Tuesday, December 23, 2014

AMWUA MWANAE KWA KUMNYONGA ADAKWA NA HEROIN

Na John Gagarini, Kibaha
ESTER Endrew (23) mkulima mkazi wa Tabata Jijini Dar es Salaam anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kumwua mwanae Marko Elibariki (2) kwa kumnyonga kwa kutumia mikono.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha, kamanda wa polisi mkoani hapa Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo linahusishwa na wivu wa kimapenzi.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 2 asubuhi eneo la Wipas mtaa wa mkoani B kata ya Tumbi wilayani Kibaha.
“Mtuhumiwa baada ya kutekeleza tukio hilo naye alijichoma tumboni kwa kisu hali iliyosababisha apate majeraha,” alisema Kamanda Matei.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya tukio baadhi ya majirani waligundua kutokana na kulalamika huku damu zikimtoka.
“Alijijeruhi tumboni kwa kisu akitaka kujiua lakini hata hivyo licha ya kujichoma hakufa na kuanza kupiga kelele ndipo majirani walipotoa taarifa polisi na mtuhumiwa kuja kuchukuliwa ambapo ilibainika kuwa alikuwa akimlaumu mumewe kuwa na mke mwingine,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema mtuhumiwa amelazwa kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi kwa matibabu huku akiwa chini ya ulinzi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SHAMBA Malela (20) mkazi wa Nianjema wilayani Bagamoyo mkoani Pwani anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupatikana na kete 136 za dawa aina ya Heroin.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa na polisi waliokuwa doria.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 22 mwaka huu majira ya saa 7:45 mchana huko Nianjema kata ya Magomeni wilaya ya Bagamoyo.
“Mtuhumiwa baada ya kutiliwa mashaka alikwenda kupekuliwa nyumbani kwake na kukutwa na dawa hizo ambazo zinadhaniwa kuwa ni za Heroin ambapo hata hivyo thamanai yake haikuweza kufahamika mara moja.
Alisema kuwa jeshi hilo linafanya doria kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya za mkoa huo ili kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu.
Mwisho.

Sunday, December 21, 2014

Saturday, December 20, 2014

RIDHIWANI AKARIBISHWA KIJIJINI MSOGA KWA SHEREHE ZA JADI

Na John Gagarini, Chalinze

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani  Ridhiwani Kikwete juzi alifanyiwa sherehe za jadi za kabila la Kikwere kama kiongozi baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge.

Sherehe hizo za jadi ambazo zilifanyika kijijini kwao Msoga ziliambatana na kukabidhiwa vitu mbalimbali vya kijadi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Baadhi ya vitu alivyoakabidhiwa na mzee wa kabila hilo Zaidi Rufunga ni pamoja na fimbo kama kiongozi, kitanda cha kamba, msuli, kigoda na kinu pamoja na vitu mbalimbali.


Sherehe hizo za kijadi ziliamabatana na ngoma ya Kikwere na ulaji wa chakula kiitwacho Bambiko ambacho hutumiwa na kabila hilo. 

 Mzee Zaidi Rufunga kulia akimkabidhi vyungu mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete wakati wa sherehe za jadi za kumkaribisha nyumbani zilizofanyika juzi kijiji cha Msoga. 




 Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani  akielekezwa jambo na mzee Zaidi Rufunga  kabla ya kula chakula cha jadi cha kabila la Wakwere kiitwacho Bambiko baada ya kukaribishwa nyumbani na kufanyiwa sherehe za jadi za kikabila zilizofanyika kwenye Kijiji cha Msoga.




Baadhi ya akina mama wakila chakula mcha jadi cha kabila la Kikwere kiitwacho Bambiko mara baada ya kumkaribisha nyumbani Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani

 Baadhi ya akina mama wakila chakula mcha jadi cha kabila la Kikwere kiitwacho Bambiko mara baada ya kumkaribisha nyumbani Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani

Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kushoto na katikati diwani wa kata ya Msoga Mohamed Mzimba na baadhi ya wageni wakila chakula cha jadi kiitwacho Bambiko mara baada ya sherehe za jadi za kumkaribisha nyumbani kwenye Kijiji cha Msoga .


