Saturday, February 13, 2016

WAATHIRIKA WA MAFURIKO WAPATIWA MAHINDI YA MSAADA

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA)  imeupatia mkoa wa pwani tani 1,283 za mahindi kwa ajili ya wahanga wa mafuriko wilayani Rufiji.
Mahindi hayo yatasagwa kwa ajili ya kuwapatia unga bure  wananchi 53,446 kwenye tarafa za Mkongo,Ikwiriri na muhoro wilayani humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini kibaha mkuu wa mkoa wa pwani injinia evarist ndikilo alisema kuwa mahindi hayo yaliwasili juzi wilayani humo.
"Tunatarajia mahindi hayo yatawawasaidia waathirika hao, kisha yatasagwa na wananchi walioathirika watapewa bure," alisema ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa tayari magari ya kubeba mahindi hayo kutoka halmashauri yameshachukua mahindi hayo ya msaada kwa kipindi cha mwezi Februari na Machi
" Pia tumeteua wafanyabiashara sita ambao watanunua mahindi kwa wakala hao kisha kuyauza kwa bei ndogo ili kila mwananchi amudu kununua," alisema ndikilo.
Aidha alisema mkakati uliopo kwa sasa wa kiwasaidia wananchi hao ni kuhamasisha wafanyabiashara kupeleka bidhaa kama Michele,unga na maharage, kufanya tathmini ya mafuriko, kuhamasisha kulima mazao ya muda mfupi Mtama, viazi, kunde na muhogo.
"Hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya kifo kilichotokana na mafuriko hayo ambayo yameathiri watu ambao wanalima kandokando ya Mto rufiji ambapo Daraja la mto muhoro limefunikwa na maji," alisema ndikilo.
Aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa misaada ya kiutu kwa waathirika wa mafuriko hayo yaliyoathiri hekta 8,133 za mpunga na hekta 7,171 za Mahindi.
Chanzo cha mafuriko hayo yalianza kuingia kijiji cha mloka tarehe 31 januari hadi februari 6 ambapo maji hayo yametokea mto rufiji unaopokea maji ya mvua kutoka mikoa Iringa, Mbeya na Morogoro.
Mwisho.

RC AWAPA MWEZI MAWAKALA MWEZI MMOJA KUWASILISHA MAPATO WANAYODAIWA NA HALMASHAURI

Na John Gagarini, Kibaha
MAWAKALA wote wanaokusanya mapato ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wametakiwa walipe makusanyo yao yote wanayodaiwa na Halmashauri ndani ya mwezi mmoja.
Agizo hilo lilitolewa jana na mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakati akifungua baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo nakusema kuwa ucheleweshaji wa fedha hizo unasababisha Halmashauri kushindwa kufanya mipango yake ya maendeleo.
Alisema kuwa baadhi ya mawakala wamekuwa wakichelewesha makusanyo na tozo mbalimbali wanazozitoza toka kwa wananchi kwa niaba ya Halamashauri hivyo wanapaswa kupeleka malipo hayo kwa wakati.
“Moja ya hoja ambazo zimekuwa zikiwasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ni kushindwa kukusanya mapato ya ndani ya mawakala kwa wakati na kukosa mikakati ya kuongeza mapato ya Halmashauri,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa suala lingine ni mikataba inayoingiwa inakuwa si mizuri na inatoa mwanya kwa wakala kuacha kuwasilisha mapato bila ya kuchukuliwa sheria kutokana na kuchelesha mapato hayo.
“Pia nashauri madiwani wajiepushe na kuomba zabuni mbalimbali katika Halamashauri ili kuepuka migongano ya kimaslahi na muweze kuisimamia vizuri kwani endapo mtakuwa na maslahi hamtaweza kuisimamia hivyo kushindwa kuleta maendeleo,” alisema Ndikilo.
Aliwataka Madiwani kusimamia fedha za makusanyo ya ndani zianarudi kwa wananchi kwa kugaramia huduma mbalimbali na miradi ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri Leonard Mlowe alisema kuwa watendaji wa halmashauri wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuwa waadilifu ili kufanikisha maendeleo kwa wananchi yanapatikana.
Mlowe amewataka watendaji hao kuwasimamia mawakala ili wahakikishe wanawasilisha fedha za makusanyo mbalimbali zinafika kwa wakati ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Mwisho.    

