Friday, December 6, 2024

HALMASHAURI YA MJI KIBAHA KUZINDUA KIBAHA SHOPPING MALL

HALMASHAURI ya Mji Kibaha inatarajia kuzindua soko la kisasa (Kibaha Shopping Mall) lililogharimu kiasi cha shilingi bilioni nane ambalo litatoa fursa za wananchi kukuza kipato chao kwa kufanya biashara mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha ofisa masoko wa soko hilo la kisasa Sabrina Kikoti amesema kuwa soko hilo limejengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu na Halmashauri ya Mji Kibaha.

Kikoti amesema kuwa huduma zote zitapatikana ambaapo bidhaa zitauzwa kwa bei ya jumla na rejareja litafungua fursa kwa wananchi wa Kibaha na litatoa ajira na kufufua uchumi wa Kibaha. 

“Mgeni rasmi kwenye ufunguzi huo anatarajiwa kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John ambapo wananchi wa Kibaha wtaanufaika kwani walikuwa wakifuata bidhaa Jijini Dar es Salaam huku wengine watapata ajira kupitia biashara,”amesema Kikoti. 

Naye ofisa mapato wa Halmashauri ya Mji Kibaha Luna Kakuru amesema kuwa jengo hilo la kibiashara lina maduka 74 ya biashara ambapo bidhaa zitauzwa kwa bei ya jumla na rejareja.

 

Kakuru amesema kuwa maratajio yao ni kukusanya kiasi cha shilingi milioni 660 kwa mwaka ambapo mapato yataendelea kuongezeka kutokana na kodi mbalimbali zitakazokuwa zikitozwa hapo ambapo wanapangisha mita za mraba kiasi cha shilingi 15,000.

 

Nao baadhi ya wafanyabiashara Charles Chandika amesema kuwa ametumi fursa kupangisha hapo ili aweze kufanyabiashara ambapo pia litachangamsha Mji wa Kibaha ambapo lengo ni kuhakikisha wanatoa huduma bora na za kisasa na kuwafikia wananchi.

 

Chandika amesema kuwa bei watakayouza ni rafiki na hawatakuwa na sababu ya kwenda mbali kuzifuata Jijini Dar es Salaam kwani wataokoa muda na gharama za nauli kufuata bidhaa mbali.  

 

Naye Lydia Vicent ambaye amenufaika kwa kuchangamkia fursa ambapo alikosa sehemu ya kufanyia biashara na wanampongeza Rais kwa kuwapatia fursa wafanyabiashara ambapo fedha zilizotolewa na serikali zimefanikisha kujenga soko hilo.

 

Vicent amesema kuwa soko hilo litafungua fursa za kibiashara kwa wananchi wengi ambapo ni sehemu ya kukuza uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na Watanzania kwa ujumla.    

 

     

 

    

WAOMBA MABORESHO YA BARABARA YA MOROGORO KUPUNGUZA FOLENI KIBAHA

WAJUMBE wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani wameiomba serikali kuhakikisha uboreshaji wa Barabara ya Morogoro ili kupunguza msongamano uliopo kwa sasa ambapo asilimia 85 ya magari kwenda nje ya Dar es Salaam yanapita barabara hiyo.

Wakizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika Mjini Kibaha Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa kwa sasa kuemkuwa na foleni kubwa sana ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kwa magari yanayotumia barabara hiyo.

Koka alisema kuwa mipango inayotarajiwa kufanywa ifanyike kwa haraka ili kukabiliana na hali hiyo ambayo imekuwa ni kero kubwa kwa watumiaji kwani foleni imekuw ani kubwa sana na kusababisha watu kushindwa kwenda kwa wakati kwenye shughuli zao.

“Tunashauri mpango wa uboreshaji uendane na ukuaji wa Mji wa Pangani na eneo la Shirika la Elimu (KEC) ni maeneo ambayo yatakuwa na uboreshaji mkubwa hivyo uboreshaji huo uzingatie maeneo hayo kupitia mpango endelevu wa uboreshaji barabara,”alisema Koka.

