Wednesday, November 30, 2022

WAWEKA MIKAKATI KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

WADAU WAENDELEA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA WILAYA YA KIBAHA



 IMEELEZWA kuwa uanzishwaji wa madawati kwenye shule na makundi mbalimbali ya jamii kutasaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa matukio yanayohusiana na vitendo hivyo.


Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwanasheria wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tanzania Zakia Msangi wakati wa kupita msafara unaotoa elimu ya kupambana ukatili wa Kijinsia ikiwa ni sehemu ya siku 16 za kupinga vitendo hivyo.

Alisema kuwa moja ya makundi yanayoathirika na vitendo hivyo ni watoto ambapo madawati hayo yataundwa kwa kushirikiana na walimu wa malezi kwenye shule.

"Madawati haya yatakuwa yakitoa elimu juu ya kupambana na ukatili wa Kijinsia na kuripoti vitendo hivyo kwenye vyombo husika ikiwemo dawati la jinsia na vyombo vingine vya sheria,"alisema Msangi.

Msangi alisema kwa shule kutakuwa na wanafunzi wawili vinara ambao watakuwa na ujasiri wa kujieleza na wenye usiri pia kutakuwa na sanduku la siri la kutolea maoni.

"Makundi mengine ndani ya jamii kama vile waendesha pikipiki nao wataunda madawati kwa ajili ya kupambana na matukio hayo ambapo itasaidia kukabili kwani ni kundi linalokumbana na mambo mengi,"alisema Msangi.

Aidha alisema kuwa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tanzania ni waratibu wa kampeni hiyo ambapo wameungana na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) ambao ndani yake kuna mashirika zaidi ya 100 kupambana na suala hilo.

Kwa upande wake ofisa Mawasiliano wa Shirika linalosaidia mashirika yanayotoa msaada wa sheria (LSF) Wilson Mtapa alisema kuwa wamewezesha msafara huo ili kupinga vitendo hivyo kwa kutoa elimu ya kupinga vitendo hivyo kwa kushirikiana na serikali na wadau wa maendeleo.

Mtapa alisema kuwa elimu hiyo inatolewa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwa ni pamoja na mashuleni madokoni na kwa vikundi vya waendesha bodaboda kwenye Wilaya msafara huo utakapopita kauli mbiu ikiwa ni Kila uhai unathamani tokomeza mauaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Alisema kuwa mashirika hayo mbali ya kupambana na vitendo hivyo pia yanatetea haki za binadamu ambapo wanatoa elimu ya namna ya kukabiliana na vitendo hivyo ndani ya jamii na msafara huo ulioanzia Dar es Salaam Pwani utapita mikoa ya Morogoro, Singida, Shinyanga, Arusha na Musoma.

Naye mwakilishi wa Shirika la Maendeleo kwa Vijana YPC ambalo liko chini ya MKUKI ambao ndiyo walikuwa wenyeji wa msafara huo Fred Mtei alisema kuwa ujumbe uliotolewa wa kukabiliana na vitendo vya ukatili umewafikia watu wengi.

Mtei alisema kuwa wao kama wana harakati wataendelea kutoa elimu na kuielimisha jamii namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.

Mkurugenzi wa Kituo Cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga alisema kuwa wamekuwa wakipokea wateja ambao wengi wao ni wa vitendo vya ukatili wa Kijinsia.

Mlenga alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na vyombo vya sheria ikiwemo Polisi na mahakama kupambana na vitendo hivyo kwenye Wilaya na Mkoa mzima wa Pwani na wanatoa elimu kwenye maeneo mbalimbali na makundi ya kijamii.

 Kwa upande wake Mratibu wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania kwa Mkoa wa Pwani Honorina Kambadu alisema kuwa wanazingatia haki na usawa mbele ya sheria na kukabili matukio ya ukatili wa Kijinsia.

Kambadu alisema kuwa baadhi ya matukio ni kama vile vipigo, unynyasaji na mauaji na kunyimwa haki zingine kwa wanawake na watoto ambao ndiyo waathirika wakuu wa vitendo hivyo.

Mwisho.

