Thursday, June 26, 2025

DMI MISSION TANZANIA KUKABILI MIMBA NDOA ZA UTOTONI









SERIKALI imesema kuwa elimu ni nguzo ya kuwalinda watoto na ukatili ndoa na mimba za utotoni na kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza haki ya msingi ya mtoto kupata elimu.

Hayo yamesemwa na Madina Mussa ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakati wa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika iliyoandaliwa na DMI Mission Tanzania.

Mussa amesema kuwa ili kutekeleza mazingira rafiki kwa watoto waweze kupata haki hiyo ya msingi imejenga miundombinu mizuri ya watoto kujisomea.

"Katika kukabiliana na ukatili na ndoa za utotoni wazazi na walezi lazima washirikiane na serikali kuhakikisha haki za msingi za mtoto zinalindwa ikiwa ni pamoja na elimu, kumlinda na ukatili na kuishi katika mazingira mazuri kwani haki za mtoto zinaanzia nyumbani,"amesema Madina.

Awali Mkurugenzi wa DMI Mission Tanzania Sister Fathima Jacintha Ran amesema kuwa dhima ya siku hiyo ni Kupanga bajeti na kuweka bajeti kwa haki za watoto.

Ran amesema kuwa lengo ni kuhakikisha ustawi, elimu, na hatma njema za watoto ikiwa ni kukumbusha wajibu wa pamoja kuhakikisha watoto wa Afrika wanapata haki za msingi za elimu bora, huduma za afya, ulinzi na fursa ya kukua.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii kitengo cha watoto Halmashauri ya Mji Kibaha Hanifa Mruma amesema kuwa mradi ulioanzishwa na shirika hilo wa kupambana na mimba za utotoni ni mzuri na utasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwa upande wake moja ya wanufaika kwenye mradi huo wa Klabu za Wanawake Vijana Chiku Hamis amesema kuwa wanalishukuru shirika hilo kwa kuwapatia vifaa kwa ajili ya kutengeneza batiki na sabuni kwa ajili ya mafunzo ya utengenezaji vitu hivyo. 

Mradi huo wa kupunguza mimba za utotoni unatekelezwa kwenye Kata tatu za Pangani, Tumbi na Kongowe.

Wednesday, June 25, 2025

MATUMLA PROMOTION KUINUA VIPAJI VYA NGUMI KIBAHA

MATUMLA Promotion ya Kibaha imeandaa pambano la ngumi kati ya Abdully Said au Dully Bwengo na Rashid Hassan au Makali litakalopigwa kwenye baa ya UEFA Kongowe Kibaha Juni 28 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na pambano hilo ambalo litasindikizwa na mapambano mengine matano Mkurugenzi wa Matumla Promotion Abuu Matumla amesema kuwa maandalizi ya awali yamekamilika.

Matumla amesema kuwa maandalizi yakiwemo ya kuwalipa fedha za awali yameshafanyika na mabondia hao watakamilishiwa fedha zao baada ya pambano hilo kukamilika.

"Taratibu za awali zimekamilika ikiwa ni pamoja na malipo ya awali kwa mabondia, vibali na ulinzi vyote viko tayari kinachosubiriwa ni siku ya pambano hilo,"amesema Matumla.

Alisema kuwa malengo ya kuandaa mapambano hayo ni kuhamasisha mchezo huo kwa vijana wa Kibaha kwani mchezo huo ni ajira na kujenga afya bora na kuwaondoa vijana kwenye vitendo hatarishi.

"Tunataka tuinue mchezo wa ngumi Kibaha ambapo pia kutakuwa na pambano la wanawake ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha wanawake nao washiriki mchezo huo kwani hata wao wanauwezo wa kushiriki mchezo huo,"amesema Matumla.

Aidha alisema kuwa mbali ya mapambano hayo pia kutakuwa na burudani za muziki zikiongozwa na mkali wa Singeli Yuda Msaliti na waimbaji wengine wakali wa miondoko hiyo ya singeli.

"Nawaomba wapenzi wa mchezo wa ngumi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vya vijana wao ili kuwapa hamasa wapende mchezo huo ambao umekuwa ukipendwa na wengi,"amesema Matumla.

