Na John Gagarini,
Kibaha
UMOJA wa Wafanyakazi
wa Viwanda na Biashara Tanzania (TUICO) kimewataka wanachama wake kukitumia
chama chao ili kujileta maendeleo.
Hayo yalisemwa hivi
karibuni mjini Kibaha na mwenyekiti wa chama hicho Betty Msimbe mara baada ya
uchaguzi wa chama hicho ambapo alifanikiwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho
Msimbe alisema kuwa
baada ya kupata nafasi hiyo ya kukiongoza chama hicho atahakikisha kuwa
wanachama wanapata maendeleo kwa kutumia chama chao ambacho kina lengo la
kuwaletea umoja na kutetea haki zao.
“Malengo yangu ni
kuongeza wingi wa wanachama, kutetea haki za wafanyakazi kuhakikisha mkoa
unavuka malengo yake ya kazi, haki na maslahi ya wafanyakazi sehemu za kazi,”
alisema Msimbe.
Alisema kuwa atafanya
mafunzo maeneo ya kazi ili wafanyakazi wapate elimu juu ya haki zao na elimu
kwa viongozi wa matawi kuhusu kutetea maslahi ya wafanyakazi ili waweze
kuboresha utendaji kazi wao.
“Kikubwa ninachokiomba
toka kwa wanachama na viongozi wenzangu ni ushirikiano ambao utasaidia
kukipeleka mbele chama na kufikia malengo ya kuhakikisha haki za wafanyakazi
zinapatikana,” alisema Msimbe.
Naye Naibu Katibu Mkuu
Msaidizi sekta ya biashara TUICO Taifa Peles Jonathan alisema kuwa atahakikisha
anasimamia haki na maslahi ya wafanyakazi kwa nchi nzima na kufanya umoja huo
kuwa na demokrasia ya uwakilishi wa kulinda na kutetea haki za wanachama.
Jonatahan alitoa wito kwa sekretarieti kufanya kazi kwa pamoja ili
chama kiweze kufikia malengo waliyojiwekea ili kuwaunganisha kwa pmoja wafanyakazi
ili waweze kuwajibika vizuri.
Katika uchaguzi huo
ambao ulisimamiwa na katibu wa chama hicho Kassim Matewele ambaye alimtangaza
Msimbe kuwa mshindi kwa kura (41) ambaye alimshinda Abimelick Magoma aliyepata
kura (18).
Kwenye nafasi ya
wajumbe wa kamati ya utendaji mkoa nafasi mbili nafasi ya Viwanda ni Hasan Kindagule aliyepata kura (35)
na Msaidizi wake Athuman Makonga kura (22), upande wa Biashara Shukuru Goso
aliyepata kura (32) na msaidizi wake Joyce Kalumuna kura (29).
Kwa upande wa Fedha
Furaha Mbwambo alishinda kwa kupata kura
(45) na msaidizi wake ni Zaituni Mtoro aliyepata kura (41), Huduma na ushauri
mshindi alikuwa ni Tumaini Kivuyo na msaidizi wake Kandrid Ngowi ambaye alipata
kura (35).
Waliochaguliwa Mkutano
Mkuu Kanda, Viwanda ni Masiku Serungwi aliyepata kura (35), biashara ni Kamatanda
Kamatanda aliyepata kura (57), Fedha Furaha Mbwambo aliyepata kura (60), kwa
upande wa huduma na ushauri mshindi alikuwa ni Kandrid Ngowi aliyepata kura (40).
Wajumbe wa mkutano
mkuu Taifa upande wa Viwanda mshindi ni
Athuman Makonga kura (59), Biashara ni Shukuru Ngoso kura (58), Fedha Zaituni
Mtoro kura (57) na huduma na Ushauri Margareth Chaleo kura ( 45).
Mwisho.
Na John
Gagarini, Mkuranga
KIJIJI
cha Mwanambaya Kata Mipeko wilaya ya Mkuranga kimewaomba wadau mbalimbali wa
maendeleo kuwasaidia kupata kiasi cha milioni 150 kwa ajili ya mradi wa kuvuta maji
kutoka kijiji jirani cha Kisemvule.
Akizungumza
na waandishi wa habari msemaji wa kijiji hicho Abubakar Sisaga alisema kuwa
wanakabiliwa na changamoto kubwa ya maji hivyo wameanza mchakato wa kuvuta maji
kutoka kijiji cha Kisemvule.
