Friday, March 31, 2023

MAHAKIMU NA MAJAJI WAPATIWA MAFUNZO

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAHAKIMU na Majaji wamepatiwa mafunzo ya siku mbili kuhusu wajibu wa Mahakama katika kutunza na kulinda uhuru wa kujieleza pamoja na haki za binadamu nchini.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) likiwa Ni kukumbushana masuala mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mratibu wa Mtadao wa THRDC, Onesmo Olengurumwa akizungumza na waandishi wa habari  jijini dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa Mahakimu na Majaji nchini amesema lengo ni kukumbushana wajibu katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Aidha amesema kuwa umekuwepo na mabadiliko mengi ya kisheria na masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu hivyo wao kama watu ambao wanatoa haki kila siku katika Mahakama, wanapaswa kuyafahamu ili kulinda haki za binadamu na uhuru wa kujieleza

Amesema pia mafunzo mengine ambayo yatatolewa ni masuala ya maadili kwa Mahakimu na Majaji katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa haki katika maeneo yao.

Amesema Suala la maadili ni jambo la muhimu sana katika mahakama zetu nchini hivyo mafunzo haya pia yatasaidia kuwakumbusha Mahakimu na Majaji wajibu wao wa kutenda haki kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.

Naye Naibu katibu mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (JMAT) Mary Kallomo, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kila siku katika kulinda haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

NAIBU WAZIRI KIKWETE ATEMBELEA WANANCHI WA MKANGE


Kuzungumza na Wananchi na kueleza hatua mbalimbali zilizofikiwa na serikali yetu katika kutatua changamoto zinazotokana na shughuli za maendeleo ikiwemo miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri yetu. 

Nimetumia nafasi hiyo kuwakumbusha mabadiliko mbalimbali yanayofanyika katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Afya, Elimu, Huduma za Jamii, Miundombinu, Maji, Utumishi wa Umma n.k. Ahadi yetu ni kuendelea kuwatumikia na kutatua changamoto zetu.#TukoPamoja #Chalinze #KaziInaendelea

TANESCO YATAKIWA KUWEKA KITENGO CHA KERO KININSIA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetakiwa kuweka kitengo maalumu kitakachoshughulika na kusikiliza kero za kijinsia ili kuweka usawa wa kijinsia katika shirika hilo.

Hayo yamesemwa Jijini hapa na Naibu Waziri wa Nishati,Stephen Byabato katika uzinduzi wa Programu ya Mpango wa Jinsia wa miaka minne(2023-2027)wa TANESCO kwa kusirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa umeme wa Tanzania hadi Zambia(Tanzania-Zambia Transmission Interconnector Project-TAZA).

Naibu Waziri Byabato amesema kuwa Shirika hilo limekuwa likishughulikia masuala ya jinsia kwa namna mbalimbali hivyo kwasasa ni wakati muafaka wa kuwa na kitengo kitakachokuwa na bajeti,uongozi wa kitengo chenye uelewa na uweledi wa kusikiliza kero za kijinsia mbalimbali zitakazojitokeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,Maharage Chande amesema kuwa lengo la programu hiyo kuwa ni kutatua changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanawake katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kukuza ajira zao ili kuongeza idadi ya wanawake wanaoajiriwa.

Mkurugenzi Chande ametaja maeneo ya kimkakati yatakayopewa kipaumbele kuwa ni kuiboresha sera ya Shirika na kujenga uwezo ili sera iende sambamba na masuala ya kijinsia,kuwepo na taarifa sahihi zinazohusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwenye Taasisi,kuruhusu fursa ya ukuzaji wa taaluma kwa wafanyakazi wanawake hasa wanaofanyakazi kwenye miradi na kuwepo kwa nafasi ya mafunzo kwa vitengo kwa wafanyakazi wanawake waliopo kazini ili kuwajengea uwezo kuelekea kwenye ajira kamili.

Aidha  kuhusu mradi wa kusafirisha umeme wa Tanzania hadi Zambia (TAZA),Chande ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO wanatekeleza ujenzi wa mradi wa upanuzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka katika kituo cha kupokea,Kupoza na kusafirisha umeme mkubwa cha Tagamenda Iringa kwenda kwenye nchi zilizopo kusini mwa Tanzania(Southern African Power Pool)kupitia Kisada Iringa,Iganjo Mbeya na Nkangamo Tunduma Songwe.

Chande amekitaja kituo hicho cha Tagamenda kuwa ni kitovu cha kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220 kwenda kwenye mikoa takribani 18 nchini.

Na kwa upande mwingine kituo hiki kimeunganishwa na kituo cha umeme cha zuzu Dodoma ili kusafirisha umeme mkubwa kwenda kwenye nchi zilizopo Mashariki mwa Tanzania ambazo ni Kenya,Uganda na Ethiopia kupitia mradi wa kuunganisha umeme baina ya Kenya na Tanzania(Kenya-Tanzania Power Interconnection Project-KTPIP)

Thursday, March 30, 2023

DK SAMIA ANA LENGO LA KUBORESHA AFYA KISARAWE.