Thursday, June 19, 2025

DIWANI KATA YA MBWAWA JUDITH MLUGE AELEZA MAFANIKIO YA MIAKA 5

KATA ya Mbwawa Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani imeweza kufungua barabara 35 kwenye kata kupitia fedha za mapato ya ndani kiasi cha shilingi milioni 10 zilizotolewa kwenye kila kata.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio kwa kipindi cha miaka mitano Diwani aliyemaliza muda wake wa Kata hiyo Judith Mluge amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano maendeleo makubwa yamepatikana.

Mluge amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na upatikanaji wa huduma ya maji ambayo haikuwepo ikiwa ni asilimia 80, umeme unapatikana kwa asilimia 80 hadi 100.

"Kuhusu suala la afya kwenye zahanati za Kata hiyo kwa sasa dawa zinapatikana kwa asilimia 90 na ukarabati wa jengo la mama wajawazito liko mbioni kukamilika,"amesema Mluge.

Aidha amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto za mimba kwa wasichana wanaendelea na ujenzi wa bweni kwenye shule ya sekondari ya Mbwawa.

"Katika kipindi hicho tumefanikiwa kujenga ofisi ya kata pia nimekinunulia chama kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na Mungu akipenda ujenzi utaanza mwakani,"amesema Mluge.

Amesema kuwa kwa upande wa mikopo asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri fedha zilitolewa lakini baadhi wameshindwa kurejesha mikopo kiasi cha shilingi milioni 88.

"Changamoto tuliyoipata ni baadhi ya wakazi wanaokaa ngambo ya mto Ruvu ambapo tulitaka kujenga daraja lakini Mto huo umekuwa ukibadili mwelekeo,"amesema Mluge.

Ameongeza kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia fedha kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano.

Sunday, June 15, 2025

RIDHIWANI KIKWETE AKISHIRIKI MAADHIMISHO UELEWA KUHUSU ALBINO

Nimeshiriki shughuli za kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uelewa Kuhusu Albino.

Shughuli hii iliongozwa na Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa , Waziri Mkuu wa JMT , zilizofanyika katika viwanja wa Mwanga Mkoani Kigoma tarehe 13 Juni 2025.

Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka na utumika kukumbushana umuhimu wa kushirikisha wenye Ualbino, Haki zao, umuhimu wa serikali kuendelea kuangalia maslahi na ulinzi wao.  

Katika Shughuli ya Mwaka huu mtandao maalum wa kusajiri watu wenye Ulemavu unaowezesha usajiri kwa njia ya Elektronik hata kwenye maeneo yaliyo nje ya mtandao nao ulizinduliwa. 

Mfumo huo unawezesha taarifa za watu wenye ulemavu kuchukuliwa na kuchambuliwa ambapo zitaiwezesha serikali kupata taarifa za kina zitakazowezesha kupanga mipango ya maendeleo ikiwemo kuwashirikisha wenye Ulemavu.  


Waziri Mkuu wa JMT alitumia nafasi hiyo pia kutoa maagizo mahsusi kwa wakuu wa Mikoa na wadau waliokuwapo kuhusu matumizi sahihi ya mtandao huo na kuwashirikisha watu wenye Ulemavu kwa jumla katika shughuli mbalimbali ikiwemo Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadae Mwezi Oktoba mwaka huu uku akiwahamasisha watu wenye Ualbino nao kujitokeza kushiriki uchaguzi huo.

Friday, June 13, 2025

SUBIRA MGALU ATOA GARI KWA (UWT) BAGAMOYO

MBUNGE wa Mkoa wa Pwani Subira Mgalu ameupatia gari uongozi wa Jumuiya ya Wanawake CCM kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo aina ya Noah Mgalu amesema kuwa moja ya nadhiri aliyojiwekea kipindi cha nyuma ilikuwa ni kuhakikisha anainunulia chombo cha usafiri Jumuiya hiyo ili kurahisisha utendaji kazi.

Mgalu amesema kuwa ni vyema gari hilo likatumika kutafuta kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan huko kwenye matawi kwa kuwakumbusha wananchi kile kilichofanyika kwenye maeneo yao.

"Gari hili likatumiwe na Jumuiya zote za chama ikiwemo Wazazi na Vijana ili ziweze kufanikisha malengo ya chama chetu,"amesema Mgalu.