Friday, December 19, 2014

HABARI ZA PWANI

Na John Gagarini, Chalinze
KATIKA kutekeleza mpango wa Matokeo ya haraka (BRN) Wizara ya Afya imesema kuwa iko katika maongeza na wafadhili kwa ajili ya kujenga viwanda vya kuzalisha dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali badala ya kutegemea kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.
Asilimia 80 ya dawa zinaotumika zinaagizwa toka nje ya nchi na kuifanya nchi kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kuagiza dawa hizo ambapo endapo kutakuwa na viwanda vingi kutasaidia kupunguza gharama.
Hayo yalisemwa na katibu mkuu wa Wizara ya Afya Donan Mmbando, kwenye Kijiji cha Msoga alipotembelea ujenzi wa kituo cha afya cha kijiji hicho na kusema kuwa dawa bado ni changamoto kubwa.
“Mpango huu kama ulivyo kwenye sekta nyingine utatupima kwa kipindi cha miaka mitatu kutuona je temeweza kufikia malengo ambapo kati ya malengo hayo ni kuhakikisha upatikanaji wa dawa, upatikanaji wa vifaa tiba na mambo mengine,” alisema Mmbando.
Alisema BRN itafanikiwa endapo kutakuwa hakuna tatizo la upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba ambavyo vimeonekana kuwa ni changamoto kubwa.
“Mbali ya changamoto ya upatikanaji wa dawa pia kuna baadhi ya watumishi wanaojihusisha na wizi wa dawa hawa sasa tutawakamata na kuwatangaza kwenye vyombo vya habari,” alisema Mmbando.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ujenzi wa Kituo hicho cha afya ambacho ni cha kisasa ni ukombozi kwa watu wa Jimbo hilo ambao hutegemea kuwapeleka wagonjwa kwenye hospitali ya Tumbi.
Ridhiwani alisema kuwa pia majeruhi wa ajali ambao walikuwa wakipelekwa Tumbi sasa watapata huduma hapo ambapo wanatarajia kituo hicho kufunguliwa mwezi Machi mwakani.
Naye diwani wa kata ya Msoga Hussein Mzimba alisema kuwa kituo hicho kinajengwa kwa nguvu ya wananchi, serikali pamoja na wadau wa maendeleo wa kata na wilaya hiyo.
Mwisho.

19,Des
Na John Gagarinii, Chalinze
KITUO cha Afya cha Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kinakabiliwa na ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa kwa kipindi cha miezi mine jambo ambalo linasababisha wagonjwa kukodisha magari kwa ajili ya kupelekwa kwenye hospitali kubwa ikiwemo ya Tumbi.
Hayo yalisemwa na Mganga mkuu mfawidhi wa kituo hicho, Dk Victor Bamba wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete alipotembelea kituo hicho na kuangalia changamoto zinazoikabili sekta ya afya.
“Changamoto hii imetokana na imetokana na gari la wagonjwa lililopo kuwa kwenye matengenezo kwa muda wote huo,” alisema Dk Bamba.
Kwa upande wake Ridhiwani alisema kuwa tayari kuna mkakati wa kuhakikisha kunakuwepo na magari ya kubebea wagonjwa matatu mkakati utakaotekelezwa mapema mwaka ujao.
“Magari hayo yatagawiwa katika kituo cha afya Chalinze, Miono na kituo cha afya Msoga ambacho kinatarajia kukamilika hivi karibuni,” alisema Ridhiwani.
Kituo cha afya Chalinze kinakabiliwa na changamotombalimbali ikiwa ni pamoja na uhaba wa madawa, chumba cha kuhifadhia maiti, vifaa vya kujifungulia mama wajawazito ambapo kwa miezi 12 sasa havijasambazwa katika kituo hicho.
Mwisho.


Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa ajali kwa sasa zinaonekana kama ugonjwa usioambukiza ambao unaua watu wengi kwa sasa hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mkurugenzi wa Elimu Mafunzo na Uenezi wa kamati ya usalama Barabarani Taifa Henry Bantu, wakati wa kilele cha siku ya usalama barabarani mkoani Pwani.
Alisema kuwa ajali kwa sasa zinaelekea kuwa ugonjwa unaoua kuliko magonjwa mengine kwani mwelekeo ndiyo unaoonekana.
“Endapo jitihada za kuzuia ajali hazitafanyika ajali ndiyo zitakuwa ni ugonjwa usioambukiza unaoua watu wengi nchini kwa sasa lakini hata hivyo baraza linajitahidi kuhakikisha ajali zinapungua,” alisema Bantu.
Bantu alisema kuwa madereva wanapaswa kuwa makini katika uendeshaji wa magari ili kupunguza ajali zisizo za lazima.
“Ajali nyingi siyo bahati mbaya kama wanavyosema watu bali ajali zinatokana na uzembe na si mpango wa Mungu hivyo umakini unatakiwa kuwepo,” alisema Bantu.
Awali akisoma risala ya kamati ya usalama barabarani mkoa Shaban Nkindwa alisema kuwa katika kipindi cha Januari Mosi hadi Novemba 30 jumla ya watu 556 walifariki dunia.
Nkindwa alisema kuwa ajali kwa jumla zilikuwa 1,859 za vifo zilikuwa 424 huku zilizojeruhi zikiwa 1,126 na watu waliojeruhiwa walikuwa 2,601.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limekusanya kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mbili kutokana na makosa madogo madogo ya usalama barabarani yaliyotokea kwa kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu.
Akisoma risala ya kamati ya usalama barabarani mkoa wa Pwani, wakati wa kilele cha siku ya usalama barabarani zilizofanyika jana mjini Kibaha, Shaban Nkwinda alisema kuwa fedha hizo zilitokana na makosa yaliyotokana na makosa yaliyofanywa na madereva.
Nkwinda alisema kuwa makosa yaliyokamatwa yalikuwa 80,786 ambapo ni ongezeko la ajali 23,839 sawa na asilimia 41.8 ikilinganishwa na mwaka jana.
“Makosa yaliyolipiwa yalikuwa 80,259 ikiwa ni ongezeko la ajali 24,293 sawa na asilimia 43.4 ikilinganishwa na mwaka jana,” alisema Nkwinda.
Alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka jana mkoa uliweza kukusanya kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni moja kutokana na makosa 56,946 kutokana na makosa yaliyolipiwa na 55,966.
Mwisho.


Tuesday, December 16, 2014

TATIZO LA MAJI CHALINZE KUWA HISTORIA NA KIBAHA YAENDELEA KUKIMBIZANA NA MAABARA

Na John Gagarini, Kibaha
CHANGAMOTO ya maji wilayani Bagamoyo mkoani Pwani huenda ikawa historia baada ya serikali ya India kutoa kiasi cha bilioni 800 kwa ajili ya mradi wa maji wa Wami Chalinze.
Akizungumza na waandishi wa habari mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa fedha hizo zitasaidia kukabiliana na tatizo hilo ambalo limekuwa likiwasumbua wananchi wa wilaya hiyo.
Ridhiwani alisema kuwa fedha hizo ambazo ni sehemu ya mkopo baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa nchi ya India alipotembelea nchini hivi karibuni.
“Fedha hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha mradi huo ambao umekwama kwa baadhi ya maeneo kutokana na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kutotengeneza miundombinu kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema Ridhiwani.
Alisema mbali ya kujenga miuondombinu ya kufika kwenye vijiji mbalimbali pia fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kujenga mabwawa ya muda kwa ajili ya kuhifadhi maji na kuchujia maji.
“Wakati mwingine maji yamekuwa yakitoka machafu kutokana na maji kuingiwa na tope hasa pale mvua inaponyesha hivyo tunatarajia kuwe na matanki ambayo yatachuja maji kwani yaliyopo ni machache,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema pia kutajengwa vioski na matenki kwenye vitongoji na vijiji 20 kwani baadhi viko umbali mdogo  kwenye baadhi ya matenki lakini havipati maji.
Alibainisha kuwa Jimbo la Chalinze baada ya muda mfupi itaepukana na adha ya maji kwani watakuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama kupitia mradi huo kama baadhi ya maeneo.
Na John Gagarini, Kibaha
WILAYA ya Kibaha mkoani Pwani imefikia asilimia 80 ya ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari na inatarajia kukamilisha ujenzi huo mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa wilaya hiyo imeweza kujenga maabara 53 katika kipindi cha miezi miwili cha agizo la Rais Dk Jakaya Kikwete.
Kihemba alisema kuwa kulikuwa na changamoto kubwa ambazo zimechangia ujenzi huo kushindwa kukamilika kwa asilimia 100 ambapo kwa sasa zimebakia maabara 10.
“Changamoto kubwa ilikuwa ni wenyeviti wa mitaa na viji kujiuzulu kabla ya uchaguzi kwani wao ndiyo wahamasishaji wakuu wa kukusanya michango pia mwitikio wa wananchi kuchangia kuwa mdogo na suala la akaunti ya Tegeta Escrow kushusha uchangiaji kutokana na wapinzani kutumia sababu ya wananchi wasichangie,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa wilaya yetu ina jumla ya shule 21 ambapo kila shule inatakiwa kujenga maabara 3 hivyo kufanya wilaya kuhitaji maabara 63 na thamani ya kila maabara ni shilingi milioni 60.
“Tunawashukuru wadau wetu mbalimbali wa maendeleo na wananchi ambao walitusaidia fedha kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa maabara hizi na tunaendelea kuwaomba watusaidie ili tuweze kukamilisha ujenzi huo kama tulivyopanga,” alisema Kihemba.
Mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha alisema kuwa anamshukuru Rais kwa kuwapa msukumo wa ujenzi wa maabara kwani kwa kipindi kifupi maabara nyingi zimejengwa ambazo zitakuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi.