Tuesday, November 29, 2022

WAZIRI MKUU MAJALIWA ASEMA VIJANA WANAAJIRIKA


Na John Gagarini, Mkuranga

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa nchi inauwezo wa kuzingatia Utumishi kwenye sekta binafsi ili wawekezaji watumie vijana wa hapa nchini na kuachana na mawazo ya kuleta wafanyakazi kutoka nje ya nchi kwani Watanzania wanaajirika na ni waaminifu.

Majaliwa aliyasema hayo Kisemvule Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani alipokuwa anazindua kiwanda na mabati cha Lodhia Group of Company na kusema kuwa vijana wa Kitanzania wanauwezo wa kufanya kazi na hakuna sababu ya wafanyakazi kutoka nje ya Tanzania.

Alisema kuwa vijana wa Kitanzania wanaajirika na wanafanya kazi kwa bidii na kwa sasa hata vitendo vya kutopenda kufanya kazi hilo halipo tena wanawajibika ipasavyo. 

"Waajiriwa zaidi ya 3,000 kitendo cha kutoa ajira umesaidia sana tutakuunga mkono uendelee kutoa vijana ambao wako mtaani itasaidia kufanya nchi kuwa na amani nchi imepanua wigo na fursa za uwepo wa viwanda,"alisema Majaliwa.

Aidha alisema uwepo wa kiwanda hicho umesaidia kutoa ajira na hiyo ni fursa kwa wengine inasaidia kuzalisha na kupanua wigo ili kusaidia watu wengine zaidi hapa ni ajira zaidi ya 2,500 hilo ni jambo kubwa.

"Serikali ya awamu ya sita imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kuja kuwekeza kwa wale wa ndani na nje maelekezo tuliyopewa kuanzia kuomba kuwekeza na kuanza uwekezaji ni kuhakikisha hawapati shida wala kikwazo chochote ili kila upande unufaike mwekezaji na mwananchi,"alisema Majaliwa. 

Aliongeza kuwa kampuni hiyo ni moja ya kampuni inayolipa kodi kubwa nchini ambapo inalipa zaidi ya bilioni 40 kwa mwezi ni kama lulu watatatua changamoto zinazoikabili kwani nachangia pato la serikali na kusaidia huduma za jamii na inamuunga mkono Rais kwa kupunguza changamoto ya ajira.

"Hapa Tanzania ni sehemu salama ya uwekezaji tunatambua na tunaheshimu uwekezaji huu kwani huyu ni wa kuenziwa na Halmashauri ili wapate fedha zaidi na hatimaye nchi inufaike hakika leo nimefurahi sana kutembelea kiwanda hichi ambapo Arusha nlitembelea walikuwa na kiwanda kidogo sana uwekezaji mkubwa na malengo kuweka mradi mkubwa zaidi naifurahi kutembelea,"alisema Majaliwa.

Alibainisha kuwa kiwanda hicho kinachozalishwa chuma mbalimbali zikiwemo nondo ni kikubwa kuliko viwanda vyote alivyotembelea na kuweka jiwe la msingi la kiwanda ukubwa wake ni hekari nane na nusu kitatengeneza bati.

"Uwepo wa viwanda vya nondo, plastiki, mabomba ya maji na bati itasaidia bidhaa kwani zitapatikana hapa nchini badala ya kuagiza nje na pia zina ubora bado eneo dogo kufikia kiwanda cha Afrika Mashariki itafikia hatua hiyo na kuwa kiwanda kikubwa hapa Afrika Mashariki,"alisema Majaliwa.

Aliongeza kuwa uwepo wa viwanda vijana Teknolojia na hilo limepewa kipaumbele ili wajifunze kupitia mitambo hiyo ya kisasa ni faida ya uwepo wa viwanda nchi itakuunga mkono na milango itakuwa wazi na azma ya kutembelea ni kuangalia uwekezaji unaofanywa ukiwemo kwenye mabomba ya maji na serikali inaona kuwa anafunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan alisema na kuwahakikshia kuwa uwekezaji hautakwama hata kidogo.

Kwa upande wake Mwenyekiti na mwanzilishi wa kampuni hiyo Haroun Lodhia alisema kuwa kiwanda chao kinalipa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 22 kwa ajili ya umeme na gesi ambapo baadaye watakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 40,000 za chuma kwa mwezi.

