Wednesday, August 27, 2014

WALILIA FIDIA YA MASHAMBA YAO

Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI nane wa kitongoji cha Benki kata ya Igunga wilaya ya Igunga mkoani Tabora wameiomba Halmashauri ya wilaya kuwalipa fidia ya mashamba yao ambayo yamechukuliwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya upanuzi wa hospitali ya wilaya.
Wakazi hao walitoa ombi hilo kufuatia Halmashauri hiyo kuwa kimya kwa muda mrefu baada ya mashamba yao kuchukuliwa tangu mwaka 2010 nakufanyiwa tathmini mwezi Februari mwaka huu lakini hadi sasa bado hawajalipwa fidia za maeneo yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha mwenyekiti wa kamati ya waathirika hao  Daniel Shamalatu alisema kuwa mashamba yao yana ukubwa wa zaidi ya hekari 24 ambazo zilichukuliwa kwa ajili ya upanuzi huo wa hospitali ya wilaya.
Shamalatu alisema kuwa maeno yao yalichukuliwa bila ya wao kupewa taarifa ambapo mazao yao waliyokuwa wameyapanda yalifyekwa na ujenzi kuanza bila ya kupewa fidia.
“Tulipoona kimya tulikwenda mahakamani ili tuweze kulipwa fidia zetu lakini baraza la madiwani liliingilia kati na kututaka tuondoe kesi mahakamani ili tukubaliane nje ya mahakama, kweli tuliondoa kesi hiyo mahakamani lakini hakuna kinachoendelea ambapo sasa ni karibu mwaka umepita lakini tunaona kimya na tunapofuatilia halmashauri tunaambiwa suala letu linashughulikiwa,” alisema Shamalatu.
Alisema kuwa wao hawapingi ujenzi huo lakini wanachotaka ni kulipwa fidia kutokana na ukubwa wa mashamba yao na si kiwanja kimoja kila heka kama walivyotaka kufanya na pia wanataka kujua malipo yao yatafanyika lini.
 Akitolea ufafanuzi suala hilo kwa njia ya simu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Rustika Turuka alisema kuwa ni kweli mashamba yao yalichukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa hospitali hivyo kutakiwa kupisha ujenzi huo kufanyika.
Turuka alisema kuwa kwa sasa maeneo hayo tayari yameshafanyiwa tathmini na taarifa ya uthamini imepelekwa wizarani kwa ajili ya kuandaliwa malipo baada ya kujua takwimu sahihi kutokana na maeneo hayo na kiasi ambacho watastahili kulipwa ili halmashauri itenge bajeti kwani maeneo mengine ambayo yalichukuliwa wamelipwa na wao watalipwa mara taratibu zitakapokamilika.
“Mthamini toka Tabora alishafika na kufanya kazi hiyo na kwa sasa tunachokisubiri ni taarifa toka wizarani baada ya kuipitia tathmini hiyo ili watu wanaodai fidia waweze kulipwa hivyo wanapaswa kuwa na subiri kwani mambo haya lazima yafuate taratibu na kila mtu atapewa haki zake pia eneo hilo  kwa sasa ni mji haipaswi kuwa na mashamba,” alisema Turuka
Aidha alisema wanasubiri taarifa hiyo ambayo itaonyesha ni kiasi gani wanastahili kulipwa na ndipo watatafuta fedha hizo kisha kuwalipa watu ambao wanadai ila wanataka walipwe haraka lakini serikali ina taratibu zake za kufanya malipo.
“Masuala ya malipo ya fidia za viwanja si suala la haraka linachukua muda mrefu hivyo lazima wawe na subiri wakati masuala yao yanashughulikiwa ambapo maeneo mengine tayari wameshalipwa hivyo na wao wanapaswa kuwa na subira na kila mtu atapata malipo yake,” alisema Turuka.
Mwisho.