Alisema kuwa katika mpango endelevu huo wa uboreshaji barabara pia uangalie kwa kuwa na barabara za juu na vivuko au madaraja kwa ajili ya watu kuvuka na eneo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi ni kuanzia Mizani ya zamani hadi Kwamathias.

“Pale Picha ya Ndege na Mkuza nako ni kipaumbele kwa kuwa ndiyo kwenye maungio napo papewe kipaumbele wakati wa mpango endelevu wa uboreshaji wa barabara zetu kwani mji wetu kwa sasa umekuwa na magari ni mengi sana,”alisema Koka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Muharami Mkenge alisema kuwa barabara hiyo ya Morogoro ni changamoto kubwa sana hivyo inapaswa iangaliwe kwa ukaribu ili kupunguza kero hiyo ya msongamano wa magari ili wasafiri waweze kwenda safari zao kwa wakati.

Mkenge alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo hivyo kuna haja ya kuboresha barabara zingine ikiwa ni pamoja na ile ya Makofia Wilayani Bagamoyo hadi Mlandizi Wilayani Kibaha yenye urefu wa kilometa 35 itasaidia kupunguza msongamano kwani magari yanaweza kupita huko kama barabara ya Morogoro kuna foleni kubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa kuwe na maombi maalumu ambayo yatakuwa ni vipaumbele kwa ajili ya kuwaondolea kero ya wananchi kwani barabara ni kiungo muhimu cha maendeleo.

Kunenge alisema kuwa mahitaji ya barabara kwa Mkoa ni makubwa lakini changamoto iliyopo ni upatikanaji wa fedha hivyo ni vema kukawa na vipaumbele ili vianze na baadaye kufuatiwa na mahitaji mengine.

Kwa upande wake meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage amesema mpango uliopo ni uboreshaji wa barabara za zamani na upanuzi wa maeneo yenye msongamano wa magari.

Mwambage amesema kuwa kwa upande wa barabara ya zamani ya kuanzia Sheli mpaka DAWASA wamefanya kazi za matengenezo kwa kuchonga barabara, kuweka kifusi cha udongo na changarawe,upanuzi wa maingilio yote mwanzo na mwisho ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa makalavati yaliyopo, kujenga mitaro ya zege na kuchimba mitaro ya kawaida.

Amesema katika kipande cha Picha ya Ndege-Msufini kazi zilizofanyika ni pamoja na kuchonga barabara, kuweka kifusi cha changarawe na kujenga makalavati.

Aidha ukarabati wa Barabara ya zamani ya Morogoro umefanyika kuanzia Mlandizi-Ruvu JKT, TRC Relini-Mzunguko wa Vigwaza na upanuzi wa maeneo ya miji kwa Barabara kuu ya Morogoro umefanyika eneo la Kwa Mwarabu mita 350, TANESCO mita 290 na Chalinze mita 850 ili kupunguza msongamano kwa eneo la kuingia mji wa Chalinze.

Mwisho.

MAFIA WALILIA BOTI ZA MWENDOKASI


WANANCHI wa Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani wameiomba Serikali kuwapatia huduma ya boti zinzokwenda haraka badala ya kutumia boti ambazo hutumia masaa mengi baharini ambapo kwa sasa usafiri wa baharini umerahisishwa kama ilivyo kwa wasafiri wanaoenda Zanzibar.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafia Juma Ally kwenye kikao cha bodi ya barabara ya Mkoa wa Pwani kilichofanyika Mjini Kibaha.

Ally lisema kuwa wanaishukuru serikali kuwapatia boti kwenda Mafia lakini boti hiyo hutumia masaa mengi ambapo ni kati ya masaa sita au saba tofauti na boti zinazoenda Zanzibar ambazo hutumia nusu ya masaa hayo.

“Usafiri tunaotumia unasaidia lakini ungeboreshwa kwa kupata boti ambazo zinatumia injini badala ya hizoi ambazo zinatumia kasi ili tusafiri kwa haraka tofauti na ilivyosasa,”alisema Ally.

