Tuesday, July 16, 2024

VIONGOZI WA DINI WAHAMASISHA WANAWAKE KUSHIRIKI CHAGUZI NA KUJIINUA KIUCHUMI





VIONGOZI wa Dini Halmashauri ya Mji Kibaha wamekuja na mkakati wa kuhamasisha ushiriki wanawake na wasichana katika uongozi na haki za kiuchumi.  

Aidha wametakiwa kuwania nafasi za uongozi kwani nao wanauwezo wa kuwa viongozi na haki yao washiriki ili walete maendeleo ndani ya jamii na nchi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mchungaji James Machage  wa Kanisa la Sabato Visiga wakati wa mafunzo ya Ushiriki wa wanawake na Wasichana katika Uongozi na Haki za Kiuchumi kwa Viongozi wa Dini yaliyofadhiliwa na UN WOMEN.

Mchungaji Machage amesema kuwa licha ya changamoto kubwa ya mila na baadhi ya imani lakini wataendelea kutoa elimu ya ushiriki kwenye uchaguzi na fursa za kiuchumi kwani wanauwezo wa kuwa viongozi.

Amesema kuwa watahakikisha wanasaidia wanawake ili waweze kupata haki zao na kuwatia moyo ili wajue fursa zilizopo kwani uongozi wa nchi unajali wanawake kwa kuwapatia fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo kupitia vikundi.

Naye Julieth Faustine katibu wa Kanisa la Katoliki Pangani amesema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kujua masuala ya uwiano kila linalofanyika lizingatie haki kwa wote na utendaji wa kazi bila ya kubagua kuwa baadhi ya kazi ni za wanawake na wanaume.

Faustine amesema kuwa kuna baadhi ya mila zinamkandamiza mwanamke ikiwa ni pamoja na ukeketaji kwa watoto wa kike, kunyimwa elimu, kunyimwa urithi wa ardhi na kutothaminiwa jambo ambalo atalipigia kelele ili jamii iachane na mila hizo.

Kwa upande wake Abdala Ngulengule amesema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea chachu ya kwenda kuwahamasisha wanawake kushiriki kwenye fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mweishoni mwa mwaka huu.

Ngulengule amesema kuwa mfano kwenye Kata ya Pangani kuna mitaa nane lakini yote ilikuwa ikiongozwa na wanaume hivyo wanatarajia kuwa na mabadiliko makubwa kwenye uchaguzi huo kwani wanawake wengi wamehamasika kushiriki uchaguzi huo ili wapatikaneviongozi wanawake angalau wawili au watatu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Kibaha Leah Lwanji amesema kuwa  wanaendelea kuwahamasisha wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili waweze kuingia kwenye vyombo vya maamuzi na kuwa na usawa katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ili waweze kujiinua kiuchumi na kupata fursa zilizopo ndani ya jamii.

Lwanji amesema kuwa Halamshauri inachokifanya ni kuwandaa wanawake kuwa na miradi mbalimbali ya kiuchumi kwa kuanzisha vikundi na kuwaunganisha katika taasisi za kifedha ambazo hutoa fursa za mikopo, mitaji, mafunzo  na masoko.

“Wanawake wengi wanakuwa na unyonge hivyo kushindwa kujiamini hivyo kupitia mradi huu tunawajengea uwezo kwani wakiwa na uwezo wa kiuchumi watakuwa na uwezo wa kujiamini na kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwania nafasi za uongozi ndani ya jamii,”amesema Lwanji.

Naye mratibu wa mradi wa (WLER) Maria Nkangali amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uelewa viongozi hao wa dini ili wakatoe elimu juu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi kuleta maendeleo kwa wananchi.

Nkangali amesema kuwa wanatoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali ili yatambue mchango wa wanawake na wasichana kwenye suala la maendeleo bila ya kujali jinsi. 

Mafunzo hayo siku moja yamewahusisha Viongozi wa Dini kwenye Kata mbalimbali na wataalamu wa idara mbalimbali za Halmashauri hiyo.  