Lodhia alisema kuwa kwa siku za baadaye watazalisha umeme wao wenyewe ambapo wataanza kuzalisha megawati tano na baadaye kva 25 na wanaishukuru serikali kwa kuwawekea mazingira mazuri kuendesha shughuli zao.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdala Ulega alisema kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliopo kwenye Wilaya ya Mkuranga na wingi wa magari yanayokwenda mikoa ya Kusini wangeomba barabara ya Kusini ipanuliwe na kuwa ya barabara nne.

Ulega alisema kuwa barabara hiyo kuanzia Mbagala Rangitatu kwenda Mwandege Vikindu na kuendelea ingepanuliwa ili bidhaa ziweze kwenda kwa urahisi na pia hapo Mkuranga viwanda vingi tumia umeme mkubwa na hakuna gari la Zimamoto ikitokea moto itakuwa ni shida sana hivyo wapatiwe huduma ya gari hilo.

Mwisho.


Friday, November 25, 2022

CHANJO COVID-19


VIJANA WAJITOKEZE KUCHANJA COVID-19

VIJANA nchini wametakiwa kujitokeza kupata chanjo ya ugonjwa COVID 19 na waachane na dhana potofu kuwa hawawezi kuambukizwa ugonjwa huo.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mtaalam wa chanjo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Caroline Akim alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na chanjo ya COVID 19. 

Akim alisema kuwa moja ya kundi kwenye jamii ambalo halijitokezi kuchanja wakidhani kuwa hawawezi kupatwa na ugonjwa huo hivyo kuwa hatarini kuambukizwa ugonjwa huo.

"Vijana wanadhana kuwa hawawezi kupata ugonjwa huo kwani baadhi hawana dalili ya maambukizi licha ya kuwa wao ndiyo wenye pilika pilika nyingi,"alisema Akim.

Alisema kuwa vijana ni kundi ambalo linahimizwa kupata chanjo kutokana na kuwa na mizunguko mingi kwenye jamii na kuwa rahisi zaidi kueneza ugonjwa huo pale wanapoupata.

"Wajawazito pia wanahimizwa kupata chanjo ya COVID-19 kwani wakipata ugonjwa huu wako kwenye hatari ya mimba kutoka au mtoto kuzaliwa kabla ya wakati na hata wanaonyonyesha wanakumbushwa kuwa chanjo ni salama kwao haina madhara kwa mtoto" alisema.

Aidha alisema kuwa waandishi wanatakiwa  sasa kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchanja lakini pia faida zake ili kuepuka kuingia kwenye athari wanapopata ugonjwa huo.

Naye Mratibu wa chanjo mkoa wa Pwani Abas Hincha alisema kuwa wanatarajia kuanza kampeni ya chanjo ya COVID-19 inaanza Novemba 25 na watawafikia wananchi ambao bado hawajapata chanjo.

Hincha alisema kuwa Mkoa huo unatarajia hadi kufikia Desemba 30 kuwafikia wananchi 757,465 na kwamba hadi kufikia Novemba 22 walengwa 468,187 tayari wamepata chanjo sawa na asilimia 63.

Saturday, November 19, 2022

SAMIA AASA VIONGOZI WA DINI JUU YA AMANI



Wellu Mtaki, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaasa viongozi wa dini hapa nchini kuendelea kushikamana na serikali kudumisha uzalendo na amani ya nchi .

Amebainisha hayo leo Novemba 19.2022 Jijini Dodoma katika sherehe ya Jubilee ya miaka 50 ya Kanisa la Waadventista Wasabato Jiji la Dodoma ambapo amesema amani ndiyo msingi wa utulivu wa nchi.

Ametumia fursa hiyo kulipongeza Kanisa la Waadventista Wasabato kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha amani na kuendelea kushirikiana na serikali kwa miradi mbalimbali ya huduma za kijamii ikiwemo katika sekta za afya,elimu na kusaidia wenye uhitaji.

Aidha amekipongeza kikundi cha uimbaji cha watoto wa shule ya Msingi na awali cha Ellen White pamoja na Kwaya ya Nyarugusu SDA kutoka mkoani Geita kwa kuimba wimbo wenye uzalendo na upendo wa taifa la Tanzania.

