Na
John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI
ya Mji Kibaha mkoani Pwani imesema kuwa haijarudisha hazina fedha za ujenzi wa
barabara kiasi cha shilingi milioni 700 bali fedha hizo zilichelewa kutumika
kutokana na makandarasi kukiuka taratibu za ujenzi.
Hayo
yalisemwa jana na mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo Adhudadi Mkomambo,
kwenye kikao cha madiwani kilichofanyika mjini Kibaha.
Mkomambo
alisema kuwa kwenye kikao cha bunge kilichopita waziri wa ujenzi John Magufuli
alisema kuwa mji huo umeshindwa kutumia fedha hizo kwanini waombe fedha
nyingine.
“Licha
ya Halmashauri kupata mafanikio makubwa kwa mwaka uliopita ikiwa ni pamoja na
kuweza kukusanya fedha kiasi cha zaidi ya bilioni moja changamoto kubwa ni ya
makandarasi wa barabara kushindwa kazi hivyo kushindwa kulipwa kwa wakati,”
alisema Mkomambo.
Alisema
kuwa matatizo mengi ya kihandisi kwani baadhi yao walioomba kazi hawajasajiliwa na wengine
wametumia hati feki kupata kazi hizo licha ya kwamba mchakato wa kuwapata
ulizingatia taratibu za kihandisi.
“Fedha
hizi tunatarajia ifikapo Septemba 30 tutakuwa tumezifanyia kazi fedha hizo ili
kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa ya kuboresha barabara za mji wetu
ambao kwa sasa ndiyo unajengeka,” alisema Mkomambo.
Aidha
alisema kuwa fedha hizo zipo na hazijarudishwa hazina tutahakikisha kuwa
halmashauri inafanya tathmini ya hali ya juu kuwapata makandarasi bora ili
kuachana na wakandarasi feki.
Aliwataka
watendaji wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi
ili waweze kuwaletea maendeleo kwani bila ya wao kuwa na uchungu hawataweza
kuwafikisha kwenye maisha bora.
Mwisho.
Na
John Gagarini, Bagamoyo
MEYA
wa Mji wa Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu amewataka waumini wa dini za
Kikristo na Kiislamu mkoani Pwani waungane katika kipindi hichi cha mfungo
kuiombea nchi ili isiingie kwenye mgawanyiko wa kiimani.
Aliyasema
hayo wakati alipokuwa akitoa chakula cha futari kwenye shule za sekondari za
Kimange, Changarikwa, Lugoba, Wazee wa CCM wa kata ya Lugoba na kata ya Miono
wilayani humo.
Sharifu
alisema kuwa viongozi na waumini wa dini wana nafasi kubwa ya kuweza
kuhakikisha kuwa nchi ina amani kwa kufanya maombi ikiwa ni pamoja na kufunga.
“Nawaombeni
waumini na viongozi wa dini zote kuliombea Taifa ili lisiingie kwenye machafuko
ambayo yatasabisha amani kutoweka hivyo watu na nchi kushindwa kufanya shughuli
za maendeleo,” alisema Sharifu.
Meya
huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo alisema
kuwa mbali ya viongozi wa dini na waumini kufanya maombi maalumu pia viongozi
na wafuasi wa vyama vya siasa nao wanapaswa kutochochea uvunjifu wa amani.
“Endapo
nchi itaingia kwenye machafuko hakuna kitakachoweza kufanyika kwani watu
hawataweza kusali hata hao wanasiasa hawataweza kufanya siasa hivyo ni vema
wanasiasa nao wakafanya siasa ambazo hazitaleta chuki na kuwagawa watu kutokana
na itikadi za dini na siasa,” alisema Sharifu.
Aidha
alisema kuwa watu wanapaswa kuheshimu mamlaka zilizopo na kushangazwa na baadhi
ya wanasiasa kuchochea vurugu hali ambayo si nzuri kwani vita ikitokea athari
hazitaangalia chama, dini wala rangi.