Sisaga alisema
kuwa awali walikuwana wazo la kuchimba visima lakini kutokana na uwezo kutokana
na gharama za uchimbaji kisima kuwa ni kubwa.
“Tunawaomba
wadau mbalimbali wa maendeleo wajitokeze kutusaidia tufanikishe zoezi hilo la
uvutaji maji ili kukabiliana na changamoto hiyo ya ukosefu wa maji kwani kwa
sasa wanatumia maji ya visima vifupi ambavyo kipindi cha kiangazi hukauka,” alisema
Sisaga.
Alisema kuwa
endapo watafanikiwa kupata maji yatawasaidia kuweza kutumia muda wao kwa ajili
ya kufanya shughuli za maendeleo tofauti na sasa wanatumia muda mwingi kuhangaika
na maji jambo ambalo ni changamoto kubwa.
“Mbali
ya changamoto ya maji kijiji kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni za
kawaida lakini wanakijiji wanajitahidi kuzitatua kadiri ya uwezo wao hivyo
tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutuunga mkono kwenye jitihada zetu za
kuleta maendeleo,” alisema Sisaga.
Aidha alisema
kuwa wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kwa pamoja waweze
kufanikiwa na kujikwamua na hali duni na kujiletea maendeleo.
Naye Mwenyekiti
wa kijiji hicho Leyla Chabruma alisema kuwa wana ushirikiano mkubwa na wadau wa
maendeleo ambao wanashirikiana na wananchi kwa ujumla hali inayoleta maendeleo
ndani ya kijiji hicho ambacho kinategemea mapato yake kwa mauzo ya bidhaa
mbalimbali ikiwemo mashamba, viwanja na vitu mbalimbali.
MWISHO.
Na John
Gagarini, Kibaha
BAADHI
ya wafanyabiashara na wasafiri wanaotumia kituo cha mabasi cha Maili Moja wameiomba
Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kuhakikisha wanatatua tatizo la taa kutowaka
kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na kuwasababishia usumbufu mkubwa wataumiaji wa
stendi hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari moja ya wafanyabiashara wanaofanya biashara kwenye
stendi hiyo nyakati za usiku Said Pengo alisema kuwa wamekuwa wakifanya
biashara kwenye mazingira magumu kwenye eneo hilo.
Pengo alisema
kuwa ukosefu wa taa hapo stendi ni changamoto kubwa sana inayowafanya kushindwa
kufanya biashara kwa vizuri kutokana na kuzingirwa na giza.
“Tunaiomba
Halmashauri yetu itusaidie tuweze kupatiwa huduma ya taa kwani taizo la ukosefu
wa taa linatusababishia usumbufu mkubwa na tunashindwa kufanya biashara zetu
kwa uhuru kutokana na giza linalokuwa linatanda,” alisema Pengo.
Alisema kuwa
ni hatari kwa hali ya usalama wao pamoja na wateja wanaotumia eneo hili la stendi
ya Maili Moja ambayo inatumiwa na watu wengi.
Kwa upande
wake mwenyekiti wa mtaa wa Maili Moja Chichi Mkongota alikiri juu ya ukosefu wa
umeme kwa kipindi hicho na kusema tayari alishatoa taarifa kwa mamlaka husika
juu ya tatizo hilo.
Mkongota
alisema kuwa alipotoa taarifa Halmashauri aliambiwa kuwa wanafanya utaratibu wa
kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kupata taa za muda
ili kukabiliana na tatizo hilo.
Naye Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Jenifa Omolo alisema kuwa tatizo lililopo ni
kubwa kidogo kwani taa zilizowekwa zimeharibika na wanafanya mchakato wa kupata
nyingine.
Omolo alisema
taa zote 16 zilizopo hapo stendi zimeharibika ambapo gharama zake pamoja na
kufungwa ni kiasi cha shilingi milioni 18 ambazo wanazitafuta kwa ajili ya kuzifunga.
“Tunafikiria
kwa sasa tufunge taa za kawaida kwani hizo zilizopo ziliharibika na si mara ya
kwanza kuzifunga kwani kila wakati zimekuwa zikiharibika,” alisema Omolo.
Aidha alisema
kuwa wanahangaika kutafuta fedha hizo ili kuondoa changamoto hiyo ambayo
imekuwa kero hata kwa wakala wanaokusanya ushuru wa stendi kutokana na usalama
kuwa mdogo.
Mwisho.