Na John Gagarini,
Kibaha
KITUO cha Afya cha
Mkoani wilayani Kibaha mkoani Pwani kinakabiliwa changamoto ukosefu wa
vitanda 40 kwenye wodi ya wajawazito
hali inayosababisha kitanda kimoja kulaliwa na akinamama wanne.
Hayo yalibainika
wakati wa ziara ya Jumuiya ya Wazazi ya Kibaha Mjini na kwenye kituo hicho
kilichopo mjini Kibaha kwenye maadhimisho ya wiki ya Jumuiya hiyo.
Ziara hiyo ya
kutembelea kituo hicho iliongozwa na mlezi wa Jumuiya ya Wazazi Selina Koka
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ambayo huambatana na shughuli mbalimbali za
Kijamaii.
Ofisa Muuguzi wa Kituo
hicho Prisca Nyambo alisema kuwa changamoto hiyo ni kubwa sana kwani vitanda
vilivyopo ni nane.
“Kama mnavyoona
vitanda viko nane tu kwa ajili ya mama wajawazito lakini idadi ya wajawazito
wanaokuja kwa mwezi ni 250 hadi 300 ambapo idadi hiyo ni kubwa sana kwa kituo
chetu,” alisema Nyambo.
Nyambo alisema kuwa
idadi ya wajawazito waliojifungua mwezi Januari walikuwa 342 na Februari
walikuwa 344 ambapo hadi Machi 31 mama wajawazito 300 walikuwa tayari
wameshajifungua.
“Idadi ya mama
wajawazito wanaohudumiwa hapa ni wengi sana na tunaomba wadau mbalimbali
wajitokeze kuchangia vitanda na magodoro yake ili tukabiliane na changamoto
hii,” alisema Nyambo.
Aidha alisema kuwa
vifo vya watoto kwa mwezi Januari ilikuwa ni tisa na mwezi Februari vilikuwa
vifo saba ambavyo vinatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na akinamama
hao kwenda wakiwa katika hatua za mwisho kabisa pamoja na matumizi ya dawa za
kienyeji za kuongeza uchungu.
Kwa upande wake mlezi
huyo wa Jumuiya ya Wazazi Selina Koka alisema kuwa anaguswa na hali hiyo ambapo
alitoa vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya kujifungulia zikiwemo dawa, pamba na
vifaa vy kukatia vitovu.
Selina alisema kuwa
changamoto zingine atazifanyia kazi kwa kushirikiana na mbunge wa Jimbo hilo
Silvestry Koka ili kuwaondoa adha wanayoipata akianamama wajawazito wanaokwenda
kujifungua kituoni hapo.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
MTOTO Joel Roman (3)
wa mtaa wa Ungindoni wilayani Kibaha mkoani Pwani amefariki dunia baada ya
kutumbukia kwenye kisima cha maji alipokuwa akicheza.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Geofrid Nombo
alisema kuwa mtoto huyo aliondoka nyumbani na kuelekea kisimani akiwa peke
yake.
Nombo alisema kuw atukio
hilo lilitokea Machi 30 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi baada ya mtoto huyo
kuondoka bila ya mama yake Marry Ngowi kujua.
“Alipoondoka mama yake
alimtafuta bila ya mafanikio ndipo alipowaambia majirani wenzake kisha kuanza
kumtafuta na ndipo walipokuta ndala zake zikiwa nje ya kisima huku yeye akiwa
amedumbukia kwenye kisiama hicho,” alisema Nombo.
Aidha alisema kuwa
mtoto huyo alikuwa akienda na mama yake kisimani hapo hivyo akawa amekariri
eneo hilo ambalo si mbali na nyumba waliyokuwa wakiishi.
“Kisima hicho cha maji
ni kirefu unaokaribia kufika futi tano na hutumiwa na watu wa eneo hilo kwa
ajili ya matumizi ya kufulia na kuogea wakati wa kiangazi lakini kwa bahati
mbaya kilikuwa wazi na hakikuzibwa juu,” alisema Nombo.
Aliongeza kuwa
kutokana na tukio hilo alimwamuru mmiliki wa kisima hicho ambaye alimtaja kwa
jina moja la Frank akifunike au akifukie ili kuepusha matukio kama hayo
yasiweze kutokea. Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Chalinze
KIJIJI cha Wafugaji
cha Mindutulieni kata ya Lugoba wilayani Bagamoyo kinapoteza ngombe zaidi ya
600 wanaokufa kutokana na ugonjwa wa Ndigana unaosababisha hasara ya shilingi
milioni 200 kila mwaka.
Akisoma risala ya
wanakijiji hao ofisa mtendaji Meisi Sokoroti kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze
Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara yake alisema kuwa ugonjwa huo umekuwa
unawatia hasara kubwa.
Sokoroti alisema kuwa
vifo vingi vinatokana na baadhi ya magonjwa ukiwemo huo ambao unawaletea ngombe
homa kali na kusababisha vifo .
“Hata hivyo baadhi ya
dawa zimekuwa na gharama kubwa ambapo dawa kama Butalex inauzwa kwa bei ya
shilingi 50,000 hali ambayo inawasababisha baadhi ya wafugaji kushindwa kumudu
gharama hiyo,” alisema Sokoroti.
Alisema kuwa tatizo
hilo la ngombe kufa kwa wingi lmedumu kwa kipindi cha miaka minne sasa ambapo
dawa mbalimbali za mifugo zimekuwa zikiuzwa kwa gharama kubwa sana.
“Ili kukabiliana na
changamoto hii tunaomba serikali ituletee dawa za mifugo zenye ruzuku ya
serikali ili kupunguza hasara hiyo,” alisema Sokoroti.
Aidha alisema kuwa ni
vyema serikali ikavitumia vyama vya wafugaji katika kuwapatia ruzuku ya dawa
kwani kwa sasa wauzaji wa dawa hizo wanawauzia kwa gharama kubwa mno.
Kwa upande wake
alisema kuwa kutokuwa na madawa ya ruzuku kumetokana na ufinyu wa bajeti toka
halmashauri lakini mara bajeti itakapokuwa nzuri wataweka ruzuku kwenye dawa
hizo.
Ridhiwani alisema kuwa
changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha ndiyo unachangia changamoto hiyo na kuwa
serikali inafanyia kazi suala hilo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa mabaraza ya
wafanyakazi katika sehemu za kazi ni vyombo muhimu katika kuongeza ufanisi wa
kazi ikiwa ni pamoja kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu maslahi ya
wafanyakazi taasisi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki
mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akifungua
mkutano wa Baraza la Wafanyakzi wa Ofisi ya Rais Tume ya Mipango.
Ndikilo alisema kuwa wajibu wa
mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri
na watumishi wanatambua wajibu wao na haki zao na wanazingatia maadili ya
utumishi wao ili kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi wenye tija, staha na
upendo.
“Hata kama kutakuwa na sera, sheria
na kanuni nzuri za kazi kama hakuna malenbgo ya pamoja na ushirikiano baina ya
mwajiri na mwajiriwa ni vigumu taasisi hiyo kuwa na tija hivyo mabaraza yana
wajibu wa kumshauri mwajiri ili kuleta tija na mashikamano wa pamoja,” alisema
Ndikilo.
Alisema kuwa si vizuri kwa watumishi
kutumia muda mwingi katika kudai maslahi mazuri zaidi kuliko kupima kiwango cha
utekelezaji wa wajibu wao wa kazi hivyo viongozi wa mabaraza wana wajibu
wa kuwahimiza wafanyakazi kutimiza wajibu wao ili kufikia malengo.
“Nyie mmepewa majukumu makubwa
kitaifa kama vile kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Taifa
na kufanya mapitio ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano
kuandaa mwongozo wa usimamizi wa utekelezaji wa umma na kukamilisha tafiti
mbalimbali zinazoharakisha maendeleo ya uchumi wan chi yetu na mahitaji ya
kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya maendeleo mwaka 2015,” alisema Ndikilo.
Kw upande wake mwenyekiti wa baraza
hilo Florence Mwanri alisema kuwa tume imeendelea kukabiliana na changamoto ya
upatikanaji wa fedha katika kutekeleza majukumu yake pamoja na kupata wataalamu
wenye weledi.
Mwanri ambaye pia ni Naibu Katibu
Mtendaji anayesimamia klasta ya huduma za jamii na idadi ya watu alisema kuwa
katika kuhakikisha watumishi wanafanya kazi iapasavyo wamekuwa wakiwajengea
uwezo kupitia mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi ili
kuwaongezea ufanisi katika utendaji kazi wao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKE wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha
Mjini Selina Koka anatarajia kuanzisha mfuko wa kutoa mikopo isiyokuwa na riba
kwa wajasiriamali wa jimbo hilo utakaojulikana kama Chap Chap wa kuwasaidia
waweze kuinua uchumi wao.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa
mkutano na wajasiriamali wanawake ambao wamewezeshwa mafunzo ya utengenezaji wa
bidhaa mbalimbali.
Selina alisema kuwa ameamua kufanya
hivyo kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wajasiriamali kwani taasisinyingi za
kifedha zinaweka riba kubwa kwenye mikopo.
“Wajasiriamali wengi wanashindwa
kuendeleza shughuli zao kutokana na riba kubwa wanazotozwa ambazo haziwezi
kuwakomboa kiuchumi lakini mfuko huu utakuwa hauwatozi riba yoyote,” alisema
Selina.
Alisema kuwa mkopo huo utaanzia kiasi
cha shilingi 50 hadi 200,000 lakini lengo ni kwa wale wenye biashara ndogo
kabisa.
“Tunatarajia kuwakopesha watu mmoja
mmoja na vikundi kwa kupitia kwa mabalozi, wenyeviti wa mitaa na madiwani
kwenye kata zote 11 za Kibaha Mjini bila ya kujali itikadi ya chama lengo ni
kuwainua wajasiriamali,” alisema Selina.
Aidha alisema hadi sasa tayari hadi
sasa wamevifikia vikundi 150 na kutumia gharama ya kiasi cha shilingi milioni
150.
Alibainisha kuwa mfuko huo unatrajia
kuanza kukopesha kabla ya mwishoni mwa mwaka huu na kusema kwa sasa wako kwenye
taratibu za kuandaa namna ya kutoa mikopo hiyo kisheria na kuwataka wale
watakaokopeshwa wawe waaminifu katika kurejesha.
Kwa upande wake Mbunge huyo alisema
kuwa anampongeza mkewe kwa kuweza kumsaidiaa katika kuwawezesha wajasiriamali
hususani wanawake.
Koka alisema kuwa yeye kwa
kushirikiana na mke wake watahakikisha malengo ya kuanzishwa mfuko huo
yanafikiwa ili kuwakwamua wanakibaha.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
VIONGOZI wa dini wametakiwa kuacha
kujiingiza kwenye siasa badala yake wawahudumie waumini wao katika masuala ya
kiroho.
Hayo yalisemwa na Mwangalizi mkuu wa
Kituo cha Maandiko cha (PMC) kilichopo Kibaha mkoani Pwani, Mchungaji Gervase
Masanja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mch Masanja alisema kuwa viongozi wa
dini kazi yao kubwa ni kuwaelekeza mambo muhimu ya kumjua Mungu pamoja na
kuishi kwa amani baina ya mtu na mtu na taifa kwa taifa.
“Viongozi wa dini tuna kazi kubwa
kwani waumini wanahitaji huduma kubwa za kiroho hivyo haipendezi kujiingiza
kwenye siasa na tudumishe amani iliyopo hapa nchini,” alisema Mch Masanja.
Alisema kuwa kazi ya siasa ni vema
ikaendeshwa na wanasiasa wenyewe huku viongozi wa dini wakiwa ni wapatanishi na
walinda amani ya nchi.
“Pia tusisahau kushiriki kwenye
masuala makubwa yaliyopo mbele yetu yakiwemo kujiandikisha kwenye Daftari la
wapiga kura, kura za maoni ya katiba inayopendekezwa na kushiriki kwenye
uchaguzi mkuu mwezi Oktoba,” alisema Mch Masanja.
Aidha alisema anawaomba wakristo na
wananchi kujitokeza kwa wingi katika upigaji wa kura ya maoni ya katiba
inayopendekezwa na si kususia.
“Kuipigia kura katiba inayopendekezwa
ni haki yako ya msingi hivyo mwananchi hupaswi kuisusia na kura utakayopiga ni
siri yako lakini si vema kutopiga kura hiyo kwa mustakbali wan chi yetu,”
alisema Mch Masanja.
Mwisho.