Monday, February 8, 2016

WATU 53,000 WAKUMBWA NA MAFURIKO PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
WATU 53,446 wilayani Rufiji mkoani Pwani wamekumbwa  na mafuriko hali iliyowafanya wazungukwe na maji na kuhitaji msaada kufuatia mvua za Vuli zinazoendelea hapa nchini.
Aidha tayari boti mbili za uokozi tayari zimepelekwa kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kuwaondoa watu hao waliozungukwa na maji na kuwapeleka sehemu salama.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu toka kwenye eneo la tukio, Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa maji hayo ambayo yametoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkoa wa Morogoro.
“Vijiji vingi wilayani humo vimezingirwa na maji na watu wengi waliokumbwa na kadhia hiyo ni wale waliohamia mashambani kwa ajili ya kilimo na kukutwa na maji hayo pamoja na nyumba ambazo ziko mabondeni,” alisema Ndikilo.  
Alisema kuwa mvua hizo ambazo zilizoanza kidogo kidogo tangu Januari 31 mwaka huu zimeathiri zaidi kwenye maeneo ya kata za Mwaseni, Tarafa ya Mkongo, Tarafa ya Ikwiriri na kata ya Muhoro.
“Kutokana na athari za mvua hizo hekta zaidi ya 7,000 za Mahindi na hekta zaidi ya 8,000 za Mpunga  zimesombwa na maji na tayari mkoa umewasiliana na Waziri Mkuu kwenye kitengo cha Wakala wa mazao kuomba msaada wa chakula tani 1,280 za mahindi,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa wameteua wafanyabiashara sita kwa ajili ya kununua mahindi na kuyasaga kwa ajili ya chakula ikiwa ni njia ya kuwasaidia wananchi pia kukabili mfumuko wa bei ambao unaweza kujitokeza kutokana na hali hiyo.
Katika hatua nyingine mkoa umeomba tani 10 za mbegu za mahindi na tani tano za mbegu za Mtama kwa ajili ya kupanda kukabiliana na athari ya mazao ambayo yamesombwa na maji ya mvua za Vuli ambazo wiki ijayo zitaanza mvua za Masika.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imeombwa kuipatia Idara ya Ziamamoto mkoani Pwani vifaa kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya moto na kuokoa watu wanaokumbwa na majanga mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto mkoani Pwani Goodluck Zelote alisema kuwa kutokana na uhaba wa vifaa baadhi ya wilaya hazina vituo vya zimamoto.
Zelote alisema kuwa kwenye mkoa wa Pwani kati ya wilaya sita ni wilaya tatu tu za Kibaha, Bagamoyo na Mafia ndiyo zenye vikosi hivyo huku wilaya za Kisarawe, Rufiji na Mkuranga zikiwa hazina huduma hiyo.
“Ingependeza angalau kila wilaya kuwa japo na kikosi cha Zimamoto na uokoaji japo hakitaweza kutoa huduma kwenye eneo lote lakini angalau zingesaidia ambapo kwa sasa utendaji kazi unakuwa mgumu,” alisema Zelote.
Alisema kuwa vifaa hivyo ni magari pamoja na vifaa vya uokoaji ambapo alitoa mfano wa ajali ya moto ambayo ilitokea hivi karibuni Chalinze walifika na kunusuru nyumba yote kuteketea kwa moto lakini kutokana na umbali uliopo walinusuru vyumba kadhaa.
“Kwa sasa tunachokifanya ni kutoa elimu zaidi ya kujikinga na kuzuia moto kwa kutumia vifaa vya kuzimia moto ambavyo kila mtu anapaswa kuwa navyo kuanzia kwenye maeneo ya huduma hadi majumbani,” alisema Zelote.
Aidha alisema kuwa moja ya changamoto wanayoipata ni ujenzi holela ambao hauzingatii mipango miji hali ambayo inasababisha magari ya kuzimia moto kushindwa kufika kwenye nyumba ambazo zinawaka moto na kuwataka watu wazingatie kanuni za ujenzi.
Mwisho.  



