Wednesday, January 21, 2015

MAJAMBAZI YAUA ASKARI WAWILI

Na John Gagarini, Kibaha

ASKARI wawili wa Jeshi la Polisi Kituo cha Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani wamekufa baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuwashambulia kwa silaha baada ya kuvamia kituo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu toka eneo la tukio Ikwiri wilayani Rufiji Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa majambazi hao walitumia silha kuwaua askari hao.

Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 8 kwenye kituo hicho cha Polisi cha Ikwiriri. Aliwataja askari waliokufa kuwa ni usiku Askari waliokufa ni namba E 8732 CPL Edger Milinga na WP 5558 PC Judith Timoth.

Alisema kuwa licha ya kufanya mauaji hayo pia walifanikiwa kupora silaha aina mbalimbali zikiwemo SMG 2, SAR 3, Ant Riot 1, mali ya serikali na S/Gun Protector mali ya kampuni ya Sigara Tanzania.

Aidha alisema kuwa pia watu hao waliharibu kwa kulipiga risasi gari la polisi la kituo  hicho lenye namba za usajili PT 1965.


Mwisho.

Wednesday, January 14, 2015

MRADI WAMI CHALINZE KUNUFAISHA 271,000

Na John Gagarini, Chalinze

MRADI wa Maji wa Wami Chalinze awamu ya tatu  mara utakapokamilika unaratajia kuwafikia wananchi 271,000 wa Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.

 Aidha mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 60 unatarajia kuanza mwezi Machi mwaka huu utapunguza tatizo la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Chalinze ambao wanahudumiwa na mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) Mhandisi Christer Mchomba alisema katika awamu hiyo itaongeza mitandao ya maji kwenye vitongoji 210 kutoka kwenye vijiji 47 ambavyo vilifikiwa kwenye utekelezaji wa awamu ya pili iliyoanza mwaka 2008.

 “Katika awamu ya tatu ya mradi huu yatajengwa pia matenki ya kuhifadhia maji kwenye vijiji 20 vya awamu ya kwanza kikiwamo kijiji cha Bwiringu, Msata, Lugoba, Msoga, Mandela na vingine ambavyo havikujengewa matenki,” alisema Mhandisi Mchomba.

Mhandisi Mchomba alisema kwa sasa awamu ya pili ,wizara inakamilisha ujenzi wa nyongeza ya chujio la maji ambalo litaongeza wingi wa maji yanayosafishwa na kuzalishwa.

Alisema kuwa watajenga tanki kubwa eneo la Mazizi lenye uwezo wa kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 200,000 pamoja na vituo vya maji kwenye vijiji na vitongoji vyote kwenye Jimbo hilo.

“Kwa sasa wanazalisha maji kwa asilimia 85 tu kutokana na mashine kushindwa kufanya kazi kikamilifu ambapo kwa siku ni mita za ujazo 2,000 badala ya 5,000 kwa siku,” alisema Mhandisi Mchomba.  

Kwa upande wake ofisa maabara wa mradi huo Riziki Kacheche alisema  kuwa maji ghafi yanapokuwa machafu zaidi tope huziba na kuzuia maji kuchukuliwa katika kiwango kinachotakiwa kwenda kusafishwa na hivyo kusabababisha uwezo wa kuzalisha maji na kuyasafisha kuwa mdogo.