Alisema kuwa boti hizo za sasa zinatumia pangaboi lakini tunashauri tupatiwe zile ambazo ni jeti ambazo mwendo wake ni wa kasi.

“Tukipata boti za mwendo kasi hata watalii wataongezeka lakini kwa sasa wtaalii ni wachache kwani tunapata watalii 10,000 lakini usafiri huo ukipatikana wataongezeka na tutakuwa na watalii wengi hivyo kuongeza mapato ya Halmashauri yetu,”alisema Ally.

Aidha alisema kuwa kutokana na kutokuwa na boti hizo za mwendokasi kabla ya kufanya safari lazima kuwe na maji mengi jambo ambalo ni changamoto kubwa lakini ingekuwa boti za kasi zingefanya safari tu bila ya kusubiri maji kuwa mengi.

“Ombi letu lingine tunaomba Bandari ya Kisiju Wilayani Mkuranga iboreshwe ili itumika kwani kula ni rahisi tofauti na Bandari ya Nyamisati iliyopo Wilayani Kibiti hilo nalo tunaomba lifanyiwe kazi kikubwa ni kurahisisha usafiri wa wakazi wa Mafia,”alisema Ally.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa pwani akitoa ushauri alisema kuwa jambo kubwa ni kuangalia maslahi mapana ya wananchi hivyo miradi mbalimbali izingatie vipaumbele kutokana na maeneo na vitakavyoendana na vipaumbele vya Rais.

Kunenge alisema kuwa wajumbe wanapaswa kuangalia vipaumbele kwa uhalisia kwani fedha ni ndogo hasa ikizingatiwa nchi ilfanya uchaguzi ambao umetumia gharama kubwa hivyo kuwe na vipaumbele katika utekelezeji wa miradi.


TARURA PWANI

Thursday, December 5, 2024

*LYDENGE AZURU GEREZA LA KIGONGONI* 


Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Sophia Lydenge amewaongoza askari wa kike toka Wilaya hiyo kutoa msaada kwa wafungwa wanawake wanaotumikia adhabu ya kifungo kwa makosa mbalimbali kwenye gereza la Kilimo Kigongoni Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani. 

Lydenge ameeleza wakiwa  kwenye maadhimisho ya kupinga siku 16 za ukatili wa wanawake na wasichana,  wana mtandao wa Polisi wanawake Wilaya ya Kipolisi Chalinze waliona wafike kwenye gereza la Kigongoni ili kutoa msaada huo kwa wanawake wanaotumikia adhabu ya kifungo wakiwa na imani kuwa watabadilika kimatendo na kuwa mfano wa kuigwa watakapokuwa wamemaliza kutumikia adhabu zao. 

Miongoni mwa vitu vilivyokabidhiwa leo ikiwa ni mwendelezo wa kusaidia makundi yenye uhitaji kwenye Jamii ni pamoja na Cherehani moja, mafuta ya kupaka, taulo za kike pamoja na sabuni za kufulia na kuogea.

Aidha, Lydenge ameomba uongozi wa gereza kupokea Cherehani hiyo na ikatumike kwenye kuwafundisha wanawake waliopo gerezani ili wakitoka wawe na ujuzi wa kazi ya kufanya.

Akipokea msaada huo Mrakibu Msaidizi wa Magereza Kaziro Ambros kwa niaba ya Mkuu wa gereza hilo amewashuku mtandao mtandao wa Polisi wanawake Wilaya ya Kipolisi Chalinze na kuahidi Cherehani iliyopokewa itatumika kwa lengo kusudiwa kwa kutumika kama nyenzo ya kufundishia ushonaji kwa wafungwa wanawake ili kuweza kuwajenge uwezo kwenye eneo la ushonaji.