Mwisho.

Monday, December 15, 2014

SOKA WANAWAKE PWANI WAINGIA KAMBINI KUJIANDAA TAIFA CUP

Na John Gagarini, Kibaha
TIMU ya soka ya wanawake ya mkoa wa Pwani imeingia kambini kwenye shule ya sekondari ya Baden Powell iliyopo wilayani Bagamoyo kujiandaa na mchezo wake na timu ya mkoa wa Morogoro utakaochezwa Desemba 28 mwaka huu.
Mchezo huo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi wilayani Kibaha wa kuwania kombe la Taifa kwa wanawake.
Akizungumza na gazeti hili mjini Kibaha, katibu wa chama cha soka la Wanawake (TWFA) mkoa wa Pwani Florence Ambonisye alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri.
Ambonisye alisema kuwa timu hiyo inanolewa na mchezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake Hilda Masanche iliingia kambini wiki iliyopita.
“Timu inatarajiwa kurejea Desemba 26 wilayani Kibaha ambapo itaingia kambini kwenye kambi ya Ruvu JKT Mlandizi siku mbili kabla ya mchezo huo,” alisema Ambonisye.
Aidha alisema kuwa timu hiyo itaongezewa wachezaji wanne mara itakaporudi Kibaha ili kuipa nguvu timu hiyo inayoundwa na wachezaji wengi vijana ambao ni wanafunzi shule za sekondari.
“Changamoto kubwa inayoikabili timu hiyo ni ukosefu wa vifaa kwani wachezaji wanatumia vifaa vyao binafsi walivyoendanavyo kambini,” alisema Ambonisye.
Alibainisha kuwa wanatarajia kushinda mchezo huo kwani timu yao imejiandaa vyema na mchezo huo licha ya kuwa wapinzani wao nao wako vizuri na wana uhakika wa kuingia 16 bora.
Mwisho.

CCM YAONGOZA MATOKEO YA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA, VITONGOJI NA VIJIJI

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani kimeonyesha kufanya vizuri kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji ambapo kwenye matokeo ya awali kimeonekana kushinda maeneo mengi.
Katika Jimbo la Mafia CCM ilishinda vitongoji  96 kati ya 136 sawa na asilimia 70 Chama Cha Wananchi CUF asilimia 40 sawa na asilimia 29,katika vijiji  CCM ilishinda vijiji 19 kati ya 23 sawa na asilimia 82.6 CUF vijiji 4 sawa na asilimia 17.3.
Katika Jimbo la Kibaha Mjini kati ya mitaa iliyopo 73 ,CCM imeshinda mitaa 62 sawa na asilimia 84.9, huku wapinzani wao Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakishinda kwenye mitaa 10 sawa na asimilia 13.7.
Katika Jimbo Kibaha  Vijijini kwenye Vijini 32 CCM ilishinda mitaa 31 , ambapo kwenye mitaa 10 ilishinda bila kupingwa sawa na asimilia 96.9 ,upinzani ilishinda kijiji kimoja sawa na asimilia 13.1, kati ya vitongoji 106 CCM ilishinda vitongoji 98 sawa na asilimia 92.5,upinzani vitongoji 4 sawa na asilimia 3.8.
Katika Wilaya ya Bagamoyo vijiji vilivyopo ni 75 CCM ilishinda vijiji 67 sawa na asilimia 90.5 na vijiji 8 havijafanya uchaguzi, kati ya vitongoji  610 CCM ilishinda 540 sawa na asilimia 88.5 na vitongoji 45 havijafanya uchaguzi ambapo wapinzani walishinda vitongoji sawa na  asilimia 4.1.
Wilaya ya Bagamoyo haijafanya uchaguzi katika vijiji 8 na vitongoji 45 kutokana na uhaba wa vifaa ikiwemo katasi husika za viti maalum na kuchanga majina ya wananchi na nembo za vyama vya siasa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Ibrahim Matovu alithibitisha kutokea kwa mabadiliko ya uchaguzi katika maeneo hayo ambapo alisema uchaguzi huo baadhi ya maeneo ulifanyika jana na kwingine utafanyika leo desemba 16.

Mwisho