao ni hewa na wamekuwa wakilipwa mishahara huku hawafanyi kazi wanachukua mishahara ya bure,” alisema Mwanga.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kutokana na kubainika watumishi hao 83 hewa wilayani Bagamoyo kwa sasa mkoa wamefikia watumishi hewa 272.

Ndikilo alisema kuwa zoezi hilo bado linaendelea na kukipongeza kikosi kazi cha wilaya hiyo kuweza kuwabaini watumishi hao hewa na itaendelea kuchunguza hadi kuondoa kabisa suala hilo.


Mwisho.

Tuesday, July 5, 2016

WAFUGAJI WATAKA WASIONDOLEWE CHAURU

Na John Gagarini,Bagamoyo

WAFUGAJI wanaoishi kwenye Kitongoji cha Msigala Kijiji cha Visezi kata ya Ruvu wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamepinga kupelekwa Kitongoji cha Mnanyama kutokana na kutokuwa na huduma za kijamii.

Wakizungumza na waandishi wa habari Kijijini hapo wamesema kuwa eneo walilopangiwa halina huduma hizo ndiyo sababu ya wao kuendelea kukaa hapo walipo sasa.

Akizungumzia juu ya hali hiyo Lupina Kirayo alisema kuwa chanzo cha wao kutakiwa kuondoka ni kutokana na madai ya wakulima wa shamba la Chama Cha Ushirika wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) kuwa ngombe wao wamekuwa wakiingia kwenye mashamba na kuharibu mazao.

Kirayo alisema kuwa wao wako hapo kwa muda mrefu lakini wanashangaa kutakiwa kuondoka na kwenda Mnanyama ambako hakuna huduma hyoyote ya Kijamii.

“Zamani kijiji hicho kiliweka njia kwa ajili ya ngombe kupita kwenda kunywa maji mtoni lakini wakulima walifunga njia ya kupita ngombe na ndiyo chanzo cha migogoro ya wakulima na wafugaji ilipoanza,” alisema Kirayo.

Alisema kuwa tatizo kubwa linatokana na baadhi ya wafugaji wanaoleta mifugo toka maeneo ya mbali kwa ajili ya kwenda kuuza ngombe kwenye mnada wa Ruvu ndiyo wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye shamba hilo la ushirika wakitafuta maji.

Aidha alisema kuwa wao kama wenyeji wa Kitongoji hicho wako makini na mifugo yao ambapo wakati mwingine wachungaji wao wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti ngombe na kuingia kwenye shamba hilo ambapo wamekuwa wakiwafukuza wachungaji wazembe ili kuondoa migongano na kuomba radhi na kutaka kuwe na maridhiano na kuangalia njia nzuri ya kudhibiti mifugo isiingie kwenye shamba hilo lakini siyo kuwaondoa hapo.

Naye Elizabeth Meja amesema kuwa yeye alizaliwa hapo na kipindi cha nyuma wamekuwa wakiishi vizuri lakini kwa sasa wanaambiwa waondoke ambako kule huduma ya afya hakuna ambapo kwa akinamama hasa pale wanapokuwa wajawazito huhitaji kupata huduma za mara kwa mara.

Meja alisema kuwa sehemu wanayotaka kuhamishiwa kuna umbali wa km 20 hadi kufika kwenye huduma za afya na hata watoto wanapozaliwa hupaswa kupelekwa kliniki lakini kutokana na umbali huo itakuwa ni matatizo pia watoto wao kwa sasa licha ya kutumia masaa zaidi ya mawili kwenda shule ni karibu tofauti na wakienda kule hatapata fursa ya kusoma kutokana na umbali huo.

“Hata suala la maji ni tatizo kwani hapa tunatumia maji ya shilingi 20,000 kwa siku lakini kule tunakotakiwa twende maji hakuna kabisa hivyo ni vema wakaweka miundombinu kwanza ili huduma kama hizo zipatikane,” alisema Meja.