Sunday, February 7, 2016

WANANCHI WATAKIWA KUTOWAHIFADHI WAGENI

Na John Gagarini, Kibaha
IDARA ya Uhamiaji Mkoani Pwani imewataka  wananchi kutokubali kukaa na wageni ambao si raia Watanzania kwani ni kinyume cha taratibu na endapo watabainika watachukulia hatua za kisheria kwa kuwatunza wageni.
Hayo yalisemwa na Naibu Kamishna wa Idara hiyo Grace Hokororo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisni kwake mjini Kibaha na kusema kuwa kuna watu wanaishi na wageni jambo ambalo ni kosa kisheria.
Hokororo alisema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiishi na wageni majumbani mwao wengine wakiwa wamewapangisha, wamewaajiri au kuwapangisha kwenye nyumba zao kama Raia wa Tanzania bila ya kufuata taratibu.
“Mgeni yoyote anapoingia nchini anapaswa kufuata taratibu na lazima serikali au idara hivyo watu wanaokaa nao au kufanya nao shughuli yoyote bila ya kufuata taratuibu za nchi ni kosa na endapo wanagundua kuwa siyo raia wanapaswa kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe kwa mhamiaji haramu,” alisema Hokororo.
Alisema kuwa changamoto inayowakabili ni uchache wa watumishi hali ambayo inawafanya washindwe kuwadhibiti wahamiaji haramu hao ambao wamekuwa wakileta athari nyingi kwa raia  endapo atakaa kinyemela bila ya kufuata taratibu.
“Kuna athari mbalimbali zinazotokana na Raia wa nje kuishi bila ya kibali ikiwa ni pamoja na kunyakua rasilimali kama vile mashamba na vitu vingine lakini akiishi kwa kufuata taratibu kuna namna ya kupewa rasilimali bila ya kumwathiri mwenyeji,” alisema Hokororo.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine ni mkoa kutawanyika na njia za kuingilia ni nyingi kwa kupitia kwenye Bahari ambako hakuna vyombo vya kufanya doria kwenye bandari ambazo nyingine ni bubu ambazo zinatumika kama milango ya kuingilia.

Mwisho.

Monday, February 1, 2016

UWAMAMI WATAKA SULUHU NA HALMASHAURI KISARAWE

Na John Gagarini, Kisarawe

UMOJA wa Wafanyabiashara wa Mazao ya Misitu Wilayani Kisarawe mkoani Pwani (UWAMAMI) wameomba suluhu na Halmashauri ya Wilaya ili waache mgomo wa kufanya biashara hiyo kwa kurejeshewa fedha zao za faini ambazo walitozwa kimakosa.

Wafanyabiashara hao walisema kuwa wataachana na mgomo huo endapo Halmashauri hiyo hiyo itawarudishia fedha zao kiasi cha zaidi ya shilingi milioni nne ambazo wafanyabiashara hao walipigwa kinyume cha taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa umoja huo Mohamed Dikata alisema kuwa mgomo huo utaendelea hadi pale Halmashauri itakapowarejeshea fedha zao kwani hali hiyo imeathiri biashara zao hasa ikizingatiwa walikiri kuwa walifanya makosa katika upigaji fani huo kwa wafanyabiashara ambao walizidisha mzigo wa mazao ya misitu walipokuwa wakiitoa mashambani.