Monday, December 2, 2024

MAONYESHO YA WIKI YA UWEKEZAJI NA BIASHARA PWANI KUFANYIKA MAILI MOJA KIBAHA KUANZIA DESEMBA 16 HADI 20 MWAKA HUU

JUMLA ya watu 25,000 wanatarajiwa kuhudhuria maonyesho ya wiki ya Uwekezaji na Biashara yatakayoshirikisha washiriki 550 yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 16 hadi 20 mwaka huu.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Kunenge amesema kuwa maonyesho hayo yatafunguliwa Desemba 17 na yatafanyika kwenye viwanja vya iliyokuwa stendi ya zamani ya Maili Moja Kibaha.

"Maonyesho hayo ni ya nne kufanyika ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2018, 2019, 2022 na mwaka huu ambapo watu watatoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa wakati wa maonyesho watu watakaohudhuria watapata fursa za kujifunza, kuona fursa zilizopo, kuona teknolojia gani zinatumika na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika Biashara na kujipatia bidhaa.

Ameongeza kuwa mkoa umejipanga vizuri hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa una viwanda 1,553 na tangu Rais aingie madarakani viwanda vikubwa ni 78.

Friday, November 29, 2024

WENYEVITI WAAPISHWA WATAKIWA WASIUZE ARDHI


WENYEVITI wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa hivi karibuni kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa wasijihusishe na uuzaji ardhi ili kuepukana na migogoro ya ardhi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa wakati wa kuapishwa kwa wenyeviti hao pamoja na wajumbe wa Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri hiyo.

Shemwelekwa alisema kuwa wenyeviti hao waachane na masuala ya uuzaji ardhi kwani inayohusika ni Halmashauri kwani baadhi yao walikuwa wakijihusisha na uuzaji ardhi.

"Msijihusishe na masuala ya uuzaji ardhi pia itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi hivyo wao wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo,"alisema Shemwelekwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mussa Ndomba alisema kuwa wenyeviti wasifanye vita na watendaji wa mitaa kama kuna jambo waangalie namna ya kutatua.

Ndomba alisema kuwa wale ni wataalamu wasigombane nao kwani hawatafanya kazi vizuri na wanaweza kuwakwamisha kwani wanambinu nyingi wanaweza kuwakwamisha kwenye majukumu yao hivyo washirikiane nao na kama kuna changamoto wakae nao chini ili kutatua na kurekebishana.

"Masuala ya mihuri nimelisikia wananchi wapate huduma bure bila ya gharama na kuhudumiwa haambiwi toa fedha sijui ya nini anatakiwa apate huduma bora na kwa wakati,"alisema Ndomba.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa jukumu lao kubwa kurudisha deni kwa wananchi ambao wamewakopesha kura walizowapigia na wanatakiwa kuwatumikia na wasinunue bali wapewe huduma bure.

Koka alisema kuwa wanapaswa kuwatumikia na kuwashirikisha kwenye vikao pia waitishe mikutano na kuwapatia mrejesho wa masuala mbalimbali na kutekeleza mipango wanayoiweka.

Mbunge wa Wafanyakazi Mkoa wa Pwani Dk Alice Kaijage alisema kuwa wananchi wamefanya jambo zuri kuwachagua viongozi hao kutoka CCM kwani wana uwezo mzuri wa kusimamia miradi ya maendeleo ambayo mipango huanzia ngazi ya Mitaa na kupitishwa Bungeni.

Kaijage aliwapongeza viongozi hao wa Serikali za Mitaa kwa ushindi walioupata nakuwataka  wakafanye kazi kwa kuwatumikia wananchi na kazi zao wanapozifanya wanapaswa kumtanguliza Mungu.

Moja ya wenyeviti walioapishwa Elizabeth Nyambilila alisema kuwa kipaumbele chake cha kwanza atakachoanza nacho ni kuhamasisha ujenzi wa shule ya msingi.

Nyambilila alisema kuwa tayari walishaanza mikakati kwanza ni kupata eneo hivyo wataenda kutafuta eneo kwa ajili ya kufanya ujenzi hio ili kuwapunguzia changamoto watoto wa mtaa huo kusoma mbali.