Tuesday, July 9, 2024

YODAMEFO YAHITAJI MILIONI 10 UJENZI KITUO










SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la (YODAMEFO) la Picha ya Ndege Wilayani Kibaha linahitaji kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kujenga kituo cha ufundi kwa vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Mwanzilishi wa kituo hicho Anne Balisidya alisema kuwa wameshaanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa baadhi ya vijana wanaolelewa na kituo hicho.

Balisidya alisema kuwa kwa sasa wanatumia eneo dogo ambalo halitoshelezi kwa ajili ya shughuli hizo ambazo zinawaandaa vijana kuwa na ujuzi mbalimbali.

"Malengo ni kuwa na kituo kikubwa ambacho kitawakusanya vijana na kuwapatia mafunzo mbalimbali ya ufundi lakini kwa kuanzia tumeanza na masuala ya ujasiriamali ikiwemo utengenezaji wa batiki, sabuni za maji na bidhaa nyingine ,"alisema Balisidya.

Alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na vikao kwa ajili yafanya maandalizi ya chakula hicho cha hisani na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kufanikisha shughuli hiyo.

"Tumeona kuna faida kubwa kwa vijana kujifunza ujasiriamali kwani wameshaanza kuzalisha na wanauza wanapata fedha hivyo tukiwa na eneo maalum kwa ajili ya vijana kupata ujuzi,"alisema Balisidya.

Naye Mkurugenzi wa shirika hilo Ndesario Materu alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa fedha hivyo kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Materu alisema kuwa hawana wafadhili hivyo hujikuta wakitekeleza majukumu yao kwa ugumu kutokana na kutokuwa na vyanzo vya mapato ya kufanyia shughuli zao.

Kwa upande wake Sechelela Ndyanao alisema kuwa wanahidumia watoto waishio kwenye mazingira magumu wakiwemo wasichana walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na kupata ujauzito.

Ndyanao alisema kuwa wanawapatia ujuzi ambao utawasaidia kuwapatia kipato ili kiwasaidie na watoto wao na kwa wale wavulana waweze kujitegemea.

Saturday, July 6, 2024

WATUMISHI WA HALMASHAURI WATOA MISAADA MAKAO TISA YA WATOTO






WATUMISHI wa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kushirikiana na Watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha pamoja na wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya CRDB wametoa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 4.2 kwa makao tisa ya vituo vya kulea yatima.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa watoto hao kwenye sherehe ya makabidhiano iliyofanyika kwenye kituo cha Shallom kilichopo Kidenge Kata ya Mkuza Wilayani Kibaha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alisema kuwa wako na watoto hao hivyo wasijione wapweke.

Shemwelekwa amesema kuwa wao na watoto hao ni familia moja hivyo wameamua kuwasaidia ili kuwapa faraja na amani hivyo wasijione wapweke na hakuna yatima na serikali inapenda watoto ndiyo sababu ikaweka elimu bure ili watoto wapate haki ya msingi ya kupata elimu.

"Serikali inawapenda kama isingekuwa kulipiwa hali ingekuwaje watoto hawa ni familia yetu wanahitaji sukari, madaftari na mahitaji mengine na tukiwasaidia tunaweka hazina mbinguni na sisi tutaendelea kuwasaidia,"amesema Shemwelekwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa anapongeza wadau waliofanikisha kupatikana kwa misaada hiyo.

Mussa amesema kuwa wamejikita katika kuhakikisha watoto hao wanapata elimu kama ilivyo kwa watoto wanaoishi na familia zao kwani elimu ni haki yao. 

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Faustina Kayombo amesema kuwa Halmashauri ina makao tisa yenye watoto 601 na yote yamesajiliwa kisheria na kwa upande wa mafanikio ni makao kuwa na majengo bora.

Kayombo amesema kuwa changamoto ya watoto kuishi kwenye mazingira magumu ni pamoja na kubakwa, wazazi kupoteza upendo, mahusiano mabaya na wazazi.

Mmiliki wa Kituo cha Shallom Lilian Mbise amewashukuru watumishi na wadau hao kujitolea misaada hiyo kwa vituo vyao kwani vitadaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mahitaji ya shule, magodoro, madaftari, kalamu, penseli, vichongeo, rula, mafuta ya kujipaka, mafuta ya watu wenye ualbino.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani wa Halmashauri, wazee maarufu, viongozi wa dini, makundi mbalimbali yanayomuunga mkono Rais, vikundi vya sanaa na wananchi.


Friday, July 5, 2024

KPC YATAKA WATOTO KUJILINDA

MKURUGENZI wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga ametaka watoto wajilinde kwa kutotembea usiku na kwenda kwenye mabanda ya video na kulindana wao kwa wao ilikuepuka vitendo vya ukatili.

Mlenga ameyasema hayo wakati wa Siku ya Mtoto wa Afrika kimkoa iliyofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mjini Kibaha.

Mlenga amesema kuwa pia wasipokee zawadi au kuomba fedha kwa watu wasiowafahamu na wazazi wawalinde watoto kwa kutokuwa wakali na kuwahusisha na masuala ya dini ili wawe na hofu ya Mungu.

Akisoma risala ya watoto wa mkoa wa Pwani Evelin Mhema amesema kuwa baadhi ya changamoto ni pamoja kufanyiwa vitendo vya ukatili mimba za utotoni, ubakaji, vipigo na vitendo vingine vinavyowanyima haki zao.

Mhema amesema kuwa watashirikiana na viongozi wakiwemo walimu ili waweze kufikia ndoto zao walizojiwekea kwa kusoma kwa bidii na kutii wazazi na walezi wao.

Kwa upande wake Said Mwinjuma amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa changamoto kwa vijana na kusababisha mmomonyoko wa maadadili.

Mwinjuma amesema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwalinda watoto wao kwa kuwapatia malezi bora ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya na wasiwaache wajilee wenyewe na wawapatie elimu na stadi za kazi.


MAREKANI YAADHIMISHA SIKU YA UHURU WAKE

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe Dkt Michael Battle akitoa hotuba yake kwa Kiswahili jana jioni katika hafla ya kuadhimisha siku ya Uhuru wa Marekani maarufu kama  Julai 4, katika makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam.

Julai 4 ndio siku kuu ya nchini Marekani, ikiadhimisha kupitishwa kwa Tamko la Uhuru mnamo Julai 4, 1776  na Rais Thomas Jefferson, alipottangaza kupatikana kwa uhuru wa koloni kumi na tatu za Marekani kutoka utawala wa Uingereza.

Umuhimu wa Julai 4 kwa Wamarekani unatokana na sababu kadhaa kuu. Katika siku hii, Kongresi yao ilipitisha rasmi Tamko la Uhuru, ambalo lilielezea matamanio ya koloni kuunda taifa tofauti lililo huru kutoka utawala wa Uingereza.

Tamko hilo la Uhuru lilikuwa alama ya uhuru kamili na demokrasia. Liliainisha misingi ya msingi ya uhuru, usawa, na kutafuta furaha, ambayo ina maana kubwa kwa maadili ya Marekani.

Kupitishwa kwa Tamko kuliweka msingi wa Vita vya Mapinduzi, hatimaye kupelekea kuanzishwa kwa Marekani kama taifa huru. Ushindi katika vita na mkataba wa amani uliofuata na Uingereza ulithibitisha Julai 4 kama tarehe muhimu katika historia ya Marekani.

Kwa Wamarekaniu, kuadhimisha siku ya Uhuru  Julai 4 kumekuwa jadi ya muda mrefu, ikitia nguvu umoja wa kitaifa na uzalendo. 

Siku hiyo huadhimishwa na sherehe mbalimbali, ikiwemo fataki, gwaride, matamasha, na mikusanyiko ya familia, ambayo huleta watu pamoja kusherehekea urithi wao wa pamoja.

Ingawa tarehe nyingine, kama vile kusainiwa kwa Katiba au kumalizika kwa Vita vya Mapinduzi, pia ni muhimu, Julai 4 ina umuhimu wa  kipekee wakati ambapo koloni za Marekani zilichukua msimamo thabiti kwa uhuru wao.  Siku hii tangu hapo imekuwa sikukuu ya kitaifa inayoheshimu misingi ya nchi na roho ya kudumu ya watu wake.