     

Tuesday, August 26, 2014

Na John Gagarini, Kibaha
RAIA wa nchi ya Ethiopia Dawita Alalo (25) amekufa alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya cha Chalinze kata ya Bwiringu wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Marehemu alikuwa ni kati ya raia 48 wa nchi hiyo walikamatwa wakiwa kwenye msitu wa kijiji cha Visakazi Ubena Zomozi tarafa ya Chalinze Agosti 22 mwaka huu, baada ya kuingia nchini bila ya kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa marehemu ni miongoni mwa wahamiaji haramu 11 waliokuwa wamelazwa kituoni hapo wakipatiwa matibabu.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 26 majira saa 7:30 usiku alipokuwa akipatiwa matibabu kituoni hapo baada ya kuugua ugonjwa wa malaria.
Wakati huo huo mlinzi wa baa ya Silent Inn Jamat Mandama (55) amefariki dunia baada ya kunywa pombe nyingi bila ya kula chakula.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 mwaka huu majira ya saa 1 usiku huko Umwe kata ya Ikwiri wilayani Rufiji.
Aidha alisema kuwa mlinzi huyo alikutwa amekufa akiwa lindoni kwenye baa hiyo.
Na John Gagarini, Kibaha
ASKARI sita wa jeshi la polisi mkoani Pwani wamenusurika kifo kutokana na ajali ya barabarani baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongwa na lori la mizigo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kaimu kamanda wa polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa askari hao walikuwa doria.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 26 majira ya saa 9:30 usiku eneo la Maili Moja Ujenzi wailayani Kibaha barabara kuu ya Dar es Salaam Chalinze.
Alisema kuwa gari hilo lenye usajili namba PT 2012 lilikuwa likiingia kwenye kituo cha mafuta cha Delina na kugongwa na lori hilo lenye namba za usajili T 927 CAU na tela namba T 769 CJX.
“Lori hilo bada ya kuligonga gari hilo lapolisi kwa nyuma likaenda kugongana na lori lingine lililokuwa likielekea Jijini Dar es Salaam lenye namba T 672 BAC lenye tela namba T 672 BBW,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alibainisha kuwa askari watatu walijeruhiwa vibaya ambao ni namba F 4333 DC Tamimu ambaye amevunjika mguu wa kulia mara mbili, WP 6100 DC Jaqline ambaye amejeruhiwa kichwani na H 3348 DC Armand ambaye amejeruhiwa kichwani na kifuani.
“Askari wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo tunaendelea kumtafuta dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Mwisho.

   

Sunday, August 24, 2014

PINGENI VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA

Na John Gagarini, Kibaha
WANAWAKE nchini wametakiwa kutokubali kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuhofia kutengwa na familia zao badala yake wawe watoa taarifa ili kuwadhibiti watu wanaoendeleza vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria na uvunjaji wa haki za binadamu.
Tabia ya kuficha ukatili wa kijinsia imesababisha wahusika kujikuta wakiathirika kutokana na vitendo hivyo ambavyo vimeshamiri kutokana na kuendelea kwa usiri ndani ya familia.
Hayo yalisema jana mjini Kibaha na mkurugenzi wa benki ya Wanawake Tanzania Magreth Chacha, wakati wa uzinduzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Pwani (PWMO).
Chacha alisema kuwa baadhi ya wanawake wamekuwa wakificha vitendo hivyo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wanaume wasiokuwa na huruma.
“Vitendo vya ukatili wa kijinsi vimekuwa vikifanywa ndani ya familia huku wanawake amabao ndiyo wahanga wa matukio hayo wamekuwa wakikaa kimya kuhofia kutengwa na familia zao jambo ambalo limesababisha vitendo hivi kuendelea,” alisema Chacha.
Alisema kuwa baadhi ya vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na watu wa karibu wa familia wakiwemo wanandoa na ndugu hali ambayo inasababisha taarifa hizo kufichwa huku walengwa wakiendelea kuathiriwa na vitendo hivyo viovu na vya ukatili.
“Baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na wanawake kupigwa, kutumikishwa kingono, kubakwa, watoto kubakwa, kulawitiwa, kufanyishwa kazi licha ya kuwa na umri mdogo na vitendo vingine vinavyokwenda kinyume cha sheria na haki za msingi za binadamu,” alisema Chacha.
Kwa upande wake mwenyekiti wa (PWMO) Mwamvua Mwinyi alisema kuwa lengo la kuanzishwa chama hicho mbali ya kutetea haki za waandishi wanawake pia ni kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
“Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku kutokana na baadhi ya wanajamii hususani wanawake kutokuwa katika kutoa taarifa za vitendo hivyo hali inayofanya kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia,” alisema Mwinyi.
Aliiomba jamii kwa kushirikiana na vyombo vya sheria kwa kutoaa taarifa juu ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili hususani maeneo ya pembezoni mwa miji, chama hicho kilianzishwa mwaka jana na kina jumla ya wanachama 15.