Akikabidhi gari hilo kwa Katibu wa  Wilaya ya Bagamoyo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mery Chatanda amempongeza  Mbunge huyo kwa jinsi ambavyo amekuwa akijitoa kwa Jumuiya hiyo.

Chatanda amewataka viongozi wa Bagamoyo kuhakikisha wanaitumia gari hiyo kwa makusudio yaliyokusudiwa ili kurahisisha shughuli za utendaji wa Jumuiya

Friday, June 6, 2025

CHOKALA AISHUKURU SERIKALI KUTOA BILIONI 4.2 ZA MAENDELEO KATA YA TUMBI

DIWANI wa Kata ya Tumbi Halmashauri ya Mji Kibaha Raymond Chokala amesema fedha zilizotolewa na serikali kiasi cha shilingi bilioni 4.2 kwa kipindi cha miaka mitano zimeleta maendeleo makubwa kwenye Kata hiyo.

Akizungumza kwenye Mkutano wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ilani kwa kipindi cha miaka mitano 2020-2025 kwa wanachama wa CCM na wananchi wa Mitaa ya Mwanalugali A na B Chokala amesema Kata hiyo imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Chokala amesema fedha hizo zimetumika vizuri kwenye sekta za elimu, afya, vikundi vya kiuchumi kupitia asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri, barabara, maji, umeme, kilimo na mifugo.

"Tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha hizo ambazo matokeo yake yameonekana kwani huduma zimeboreka licha ya changamoto chache ambazo zimeendelea kutatuliwa kulingana na bajeti inayopatikana,"amesema Chokala.

Amesema mafanikio hayo yametokana ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa baina ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka, wananchi, viongozi na watendaji wa serikali bila kusahau chama tawala CCM ambao ndiyo wasimamizi wa ilani.

WAKALA WA VIPIMO (WMA) YATAKA VIPIMO VIHAKIKIWE KILA MWAKA






WAKALA wa Vipimo Nchini (WMA) imetaka vipimo vya ujazo urefu na uzito wakati wa kupima bidhaa au kuhudumia wananchi lazima vihakikiwe kila baada ya miezi 12.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Kituo cha (WMA) kilichopo Misugusugu Wilayani Kibaha Mkoani Pwani Charles Mavunde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Mavunde amesema kuwa uhakiki huo ni takwa la kisheria ya vipimo sura 340 namba 19 ya mwaka 2002 inataka vipimo vinavyotumika kupima katika biashara au huduma nyingine za kijamii lazima vihakikiwe ndani ya muda huo.

Amesema kuwa sheria inatoa adhabu kwa mtu ambaye hata hakiki vifaa vinavyotumika katika kubebea au kupimia ambapo faini ni kati ya shilingi 100,000 hadi milioni 20 au kifungo jela miaka miwili.

"Kipimo chochote  kinachopima kuhudumia wananchi kinatakiwa  kufanyiwa uhakiki kila baada ya miezi 12 pia tunawapongeza wananchi kwa kuwa  na mwamko   kwenye uhakiki wa dira za maji kwani ni mkubwa," amesema Mavunde.

Amesema wanatarajia kuhakiki mita za maji  zaidi ya 87,000 kufikia mwishoni wa mwezi Juni 2025 ili kutambua usahihi wake kabla ya kwenda kufungwa kwa wateja na wamefanya zoezi la  uhakiki wa mita za umeme zaidi ya 5,500 za umeme mkubwa wa viwanda vya Mkoa wa Dar  es Salaam na mikoa mingine ili kuona kama zipo sahihi kulingana na matumizi viwandani. 

"Kwa upande wa dira za maji katika kipindi cha Julai  hadi Mei mwaka huu tayari wamehakiki dira  57,997 huku wakiwa na uwezo wa kuhakiki dira 100,000 kwa mwaka

Naye Ofisa  Vipimo  Mkuu Gaudence Gaspery amesema kuwa hivi sasa wanahakiki dira za  maji kwa kutumia mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuhakiki dira 10 kwa wakati mmoja.

Gaspery amesema kuwa baada ya kuhakikiwa na kuonekana zinafaa kwa matumizi huwekewa rakili yenye rangi ya chungwa  na ambazo zitagundulika zinahitaji kufanyiwa marekebisho hurekebishwa huku zile ambazo zitagundulika kwamba hazifai huteketezwa.