Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo amewataka wadau wa
mchezo wa bao kuwafundisha vijana ili kuendeleza mchezo huo ambao ulipendwa na
wapigania uhuru wa nchi akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Alitoa rai hiyo mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na
viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Kibaha Mjini wakati wa juma la jumuiya hiyo
lililoadhimishwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo mchezo wa bao uliodhaminiwa na
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ili kumuenzi Baba wa Taifa
aliyekuwa akiupenda mchezo huo.
Ndikilo alisema kuwa kwa sasa mchezo huo unachezwa zaidi na
wazee kuliko vijana hivyo kuna umuhimu wa kuwafundisha vijana ili waupende
mchezo huo na kuuendeleza.
“Tunampongeza mbunge kudhamini mashindano ya bao ambayo yalishirikisha
timu kutoka mitaa yote ya kata 11 za Kibaha Mjini na kuwashirikisha wazee huku
vijana wakiwa ni wachache,”alisema Ndikilo.
Alisema kuwa ili kumujenzi Baba wa Taifa wadau mbalimbali wa
mchezo huo wanapaswa kuwaweke mazingira mazuri ya kushiriki mchezo huo ambao ni
maarufu kwa wakazi wa mikoa ya Pwani.
Kwa upande wake Koka alisema kuwa lengo la kudhamini
mashindano ni kuuhamasisha mchezo huo ili usipotee na kuwafanya wazee nao
wapate kushiriki michezo.
Koka alisema kuwa ataendelea kuhamasisha mchezo huo hasa kwa
vijana ili uweze kupendwa na kuwavutia wengi kuliko kungangania baadhi ya
michezo kwani hata huo una nafasi yake.
Katika mashindano hayo timu ya Kata ya maili Moja ilifanikiwa
kuwa bingwa na kujinyakulia kiasi cha shilingi 300,000 huku kata ya Kibaha
wakijinyakulia 200,000 na kata za Mkuza, Mbwawa, Misugusugu, Tumbi, Visiga,
Pangani, Kongowe na Picha ya Ndege zilijinyakulia 100,000 kila moja kwa
ushiriki wao.
Aidha mashindano ya kukuna nazi wanawake Zuhura Rashid
alijinyakulia 70,000, akifuatiwa na Sara Alfred aliyejipatia 50,000 huku Zuhura
Ally akipata 30,000 huku washiriki wengine wakijinyakulia 20,000 kila mmoja kwa
ushiriki wao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani amemwomba mkuu
wa mkoa wa Pwani kuzihimiza Halmashauri kuwawezesha wajasiriamali wanawake na
vijana kupata asilimia 10 ya mikopo kwa ajili yao.
Aliyasema hayo mjini Kibaha mbele ya mkuu wa mkoa huo Evarist
Ndikilo alipokuwa akiongea na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Mji wa Kibaha
wakati wa maadhimisho ya juma la Wazazi.
Koka alisema kuwa upatikanaji wa fedha hizo toka halmashauri
ni changamoto kwa makundi hayo hali inayowafanya walalamike kutopatiwa fedha
hizo ambazo zimetengwa kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali.
“Mkuu wa mkoa naomba usaidie uwaandikie barua wakurugenzi wa
Halmashauri za wilaya za mkoa huu kuhakikisha zinawapatia fedha hizo makundi ya
akinamama na vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuendeleza shughuli zao
za ujasirimali,” alisema Koka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Kibaha Mjini Dk Athuman
Mokiwa alisema kuwa moja ya changamoto ianyowakabili ni ukosefu wa fedha kwa
ajili ya kupima kiwanja chao kilichopo Simbani.
Dk Mokiwa alisema wanaomba Halmashauri iwapimie kiwanja chao
ili waweze kuwa hati ya umiliki na kuweza kuweka wawekezaji ili Jumuiya iweze
kujiongezea kipato.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo alisema kuwa
maombi yote yaliyotolewa na Jumuiya ya Wazazi yapelekwe kwa maandishi ofisini
kwake ili aweze kuwafikishia ujumbe wahusika.
Ndikilo aliipongeza Jumuiya hiyo na kusema ndiyo Jumuiya
kiongozi kwani imeyabeba makundi yote ya chama wakiwemo vijana, akinamama na
wazee hivyo lazima iwe mfano wa kuwa muhimili wa chama.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe
IMEELEZWA kuwa uanzishwaji wa Masjala za Ardhi kutasaidia kukabiliana
na migogoro na kupandisha thamani ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye vijiji
mkoani Pwani.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Chakenge wilayani
Kisarawe wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo alipotembelea
Masjala ya Kijiji hicho, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Cheyo
Nkelege alisema kuwa uanzishwaji wa Masjala hizo huwafanya wanakijiji kuwa na
hati za umiliki za kimila.
Nkelege alisema kuwa Masjala hizo zina faida kubwa hususani
kwa wananchi wa vijijini kwani wanaweza kuwa na hati miliki za mashamba yao
ambazo zinaweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwemo dhamana na rehani.
“Faida za kuanzishwa Masjala hizi kwanza inasaidia kupata
hati za umiliki za kimila, kurasimisha ardhi kwa wawekezaji, kuongeza thamani
ya ardhi, kuhifadhi nyaraka za ardhi na kupunguza migogoro ya mipaka ambayo
imesababisha hadi vifo,” alisema Nkelege.