Mwisho

Tuesday, January 13, 2015

VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA NA VIJIJI WAASWA NA WANANCHI WAHAKIKISHIWA KUPATA UMEME


 Na John Gagarini, Bagamoyo
VIONGOZI wa serikali za mitaa na vijiji wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani waliochaguliwa hivi karibuni wametakiwa kusoma mapato na matumizi ili kuepuka kuenguliwa kwenye nafasi zao kama baadhi yao waliopita kukataliwa na wananchi.
Moja ya changamoto zilizosababisha viongozi hao waliopita baadhi yao walienguliwa na wananchi huku wengine wakishindwa kurudishwa kwenye kura za kuteuliwa kuwani uongozi kwenye uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Hayo yalisemwa Bagamoyo na katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kombo Kamoto alipozungumza na wananchi wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo Ridhiwani Kikwete kwenye  vijiji vya kata za Kibindu, Mbwewe, Mdaula, Bwiringu, Fukayosi, Miono na Kiwangwa.
Kamote alisema kuwa viongozi hao waliochaguliwa na wananchi hasa wale wanaotoka chama hicho kwani hawana budi kuwatumikia wananchi ipasavyo kwa lengo la kuwatatulia changamoto ambazo zinawakabili katika nyanja mbalimbali kwenye huduma za kijamii.
“Mmechaguliwa na wananchi kwa heshima ya chama chetu, hususani kusoma mapato na matumizi hivyo niwasihi mchape kazi kama sheria na taratibu zinavyowaongoza, sitopenda kusikia wananchi wakilalamikia kuhusu utendaji wenu, mtambue mwaka huu mmeapishwa na mahakimu tofauti na miaka yote, hivyo yeyote atayekiuka kiapo hicho ataondolewa kwenye nafasi yake,” alisema Kamote.
Alisema kuwa viongozi hao watatakiwa kuitisha mikutano na kusoma mapato na matumizi kwa wananchi ili waweze kujua yanayofanyika kwenye maeneo yao.
Viongozi hao pia waliaswa kutokuwa madalali wa kuuza ardhi kiholela na kuwakandamiza wananchi ambao wakati mwingine hawajui haki zao za msingi.
“Baadhi waliondolewa kutokana na kushindwa kuitisha mikutano ikiwa ni pamoja na kushindwa kusoma mapato na matumizi hali iliyowafanya waondolewa madarakani au kushindwa kwenye uteuzi wa kuwania nafasi hizo, alisema Kamote.
Aidha alisema kuwa inashangaza kuona baadhi ya viongozi wanakuwa vinara wa kuuza maeneo na kama yupo kiongozi aliyekuwa anafanya hivyo wanapaswa kuacha na kuwa waadilifu ili kulinda nafasi walizopata.
“Viongozi huu si muda wa kuanza majigambo ama kujivunia nafasi mlizoshika  bali mnatakiwa kutimiza wajibu wenu kwa kusimamia ilani ya chama cha mapinduzi ili kuleta maendeleo kwa wananchi,” alisema Kamote.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete aliwaomba viongozi hao kufanya kazi kwa bidii ili chama kiendelee kuaminika na kushika dola .
“Fanyeni kazi bila kubagua watu ,watumikieni pasipo kujali itikadi za kisiasa na hiyo ndio sifa pekee ya kiongozi wa sasa asiyejali udini,ukabila wala chama alichopo,”alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema kuwa yeye akiwa mbunge ataendelea kuwatumika ipasavyo katika kuwaondolea changamoto zinazowakabili.
mwisho.
Na John Gagarini,Chalinze
KILIO cha baadhi ya wananchi wa Jimbo la Chalinze kukosa umeme huenda kikaisha baada ya kuhakikishiwa kuwa watapata huduma hiyo kuanzia m,waka huu kupitia miradi ya umeme vijijini kupitia wakala wa umeme Vijijini (REA).
Changamoto hiyo itapungua kwenye maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo katika vijiji ambavyo vipo kwenye awamu ya awamu ya tatu inayotarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka huu kupitia miradi hiyo ya REA.
Akiwahutubia wananchi wa vijiji vya Kibindu, Mbwewe, Mdaula, Bwilingu, Fukayosi, Kiwangwa na Chalinze mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa serikali ya CCM imejipanga kuikabilia changamoto hiyo.
“Kila maeneo niliyopita nimekutana na malalamiko  kutoka kwa wananchi juu ya kukosa umeme wakati vijiji vingine vya kata hizo vikiwa vimepata umeme na kuhoji huku wao wakiona kwa macho umeme umepita juu na kwenda maeneo jirani,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alise kuwa anatambua umuhimu wa umeme hivyo amekuwa akifanya jitihada za kufuatilia na ndio maana amelazimika kufuatana na meneja wa miradi ya umemem mkoani Pwani Leo Mwakatobe ambaye anatolea ufafanuzi suala hilo.
“Mfano eneo la Kiwangwa halikuwepo katika umeme unaosambazwa na REA lakini baada ya kufanya juhudi hizo fedha zimepatikana hivyo utakuwa wa REA ambapo tanesco imetoa sh.milioni 420 na REA sh.milioni 800,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema kuwa fedha hizo tayari ziko na kazi ya kuanza kusambaza umeme itaanza wakati wowote, kwani anajua umuhimu wa umeme lakini wananchi na kuwaomba wananchi wafahamu juhudi za serikali.
Kwa upande wake  mhandisi wa Tanesco mkoa wa Pwani, Mhandisi Leo Mwakatobe, alisema wanaendelea kumalizia utekelezaji wa awamu ya pili wa mradi wa REA na kazi iliyobaki ni mkandarasi kuanza kazi wakati wowote kuanzia mwezi huu.
Mwakatobe fedha kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme zimepatikana, hivyo wananchi wenye kuhitaji waanze kuchukua fomu.kinachotakiwa wawe na picha mbili na kitambulisho cha aina yoyote.
Mwisho