Aliwataka
Watanzania kutokubali kugawanywa kwani endapo watakubali hali hiyo kuingia
nchini itasababisha watu waishi kwenye hali ngumu na kushindwa kuwa na amani
ambayo iko kwa sasa.
Mwisho.
Na
John Gagarini, Kisarawe
BAADHI
ya wakazi kutoka mikoa mbalimbali wamevamia msitu wa hifadhi wa Ruvu Kusini na
kufanya uharibifu mkubwa kwa kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na mbao kwenye
maeneo mbalimbali ya vijiji kikiwemo Kijiji cha Mtamba wilaya ya Kisarawe
mkoani Pwani.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwenye kijiji hicho wakati wa operesheni ya kuwaondoa
wavamizi hao, ofisa wa kampeni ya (Mama Misitu) kupitia shirika lisilo la Kiserikali
la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), kwenye hifadhi ya Ruvu Kusini
Yahaya Mtonda amesema kuwa licha ya watu hao kufukuzwa lakini bado wanaenbdelea
na uharibifu.
Mtonda
amesema kuwa Mama Misitu ni kampeni yenye lengo la kuzuia na kupunguza uvunaji
haramu wa mazao ya misitu na kuboresha utawala bora kwenye sekta ya misitu ili
jamii ipate manufaa na misitu hiyo.
Amesema
kuwa kweli hali ilikuwa mbaya kabla ya mradi huo wa miaka mitano kuanza kwani
watu hao wamekuwa wakiwaondoa lakini bado wanarudi ambapo wamnevamia msitu huu
na kukaa kwenye vijiji vilivyo jirani na hifadhi na kufanya uharibifu mkubwa
licha ya kuwachukulia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaifisha vyombo
vyao vya usafiri kama vile magari, pikipiki na baiskeli na kuwapiga faini au vipiga
mnada lakini bado wanendelea.
Amesema
kuwa watu hao wamevamia kijiji hicho kwenye eneo linaloitwa kwa Bibi Hindu na
kujifanya wanaishi hapo ambapo ni jirani kabisa na hifadhi hiyo ambapo
wakishafanya shughuli za kuharibu misitu hurudi kijijini ili kuficha kile
wanachokifanya.
Aidha
amesema kampeni ya Mama Misitu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa licha ya
changamoto hizo za wavamizi kurejea mara kwa mara, lakini wameweza kuwawezesha
wanajamii kuanzisha kamati za uhifadhi misitu ambapo endapo watakamata mali za
wahalifu hao asilimia 20 ya vifaa vinavyokamatwa mara baada ya kuuzwa kwa nji ya
mnada hubaki kijijini.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Nasoro Mzeru amesema kuwa watu hao
walipewa notisi ya kuondoka miezi mili iliyopita lakini wanaonekana kukaidi
agizo hilo la
serikali.
Mzeru
amesema kuwa eneo hilo
lilitengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu lakini watu hawea walivamia na
kufanya makazi huku wakijihusisha na uharibifu wa msitu huo wa Ruvu Kusini na
kila wakati wanaondolewa lakini wanarudi.
Mwenyekiti
huyo amesema mbali ya kuharibu misitu pia wamekuwa wakijihusisha na vitendo
viovu vikiwemo vya ubakaji, uvutaji bangi, uuzaji wa pombe haramu na wanawake
kufanyabiashara za ngono jambo ambalo ni hatari na eneo hili ni hatarishi kwani
watu hao licha ya kuitwa waishi kijijini wamekataa na kukaa kwenye eneo hilo la
kwa Bibi Hindu,” alisema Mzeru.
Aidha
amesema kuwa makazi ya yalichomwa moto hivi karibuni kwa lengo la kuwaondoa na
kutakiwa kuondoka ambapo baadhi yao
waliondoka lakini wengine walirudi na kuendelea na uharibifu wa msitu.