Naye mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Msigala Otiniel Mbura alisema kuwa tayari serikali iliamua wafugaji hao kwenda huko ili kuondoa migogoro inayojitokeza kila wakati.

Mbura alisema kuwa ni vema wafugaji hao wakenda kwanza na serikali itawapelekea huduma kuliko hivi sasa wanavyokataa kwenda huko walikopangiwa.


CHAURU YAWATAKA WAFUGAJI KUONDOA NGOMBE KWENYE SHAMBA LAO

Na John Gagarini, Bagamoyo

UONGOZI Chama Cha Ushirika wa Wakulima wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) wamewataka wafugaji walioko kwenye shamba hilo kuhamisha mifugo yao ambayo imekuwa ikifanya uharibifu wa mazao pamoja na miundombinu ya umwagiliaji.

Akizungumza kwenye kikao cha wakulima na wafugaji waliopo kwenye shamba hilo ambalo liko kwenye kitongoji cha Msigala Kijiji cha Visezi kata ya Ruvu wilayani Bagamoyo mwenyekiti wa chama hicho Sadala Chacha amesema kuwa uharibifu uliofanywa ni mkubwa sana.

Chacha amesema kuwa kutokana na baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye shamba hilo la umwagiliaji la mpunga kumewasababishia hasara kubwa wanachama wake na uharibifu wa miundombinu.

Amesema kuwa serikali ilishawatengea eneo lao liitwalo Mnyanama lakini hawataki kwenda wakidai kuwa hakuna huduma za kijamii jambo ambalo limewafanya waendelee kukaa hapo na huku mifugo hiyo hasa ngombe wakiendelea kufanya uharibu wa miundombinu na kula mazao ya wakulima.

Aidha amesema kuwa wamekuwa wakikaa vikao vya mara kwa mara ili kujaribu kuangalia utaratibu wa namna ya kufuga na wao kulima lakini wao wamekuwa wakilishia mifugo kwenye mashamba hayo ya wakulima na kusababisha ugomvi mara kwa mara.

Ameongeza kuwa wamechoshwa na vitendo hivyo vya wafugaji vya kuingiza ngombe kwenye shamba hilo huku sheria aikikataza mifugo kuingia kwenye eneo hilo lakini utekelezaji wa suala hilo umekuwa mgumu kwani mifugo bado inaingizwa shambani hapo.

Kwa upande wake mmoja wa wafugaji Lupina Kirayo amesema kuwa tatizo kubwa linatokana na baadhi ya wafugaji wanaoleta mifugo toka maeneo ya mbali kwa ajili ya kwenda kuuza ngombe kwenye mnada wa Ruvu ndiyo wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye shamba hilo la ushirika wakitafuta maji.

Lupina amesema kuwa wao kama wenyeji wa Kitongoji hicho wako makini na mifugo yao ambapo wakati mwingine wachungaji wao wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti ngombe na kuingia kwenye shamba hilo ambapo wamekuwa wakiwafukuza wachungaji wazembe ili kuondoa migongano na kuomba radhi na kutaka kuwe na maridhiano na kuangalia njia nzuri ya kudhibiti mifugo isiingie kwenye shamba hilo lakini siyo kuwaondoa hapo.

Naye mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Msigala Otiniel Mbura amekiri kutokea changamoto ya ngombe kuingizwa kwenye shamba hilo na kusema kuwa ili kuondoa tatizo hilo ni wafugaji hao kuondoa mifugo hiyo na kuipeleka kule walikopangiwa.

Mbura amesema kuwa wafugaji hao hawataki kwenda huko kwa madai kuwa hakuna huduma za kijamii kama zahanati, shule na malambo ya maji kwa ajili ya mifugo yao hali ambayo imefanya ugomvi kwenye shamba hilo kutokwisha kwa muda mrefu sasa.