Monday, January 12, 2015

CHALIWASA YAKANUSHA MASHINE KUUZWA KENYA NA MAGAREZA YAPONGEZWA

Na John Gagarini, Wami
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) imekanusha uvumi kuwa mashine za uzalishaji wa maji zimeuzwa nchini Kenya hali ambayo imesababisha maji kukatika mwezi mzima.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake    Meneja wa mamlaka hiyo Injinia Christer Mchomba alisema kuwa uvumi huo si wa kweli kwani mashine zote zipo na zinatumika kama kawaida.
Injinia Mchomba alisema kuwa uvumi huo umekuja kutokana na maji kutokutoka kwa sababu ya mashine hizo kuvuta uchafu ambao umesababisha kuziba na kushindwa kupitisha maji.
“Tatizo la maji kushindwa kutoka hakutokani na mashine kuuzwa bali ni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwenye mkoa wa Morogoro ambapo ndiyo chanzo cha mto Wami na kusababisha uchafu kuwa mwingi na mashine kuziba na kuharibika hivyo maji kushindwa kutoka,” alisema Injinia Mchomba.
Alisema kuwa tatizo ni tekeo ambapo kwa sasa linawekwa ambalo likikamilika litasaidia kuchuja uchafu tofauti na ilivyokuwa mwanzo kwani maji zamani yalikuwa masafi na yalikuwa hayana uchafu.
“Uchafu huo unatokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na watu wanaojihusisha na uchimbaji wa madini, kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji na uchafuzi wa mazingira hivyo kusababisha uchafu mwingi kuja na maji,” alisema Injinia Mchomba.
Alisema kuwa ukarabati wa mashine hizo unaendelea ambapo umefikia asilimia 85 na baada ya miezi miwili au mitatu tatizo la ukosefu wa maji Chalinze litakuwa ni historia
“Tuna mitambo 30 na mingine mipya hata hatujaifungua iweje watu waseme kuwa imeuzwa wakitaka ukweli waje hapa ili waione kuliko kusema tu bila ya kujua ukweli na waache kuvumisha vitu ambavyo havina ukweli,” alisema Injinia Mchomba.
Aidha alisema kuwa kwa sasa kuna mradi unaotekelezwa ambao utavifikia vitongoji vyote vya Jimbo la Chalinze ambapo awamu ya tatu utatumia bilioni 60 hadi kukamilika.
Mwisho.   
Na John Gagarini, Ubena
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amelipongeza Jeshi la Magereza mkoani Pwani kwa ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya Sekondari ya Bwawani kwa gharama nafuu.
Aliyasema hayo wakati akizindua madarasa hayo kwa ajili ya wanafunzi wa kutwa wa shule hiyo ambayo inamilikiwa na Jeshi hilo la Magereza eno la Ubena.
Ridhiwani alisema kuwa Jeshi hilo limeonyesha uzalendo wa hali ya juu na kutumia vizuri rasilimali fedha kwa kujenga madarasa hayo yenye mawili thamani ya shilingi milioni 31.8.
“Haya ndiyo mambo tunayoyataka kwa kufanya ujenzi wa vitu vya umma kwa matumizi mazuri ya fedha na ujenzi bora hivyo taasisi nyingine za serikali zinapaswa kuzingatia ujenzi kama huu,” alisema Ridhiwani.
Alisema baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikifanya ujenzi wa kawaida kwa gharama kubwa huku ukiwa haujazingatia ubora wa ujenzi wa majengo ambayo hutumiwa kwa muda mrefu.
Aidha alizitaka halmashauri kuwatumia wataalamu wa Magereza katika ujenzi wa majengo mbalimbali ambapo ujenzi wao unazingatia ubora matumizi bora ya rasilimali fedha.
Awali akimkaribisha mbunge huyo mkuu wa Magereza mkoa wa Morogoro  Kato Lugainunula ambaye alimwakilisha mkuu wa Magereza nchini John Minja, alisema kuwa lengo la Magereza ni kuihudumia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu.
Lugainunula alisema kuwa awali shule hiyo ilitumika kutoa elimu ya sekondari kwa watumishi wa Magereza ambao walikuwa hawajapata elimu ya sekondari lakini waliondoa utaratibu huo na kutoa elimu kwa wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali.
Naye kaimu mkuu wa shule hiyo ya Bwawani Emanuel Lwinga alisema kuwa madarasa hayo ni kwa ajili ya wanafunzi wa kutwa ujenzi wake ulitumia muda wa miezi mitano hadi kukamilika kwake.
Lwainga alisema kuwa kila darasa lina uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 40 na 45 ambapo shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 396 wakiwemo wale wa kidato cha tano na shule hiyo ni moja ya shule zinazofanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne kimkoa.