RAIS DR SAMIA ANA LENGO LA KUIFANYA SEKTA YA AFYA  KUWA YA MFANO ZAIDI KISARAWE -DR JAFO

Na Mwandishi Wetu, Kisarawe 

WAZIRI wa nchi ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira (Mb) Jimbo la Kisarawe Mhe Dkt. Selemani Said Jafo amekabidhi vifaa mbalimbali vya afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuboresha huduma za afya katika wilaya hiyo kwa Vijiji 66 Fedha ikiwa ni kutoka kwa Mhe Rais Samia na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM katika Kutekeleza ilani ya 2020-2025.

Katika makabidhiano ya vifaa hivyo Mhe Dr Jafo amewapongeza watendaji wa Idara ya  afya katika hospitali hiyo kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuwahudumia wagongwa na pia ameahidi kuwa nao karibu ili kutatua baadhi ya changamoto wanazokutana nazo katika utoaji wa huduma kwa ujenzi wagonjwa.

Aidha wananchi wameishukuru serikali kwa kuwasaidia upatikanaji wa vifaa hivyo kwani vita saidia kupunguza usumbufu wa upatikanaji wa huduma ya matibabu hospitalini hapo

Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita Kwa kupendelea zaidi Kisarawe katika Upatikanaji wa Huduma ya Afya Kwa kuipatia Vifaa Tiba na fedha mbalimbali kwa Ajili ya Afya ambayo inaifanya Halmashauri ya Wilaya Kisarawe kuwa Nzuri katika Huduma za Afya.

Wednesday, March 29, 2023

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora ametembelea mradi wa Nyumba Za Watumishi Magomeni

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora  ametembelea mradi wa Nyumba Za Watumishi Magomeni na kuongea na watendaji wa Shirika la Nyumba la Watumishi( WATUMISHI HOUSING INVESTMENT), na kuwakumbusha kuendelea kusimamia msingi wa uwanzishwaji wa shirika hilo pasi kusahau kuendelea kujenga nyumba za Watumishi sehemu zenye uhitaji mkubwa kimkakati. #KaziInaendelea #WHI

Tuesday, March 28, 2023

KIKWETE AKUTANA NA TAASISI YA UONGOZI

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Ndg. Ridhiwani Kikwete, amezunumza na Watendaji wa Taasisi ya @UONGOZI mapema leo na kuwaasa kuendelea na kazi nzuri wanayoifanya bila kusahau msingi wa kuanzishwa kwa taasisi hiyo. #KaziInaendelea #UongoziBora

Sunday, March 26, 2023

WAZIRI UMMY AFIKA KWENYE VIJIJI UGONJWA WA MARBURG ULIPOANZIA


WAZIRI UMMY AFIKA KWENYE VIJIJI UGONJWA WA MARBURG ULIPOANZIA

Na. WAF - Bukoba, Kagera

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kutembelea vijiji vya Kata ya Maruku na Kanyangele vilivyopo Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera kwa lengo la kujionea hali inavyoendelea baada ya kutangazwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg Mkoani humo. 

Katika Ziara hiyo, Waziri Ummy ameambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Zabron Yoti pamoja na Mwakilishi wa Shirika la UNICEF Tanzania Bi. Shalini Bahuguna ili nao wajionee hali ya ugonjwa huo inavyoendelea kudhibitiwa nchini Tanzania. 

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa sasa hali ni salama na kuwataka Wananchi wa vijiji hivyo, wana Kagera na watanzania kwa ujumla kuondoa hofu na kuendelea na shughuli zao kwa kuwa Serikali inawajali Wananchi wake.

“Niwatoe hofu Watanzania tuendelee kufanya kazi zetu lakini tuzingatie maelekezo ya Serikali ya kujikinga na ugonjwa huu kwa kuepuka kushikana mikono hususan kipindi hiki lakini pia tujitahidi kunawa mikono mara kwa mara na maji tiririka kwa sabuni.” amesema Waziri Ummy

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na juhudi za kuhakikisha ugonjwa huo unamalizika kwa haraka na hautatokea tena katika maeneo hayo. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kanyangele Bw. Hamim Hassan ameishukuru Serikali kwa kufanya juhudi kubwa ambapo hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeongezeka kuwa na ugonjwa huo. 

“Hatua za haraka za Serikali kupitia Wizara ya Afya zilizochukuliwa za kuwaweka sehemu maalumu waliokuwa karibu na wagonjwa imesaidia sana kutoendeleza maambukizi kwengine na hali ni shwari kwa sasa.” amesema Bw. Hassan