Mwisho.

MWANARIADHA AOMBA WAFADHILI AENDE KAMBINI KENYA

Na John Gagarini, Kibaha
MWANARIADHA John Mwandu wa mkoani Pwani amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia kwa hali na mali ili aweze kwenda kambini Eldoret nchini Kenya kwenye kambi aliyotokea mkimbiaji maarufu duniani David Rudisha wa nchi hiyo.
Rudisha ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 amekuwa akiwandaa vijana wengi wa nchi ya Kenya kwa ajili ya kuinua vipaji vya vijana ambapo Mwandu ameomba kujiunga na kambi hiyo na tayari amekubaliwa kujiunga nayo kwa ajili ya mazoezi yam bio za mita 1,500.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha Mwandu alisema kuwa tayari ameruhusiwa kwenda kwenye kambi hiyo kwa mwaka mmoja lengo kubwa likiwa ni kujiandaa na mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2016 yatakayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil.
 “Lengo langu la kwenda Kenya ni kujifunza mbinu wanazozitumia katika mchezo huo na kuwafanya kuwa mabingwa wa dunia wa riadha, kwani Mungu akipenda Olimpiki ijayo nitahakikisha naiwakilisha nchi yangu na kuiletea medali kwani inawezekana na diyo sababu ya kuanza maandalizi mapema,” alisema Mwandu.
Alisema anatarajia kwenda huko mwezi Desemba mwaka huu kwa ajili ya kambi hiyo ambayo ni nzuri na imetoa wakimbiaji wengi na ana uhakika akifanikiwa kwenda huko atarudi akiwa na mbinu nyingi za ukimbiaji ambazo anaamini zitamfanya aweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.
“Changamoto kubwa niliyonayo ni ukosefu wa fedha za kuweza kunipeleka kwenye kambi hiyo lakini naamini Mungu ataniwezesha kuweza kufanikisha kwenda kwenye kambi hiyo ambapo tayari nimeshafanya mawasiliano na Rudisha na ameahidi kunisaidia,” alisema Mwandu.
Aidha alisema kuwa Tanzania inashindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kutokana na wachezaji wanaochaguliwa hawana uwezo na huchaguliwa kwa upendeleo na wale wenye uwezo kuachwa hali ianayosababisha kutofanya vizuri.
Alibainisha kuwa aliwahi kushinda kwenye mbio za Afrika Mashariki chini ya miaka 17 akiwa anasoma Tegeta High School alikuwa wa pili, Tabora Marathon kilomita 21, mashindano ya Voda Com kilomita tano ambapo alishika nafasi ya pili na Ruaha Marathon kilomita sita ambapo alishika nafasi ya tatu.
Mwisho.

Saturday, August 23, 2014

PWANI WAZINDUA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI WANAWAKE (PWMO)

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha akiongea wakati wa uzinduzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani, kushoto ni mwenyekiti wa chama hicho Mwamvua Mwinyi na kulia ni mlezi wa chama Selina Koka. 


 mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Pwani Mwamvua Mwinyi akiongea wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika mjini Kibaha kulia ni mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Maragareth Chacha

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha katikati akionyesha hati ya busajili ya chama hicho kushoto ni mwenyekiti wa chama hicho Mwamvua Mwinyi na kulia mlezi wa chama Selina Koka.

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha katikati akiongea wakati wa uzinduzi wa chama cha waandishi wa wanawake mkoani Pwani

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha katikati akiakata utepe kama ishara ya uzinduzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoani Pwani kulia ni mlezi wa Selna Koka na kushoto mwenyekiti wa chama hicho Mwamvua Mwinyi

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha akikata keki wakati wa uzinduzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani 

 moja ya wadau wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Pwani akiongea kwenye uzinduzi wa chama hicho uliofanyika mjini Kibaha.

















 moja ya waandishi wa habari ambaye alikuwepo kwenye uzinduzi wa chama cha wandishi wa habari wanawake mkoani Pwani akichangia hoja 

 picha ikiwaonyesha viongozi na wadau wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoani Pwani wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa chama hicho

 wadau wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani wakiongea na mgeni rasmi wa uzinduzi wa chama hicho Margareth Chacha 





 wadau wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani wakibadilishana mawazo mara baada ya uzinduzi wa chama hicho.