  Mwisho.

Thursday, January 8, 2015

CHANGAMOTO YA MAJI NA VIONGOZI WAUZA KIJIJI

Na John Gagarini, Chalinze
UONGOZI wa Mradi wa maji wa Wami Chalinze wilayani Bagamoyo umetakiwa kutoa taarifa juu ya ukosefu wa maji ambao kwa sasa umedumu takribani mwezi mzima ambapo baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wapotosha ukweli kuhusu tatizo hilo.
Hayo yalisemwa na diwani wa kata ya Bwilingu Nassa Karama katika viwanja vya Masoko wakati mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alipokwenda kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo.
Karama alisema kuwa maji kwa sasa ni kilio kikubwa kwa wakazi wa mjin huo  huku wao wakiwa hawana utaalamu wa kujua tatizo la ukosefu wa maji linatokana na nini hivyo kushindwa kuwapa majibu sahihi wananchi ambapo hali hiyo imesababishwa ndoo kuuzwa kwa shilingi 700 kutoka shilingi 200.
“Suala la kutotoka kwa maji ni la kitaalamu na wahusika wa mradi wa maji wa Wami Chalinze wanapaswa kutoa taarifa juu ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa maji ili majibu yasitolewe na wanasissa ambao wanatumia fursa hiyo kupotosha ukweli wa tatazi hilo,” alisema Karama.
Alisema kuwa wananchi wanapata usumbufu mkubwa kwani kwa sasa wananunua maji kwa baadhi ya watu wenye magari ya kuuza maji ambapo kabla ya tatizo hilo walikuwa walikuwa wakinunua kwa sh.200 na sasa ni sh.700 hali inayosababisha kuwapa wakati mgumu baadhi ya wananchi  ambao baadhi yao kipato chao ni cha chini.
“Baadhi ya wanasiasa hao wanapotosha kwa wananchi kuwa kuna mashine mbalimbali za kukamilisha mradi huo zimeuzwa Nairobi nchini Kenya jambo ambalo linachanganya wananchi na kuleta tafsiri tofauti  kutokana na tatizo hilo,” alisema Karama.
Aliutaka uongozi wa maradi kuo kutoa taarifa juu ya ukosefu wa maji ili kutowapa mwanya wanasiasa  wenye nia ya kutumia jambo hilo kama mtaji wao wa kisiasa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akijibu kuhusiana na maswali hayo alisema anafanya taratibu ya kumpeleka waziri wa maji ili aweze kwenda kutembelea maeneo yenye kero kubwa jimboni humo kujionea hali halisi ya ukosefu wa maji.
Ridhiwani alisema kuwa tatizo kubwa la ukosefu wa maji linatokana na tope linaloingia katika mitambo hali inayosababisha maji kushindwa kutokana ambapo kwa sasa wamenunua chujio kwa ajili ya kuchuja uchafu ambao umekuwa ukiziba na maji kushindwa kutoka.
Aliwataka wanasiasa kuacha kupotosha ukweli kwani si jambo zuri kupotosha wananchi  na kuwataka wataalamu kujenga tabia ya kutoa taarifa ya vikwazo vilivyopo ili wananchi wajue.
Mwisho.
Na John Gagarini, Fukayosi
BAADHI ya  viongozi wa Kijiji cha Kidomole wilayani Bagamoyo mkoani Pwani waliohusika kuuza ardhi ya Kijiji hicho kinyume cha sheria wametakiwa kujiandaa kusimama kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma hizo.
Viongozi hao kwa wameuza eneo kubwa la Kijiji ambapo wananchi wa maeneo hayo wanatakiwa kuondoka na kumpisha mununzi huyo ambaye amechukua eneo kubwa la kijiji.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo alisema viongozi hao lazima wachukuliwe hatua za kisheria kwa ukiukaji wa maadili ya uongozi.
“Inashangaza kuona mtu anakuja na risiti na kusema kuwa kanunua eneo lote la Kijiji na wananchi wanatakiwa kuondoka kumpisha eti mwekezaji jambo kama hili haliwezekani kwani taratibu haziruhusu na viongozi waliofanya hivi wajiandae kwa kukimbilia tutapambana nao ili haki ya wananchi ipatikane,” alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa hatakuwa tayari kuona wananchi hao wanaondolewa kwani sheria za ardhi haziruhusu kuuza eneo la Kijiji zaidi ya hekari 50 zaidi ya hapo lazima suala hilo lipelekwe kwa kamishana wa ardhi.