Thursday, July 4, 2024

UMAUKI WAPANDA MITI KWENYE MAENEO YALIYOCHIMBWA MCHANGA







CHAMA cha Ushirika cha Umoja wa Wanamazingira na Udhibiti wa Uchimbaji Mchanga Kibaha (UMAUKI) kimeanzisha mradi wa upandaji wa miti katika maeneo yaliyoathiriwa na uchimbaji wa mchanga na shughuli ambazo si rafiki wa mazingira. 

Hayo yamesemwa na Meneja wa chama hicho Hay Mshamu wakati wa unzinduzi uliofanyika Mwendapole Kibaha.

Mshamu amesema kuwa chama kimeendelea na shughuli za kudhibiti uharibifu wa Mazingira unaotokana na sababu mbalimbali zikiwemo uchimbaji wa mchanga kiholela, ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa vyanzo vya maji.  

"Tulitekeleza mradi wa upandaji wa miti ya kivuli na matunda kuzunguka katika mipaka na katikati mwa eneo la shule ya Msingi Muungano,"amesema Mshamu.

Amesema kuwa mradi ambao umekamilika kwa 100 na sasa watoto wetu wananufaika na uwepo wa miti hiyo tumeendelea kufanva kazi mbalimbali rafiki wa mazingira hadi kufikia sasa.

Aidha amesema kuwa pia wanajihusisha na uvuvi, ufugaji wa nyuki lengo likiwa ni kulinda mazingira ili yawe salama na kurejesha uoto wa asili ambao umetoweka kutokana na uharibufu wa mazingira.

"Tunahitaji kiasi cha shilingi milioni 6.5 kwa ajili ya mradi wa kilimo cha matunda ya pasheni na papai ambapo tulianzisha kuanzia miche hadi kupanda lakini nguvu imeishia hapo huku tukihitaji kupata uzalishaji mzuri,"amesema Mshamu.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Kilimo Halmashauri ya Mji Kibaha Suzana Mgonja amesema kuwa chama hicho kinapaswa kutumia wataalam wa kilimo ili waweze kuzalisha kwa ubora.

Mgonja amesema kuwa wao wako tayari kushirikiana na wakulima ili kuhakikisha wanainuka na kulima kilimo bora na chenye manufaa siyo kilimo kisicho na tija.

Wednesday, July 3, 2024

MTAA MAILI MOJA A WAJENGA OFISI

 





UONGOZI wa Mtaa wa Maili Moja A umetimiza ahadi yake ya kujenga ofisi ambapo Diwani wa Kata ya Maili Moja aliizindua ofisi hiyo na kuondokana na ofisi waliyokuwa wamepanga.

Akiwaaga wananchi wa Mtaa huo kwente mkutano wa hadhara Mwenyekiti wa Mtaa huo Yassin Mudhihiri amesema wanawashukuru wananchi kwa kufanikisha ujenzi huo.

Mudhihiri amesema kuwa ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 95 lakini imeanza kutumika na wananchi wanapata huduma kwenye ofisi hiyo iliyoko eneo la Minazini.

"Tumemalia muda wetu wa uongozi wa kipindi cha miaka mitano ambapo mafanikio mengine ni kupata mradi wa barabara za lami, kurasimisha ardhi, kudhibiti wizi, kupata mradi wa Tasaf wa ujenzi wa barabara na mambo mengine ya maendeleo,"amesema Mudhihiri. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Ramadhan Lutambi akizindua ofisi hiyo amesema kuwa  uongozi uliomaliza muda wake umefanya kazi kubwa ya kujenga ofisi hiyo.

Lutambi amesema kuwa mtaa utapunguza gharama za kila mwezi za kulipa kodi hivyo fedha walizokuwa wakilipa kodi zitatumika kwenye matumizi mengine.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Maili Moja Methew Mkayala amesema kuwa mafanikio yote hayo yanatokana na utekelezaji wa ilani ya Chama.

Mkayala amesema kwa sasa wanajiandaa na uchaguzi wa wenyeviti wa serikali za Mitaa utakaofanyika hivi karibuni na kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.