WAETHIOPIA 48 WASHIKILIWA KWA KUINGIA NCHINI KINYEMELA

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia raia 48 wa nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini Kibaha Kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa watuhumiwa hao walitelekezwa vichakani.

Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 21 mwaka huu majira ya saa 7 usiku katika Kijiji cha Visakazi Ubena Zomozi tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Alisema kuwa Wethiopia hao waligunduliwa na askari Magereza wa Gereza la Ubena aitwaye Sospeter ambaye aliwakuta porini alipokuwa akifanya shughuli zake na kutoa taarifa polisi.

"Kati yao 11 wanaumwa na wamepelekwa kituo cha afya cha Chalinze kwa ajili ya matibabu baada ya kuonekana wakitapika baada ya kupewa chakula na walionekana wakiwa na hali mbaya ya kiafya huku wale wengine wakiwa wamehifadhiwa kwenye kituo cha polisi cha kiwilaya," alisema Kamanda Mwambalaswa.

Aidha alisema kuwa raia hao wa Ethiopia wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 40 na wanatarajiwa kukabidhiwa idara ya Uhamiaji kwa ajili ya taratibu zingine ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazowakabili.

Wakati huo huo mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya (25) na (28) amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamaba ya katani.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 22 mwaka huu majira ya saa 2 usiku Kijiji cha Kibiki kata ya Bwiringu Tarafa ya Chalinze.

"Mfanyakazi wa shambani wa mwenyekiti wa Kijiji hicho alimpa taarifa bosi wake aitwaye Ally Hussein (47) kuwa kuna mtu kajinyonga kwenye banda lake ambaye naye alitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo," alisema kamanada Mwambalaswa.

Aliongeza kuwa marehemu aliacha ujumbe amabo uliandikwa kwenye karatasi kuwa anawaachia dunia ili waishi miaka 120, hakuna mtu aliyekamatwa na polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

mwisho.  

Thursday, August 21, 2014

UTINGO AFA AJALINI OFISA WA OFISI YA DCI ANUSURIKA AJALINI

Na John Gagarini, Kibaha
UTINGO wa lori la mizigo Adam Rashid (28) mkazi wa Bwiringu kata ya Pera wilaya ya Bagamoyo amekufa baada ya lori alilokuwa akisafiria kugongana na lori lingine
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa malori hayo yaligongana uso kwa uso.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 19 mwaka huu majira ya saa 10 jioni eneo la Sweet Corner.
“Marehemu alikuwa kwenye gari namba T 650 BED aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa na na Ramadhan Mwarami (40) mkazi wa Bwiringu likiwa limebeba simenti likitokea Jijini Dar es Salaam kwenda Chalinze,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alisema kuwa lori alilokuwa amepanda marehemu liligongana na lori lenye namba za usajili T 853 APA aina ya Fuso ambalo lilikuwa likitokea mkoani Mbeya kwenda Dar es Salaam likiwa limebeba Mahindi likiendeshwa na Shan Iddi (28) mkazi wa Mwanga liligongana na lori hilo na kusababisha kifo hicho.
Aidha alisema kuwa dereva wa lori alilokuwa amepanda marehemu aliumia kidogo ambapo marehemu alifariki dunia wakati akipata matibabu kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani ya Tumbi.
Wakati huo huo Ofisa Mwandamizi wa jeshi hilo anayeshughulikia majalada ya kesi katika ofisi ya mkurugenzi wa makosa ya jinai  (DCI) Ilembo amenusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kugonga mti.
Akifafanua kuhusiana na tukio hilo Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa ofisa huyo alikuwa akitokea mkoani Iringa kikazi.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 20 mwaka huu majira ya saa 9 alfajiri eneo la Vigwaza kata ya Pera wilayani Bagamoyo.
“Chanzo cha ajali hiyo ni gari hilo la polisi kutaka kugongana uso kwa uso na gari lingine baada ya kulipita gari lililokuwa mbele yao na alipotokeza akakutana na hilo gari hali iliyofanya dereva akwepe kisha kuserereka kwenye mtaro na baadaye kugonga mti,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa gari hilo lilipasuka matairi na vioo vilivunjika ambapo gari lililohusika na tukio hilo halikuweza kusimama mara baada ya tukio hilo

Mwisho.