“Sisi tunatoa huduma kwa wananchi hivyo tunaomba Halmashauri warudishe fedha hizo ambazo ni sehemu ya mitaji yetu na tumejaribu kukaa mara kadhaa bila ya kufikia muafaka kwani wao wanataka kutulipa kidogo kidogo fedha zetu jambo ambalo hatujaliafiki tulipigwa faini ambapo wengine walipigwa faini na kufikia zaidi ya milioni moja na kutoa fedha taslimu kwani nini  wao warejeshe kwa mafungu kwani sehemu ya fedha tulizotoa ni za biashara hivyo kuyumbishwa katika shughuli zetu za kibiashara," alisema Dikata.

Aidha alisema kuwa wanataka watumishi wa Halmashauri waliohusika waondolewe kwani wamekiuka taratibu za kazi zao kwa kuwalipisha faini zisizostahili kwani si mara yao ya kwanza hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Walitupiga faini ya shilingi 16,000 kwa kila gunia badala ya shilingi 1,600 kwa gunia ambalo linakuwa limezidi na sisi hatukatai kulipa faini ambayo ni halali tunachopinga ni kuzidishiwa mara 10 zaidi ya faini halali,” alisema Dikata.

Jitihada za kumpata mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe hazikufanikiwa kwani alikuwa nje ya ofisi kikazi ambapo kaimu wake naye hakupatikana hata hivyo ofisa Mipango wa Patrick Alute alikiri kuwa na tatizo hilo na kusema kuwa mazungumzo yanaendelea baina ya wafanyabiashara hao.

Alute alisema kuwa Halmashauri inaendelea na mazungumzo ili kufikia muafaka, umoja huo hujihusisha na biashara ya uuzaji wa mkaa pamoja na kuni ambapo gunia moja hulipiwa kiasi cha shilingi 20,000 kama ushuru wa Halmashauri.

Mwisho.    

Wednesday, January 20, 2016

MAMA NA WATOTO WAKE WAWILI WAFA KWA RADI WATATU WAJERUHIWA

Na John Gagarini, Pwani
MVUA zinazoendelea kunyesha hapa nchini zimeendelea kuleta madhara baada ya Mama na watoto wake wawili kufa huku watu wengine watatu wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu ofisa mtendaji wa kata ya Mchukwi wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Ami Lipundundu alisema kuwa familia hiyo ilikuwa ikiota moto baada ya kuchota maji ya mvua.
Lipundundu alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 18 mwaka huu majira ya saa 11 jioni kwenye Kijiji cha Mchukwi B walipokuwa wanaota moto baada ya mvua kunyesha.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Decilia Simba (42) watoto wake Debora Simba (4) na Amani Matimbwa 1 na nusu huku waliojeruhiwa wakiwa ni Maua Ngwande (13) anayesoma darasa la sita shule ya Msingi Mchukwi, Suzana Daudi (12) na mdogo wa marahemu aitwaye Mama Tariq.
“Marehemu alitoka kwenye kikundi cha kuweka na kukopa cha Jitegemee ambapo yeye ni mwanachama alipofika nyumbani mvua ikaanza kunyesha akawa anakinga maji ya mvua yeye na watoto wa ndugu yake,” alisema Lipundundu.
Alisema kuwa baada ya hapo waliwasha moto kwenye jiko lao ambalo liko jirani na mti wa Mfenesi na kuota kwani walikuwa wameloa ndipo radi ilipopiga ikakwepa mti ikawapiga wao.
“Marehemu na wanawe walifia njiani wakati wakipelekwa Hospitali ya Mchukwi kwa ajili ya matibabu ambapo majeruhi bado wamelaazwa hopsitalini hapo na hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Lipundundu.
Aidha alisema kuwa wiki iliyopita mtu mmoja naye alifariki kwa kupigwa na radi na mwishoni mwa mwaka jana huko Ikwiriri mtu mmoja pia alifariki dunia. Polisi mkoa wa Pwani walithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha.
Mwisho.