Kuhusu suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii Rais Samia amewaasa viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na serikali kukemea vitendo viovu ikiwemo kushirikiana katika mapambano ya dawa za kulevya na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Amesema suala la mabadiliko ya nchi ya ukosefu wa mvua katika baadhi ya maeneo amewaasa viongozi wa dini na washarika kwa ujumla kuliombea Taifa huku akitoa wito kwa viongozi wa dini kuwa mabalozi kuelimisha jamii kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo Rais Samia amehitimisha kwa kusema kuwa ni muhimu sana kutegemea neema na Baraka za mwenyezi Mungu kama isemavyo Zaburi 127:1.

Naye Mwenyekiti Kanisa la Waadventista Wasabato Union ya Kusini mwa Tanzania [STU] Mch.Dkt.Godwin Lekundayo amemhakikishia Rais Samia kuwa Kanisa litaendelea kushirikiana na serikali katika kuwajengea maadili vijana .

Mch.Lekundayo ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa serikali ya Tanzania kwa ajali ya ndege ya Precision Air iliyoua watu 19 hivi karibuni mkoani Kagera huku akisisitiza kuwa kanisa litaendelea kuiombea Tanzania kuepusha majanga.

Katibu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kusini mwa Tanzania[STU] Mch.Jeremiah Izungo amesema wao kama kanisa wataendelea kushirikiana na serikali kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta za elimu na afya.

Mch Izungo amesema kanisa linaendelea kusisitiza afya ya jamii ikiwemo kuzingatia kanuni bora za afya,lishe na kuchangia damu salama ambapo huwa kuna utaratibu wa kuchangia damu salama kila mwaka mwezi Machi.

Amesema changamoto zinazolikabili Kanisa ni pamoja na usaili wa nafasi za kazi serikalini siku ya Jumamosi ya ibaada ambapo hukosesha vijana nafasi za ajira serikalini pamoja na mitihani shuleni kufanyika siku ya Jumamosi ya ibaada.

Ameiomba serikali kuwapatia wataalam wabobezi katika hospitali za Kanisa huku akiweka msisitizo kuwa Kanisa linajitegemea haliko kwenye muunganiko wa wa Umoja wa Kikristo Tanzania [CCT].


Wednesday, November 16, 2022

WALIMU WAKUU KUPATIWA MAFUNZO NA ADEM


ADEM KUTOA MAFUNZO YA UONGOZI

Na Wellu Mtaki, Dodoma

WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) imesema imejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu 17,000.

Aidha itatoa mafunzo ya utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt Siston Masanja akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/2023.

Dkt Masanja amesema katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 wakala hiyo imejipanga kudahili Walimu 2,343 katika kozi mbalimbali pamoja na kuandaa kitabu cha kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.

Dkt.Masanja amesema moja kati ya malengo ya Wakala hiyo ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa elimu bora shuleni kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya elimu, kuziba ombwe la maarifa na ujuzi ambalo kiongozi au mtendaji hakupata katika mafunzo ya awali ya Ualimu na kuongeza idadi ya viongozi wenye maarifa ya uongozi na usimamizi wa elimu.

Kwa Upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali imeweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchini ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8.

Aidha, Msigwa ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu pamoja na wakuu wa shule kwenda kusoma ADEM.

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM ulianzishwa Agosti 31, 2001 ukiwa na majukumu ya kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa elimu katika ngazi zote na kutoa ushauri wa kitaalamu katika mambo yanayohusu uongozi na usimamizi wa elimu.

Mwisho. 

Friday, November 11, 2022

MABILIONI YATOLEWA KUBORESHA AFYA

SERIKALI YATOA BILIONI 200 UNUNUZI VIFAA TIBA NA DAWA

Na Wellu Mtaki, Dodoma

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Aidha tayari bilioni 74.3 zimetolewa katika kumaliza changamoto ya upungufu wa dawa na vifaa tiba nchini.

Dkt. Mollel amesema hayo leoJijini Dodoma Novemba 11,2022 wakati akijibu swali la Mhe. Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa viti maalumu katika kikao cha kumi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Amesema, Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kutatua changamoto za huduma za afya kwa wananchi, huku kiasi cha shilingi Bilioni 74.3 zikiwa tayari zimetolewa kati ya Bilioni 200 zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ununuzi wa dawa pamoja na vifaa tiba.

"Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga bajeti ya shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na hadi kufikia tarehe 30 Oktoba, 2022 Serikali imekwisha toa jumla ya shilingi bilioni 74.3 kwa ajili ya manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuimarisha upatikanaji wake katika ngazi zote za utoaji wa huduma za Afya,"amesema Dkt. Mollel. 

Amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya nchini kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kuweka vifaa tiba vya kisasa, kuajiri Wataalamu wa Afya pamoja na kuwapandisha madaraja ili kuongeza morali ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Akijibu swali la nyongeza Dkt. Mollel amesema, Serikali imepeleka vifaa vyenye thamani ya shilingi Bilioni 3 katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara - Kwangwa vitavyosaidia kutatua changamoto ya wananchi kwenda mikoa ya mbali kutafuta huduma hizo.

Ameendelea kusema kuwa, ifikapo Desemba 12, 2022 hospitali hiyo itaanza kutoa huduma zote, huku akisisitiza tayari CT-SCAN imeshafungwa na MRI ikisubiri chumba kikamilike ili huduma hiyo nayo ianze kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Mara na nchi za jirani.

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Serikali imejipanga katika udhibiti wa dawa kwa kutengeneza mfumo mzuri kutoka zinapotoka ngazi ya taifa mpaka zinapofika katika kituo husika, huku akisisitiza ushirikiano baina ya viongozi, kamati za afya na wananchi katika kusimamia dawa ili ziweze kuwafikia walengwa. 

Pia, ameelekeza hospitali kutumia mapato ya ndani kutatua changamoto za dawa endapo zitajitokeza ili kutatua changamoto hizo kwa wagonjwa wanaoenda kupata huduma katika maeneo hayo ya kutolea huduma. 

MTUMISHI KUKATWA MSHAHARA


BARAZA LA MADIWANI LATOA ADHABU KWA MTUMISHI WA HALMASHAURI KUKATWA MSHAHARA.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha limemchukulia hatua Mhandisi wake Brighton Kishoa kwa kumkata asilimia 15 ya mshahara kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kushindwa kusimamia mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi.

Akitoa maazimio ya kikao hicho cha baraza la madiwani cha robo mwaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Musa Ndomba alisema kuwa mtumishi huyo alisababisha mradi huo kuwa na gharama kubwa.

Ndomba alisema kuwa moja ajenda iliyojadiliwa na baraza hilo ni makosa ya kinidhamu ya kiutumishi yaliyofanywa na Mhandisi huyo wa Halmashauri hiyo ambaye hakufuata utaratibu wa manunuzi (BOQ) ya ujenzi wa nyumba hiyo.

"Kutokana na kutofuata taratibu za manunuzi kulitokea changamoto kwenye ununuzi wa vifaa kwani haukufuata bajeti iliyopangwa hivyo gharama za ujenzi kuwa kubwa,"alisema Ndomba.

Alisema baada ya changamoto hiyo kutokea ilibainika kuwa katika usimamizi wa miradi ilionekana kuna maeneo kafanya uzembe hivyo baraza la madiwani na kamati ya fedha ziliamua kumchukulia hatua za kinidhamu.

"Taratibu zote zimefuatwa kwa kamati za uchunguzi na kufanya kazi yake na zikapendekeza adhabu hiyo na hilo litakuwa fundisho kwa watumishi wengine kwa kutakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazowaongoza," alisema Ndomba.

Aidha alisema kuwa anawakata watumishi wote kuanzia Halmashauri hadi kwenye Mtaa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na wasipingane na miongozo ya kazi zao kwani miradi ya maendeleo itakuwa haina tija na kurudisha nyuma utoaji huduma kwa wananchi.

"Sisi kama baraza hatutarudi nyuma kwani tutachukua hatua kali kadiri inavyowezekana kwa mtumishi yoyote atakayeonyesha utovu wa nidhamu katika utendaji kazi wake na tutatoa adhabu kali zaidi kwa mtumishi atakayekwenda kinyume na taratibu za kazi yake na kuzorotesha utoaji huduma kwa makusudi,"alisema Ndomba.

Alibainisha kuwa hawapendi kutumia muda mwingi kujadili mtu bali wanapenda muda mwingi wautumie kujadili masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi.