Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa ili nchi iweze kuendelea watendaji na mamalaka
zikiwemo halmashauri hapa nchini zimetakiwa kuwa na uwazi na uwajibikaji ili
kuwaletea wananchi maendeleo.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mkuu wa shule kuu ya uandishi
wa habari ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt Herbert Makoye wakati akifungua mafunzo ya ufuatiliaji wa
rasilimali za Umma (PETS) kwa waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vya
Business Times na Mlimani.
Dkt Makoye alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa
wananchi juu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma zinazotolewa na serikali hivyo
kusababisha huduma muhimu za kijamii.
“Tumeona tufanya mafunzo haya kwa lengo la kuwajengea uwezo
waandishi wa habari juu ya kuweza kuandika taarifa juu ya matumizi ya fedha
hizo ambazo madhumuni yake ni kuwapunguzia kero wananchi hivyo watapata taarisa
sahihi,” alisema Dkt Makoye.
Alisema bila ya uwazi kutakuwa hakuna uwajibikaji hali ambayo
itasababisha kutokuwa na maendeleo ya haraka ya mwananchi kujikwamu na hali
ngumu ya kimaisha.
“Kupitia mafunzo haya waandishi wanapaswa kuyatumia kwa lengo
la kuwapatia wananchi taarifa sahihi juu ya michakato mbalimbali ya matumizi ya
fedha hizo na zitasaidia watendaji kuwajibika kwani watakuwa na hofu ya kufuja fedha
kwani kuna vyombo vinavyowafuatilia,” alisema Dkt Makoye.
Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa gazeti la Majira Bw Imma
Mbuguni alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi katika ufuatiliaji wa
rasilimali za umma zikiwemo fedha zinazotolewa na serikali kwa maendeleo ya
wananchi.
Bw Mbuguni alisema pia mafunzo hayo yatasaidia kuibua
mijadala mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya fedha za Umma ambapo baadhi ya
watendaji wanaonekana kutozitumia kwa malengo yaliyowekwa au mahitaji ya
wananchi.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa pamoja na Shule Kuu ya Uandishi
wa Habari ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na kampuni ya
Business Times kutokana na ufadhili wa Mfuko wa Ufadhili wa Vyombo vya Habari
(TMF).
Mwisho.