Shamba hilo la umwagiliaji mpunga lilianzishwa miaka ya 60 na lina wanachama wapatao 894 na lina ukubwa wa hekta 3,209 huku za makazi zikiwa hekta 720 ambapo baada ya mavuno ya mpunga wanachama hulima mazao mengine kama vile mahindi,ufuta na mtama pamoja na kilimo cha mbogamboga.

Mwisho.


WATENDAJI WATAKAOSHINDWA KUKAMILISHA ZOEZI LA UPATIKANAJI MADAWATI KUJIFUKUZISHA KAZI

Na John Gagarini, Kibaha

MKUU mpya wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Asumter Mshama ametoa siku 24 kwa watendaji wa kata na maofisa tarafa kuhakikisha wanakamilisha zoezi la upatikanaji wa madawati na atakayeshindwa kukamilisha zoezi hilo kwenye sehemu yake atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Mshama ametoa agizo hilo mjini Kibaha kwenye mkutano alioundaa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na watendaji hao na baadhi ya wakuu wa Idara za Elimu, Ardhi na Mazingira na kusema kuwa watendaji hao wanapaswa kukamilisha zoezi hilo ifikapo Julai 29 mwaka huu.

Amesema kuwa agizo la Rais Dk John Magufuli ilikuwa ni Juni 30 mwaka huu hivyo hakuna sababu ya watedaji hao kushindwa kutekeleza agizo hilo kwani muda uliotolewa ulishapita.

Aidha amesema kuwa Baadhi ya watendaji wamefanikiwa kukamilisha zoezi nawapongeza lakini wengine wameshindwa kukamilisha hivyo anatoa muda hadi Julai 29 wawe wamekamilisha na atakayeshindwa atakuwa kajifukuzisha kazi mwenyewe kwa kushindwa kuwajibika.

Akielezea juu ya uwezekano wa kukamilisha hilo amesema kuwa yeye kule alikotoka wilaya ya Wangingombe mkoani Njombe alipambana na kufanikiwa kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa ambapo madawati yalipatikana na kuwa na ziada ya madawati 2,000 hivyo hata Kibaha hakuna sababu ya kushindwa kufanya hivyo kwani hakuna jambo ambalo linashindikana.

Amesisitiza kuwa Maagizo waliyopewa wao wakuu wa wilaya na Rais ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini kwani haiwezekani nyumbani watoto wakae kwenye makochi au sofa lakini wakifika shule wanakaa chini lazima watendaji hao wahamasishe wananchi kuchangia miundombinu ya elimu.

Mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha amesema kuwa watendaji hao wanapaswa kuwahamasisha wananchi kuchangia unpatikanaji wa madawati hakuna haja ya kusema kuwa eti watu wagumu kuchangia.

Amesisitiza kuwa Kama mtendaji ameshindwa kukamilisha zoei hilo ni kwamba ameshindwa kazi kwani sheria zipo na wanapaswa kuzitumia ili kufanikisha zoezi hilo la upatikaaji wa madawati.

Naye mtendaji wa kata ya Kongowe Said Kayangu alikiri kuwa baadhi ya maeneo zoezi hilo limeshindwa kufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali.

Kayangu amesema kuwa watahakikisha muda uliosalia wanakamilisha zoezi hilo na kusema kuwa watajipanga vizuri ili kufanikisha zoezi hilo ili kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli ili kila mtoto aweze kukaa kwenye dawati.

mwisho.



Saturday, July 2, 2016

johngagariniblog: WAKUU WA WILAYA WAPYA WAAPISHWA PWANI

johngagariniblog: WAKUU WA WILAYA WAPYA WAAPISHWA PWANI: Na John Gagarini, Kibaha   MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakuu wapya wa wilaya wlioteuliwa na Rais Dk John...

Friday, July 1, 2016

WAKUU WA WILAYA WAPYA WAAPISHWA PWANI


Na John Gagarini, Kibaha

 

MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakuu wapya wa wilaya wlioteuliwa na Rais Dk John Magufuli mkoani humo kuinua pato la wananchi wa mkoa huo kutoka milioni 1.2 kwa mwaka hadi milioni 3 kwa mwaka.