“Inashangaza kusikia kiongozi kauza hekari zaidi ya 100 kwa mwekezaji sheria haisemi hivyo hata hizo hekari 50 lazima wanakijiji waridhie kwa kufanya mkutano mkuu ili kumpitisha muombaji lakini siyo watu wawili au watatu wanakaa huko ofisini na kuuuziana eneo kinyemela utaratibu huu haupo kisheria,” alisema Ridhiwani.

Akizungumzia kuhusiana na baadhi ya maeneo ya Kijiji kuwemo kwenye eneo la ranchi ya Taifa (NARCO) alisema kuwa uongozi wa halmashauri unapaswa kuonyesha mipaka kwani wananchi walioko kwenye eneo hilo walianza kuishi kabla ya ranchi hiyo.

Aidha alisema maeneo yote yanayomilikiwa na ranchi ya Taifa yaliwekewa mipaka na inajulikana rasmi kisheria tofauti na hapo ambapo ranchi hiyo ndo inaanza kuonyesha mipaka huku kukiwa hakuna alama yoyote na kuutaka uongozi wa ranchi kushirikiana na wananchi hao ili kuondoa malalamiko kwani wanapaswa kuondolewa kwenye maeneo hayo.
Mwisho.



Wednesday, January 7, 2015

WAKAZI CHALINZE WALALAMIKA UKOSEFU WA DAWA KITUO CHA AFYA

Na John Gagarini, Chalinze
WAKAZI wa Chalinze Mjini wameiomba Wizara ya Afya kuangalia upya mgawanyo wa dawa kwenye kituo cha Afya cha Chalinze kwani dawa zinazopelekwa kituoni hapo hazikidhi mahitaji.
Wagonjwa wengi wanaokwenda kuhudumiwa kituoni hapo licha ya kuandikiwa dawa hazipatikani na hutakiwa kununua kwenye maduka ya dawa.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ambaye yuko kwenye ziara ya kukagua masuala ya maendeleo, moja ya wakazi wa Chalinze kitongoji cha Bwiringu aliyejitambulisha kwa jina la Athuman Rashid alisema huduma ya dawa hakuna kabisa.
“Kila ukienda kupata huduma kwenye kituo cha afya Chalinze utahudumiwa vizuri lakini dawa ni mtihani kwani utaambiwa dawa hakuna nenda kanunue kwenye maduka ya dawa,” alisema Rashid.
Rashid alisema kuwa mgawanyo wa dawa kwenye kituo hicho ni mdogo licha ya kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa wengi lakini kinakuwa na upungufu mkubwa wa dawa.
“Ombi letu sisi kwa Wizara ya Afya ni kuangalia namna gani ya kukiwezesha kituo hichi kuwa na mgao mkubwa wa dawa kwani suala la dawa ni tataizo kubwa sana na linatuathiri kwani maduka ya madawa yanauza kwa bei za juu,” alisema Rashid.
Naye Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ni kweli changamoto hiyo ni kubwa sana kwenye kituo hicho na ni vema kituo hicho kikaangaliwa upya.
“Wagonjwa wamekuwa wakilalamika sana juu ya upatikanaji wa dawa kwani kituo hichi kinapewa dawa sawa na vituo vingine vya afya ambavyo havina wagonjwa wengi,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema tayari wameshaongea na Wizara hiyo na stoo ya madawa MSD juu ya kuomba kuongezewa mgao wa dawa kutokana na ukubwa wa kituo kwani mahitaji ni makubwa sana.

Mwisho.    w