Monday, January 18, 2016

NDC YAPEWA MIEZI MITATU

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imelipa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) miezi mitatu kuhakikisha linapata kiasi cha dola za Kimarekani Milioni 2.1 kwa ajili ya kiwanda cha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mmbu wanaoeneza Ugonjwa wa Malaria Tanzania Biotech Product Ltd kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Aidha alishangazwa na shirika hilo kwa kuajiri wafanyakazi 143 Julai mwaka 2015 ambao wanalipwa mishahara pasipo kuzalisha kitu chochote kwani wanapokea mishahara ya bure jambo ambalo alisema kuwa halipendezi.
Agizo hilo limetolewa jana mjini Kibaha na katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dk Adelhelm Meru alipotembelea kiwanda hicho ambacho kilizinduliwa Julai 2015 na Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Ethiopia.
Dk Meru alitoa agizo hilo kutokana na kutoridhishwa na maombi ya NDC kuomba kiasi hicho serikalini kutoka kwa Godwill Wanga Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika hilo kwa lengo la kufanya majaribio pamoja na kuanza uzalishaji.
“Serikali haiwezi kutoa kiasi hicho cha fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya huduma za jamii hivyo fanyeni kila njia kwa kukopa kwa kufanya nini ombeni hata benki ya uwekezaji nchini TIB ili mhakikishe mnapata fedha hizo na majaribio yanaanza ili uzalishaji uanze tumechelewa kwa kipindi cha miaka minne,” alisema Dk Meru.
Alisema kuwa inatosha kwani serikali ililipa gharama zote za ujenzi wa kiwanda hicho dola milioni 22 na kilitakiwa kianze kazi tangu mwaka 2012 ikasogezwa hadi Julai 2015 lakini hadi sasa ni miezi sita imepita lakini uzalishaji bado.
“hatuwezi kuwa kioja tafuteni fedha hizo dola milioni 1 kwa ajili ya majaribio na dola milioni 1.2 kwa ajili ya mtaji kwani malengo ya serikali ilikuwa na lengo kiwanda kianze kazi kwa muda uliopangwa ili kiweze kukabiliana na ugonjwa wa Malaria na ziada ya dawa kuuzwa nje ya nchi hivyo kuweza kufikia malengo yaliyowekwa,” alisema Dk Meru.
“Nataka ifikapo Mei Mosi mwaka huu mimi nije na Waziri wangu ili tuone uzalishaji unaanza mara moja kwani moja ya sera za nchi hasa katika awamu hii ya tano ni kujenga uchumi kupitia viwanda na kuwa nchi yenye uchumi wa kati ili kuleta maendeleo ya wananchi pia iko kwenye dira ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano,” alisema Dk Meru.
Awali akielezea juu ya maendeleo ya kiwanda hicho Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NDC Wanga alisema kuwa baadhi ya vifaa kwenye mashine ziliathiriwa na umeme kutokana na na kukatika katika hali ambayo ilisababisha uzalishaji ushindwe kuanza.
Wanga alisema kuwa kutokana na ucheleweshaji huo wa kuanza kufanya kazi ilibidi wataalamu kutoka nchi ya Cuba inakotoka teknolojia hiyo Labio Farm kudai gharama zaidi za ujenzi hivyo kudai fidia.
“Kiwanda hichi kinahitaji msaada hata kwa mkopo kiasi cha dola milioni 2.1 ili kuweza kukamilisha hatua zilizobakia kwani wataalamu wetu wameishiwa mtaji baada ya muda kuongezeka na kutokana na matatizo ya kuharibika vifaa vya mashine za kiwanda hichi,” alisema Wanga.
Alisema kuwa teknolojia hiyo ni mpya na mara uzalishaji utakapoanza itasaidia kukabiliana na ugonjwa wa Malaria kwani dawa hiyo ina uwezo wa kuua mazalia ya mbu na baadaye kitakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa nyingine ikiwa ni pamoja na mbolea na madawa mbalimbali.
Mwisho.