 

Aliyasema hayo jana mjini Kibaha wakati akiwaapisha wakuu hao wa wilaya wapya na kusema kuwa pato la mwananchi wa mkoa wa Pwani liko chini sana licha ya kuwa na fursa mbalimbali za kipato.

 

Ndikilo alisema kuwa kutoakana na pato hilo la wananchi kuwa dogo kiasi hicho hata mchango wa mkoa kwa Pato la Taifa ni dogo sana la asilimia 1.8 jambo ambalo linapaswa kuwekewa mkakati wa kupandisha pato hilo ili liwe na mchango mkubwa kwa mwananchi na Taifa kwa ujumla.

 

“Nawapongezeni kwa kuchaguliwa kwenye nafasi hizi na mkoa tayari umeandaa mpango kazi wake kwa ajili ya kuinua pato la mwananchi hivyo mnapaswa kuweka vipaumbele ambavyo vitasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya unayoongoza,” alisema Ndikilo.

 

Alisema kuwa hakuna sababu ya mkoa kuendelea kuwa na pato dogo huku kukiwa na vyanzo vingi vya mapato ikiwa ni pamoja na rasilimali mbalimbali kama vile uvuvi, kilimo, korosho, maliasili ikiwa ni pamoja na mbuga za wanyama na madini mbalimbali.

 

“Mfano ni majumba mengi yanayojengwa Dar es Salaam kokoto na mawe yanatoka mkoa wa Pwani hivyo hakuna sababu ya kuwa maskini tuna zao la korosho ambapo kwa msimu uliopita wakulima waliuza korosho zenye tahamani ya shilingi bilioni 18,” alisema Ndikilo.

 

Aliwataka wahakikisha wanawajibika na kutowalea watumishi ambao ni kikwazo na wenye urasimu wa kuwahudumia wananchi ambao hufika ngazi ya mkoa kulalamika ili hali ngazi za chini kuna watendaji ambao wangeweza kutatua matatizo hayo.

 

“Changamoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na suala la ulinzi na usalama, wahamiaji haramu, matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi nisingependa mambo haya yatokee tena hakikisheni mnatimiza wajibu wenu na kuwaondolea kero wananchi,” alisema Ndikilo.

 

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema kuwa moja ya changamoto ambazo atakabiliana nazo ni pamoja na wahamiaji haramu kw akudhibiti bandari 19 ambazo zimekuwa ni njia ya wahamiaji hao haramu.

 

Naye Asumpter Mshama alisema kuwa moja ya mambo atayapaa kipaumbele ni kuhakikisha fedha kwa makundi ya vijana na akinamama asilimia 10 zinatoka ili wananchi waweze kujenga uchumi wao na ule wa Taifa.

 

Wakuu wapya walioapishwa jana ni pamoja na Shaibu Nunduma wilaya ya Mafia, Filberto Sanga Mkuranga, Gulamu Kifu wilaya ya Kibiti, Asumpter Mshama wilaya ya Kibaha, Juma Njwayo wilaya ya Rufiji na Majid Mwanga wilaya ya Bagamoyo huku Happyness William hakuweza kuapishwa kutokana na dharura.

 

Mwisho.


 MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kushoto akimkabidhi zana za kufanyia kazi mkuu wa wilaya ya Kibiti Gulamu Kifu, baada ya kumwapisha kwenye hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu huyo wa mkoa

Mkuu mpya wa wilaya ya Kibaha Asumpter Mshama kulia akiapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kushoto wakati wa hafla iliyofanyika mjini Kibaha ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za mkoa huo ambao waliteuliwa hivi karibuni na Rais Dk John Magufuli

Mkuu mpya wa wilaya Rufiji Juma Njwayo kulia akiapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakati wakiapishwa wakuu wa wilaya za mkoa huo kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa huo.