Mradi
huo wa Mama Misitu kwenye hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kusini una ukubwa wa Hekta
35,000 unaofadhiliwa na nchi za Finland na Norway, ulipewa jina hilo kwa lengo
la kumuenzi mwanamke kwani endapo misitu itaharibiwa mwathirika mkuu ni
mwanamke, na unatekelezwa kwenye vijiji 16 kwenye wilaya za Kibaha na Kisarawe
ambapo hadi mwaka 2010 zaidi ya 40 za msitu huo ziliharibiwa na endapo udhibiti
hautakuwepo msitu huo utatoweka ifikapo 2025
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt Abdala Kigoda amesema kuwa
uchumi wa Tanzania
hauwezi kutegemea kilimo pekee bali viwanda ndivyo vinaweza kuinua uchumi na
kuifanya nchi kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
Ameyasema hayo kwenye Mtaa wa Zegereni wilayani Kibaha
mkoani Pwani, wakati akizindua kiwanda cha kutengenezea Jipsamu cha kampuni
kutoka China ijulukanayo kama Sun Shine Gypsum Limited Group na kusema kuwa
viwanda ndiyo moja ya vyanzo vya nchi kupata fedha nyingi.
Dkt Kigoda amesema kuwa hata nchi zilizoendela zilianza na
viwanda vidogo na viwanda vya kati hadi vikafikia kuwa na utajiri mkubwa
walionao sasa ambapo China
ni moja wapo ya nchi zilizoanza kwa utaratibu huo lakini kwa sasa iko mbali kiuchumi.
Waziri amesema kuwa Viwanda vinachangia asilimia 30 ya pato
la Taifa huku asilimia 40 ya wananchi wakiwa wameajiriwa kwenye sekta ya
viwanda hapa nchini na kufanya uchumi kutegemewa kwa kiasi kikubwa kupitia
sekta hiyo ambayo kwa sasa inaendelea kukua licha ya baadhi ya watu wakidai
kuwa eti Tanzania
haina viwanda vingi jambo ambalo si kweli.
Aidha amesema kuwa hata wajasiriamali wa tanzania wanaweza kuungana kujenga viwanda kama hivi ambavyo ni vya daraja la kati hasa ikizingatiwa
malighafi za kutengenezea bidhaa hiyo zote zinapatikana hapa hapa nchini.
Ameongeza kuwa wamiliki hao wanapaswa kutoa kipaumbele cha
ajira kwa wakazi wa Kibaha ili nao wafaidi matunda ya uwepo wa kiwanda hicho na
wasaidie huduma za kijamii na kujenga mahusiano mazuri pia wazingatie viwango
ili bidhaa hizo ziweze kuwa na soko ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry
Koka ameipongeza kampuni hiyo na kusema kuwa dhana ya kurudisha uchumi kwa
wananchi sasa imeanza kuonekana kwani baadhi ya wakazi wa hapa wamepata ujuzi
na ajira.
Koka amesema kuwa kampuni hiyo imezingatia suala la ajira
kwani hadi sasa watu 60 wamepata ajira huku baadhi yao wakipewa kazi za umeneja na si kuwa zile
za ufagizi tu kwani hayo ndiyo yanayopaswa kufanywa na viwanda vingine ili
kuweka usawa wa utendaji kazi
Amebainisha kuwa Mji uliamua eneo hilo
la Kata ya Visiga kuwa eneo la viwanda hivyo wajasiriamali na watu mbalimbali
wana nafasi kubwa ya kuweka viwanda vyao hapo na si kung'ang'ania kujenga Dar es Salaam pekee ambapo hadi sasa eneo hilo tayari kuna viwanda vinne vingine vikiwa
ni cha kusafishia mafuta, madini na nondo, vimeshajengwa.
Kiwanda hicho kilianzishwa mwaka jana na kina thamani ya
dola za Kimarekani milioni tatu na kimeajiri watu 60 na tayari kimeanza
uzalishaji ambapo bidhaa zake zinauzwa ndani na nje ya nchi.
mwisho.