Alisema kuwa faida nyingine ni kuwa na mipaka inayoeleweka na
kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekithiri baina ya wananchi na Vijiji kwa
Vijiji hivyo ni mpango mzuri unaopaswa kuigwa sehemu mbalimbali nchini.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa Ndikilo alisema kuwa Masjala
hiyo ni kichocheo cha maendeleo kwani itatunza kumbukumbu mbalimbali za ardhi
na itawaondolea umaskini.
Ndikilo alisema kuwa jambo jema kwani hati miliki hizo
zitatambulika kisheria na zitaweza kutumika kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kuweka dhamana kwa ajili ya kukopa fedha kwa ajili ya shughuli za
maendeleo.
Akisoma risala juu ya ujenzi huo Belina Denisa alisema kuwa
ujenzi huo umekamilika ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 40 bila ya
samani za ndani ambayo ni fidia iliyotolewa na kampuni ya Sun Bio Fuel kwa
kijiji hicho baada ya kuchukua shamba kijijini hapo. Kutokana na ubora wa
Masjala hiyo mkuu wa mkoa huyo aliahidi kuwapatia 500,000 na 500,000 zitatolewa
na mbunge wa Jimbo la Kisarawe Hussein Jaffo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametumia kiasi
cha zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali waliojiunga
kwenye vikundi 150.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kongamano la
wajasiriamali wa Jimbo hilo na kusema kuwa lengo ni kuwafikia wajasiriamali
woete kwenye mitaa na kata hasa wale waliojiunga kwenye vikundi.
Koka alisema kuwa vikundi hivyo vinajishughulisha na shughuli
mbalimbali za ujasairiamali ikiwemo biashara pamoja na uzalishaji wa bidhaa
mbalimbali ambazo huziuza kwenye masoko mkoani humo na nje ya mkoa.
“Tumedhamiria kuwawawezesha wajasiriamali kiuchumi kwa
kuwapatia fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi za kuweza
kujiongezea kipato na kuinua uchumi wa familia,” alisema Koka.
Alisema kuwa wajasiriamali wana uwezo wa kuinua kipato cha
jamii kwani ndiyo shughuli za kiuchumi zinazoweza kuwawezesha kumudu maisha
kuliko ajira za kuajiriwa ambazo ni chache.
“Kama mnavyojua ujasiriamali umechukua nafasi kubwa ya
kiuchumi na umewasaidia watu wengi kujiajiri hususani vijana na akinamama hivyo
kuacha kuwa tegemezi,” alisema Koka.
Kwa upande wa mke wa Mbunge huyo Selina Koka ambaye ni mlezi
wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) CCM Kibaha Mjini amekuwa akiwapatia mafunzo
ya ujasiriamali alisema kuwa kwa sasa wanawake wengi wameamka na kuendesha
familia kupitia shughuli hizo.
Selina alisema kuwa wajasirimali wanachotakiwa ni kuhakikisha
wanajiunga kwenye vikundi ili waweze kupata misaada ya fedha kwa ajili ya
kuendeshea shughuli zao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe
HOSPITALI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imekamilisha
ujenzi wa chumba kipya cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya wilaya hiyo
ambayo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya kuwa na chumba kidogo hali
iliyokuwa ikiwafanya kupeleka kuhifadhi maiti hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akisoma risala mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo
aliyetembelea hospitali hiyo ya wilaya, mganga mkuu wa wilaya Dk Happiness
Ndosi alisema kuwa hali hiyo ilikuwa changamoto kubwa.
Dk Ndosi alisema kuwa ndugu wa marehemu walikuwa wakipata
taabu kuhifadhi maiti na kuzipeleka Jijini Dar es Salaam hivyo kutumia gharama
kubwa hadi wakati wa mazishi.
“Chumba cha maiti cha zamani kilikuwa na uwezo wa kuhifadhi
maiti wawili tu na kilijengwa miaka ya 1950 hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya
kuhifadhi miili ya marehemu ambapo huwabidi kuipeleka Muhimbili,” alisema Dk
Ndosi.
Alisema kuwa chumba hicho cha sasa hivi kitakuwa na uwezo wa
kuhifadhi miili 36 kwa wakati mmoja endapo itatumika vizuri hivyo kuondoa
changamoto hiyo.
“Mradi huu umegharimu kiasi cha shilingi milioni 102 ambazo
zimetoka serikali kuu ikiwa ni maombi maalumu ambapo umekamilika kwa asilimia
99 na kwa sasa imebaki kuingiza umeme pekee na utaingia muda wowote kuanzia
sasa na mafundi wanaendelea na kazi,” alisema Dk Ndosi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe Subira Mgalu
alisema wanaishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa chumba hicho kwani
imewaondolea mzigo wa kuhifadhi maiti.
“Ilikuwa ni shida mtu akifa apelekwe Muhimbili halafua
arudishwe gharama zilikuwa ni kubwa sana hivyo imesaidia kupunguza usumbufu
hivyo watu wataweza kujipanga kuandaa shughuli za mazishi kwa nafasi,” alisema
Mgalu.
Mgalu alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo ambao umefanywa
na serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na kwa gharama nafuu
kwani sasa hawatapata usumbufu tena wa kuhifadhi maiti.
Naye mkuu wa mkoa Ndikilo alisema kuwa utu wa binadamu
utalindwa kwani kipindi cha nyuma mwili ulikuwa unazikwa harakahara kwani
ukikaa muda hata siku mbili una haribika hivyo kutoitendea haki maiti na
utawapunguzia gharama.
Ndikilo alisema watapata muda mzuri wa kuweza kuandaa mipango
ya mazishi kwa ajili ya kuwahifadhi wapendwa wao ambapo nyuma walikuwa wakikosa
muda wa kuweka mipango mizuri.
Mwisho.